Jasusi la kitanzania lilivyowatoka wanajeshi Uganda

Sehemu ya tatu

abu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 3
Habari Zinazoendana
Share
…………….
KATIKA wiki mbili zilizopita tumechapisha sehemu mbili za uchambuzi wa wa kitabu kipya kinachoitwa MATEKA MPAKANI kilichoandikwa na kachero wa Tanzania, Frown Kageuka (pichani) kumuenzi mwenzake aliyeuawa mpakani mwa Tanzania na Uganda na majasusi wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin. Leo tunaendelea na sehemu ya tatu ya mfululizo wa uchambuzi wa kitabu hicho.
……………
TULIFIKA Makindye usiku, eneo hilo lilifanana sana na Manzese ya Dar es Salaam. Kwa hakika safari yetu ilikuwa ndefu sana kwa hiyo nilihisi tumeingia ndani sana ya nchi ya Uganda na labda tulikuwa karibu na Kampala.
Tuliteremshwa ‘kikuku’ na kuingizwa katika nyumba moja ambayo nilihisi ni mahabusu. Tuliachwa humo tukiwa bado na kamba miguuni na mikononi hadi alfajiri. Usiku wote hatukuweza kuongea lakini asubuhi nilijua tupo wote pamoja baada ya Koplo Sudi kumwambia Sajini Binda kwamba ana njaa sana. Kwa kweli hata mimi nilikuwa na njaa sana lakini hatukuwa na la kufanya. Jua lilipoanza kuonesha makali yake tulifunguliwa kamba tulizofungwa na askari mmoja mwenye cheo cha Sajin.
“Mnataka chai au uji? Aliuliza Sajini huyo ambaye alionyesha ni katili sana. “Chochote unachoona tunastahili,” nilijib kwa upole. “Mimi nawapa uchaguzi nyinyi wafungwa,” alijibu Sajin huyo na kuondoka.
Dakika kama tano hivi baadaye mlango ulifunguliwa na Sajini yule yule aliyekuwapo awali, akaingia ndani akifuatiwa na askari mmoja asiye na cheo ambaye amebeba birika na vikombe vitatu vya bati.
“Haya punguzeni njaa kwa mlo huu nyie wafungwa” alitamka Sajin huyo kwa kebehi huku mwenzake akiweka birika na vikombe karibu yetu na kuondoka.
“Kwani sisi ni wafungwa?” niliuliza kwa upole huku nikimkazia macho. “Eh! Kumbe nyinyi ni kina nani?” alijibu Sajenti huyo huku akinitolea macho. “Sisi sio wafungwa bwana. Tunashangaa jinsi mlivyotukamata na kutuleta hapa.” “Hayo mimi sijui, ninachokijua nyingi ni askati mateka kutoka Tanzania kwa hiyo ni wafungwa.”
“Sisi sio askari bwana, kama mmeambiwa hivyo mmedanganywa kabisa. Mmeshindwa kuwapata askari halisi mkatukamata sisi raia na kutuita askari. Huo ni uonevu mkubwa,” nilimwambia kwa upole.
“Nyinyi watu wa Tanzania Kiswahili kirefu sana, kama siyo askari mmmefikaje hapa Makindye?” aliuliza kwa mshangao huku akituthitibishia hapo tulipo ni Makindye.
“Lakini kama sisi ni wanajeshi kama mnavyotaka tuwe, basi inabidi mtupe huduma sawa na mkataba wa Geneva unaohusu wafungwa wa kivita.” “Wewe mbona unaongea sana? Au ndiyo mkubwa?” aliniuliza kwa ukali na kuondoka zake.
“Inaonyesha hawa wanampango mbaya na sisi, hapa walipotuleta ni ndani kabisa ya nchi yao, ni maili chache tu kufika mjini Kampala. Sijui kama tutarudi salama. Iddi Amin hajawahi kuachia mtu salama na hasa waliokamatwa kimya kimya kama sisi. Ni lazima tufanye kitu ili tujiokoe” niliwaeleza wenzangu kwa sauti ya chini lakini kabla hawajanijibu mlango ulifunguliwa. Askari mmoja aliyevalia rasmi kipolisi jeshi (Military Police) alituamuru tutoke nje haraka. Hapo nje tuliwakuta askari wengine sita waliokuwa na bunduki aina ya AK 47 kila mmoja.
Tulifungwa pingu mikononi na kuongozwa hadi kwenye uwanja ambao bila ya kuamiwa nilijua ni sehemu ya kuulia watu kwa kupigwa risasi. Tulifungwa katika miti iliyokuwa mbele ya magunia mengi ya mchanga ambayo nilijua ni maalumu kwa kuzuia risasi isiende mbali ya hapo.
