Je, banda la ukubwa gani linatosha kuku wangu?

Mnazi kuyumba

New Member
Jun 7, 2013
4
37
JE, BANDA LA UKUBWA GANI LINATOSHA KUKU WANGU?

Hili ni swali rahisi sana lakini cha kushangaza, limekuwa linasumbua sana wafugaji wengi. Watu wanajijengea mabanda kiholela na kuishia kuwa na magofu makubwa ya mabanda bila kuku.

Kujibu swali hili katika ufugaji wa kuku wa kienyeji ni muhimu maana usipolijibu hakika utapata hasara kwani utajenga banda kubwa sana ambalo ni mzigo au utajenga dogo sana likakupa changamoto.

Ujenzi wa banda unachukua zaidi ya nusu ya gharama zote za ufugaji kwahiyo unatakiwa kuwa makini sana kupunguza gharama hizi. Kwani ukitumia gharama kubwa kwenye malighafi au ujenzi wa banda kubwa kupita uhitaji au uwezo wako utaangukia pua maana matumizi ya mradi wako yatazidi mapato hivyo utapata hasara.

MAMBO YA MSINGI
Mambo ya msingi kabla ya kujua ukubwa wa banda lako ni lazima ufanye maamuzi makubwa matatu:-

1. Aina ya kuku na maumbile yao.
Kila aina ya kuku inategemea ukubwa wa nafasi inayotosha kuwafuga kulingana na ukubwa wa maumbile yao. Kuku wenye maumbile makubwa wanahitaji nafasi kubwa zaidi.

2. Mtindo wa ufugaji.
Ipo mitindo mikubwa mitatu ya ufugaji. Mtindo wa kuwaachia huru nje, mtindo wa kuwafuga ndani bila kutoka nje na mtindo wa kuwafuga ndani ya uzio. Nafasi ya kuku kuvinjari inategemeana na hii mitindo.

3. Chagua idadi ya ukomo wa kuku unaoanza nao.
Kamwe hakuna marefu yasiyo na ncha. Haiwezekani kufuga idadi yoyote ya kuku bila kikomo sababu kwa kawaida rasilimali ni ndogo kuliko mahitaji kwahiyo hatuwezi kufanya kila kitu.

Kwa sababu hiyo unatakiwa kufanya uchaguzi mradi wako utaanzaje na nini ni ukomo wa idadi ya kuku unaoweza kuwafuga bila shida katika mtaji ulionao sasahivi. Chagua idadi ya kuku ambayo utaweza kuwahudumia kwa chakula, matibabu n.k

Panga kuanza kidogo na uwe unakua taratibu kwa kupata uzoefu wa kutatua changamoto za kila siku za ufugaji.

JINSI YA KUKADIRIA UKUBWA WA BANDA
Baada ya kufanya maamuzi hayo ya msingi sasa nenda kakadirie ukubwa wa banda lako.

Kanuni ni rahisi sana. Kwa mtindo wa kufungia ndani ya banda bila kuruhusu kuku kutoka nje basi kila kuku aliyekomaa atahitaji nafasi ya futi 2 za mraba.

Wakati kwa mtindo wa kuwaachia nje au kuwafungia nje ndani ya uzio, kila kuku atahitaji nafasi ya futi moja ya mraba.

Maana yake nini?

Tuchukue banda letu lina upana wa futi 10 na urefu wa futi 20.

Banda hili litakuwa na ukubwa wa Futi za mraba 200 yaani (Futi 20 X Futi 10)

Sasa kama unalenga kutumia banda hili kufuga kuku kwa mtindo wa kuwafungia ndani bila kutoka nje. Banda hili litatosha kuku 100 tu. Yaani ni sawa na kuchukua ukubwa wa banda zima gawanya kwa nafasi ya kuku mmoja. (200ft² ÷ 2ft² = 100)

Kwa upande mwingine kama unataka kufuga kwa mtindo wa kuwaachia nje au kuwafungia nje ndani ya uzio basi banda hili litatosha kuku 200 tu. (200ft² za banda zima gawanya na 1ft² za nafasi ya kuku mmoja sawasawa kuku 200).

