Je, kisheria ni lazima kila mkataba uwe wa maandishi? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je, kisheria ni lazima kila mkataba uwe wa maandishi?

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by sulphadoxine, Dec 16, 2011.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Dec 16, 2011
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  Wajibu katika mkataba wowote ni kwa pande mbili au zaidi zinazohusika ambazo zinafanya mapatano hayo. Hivyo, kisheria mapatano ni yale ambayo pande husika zimekubaliana kubanwa na sheria katika utekelezaji wake.

  Hii inatokana na ukweli kwamba mikataba yote ni mapatano lakini si kila mapatano ni mikataba. Nimewahi kusema kwa mfano ahadi za kirafiki au za ndugu katika familia (baba, mama na watoto) mara nyingi si za kimkataba na hazitambuliki kisheria.

  Kifupi ni kwamba sheria huangalia suala zima la mapatano (makubaliano au ahadi) na matokeo yake kisheria au jinsi sheria inavyoweza kuyapa nguvu mapatano husika kwani ni suala ambalo linaenda sanjari na sheria za madai.

  Kama nilivyosema awali katika mkataba wowote kuna makubaliano au mapatano kuhusu haki na wajibu kwa kila upande unaohusika na mkataba huo. Ikitokea upande mmoja umeshindwa kutimiza wajibu wake, mkataba utavunjika na upande mwingine utadai fidia mahakamani.

  Swali la msingi ni je, lazima kila mkataba uwe wa maandishi? Majibu ya swali hili yatapatikana tukiangalia moja ya aina za mikataba ambazo kisheria imegawanywa katika sehemu mbili: Kuna “Mikataba ya Kawaida” ambayo haihitaji maandishi na “Mikataba ya Fungo” ambayo huhitaji maandishi au hati rasmi.

  Hebu tuangalie tu aina ya kwanza ya mikataba yaani mikataba ya kawaida ambayo mapatano au makubaliano yake yanaweza kufanyika kwa njia yoyote ile, yaani kimaneno, au kimaandishi au kwa vitendo tu fulani au kwa jumla ya njia zote hizo tatu. Suala muhimu ni kuwepo kwa mawasiliano kati ya waundaji wa mkataba.

  Hivyo sio lazima na sio kweli kwamba ili kuwepo kwa mapatano au makubaliano yenye nguvu ya mkataba kisheria ni lazima yawe katika maandishi kama ambavyo watu wengi hudhani.

  Kwa mfano unaponunua kitu chochote dukani au sokoni au unapopata huduma ya usafiri wa basi au teksi au kupata chakula hotelini, yanakuwa ni mapatano ambayo hayajawekwa kimaandishi ingawa unaweza kuomba upate risiti au tiketi.

  Katika kesi ya FADHILI v. LENGIPENGI (1971) HCD 31mlalamikaji alidai mifugo aliyokabidhiwa na marehemu mama yake ambayo hakukabidhiwa kimaandishi. Mahakama ilisema katika mila za kiafrika mapatano yanafanyika bila maandishi na kwamba kuandika ni jambo la kisasa kwa wale waliopata “elimu ya wazungu” (elimu ya darasani).

  Katika kesi nyingine ya RUKU na MAGORI v. MAGORI (1971) HCD 161 mlalamikiwa na mtu mwingine walikubaliana kusafirisha kwa mtumbwi mboga za majani za mlalamikaji. Lakini walalamikiwa hawakuzisafirisha mboga hizo na hivyo zikaharibika. Mlalamikaji alishtaki mahakamani akitaka alipwe fidia ya sh. 3, 140 kutokana na hasara aliyopata kwa mkataba kuvunjwa.

  Wazee wa Baraza waliruhusu robo tatu ya mapatano hayo lakini Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo aliyesikiliza kwa mara ya kwanza shauri hilo alikataa na akaruhusu nusu tu ya madai hayo ambapo pamoja na mambo mengine alisema kwamba hapakuwepo na mapatano yenye nguvu kisheria kwani wahusika hawakuandikiana.

  Mlalamikaji alikata rufaa Mahakama ya Wilaya ambayo ilikubaliana na wazo la Wazee wa Baraza kwamba alipwe robo tatu tu ya madai yake. Mlalamikaji hakuridhi hivyo akakata rufaa tena kwenda Mahakama Kuu mbele ya Mheshimiwa Jaji Robert Kisanga.

  Jaji Kisanga alisema: “Wakati hakimu alipoona kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha unaosaidia uamuzi anaoupitisha, suala la kwamba mapatano ya wahusika hayakuwa katika maandishi yasingeathiri uamuzi huo. Cha muhimu ni lile kusudio kwamba wahusika walikusudia na kwa kweli waliunda uhusiano wa kimkataba, ingetosha tu kwa mahakama kuyapa nguvu mapatano hayo.”

  Hivyo kwa mujibu wa mikataba ya kawaida ambayo mingi haifanyiki kimaandishi, kinachohitajika ni ushahidi wa mapatano au makubaliano husika hata kama ushahidi huo ni wa mdomo tu.

  Kuna pia mikataba ijulikanayo kama “Mikataba Fahamifu” ambayo haihitaji maandishi yoyote. Mfano ni pale mtu anaingia hotelini au bar na kuketi halafu mhudumu anayemfahamu anamletea chakula au kinywaji ambacho anajua ndicho unapendelea.