Baada ya kufungwa kamba kuzunguka mti nilijiona nimeshakuwa mfu. Koplo Sudi na Sajini Binda walianza kulia kama watoto wadogo. Niliogopa sana hali hiyo, kwa vile nilijua Waganda hao watagundua mimi ni kiongozi wao kutokana na ujasiri wa kutoogopa kifo na pia hiyo ilinithibitishia kwamba wenzangu sasa watakuwa tayari kutoa siri zetu zote. Dakika kama mbili baadaye askari jeshi watatu walisimama hatua kama tano mbele yetu na kutulenga kwa bunduki zao.
Wakati nikianza kumuomba Mungu anisamehe makosa yangu niliyomkosea ili anipokee huko mbinguni, ghafla ilifika gari moja aina ya Jeep ikiwa na askari mmoja mwenye cheo cha kanali na mwingine aliyevaa Kaunda suti ya rangi ya kijivu ambaye nilimuhisi ni afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Iddi Amin inayoitwa SRB. Maofisa hao waliteremka kwenye gari na kutusogelea.
“Naona nyinyi ni vijana wadogo sana, kwa hiyo najua hampendi kufa au siyo?” aliuliza kanali huyo huku akitukazia macho. Wote tulikaa kimya bila kutoa jibu lolote wala kukohoa.
“Nani mkubwa kati yenu kwa cheo? Aliuliza ofisa aliyevaa kiraia lakini naye hakupata jibu.
“Nataka kuwahakikishieni kitu kimoja, atakayekuwa mkweli hatutamuua na kwa kuwa tutamhoji kila mtu peke yake inabidi hapa tuwafunge mmoja mmoja. Mtu mjeuri hapa ndio utakuwa mwisho wake” alitamka kanali huyo kwa ukali. “O.K fungua hawa wawili abakie huyu,” aliamuru aliyevaa kiraia.
Mimi na Koplo Sudi tulifunguliwa na kurudishwa mahabusu, Sajini Binda tukamwacha akiwa bado amefungwa. “Hata kama ukisema ukweli haiwezi kuwazuia kutuua. Kumbuka kiapo chako usiwe mwoga.” Nilimkumbusha Koplo Sudi. “Lakini, lakini afande….” “Shii, kumbuka kiapo , usiwe mwoga, kama ni kifo acha tukikabili.” Nilisisitiza.
Kabla ya Koplo Sudi hajaendelea kutamka neno linguine tukasikia mlio wa risasi tatu ambazo zilitufanya tupate kiwewe cha ghafla.
“Wameshamuua, wameshamuua.” Alilalamika Koplo Sudi. Mimi sikumjibu lolote bali nilimkazia macho tu, alipoona hivyo aliinuka haraka alipokaa na kuniangukia miguuni kwangu huku akilia.
“Watatuua wote afande,” alilalamika. “Wacha tufe lakini kumbuka kiapo, usiwe mwoga,” nilimjibu huku na mimi nikitoa mchozi wa chuki.
“Nisaidie afande, naogopa sana.” Alizidi kulalamika. “Nyamaza!” nilimwamuru kwa ukali, akanyamaza. Punde kidogo mlango ulifunguliwa na polisi jeshi mmoja. “Nani ndiye Koplo Sudi?” aliuliza askari huyo akiwa amesimama mlangoni. Koplo Sudi hakujibu bali aliongeza kasi ya kulia na kumfanya askari huyo aje juu.
“Nauliza nani ndiye Koplo Sudi sitaki kusikia kilio.” Alifoka. “Ni mimi, ni mimi.” Hatimaye alijibu. “Kuja hapa haraka.” Aliamuru kwa ukali. Koplo Sudi aliinuka na kumfuata.
Alipotoka mlango ukafungwa, nikabaki ndani peke yangu. Sasa nikajua siri zimeanza kutoka, kama wamemjua Koplo Sudi bila shaka Sajini Binda amekwishawaeleza mengi. Hofu ikazidi kuniingia, nikajua sasa watanishughulikia mimi kikamilifu wapate siri. Niliwaza sana bila kupata jibu lolote, tama ya kujiokoa ikaanza kujengeka polepole akilini mwangu.
“Wakishajua mimi ndiye kiongozi hasira zao zote zitaniangukia mimi.” Nilijisemea peke yangu kama mwehu. Dakika kama ishiriki baadaye nikasikia mlio wa risasi mbili nikajua Koplo Sudi naye ameshauawa. Hofu ikanizidi, nikajua zamu yangu ya kutolewa roho imekaribia. Nilimkumbuka Mungu, nikamwomba aniokoe na kifo hicho, nikalia sana, lakini sikulia kwa hofu ya kifo bali nilimlilia Mungu aniepushie balaa hilo. Kilio change kilikatizwa ghafla na sauti ya polisi jeshi aliyekuwa mlangoni.