ZINGATIA
: Ukubwa huu wa banda sio kwa ajili ya kuku unaoanza nao bali ni kwa ajili ya ukomo wa idadi ya kuku unaotegemea kumaliza nao mzunguko wako wa ufugaji.

NJIA RAHISI SANA YA KUJUA UKUBWA WA BANDA

Usichoke kwa ukokotoaji mwingi wa ukubwa wa banda. Kuna njia rahisi zaidi ya kujua hilo.

Chakufanya : Amua idadi ya ukomo wa kuku unaotaka kuwafuga bila kujali ukubwa wa maumbile yao.

Baada ya kuamua, zidisha idadi hiyo mara moja kama unataka kufuga kwa mtindo wa kuwaachia au kuwafungia nje ndani ya uzio, jibu lake ni ukubwa wa banda lako katika futi za mraba.

Mfano : Ukomo wako ni kufuga kuku 50 katika mfumo wa kuwaachia nje au kuwafungia nje ndani ya uzio. Basi unachukua 50×1=50ft²

Ikiwa unataka kuwafungia ndani bila kutoka nje basi unachukua ukomo wa idadi yako ya kufuga unazidisha mara mbili kisha unakuwa umepata ukubwa wa banda lako katika futi za mraba.

Mfano : Ukomo ni kufuga kuku 50 katika mfumo wa kuwafungia ndani bila kutoka nje. Basi unachukua 50×2=100ft²

USHAURI

1. Ongeza ukubwa wa banda taratibu jinsi ambavyo mradi wako unakua au unaongezeka. Banda la futi 3 kwa 6 linatosha kuanzia kuku wa kienyeji kisha ukaendelea kujenga kulingana na mahitaji.

2. Kabla haujamuita fundi ujenzi jua kwa hakika ukubwa wa banda na gharama za malighafi utakazotumia kujenga banda lako.

3. Kanuni ya msingi ni kupunguza gharama za ujenzi ziwe chini kadri inavyowezekana. Kumbuka kuku wa kienyeji kiasili ni ndege wa porini, anaweza kuhimili mikikimikiki ya usumbufu wa mazingira.

Kesho uwe karibu na simu yako, nitakuonesha kitu kizuri sana kitakachokusaidia kwenye ufugaji wa kuku. Usikose.

Karibu! Tuvute pamoja, akili kichwani, pesa mfukoni na Mungu moyoni.
 
JE, BANDA LA UKUBWA GANI LINATOSHA KUKU WANGU?

Hili ni swali rahisi sana lakini cha kushangaza, limekuwa linasumbua sana wafugaji wengi. Watu wanajijengea mabanda kiholela na kuishia kuwa na magofu makubwa ya mabanda bila kuku...

Mkuu ninajenga banda la mita 3x3 naweza fuga kuku wangapi wa kienyeji kwa mfumo wa kuwaachia nje?
 
Mkuu ninajenga banda la mita 3x3 naweza fuga kuku wangapi wa kienyeji kwa mfumo wa kuwaachia nje?
Yaani kwa wepesi kabisa square mita 1 inachukua kuku 5 kwa wastani. Hii ni kwa kuwafugia ndani ya banda muda wote. So kwa vipimo vyako wataingia kuku 45 (Ufugaji wa kuku wa kisasa-mfano SASSO).
 
Yaani kwa wepesi kabisa square mita 1 inachukua kuku 5 kwa wastani. Hii ni kwa kuwafugia ndani ya banda muda wote. So kwa vipimo vyako wataingia kuku 45 (Ufugaji wa kuku wa kisasa-mfano SASSO).

Kuku wa kienyeji wa kuwaachia nje.
 

Similar Discussions

4 Reactions
Reply
Back
Top Bottom