BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,825
- 287,847
Polisi wapambana na wananchi kwa risasi
na Mkolo Kimenya
Tanzania Daima
POLISI wa Kituo cha Wazo Hill, jijini Dar es Salaam, jana walilazimika kutumia risasi za moto kuwatawanya wakazi wa vijiji vya Chasimba, Wazo na Madala, ambao walifika eneo hilo kwa lengo la kuonana na Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Wananchi hao, ambao wana mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na Kiwanda cha Saruji Tanzania (TPCC), walifika katika kituo hicho baada ya kupata taarifa kuwa, Lowassa alikuwa afanye ziara kiwandani hapo.
Hata hivyo, Lowassa, ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mtambo mpya wa kiwanda hicho, hakufika na badala yake aliwakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Batilda Burian.
Wakati waziri huyo akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho kinachozalisha saruji ya Twiga, ambao ndio wanaomiliki mtambo huo, ghafla risasi zilisikika, hali ambayo ilizusha mtafaruku na kuvuruga usikivu baada ya waandishi wa habari na baadhi ya watu kutimka kuelekea zilikosikika risasi hizo.
Risasi hizo zilifyatuliwa na askari polisi kutoka mbele ya kituo hicho.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia kundi la wanakijiji hao wakiwazomea polisi, huku wakiwarushia mawe, wakishinikiza kuonana na mgeni rasmi katika uzinduzi wa mtambo huo.
Wakazi wengine walisikika wakipaza sauti zao wakisema wanataka wenzao, waliodai kuwa walikamatwa na polisi awali na kufikishwa kituoni hapo, waachiwe haraka.
Polisi waliendelea kufyatua risasi hewani, lakini wakazi hao hawakuonekana kuogopa na zaidi waliendelea kulisogelea eneo la kituo, hali ambayo iliwafanya polisi waanze kuwatawanya kwa nguvu na kufanikiwa kuwakamata baadhi yao.
Sakata hilo lilidumu kwa muda, na polisi wakafanikiwa kuwatawanya watu hao, huku wananchi zaidi ya wanne wakitiwa mbaroni, wakiwemo wanawake wawili ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali mstaafu, Fabian Massawe, ambaye alikuwepo katika hafla hiyo, alionyesha kusikitishwa na hali hiyo na akawataka wakazi hao kufuata utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao.
Kama wanaona hawakutendewa haki, ni vema waende polisi wachukue RB, kisha waende mahakamani, lakini sio kutumia njia za vurugu na vitu vingine vya namna hiyo, alisema Massawe.
Massawe alionyesha kuwashangaa wananchi hao huku akidai kuwa wao ni wavamizi wa maeneo ambayo wanayalalamikia.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kunduchi, Wamula Maranda, aliyesema kuwa, kitendo cha wananchi hao ni vurugu zisizo na msingi, kwani ni wavamizi katika maeneo hayo.
Hata nyumba hakuna katika hayo maeneo wanayodai kuwa ni ya kwao, wamevamia na hata mawe ya mipaka katika viwanja hivyo ambavyo vina wamiliki halali, wameyangoa, alisema.
Maranda alisisitiza kuwa, mara kadhaa amewasisitizia wananchi kufuata utaratibu katika kuwasilisha madai yao, lakini wamekuwa wakikaidi.
Aidha, mmoja wa wakazi hao, aliyejitambulisha kwa jina la Sheikh Lukindo Lyimo, alidai kuwa, walifika kituoni hapo kwa lengo la kutaka kuwaona wenzao ambao walikuwa wamekamatwa awali.
Sisi tumefika hapa kwa lengo la kutaka kuwaona wenzetu watano ambao walikamatwa na si vinginevyo, lakini cha kushangaza, badala ya kusikilizwa, tunaanza kufukuzwa, na kama hivi unavyoona, vurugu tupu kama tupo kwenye mapigano, na wengine wameshakamatwa na kuwekwa ndani, sasa hii ni haki kweli? alihoji.
Alisema kwa sasa hawana makazi na wanaishi porini kutokana na kufukuzwa katika maeneo ambayo walikuwa wakiishi awali, kwa kuelezwa kuwa si wakazi halali wa maeneo hayo.
Hivi karibuni, Massawe alifanyiwa vurugu na wananchi hao, alipofika katika eneo hilo kwa lengo la kutatua mgogoro huo.
Siku kadhaa baadaye, Mahakama Kuu ilitoa amri ya muda, ikiwataka wananchi hao waendelee kuishi hapo hadi hapo kesi yao itakapoamriwa.