“Unalia huku umepiga magoti na mikono juu unamwomba Mungu eee! Alitamka askari huyo kunigutua. Haraka nilifuta machozi yangu, kwa kweli nilipata nguvu mpya, hofu ya kifo ilinitoka kabisa, nilihisi ni sababu ya kilio changu kwa Mungu.
“Wewe ndiyo Luteni, siyo?” aliniuliza huku akitabasamu. “Umetumwa unite au uniulize swali?” nilijibu kwa upole huku nikitabasamu.
“Haya unaitwa,” alitamka huku akiendelea kutabasamu. Niliinuka haraka tukaongozana hadi kule kwenye uwanja wa mauaji ambako nilipaita machinjioni. Nilipofika hapo nikafungwa kamba kama awali kisha askari wanne wenye silaha wakajipanga mbele yangu wakingoja amri ya kunifyatulia risasi. Baada ya kufungwa kamba nikaoiona tena ile gari aina ya Jeep ikija na baadaye ikasimama palepale iliposimama mwanzoni. Yule kanali na mwenzake aliyevaa kiraia ambaye nilimuhisi ni afisa usalama wa taifa kutoka SRB, walinisogelea tena kama walivyofanya mwanzoni. Muda wote huo nilikuwa naichunguza ile miti kuona kama ina damu ili nipate uhakika kama wenzangu kweli wameuawa.
Hata hivyo sikuona damu yoyote katika miti hiyo kwa hiyo nikahisi umetumika ujanja wa kututisha lakini kama wametumia mbinu hiyo basi wamesahau kupata miti hiyo japo rangi inayofanana na damu.
“Wewe ndiyo Luteni Njata au siyo?” aliniuliza huyo aliyevaa kiraia. “Unaniambia au unaniuliza?” nilimjibu bila hofu. “Wenzako wote wamekubali kushirikiana nasi na wamejibu vizuri lakini tumewaua kwa ujeuri wao.” Alieleza kanali huyo.
Maneno haya niliyatafakari na kugundua wenzangu hawajauawa bali wamenigeresha mimi kwa milio ya risasi tu. “Sasa jibu maswali yetu vizuri na kwa usahihi, udanganyifu wowote utakaofanya utasababisha uwafuate wenzako huko ahera, umenielewa?” alitamka.
“Nimekuelewa bwana.” Nilijibu kwa upole. “Wewe tumeambiwa ndiyo kiongozi wa wenzako na cheo chako ni luteni, kweli?”. “Kweli” nilijibu kwa upole huku nikimkazia macho. “Unaongoza askari wangapi pale Murongo?” ofisa aliyevaa kiraia aliniuliza.
“Nawaongoza hao hao wawili waliowaambia mimi ni kiongozi wao.” “Yaani wewe ni kiongozi wa askari wawili tu, kambi gani hiyo ya watu wawili?” aliuliza kanali. “Kwani wameaambia tupo wangapi?” “Ah? Yaani wewe badala ya kutujibu maswali yetu, unatuuliza sisi maswali tukujibu?” alifoka huyo aliyevaa kiraia.
“Siyo hivyo wakubwa, maswali yenu mengine najua majibu mnayo wenyewe, sasa mimi nashangaa mkiniuliza. Mnanichelewesha bure kunipiga risasi, niuweni roho zenu zitulie.” Nilijibu kwa utulivu mkubwa uliowafanya wanishangae. “Wewe huogopi kufa?” aliniuliza kanali huku akinikazia macho.
“Kila mtu atakufa hapa duniani hata kama utamtanguliza mwenzio kufa ujue iko siku na wewe utamfuata.” Nilijibu na kuwafanya wazidi kunishangaa. “O.k. sawa bwana, sasa pale Murongo kuna kambi ya jeshi?” aliuliza kanali. “Hakuna” nilijibu kwa mkato.
“Kumbe nyinyi ni askari mnaofanya nini pale kijijini?” alifoka aliyevaa kiraia. “Tunataka kufundisha askari raia yaani mgambo.” “Mmeshaanza kuwafundisha?” alizidi kuuliza. “Bado labda mwezi ujao tutaanza.” “Kitu gani kinachowafanya muanze kufundisha mwezi ujao?” ofisa huyo aliuliza. “Bado hatujakamilisha mipango ya kupata vifaa na watu wa kuwafundisha.” “Unaona unavyojibu vizuri? Wewe sasa utakuwa rafiki yetu hatuwezi kukuua.” Alitamka kanali huku akitabasamu.