  Mtu huyo akiamua kula au kunywa chakula au kinywaji hicho atakuwa ameingia katika mkataba ambapo atapaswa kulipia chakula au kinywaji hicho hata kama hukukiagiza. Kwa matendo yake atachukuliwa kwamba ameingia katika mkataba.

  Kuna wakati fulani katika safu hii tuliwahi kuona kwamba ili makubaliano au ahadi zozote wanazowekeana watu ziwe na hadhi ya mkataba halali yanapaswa kuwa na vitu kadhaa kama vile ridhaa, huria, gharama, uwezo na uhalali wa kitu.

  Hata hivyo, kitu kingine muhimu ni kwamba makubaliano ili yafikie hadhi ya mkataba, lazima yawe yenye “nia ya kutambulika kisheria” ili upande wowote ukikiuka makubaliano hayo, upande mwingine uweze kushtaki mahakamani.

  Upande unaoshtaki mahakamani unaweza kuwa unataka kupata nafuu yoyote kama vile fidia, sitisho la muda au la kudumu, kurudisha katika hali ya kawaida ya awali, au kupewa malipo ya ziada.

  Tunachojifunza leo hapa ni kwamba sio kila makubaliano au ahadi ni mkataba ambao sheria yaweza kusimamia utekelezaji wake. Kwa mfano makubaliano yote ya nyumbani kati ya mume na mke, watoto na wazazi na ndugu wengine huwa hayana nia ya kutambulika kisheria.

  Baba anaweza kumuahidi mke wake au mtoto kumnunulia nguo nzuri kwa ajili ya sikukuu yake ya kuzaliwa, lakini akashindwa kutekeleza ahadi hiyo kutokana na kutokuwa na fedha aliyotarajia kuwa nayo. Mke au mtoto aliyetarajia kupata zawadi hiyo hawezi kumshtaki mume au baba yake mahakamani kwa kuvunja makubaliano ya ahadi hiyo.

  Hii ina maana kwamba mipango yote ndani ya familia haitambuliki kisheria, kwa vile hakuna upande wowote unaodhamiria kuyapeleka mahakamani makubaliano hayo kwa ajili ya kuyapa nguvu ya kisheria ili upande utakaovunja uwajibike kwa kulazimishwa kutekeleza au kulipa fidia ya usumbufu au maumivu.

  Kuna mifano ya kesi mbili za makubaliano ya kifamilia ambazo ni BALFOUR vs BALFOUR (1919) na JONES vs PADA VOTTON (1969). Katika kesi ya Balfour, mume alienda kufanya kazi India na kumuahidi mkewe aliyekuwa amemuacha Uingereza kwamba angekuwa anamtumia paundi 30 kila mwezi.

  Ndoa yao (akina Balfour) baadae ilivunjika. Mwanamke akamshtaki mume akitaka aendelee kumtumia zile paundi 30 kila mwezi. Mahakama iliamua kwamba mkataba huo haukuwa na nia ya kutambulika kisheria kwa vile ulikuwa makubaliano kati ya mume na mke.

  Katika kesi ya Jones na Pada, mwanamke mmoja alikuwa akiishi na mwanawe wa kiume jijini Washington, Marekani. Mtoto alikuwa ameajiriwa kama mhasibu katika ubalozi wa India. Mama akamshauri mwanae aache kazi na aende Uingereza akasomee sheria.

  Mama huyo alimuahidi mwanae kwamba akihitimu masomo hayo ya sheria atampa nyumba na pesa. Mwanae alipohitimu masomo hakupata nyumba aliyoahidiwa. Akaamua kumshtaki mama yake mahakamani. Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo kwa kutotambua kuwepo kwa mkataba uliotambulika kisheria.

  Ni mikataba gani inayotambulika kisheria? Jibu la haraka ni mikataba yote ya kibiashara hutambulika kisheria kama ilivyoelezwa katika kesi ya Kampuni ya ROSE na FRANK vs J. R. CROMPTOM (1923).

  Katika kesi hiyo Mahakama ilisema mambo yote ya kibiashara yanahitaji yafanyike kwa uangalifu na uaminifu mkubwa baina ya pande zote katika biashara husika. Kwamba iwapo upande mmoja utavunja uaminifu huo, ndipo sheria huchukua mkondo wake. Hivyo kuwepo kwa mkataba wenye nguvu ya kisheria ni muhimu

  Hata hivyo, Sheria ya Mikataba ya Mwaka 1961 ya Tanzania haitamki wazi umuhimu wa mikataba kutambulika kisheria, ikilinganisha na sheria ya mikataba ya Kenya na Uganda. Hata hivyo, kwa kuzingatia maamuzi ya kesi mbali mbali hasa ndani ya nchi za Jumuia ya Madola ambazo hufafanana kwa mfumo wa kisheria, mahakama huzingatia kanuni hiyo muhimu.
   
 2. J

  Jamuhuri Huru Member

  #2
  Dec 20, 2011
  Joined: Sep 20, 2011
  Messages: 32
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Good!! Well!! Thanks a lot
   
 3. T

  TULIBAHA Member

  #3
  Dec 25, 2011
  Joined: Jan 23, 2011
  Messages: 49
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 15
  Inatosha kabisa salphadoxine
   
 4. monongo

  monongo JF-Expert Member

  #4
  Dec 25, 2011
  Joined: Oct 25, 2011
  Messages: 370
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 35
  Nashukru kwa ufafanuzi wako mzuri wa mikataba,kweli binafsi nimejifunza,na nitaendelea kufuatilia Topic hii.
   
Loading...