“Pale Murongo kuna redio ya mawasiliano?” alizidi kuuliza ofisa huyo huku akiandika. “Ipo.” Nilijibu nikijua wenzangu wameshaeleza yote. “Ipo sehemu gani pale Murongo?” aliuliza kanali.
“Kwa kweli ni vigumu, labda twendeni nikawaonyeshe huko huko,” nilijibu kwa upole na kuwafanya wacheke sana. “Wewe mjanja sana, kweli wewe ni ofisa wa jeshi,” alisifu ofisa huyo aliyevaa kiraia.
“Hebu mfungueni kamba, huyu sasa ni rafiki yetu, ameonesha ushirikiano, tutawarudishia Murongo,” aliamuru kanali kisha wakaingia kwenye gari yao na kuondoka. Polisi jeshi mmoja alinifungua kamba na baadaye wakanirudisha mahabusu ambako niliwakuta Sajini Binda na Koplo Sudi wakinywa uji. Sikuwasemesha kitu nilikaa kwa huzuni huku nikiwakazia macho.
“Mmewaeleza mambo mengi sana mkifirikia ni njia ya kujinusuru katika mikono yao, siyo?” niliwauliza kwa upole lakini sikupata jibu. “Tuone sasa kama kweli wataturudisha Murongo baada ya kuwapa wanachokitaka,” nilizidi kueleza.
“Nani kati yenu aliulizwa juu ya masafa (frequency) ya redio yetu ya mawasiliano?” niliwauliza lakini hakuna aliyenijibu.
Hali hiyo ilinithibitishia kwamba wameeleza mambo mengi sana na sasa wanaona aibu hata kuongea na mimi. “Ndiyo maana hawakuniuliza maswali mengi kwa kuwa mengi wamekwishaelezwa na hawa.” Niliwaza.
Jioni ilipofika tulitolewa humo mahabusu tukiwa tumefungwa vitambaa vyeusi usoni na pingu mikononi, tukaingizwa ndani ya lori moja. Dakika chache baadaye lori hilo liliondoka kuelekea tusipopafahamu lakini tulitumia muda wa dakika kama ishirini au ishirini na tano hivi ndipo lori hilo liliposimama. Tuliteremshwa na kuongozwa hadi kwenye ngazi fulani ambako tuliteremka chini hadi kwenye chumba kimoja chenye hewa nzito na harufu mbaya ya mikojo na damu.
Humo tulifunguliwa vitambaa tulivyofungwa lakini ikawa sawa na tulivyofungwa kutokana na giza la humo ndani. Hali ya mahabusu ile ya Makindye ilikuwa ni afadhali kuliko hii inayotisha. Tulitulia kimya sakafuni bila kusemezana kitu kutokana na utisho wa humo ndani. Hata hivyo kwa kawaida maongezi yananoga unapoongea na mtu huku unamuona, sasa hii giza imevunja hata hamu ya kuongea.
Tulikaa humo ndani bila kufahamu kama ni jioni, usiku au asubuhi imefika. Kwa kadiri nilivyotafakari jinsi tulivyokamatwa na tulivyofanyiwa ni dhahifi kifo kilikuwa bado kinatuandama. Uchovu na njaa ndiyo vitu vya kwanza kutishia maisha yetu hasa mimi ambaye nilikuwa sijaonja kitu chochote kwa siku mbili. Wakati tukiwa bado hatujui la kufanya tulisikia sauti kutoka kwenye kipaza sauti kidogo kilichokuwa humo ndani.
“Luteni Njata na Sajini Binda kuja nje haraka.” Sauti hiyo iliamuru na wakati huo huo mlango mzito wa chuma ulijifungua tukaona mwanga kidogo mbele yetu. Mimi na Sajini Binda tuliinuka na kuuendea mlango huo lakini Koplo Sudi alimshika Sajini Binda huku akilia sana akimuomba asimuache. Nilishangaa sana kwa nini amshikilie Sajini binda badala ya mimi mkubwa wao. Hata hivyo baadaye nilihisi labda kwa vile mimi amekwishaniudhi kwa kusaliti kiapo cha jeshi letu. Sajini Binda alipoona Koplo Sudi hamuachi, akaamua kutoka naye. Tulitokea kwenye ukumbi mrefu ambako tuliwakuta vijana wawili waliovalia Kaunda suti zao maridadi wakitusibiri.
“Mmeitwa wawili mnakuja watatu, nyinyi watu vipi?” alifoka mmoja wao ambaye ni mfupi kidogo kuliko mwenzake. “Huyu mwenzetu anaogopa kubaki peke yake” alijibu Sajini Binda.
“O.K. njooni huku.” Alitamka huku akitangulia mbele. Kwa kweli humo ndani kulionesha wazi ni sehemu ya mauaji. Tuliongozana na maofisa hao katika ukumbi huo mrefu uliokuwa unawake taa hadi kwenye mlango mwingine wa chuma uliokuwa upande wa kushoto. Ofisa huyo aliugonga mlango huo kwa kutumia chuma cha kufungia nje na baada ya sekunde chache ukafunguliwa.
Bila kuongea na aliyeufungua mlango huo, akatuonyesha ishara tuingie ndani. Sajini Binda na Koplo Sudi walitangulia kuingia wakifuatiwa na mimi. Maofisa waliotuleta wakafunga mlango huo kwa nje na kuondoka zao. Humo ndani tulikuta ukumbi mrefu kidogo uliojaa harufu mbaya zaidi kuliko kule tulipowekwa mwanzo. Kulikuwa na nyororo nyingi zilizofungwa ukutani ambazo zilinijulisha ni za kufungia watu. Mbele kidogo ya ukumbi tulikuta watu wanne wamefungwa nyororo mikononi wakiwa wamesimama wima lakini vichwa vyao upande wa sura wameangushia vifuani mwao huku damu zikiwatoka mdomoni, puani na masikioni. Walionesha uhai umekwishawatoka. Kuona hivyo, Koplo Sudi alianza kutapika hatimaye akazirai.
Wakati tunamhudumia Koplo Sudi kwa kumpepea kwa mashati yetu tuliyoyavua, mlango uliokuwa juu ya ngazi mbele yetu ukafunguliwa. Wanaume sita vipande vya baba wakaingia na kusimama mbele yetu. Miamba hiyo ya watu ilikuwa vidari wazi na walivaa chupi tupu. Hakika unaweza kuzimia kabla hawajakugusa. Jinsi maumbile yao yalivyo na sura zao mbaya za kutisha ni dhahiri wamewekwa maalumu kwa ajili ya utesaji hadi kuua. Moyoni nilijua wazi tupo katika jengo maalumu la Idara ya Ujasusi ya Iddi Amin (SRB) la kuhojia watu. Tukaamriwa tuvue nguo zetu zote tubaki kama tulivyozaliwa. Baadaye watu hao wakaanza kutupiga mgongoni kwa kutumia waya fulani bila ya kutusemesha kitu. Ulikuwa ni muda wa adha kubwa ambayo tangu nizaliwe sijawahi kuipata. Koplo Sudi alizimia tena akifuatiwa na Sajini Binda lakini wauaji hao waliendelea kuwapiga hadi mimi nikaona niwaokoe.
 
Sehemu ya NNE

SAJINi Binda alipoona Koplo Sudi hamuachii, akaamua kutoka naye. Tulitokea kwenye ukumbi mrefu ambako tuliwakuta vijana wawili waliovalia Kaunda suti zao maridadi wakitusubiri.
“Mmeitwa wawili mnakuja watatu, nyinyi watu vipi?” alifoka mmoja wao ambaye ni mfupi kidogo kuliko mwenzake. “Huyu mwenzetu anaogopa kubaki peke yake,” alijibu Sajini Binda. “O.k njooni huku” alitamka huku akitangulia mbele. Kwa kweli humo ndani kulionesha wazi ni sehemu ya mauaji. Tuliongozana na maofisa hao katika ukumbi huo mrefu uliokuwa unawaka taa hadi kwenye mlango mwingine wa chuma uliokuwa upande wa kushoto. Ofisa huyo aliugonga mlango huo kwa kutumia chuma cha kufungia nje na baada ya sekunde chache ukafunguliwa.
Bila kuongea na aliyeufungua mlango huo, akatuonyesha ishara tuingine ndani. Sajini Binda na Koplo Sudi walitangulia kuingia wakifuatiwa na mimi. Maofisa waliotuleta wakafunga mlango huo kwa nje na kuondoka zao. Humo ndani tulikuta ukumbi mrefu kidogo uliojaa harufu mbaya zaidi kuliko kule tulipowekwa mwanzo. Kulikuwa na nyororo nyingi zilizofungwa ukutani ambazo zilinijulisha ni za kufungia watu. Mbele kidogo ya ukumbi tulikuta watu wanne wamefungwa nyororo mikononi wakiwa wamesimama wima lakini vichwa vyao upande wa sura wameangushia vifuani mwao huku damu zikiwatoka midomoni, puani na masikioni. Walionesha uhai umekwishawatoka. Kuona hivyo, Koplo Sudi alianza kutapika hatimaye akazirai.
Wakati tunamhudumia Koplo Sudi kwa kumpepea kwa mashati yetu tuliyoyavua, mlango uliokuwa juu ya ngazi mbele yetu ukafunguliwa. Wanaume sita vipande vya baba wakaingia na kusimama mbele yetu. Miamba hiyo ya watu ilikuwa vidari wazi na walivaa chupi tupu. Hakika unaweza kuzimia kabla hawajakugusa. Jinsi maumbile yao yalivyo na sura zao mbaya za kutisha dhahiri wamewekwa maalumu kwa ajili ya utesaji hadi kuua. Moyoni nilijua wazi tupo katika jengo maalumu la Idara ya Ujasusi ya Idi Amin (SRB) la kuhojia watu. Tukaamriwa tuvue nguo zetu zote tubaki kama tulivyozaliwa.
Baadaye watu hao wakaanza kutupiga mgongoni kwa kutumia waya fulani bila kutusemesha kitu. Ulikuwa ni muda wa adha kubwa ambayo tangu nizaliwe sijawahi kuipata. Koplo Sudi alizimia tena akifuatiwa na Sajini Binda lakini wauaji hao waliendelea kuwapiga hadi mimi nikaona niwaokoe.
“Ebu waacheni hao mimi ndiye mkubwa, nitawaeleza yote na kama kuteswa mimi ndiyo ninayestahili siyo hawa.” Nilitamka kwa taabu sana huku nikiona giza usoni.
“Usiposema utakuwa mwisho wako katika mto wa mamba,” alijibu mmoja wao. “Nitaeleza yote, kweli yote, mwiteni mkuu wa Idara ya SRB niongee naye,” nilitamka kisha fahamu zikanipotea.
Nilipozinduka nikajiona nipo sakafuni nimelala, nikainuka haraka na kuangaza macho huku na huku nikajiona bado tupo kwenye ukumbi huo huo wa kutisha. Sajini Binda na Koplo Sudi walikuwa wamelala mbele yangu huku damu zikiendelea kuwavuja mgongoni na mdomoni. Hata mimi pia nilikuwa natokwa damu kinywani na mgongoni ambako kulijaa mipasuko ya kuchapwa. Nilipoangaza kwenye mlango wa juu ya ngazi nikaona pamefungwa nikajua ile mipande ya watu imerudi ndani. Kabla sijawaza zaidi, mlango tulioingilia ulifunguliwa na kijana mmoja aliyevaa Kaunda suti ya rangi ya kijivu.
“Waamshe wenzako mje huku” alitamka kijana huyo ambaye alionyesha ni wa kabila la Kinubi ambalo limejaa katika Idara ya Usalama wa Taifa ya Idi Amin Dada. Niliinuka haraka na kuwaamsha wenzangu ambao walikuwa hoi kabisa. Mimi niliona ni nafuu tuondoke humo ndani ingawa sikujua ya huko tunakokwenda. Nilitumia karibu dakika kumi kuwazindua Sajini Binda na Koplo Sudi. Tulipojikongoja kwa maumivu makali huku tukiongozwa na kijana huyo hadi kwenye chumba kingine ambacho tuliambiwa tuvae nguo zilizomo. Kwa kweli hazikuwa nguo za kuvaa labda niite makoti ya kaki ambayo yalitusitiri kwa kuwa hatukuwa tumevaa nguo.
Baada ya kuvaa kaki hizo akatupeleka katika chumba kisafi kidogo ambamo kulikuwa na meza moja na viti vitatu. Ofisa huyo alituambia tukae sakafuni tusubiri kisha yeye akaondoka zake. Dakika kama tano hivi baadaye ofisa mwingine aliingia akatuangalia bila kutusemesha kitu kisha akaondoka zake.
Ndipo baadaye walipoingia watu wanne waliovalia Kaunda suti zao nzuri sana na walionesha dhahiri kuwa vyeo vyao ni vikubwa. Watatu walikaa kwenye viti na mmoja alibaki amesimama wima. “Nani kati yenu anayetaka kuongea na mkuu wa SRB?” aliuliza kijana aliyesimama kando ya hao walioketi vitini. “Ni mimi,” nilimjibu haraka.
“Sawa, mkuu wetu ni huyu nakaa katikati naitwa Kanali Farouk Minowa, kwa hiyo eleza yale nasema tamweleza,” alitamka kijana huyo aliyesimama ambaye alionesha dhahiri anafanya mazoezi ya judo au karate na weusi wake ulidhihirisha ni Mnubi. Nilimkazia macho huyo bosi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Idi Amin nikaamini yale niliyoambiwa kwamba Idi Amin amegawa madaraka mengi kwa watu wa kabila la Wanubi na Wakakwa ambalo ni kabila lake. Huyo Kanali Farouk alionesha wazi ni Mnubi. “Sikiliza bwana mkubwa,” nilianza kumwambia huku nikiwa nimesimama. “Mimi na hawa wenzangu tulikamatwa pale mpakani katika kijiji cha Kikagati wakati tunakunywa pombe katika Green Hotel nashangaa tunaambiwa sisi ni askari wa Jeshi la Tanzania, naomba bwana mkubwa uingilie kati jambo hili. Fanya uchunguzi ili tusiteswe bure.” Nilimwambia kwa upole.
“Nyamaza, kaa chini haraka,” aliamuru kijana aliyesimama. “Wewe ulisema nahitaji bosi yetu ili umueleze upumbavu wako? Unafikiri tunafanya mchezo? Hujui kwamba tunazo habari zenu zote zilizo sahihi?” alifoka kijana huyo huku akinisogelea.
“Nilichosema mimi ndicho ninachojua ni sahihi, sasa iwapo nyinyi mnajua zaidi kuliko tunavyojijua sisi wenyewe tupo radhi kuwasikiliza nyinyi.” Nilimjibu kwa upole bila kuogopa weusi wake kama mkaa na macho yake mekundu kama damu.
“Yaani wewe kijana nasumbua sisi, tumeacha shughuli zetu muhimu kuja sikiliza wewe kumbe huna lolote la kutuelesa sasa hii ndiyo takuwa mahakama yenu. Hatutaki Kiswahili yenu murefu ya kuzungukazunguka. Anza mashitaka kapteni.” Alifoka mtu aliyekaa kushoto kwa Farouk.
Kijana aliyesimama ambaye cheo chake kumbe ni kapteni alisogea hapo mezani na kuchukua jalada lililokuwapo.
“Luteni Njata, Sajini Binda na Koplo Sudi nyinyi ni askari wa Jeshi la Tanzania. Mnashitakiwa kwa kuvuka mpaka wa nchi yetu bila ya kibali, hilo ni kosa la kwanza na kosa lenu la pili ni kuingia Uganda na kufanya ujasusi. Je, mnalo la kujitetea kabla hamjahukumiwa?” alitamka kapteni huyo kijana.
“Tuanze na wewe kiongozi wao, Luteni Njata ebu tetea.” Aliongeza kapteni huyo. “Siwezi kujitetea kwa kosa ambalo sikulifanya. Iwapo nia yenu ni askari wa Tanzania, basi mmedanganywa, sisi siyo askari wa Jeshi la Tanzania,” nilijibu kwa ujasiri.
“O.k hamna cha kujitetea kwa hiyo mnahukumiwa adhabu ya sanamu ya kireno kwa siku tatu kisha mtaachiwa huru kwa mlango wa bustanini.” Alieleza kapteni huyo na kufunga jalada.
Kwa kweli ilikuwa ni kesi ya kuchekesha lakini ndivyo ilivyokuwa. Mwendesha mashitaka ni huyo huyo na hakimu ni huyo huyo. Baadaye wote wakaondoka, wakatuacha sisi hatujui la kufanya wala kuelewa maana ya “sanamu ya kireno’ na wala “mlango wa bustani.”
 
Sehemu ya sita


WIKI iliyopita tuliishia sehemu ambayo mimi na wenzangu tumekubaliana kuondoka kwa kuzingatia ruksa ya majasusi wa Shirila la Ujasusi la Idi Amin (State Research Bureua) baada ya kupewa hukumu ya adhabu ya sanamu la kireno. Tuliamuriwa kutoka nje ya jengo kupitia mlango wa bustanini ili kuondoka.
Nje kulikuwa na bustani nzuri iliyojaa miti midogo midogo na barabara zenye kokoto. Mbele yetu hatua kama 200 hivi iliegeshwa Landrover.
Koplo Sudi akawa na kiherehere, akatangulia kuifuata Landrover hiyo akifuatiwa na Sajini Binda. Mimi nilikuwa nyuma yao, lakini mawazo yangu yalihisi kuwa kulikuwa na hatari mbele yetu.
Sikuamini jinsi tulivyoachiwa kirahisi namna ile. Ni lazima kuna mbinu ya mwendo wa nyati aliyejeruhiwa, huenda tukiingia ndani ya Landrover hiyo italipuka au kulipuliwa.
Wakati akili yangu ikichemka kuwaza bila kupata majibu ghafla nikamwona Koplo Sudi ambaye alikuwa anajitayarisha kuingia ndani ya Landrover hiyo akianguka chini. Kabla sijamuangalia vizuri Koplo Sudi nikasikia Sajini Binda naye akitoa sauti ya kung’aka na kuanguka chini. Bila ya kuzubaa nikaruka na kujiviringisha kama gogo linalobiringika kutoka mlimani. Niliingia uvunguni mwa Landrover na kusikiliza. Wakati huo Koplo Sudi na Sajini Binda walikuwa wamelala kando huku damu zikiwavuja kwa wingi.
Utulivu waliounesha hapo chini na damu zilizokuwa zikiwatoka nilijua kuwa wameshakufa. Sasa milio ya bunduki na risasi kutoboa gari hilo zilisikika vizuri masikioni mwangu, lakini gari hilo halikulipuka. Hii ilidhihirisha kuwa landrover hiyo iliwekwa hapo kama chambo tu, haikuwa na petroli na labda hata haikuwa na injini.
Kilichonishangaza ni jinsi risasi hizo zilivyonikosa, sijui wapigaji hawakuwa na shabaha au ni Mungu tu.
“Huu ndio mlango wa bustanini, mlango wa mauaji unaotumiwa na wauaji wasioonekana wakiwa na bunduki zisizotoa mlio,” nilijisemea kama mwehu, kisha ghafla kama umeme nilitoka hapo uvunguni na kukimbia kwa kasi ya ajabu kwa mtindo wa zigizaga.
Risasi zilivuma karibu yangu na moja ikanipata begani lakini hiyo haikunifanya nipunguze kasi yangu. Nilikimbia mbio ambazo wengine wanaziita mbio za duma na swala.
Nilizunguka miti, maua na mara nyingine kujipindua kama tairi la gari linavyozunguka na hatimaye nikawa mita kama hamsini kutoka kwenye mlango mwingine wa kuingilia kwenye bustani hiyo ya mauaji. Niliacha kufuata barabara inayoelekea kwenye malngo huo ambako kulikuwa na kibanda cha walinzi, nikakimbilia upande wa kushoto bila kujua ninakoelekea.
Walinzi hao waliponiona nao walianza kunifyatulia risasi ambazo zilitoa sauti ya kutisha lakini Mungu alikwishasema hapana.
Maofisa Usalama wa Taifa wa Idi Amin nao hawakukubali kunikosa, walikuja nyuma yangu kwa kasi sana, lakini kwa vile nilishawaacha mbali hawakufanikiwa kunipata. Nilipofika kwenye seng’enge zenye miiba zenye urefu wa kama mita mbili hivi kwenda juu nikashtukia naruka kama vile karatasi kwenye upepo na kujikuta naangukia upande wa nje wa eneo hilo la wauaji. Bila kufanya ajizi nikainuka na kutimua mbio huku risasi zikiendelea lakini hazikunipata, nilikimbia mbele zaidi nikatokea kwenye barabara kubwa ya lami ambako nililiona lori moja lililobeba mifuko ya saruji likijikongoja, nikaongeza kasi ya mbio na kulirukia nyuma ambako nilijibwaga juu ya mifuko hiyo ya sementi huku nikitweta.
Nilipotazama nyuma sikuwaona maadui zangu kwa hiyo nikajua wameenda kufuata magari ili wanifuate. Tulipita eneo lililoandikwa Nakulabye na baadaye tukaelekea barabara inayoelekea eneo liitwalo Bombo, lakini tulipofika eneo la Namirembe, lori hilo lilianza kupunguza mwendo, nikahisi linakaribia kusimama. Niliruka haraka na kuanza kutembea kufuata barabara ya Balintuma hadi kwenye mzunguko wa barabara iliyooneshwa kwa kibao inaelekea Chuo Kikuu cha Makerere.
Ingawa baadhi ya watu walinishangaa na wengine walionesha nia ya kutaka kuniuliza kutokana na damu iliyokuwa ikinitoka, lakini mimi niliamua kuwapuuza nikaendelea mbele.
Wasiwasi wangu ulikuwa kukutana na polisi au askari yeyote, hata hivyo nilikuwa nawakwepa polisi na askari waliokuwa wamevaa sare kila nilipowaona.
Ghafla bila kutarajia nikaona bao kubwa mbele yangu limeandikwa “Namirembe Cathedral”. Nilihisi hapo ndipo mahali pekee ambapo naweza kuonewa huruma, kwa hiyo nikaangaza macho huku na huku kuthibitisha hakuna anayenifuata au kuniangalia kisha haraka nikaingia kwenye mlango wa uwa wa ukuta wa kanisa hilo ambamo ndani nilikuta kanisa liko wazi, kwa hiyo nikaingia.
Humo ndani ibada ilikuwa inaendelea na waumini wapatao kama hamsini hivi walishiriki ibada hiyo iliyokuwa ikiongozwa na padre mzungu.
Nikatafuta sehemu nzuri ya peke yangu nyuma nikakaa kusikiliza ibada hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kwa lugha ya Kiingereza.
Mwisho wa ibara watu wote walitoka nje lakini mimi nikabaki humo humo. Nilipiga goti nikainamisha kichwa na kuanza kububujikwa machozi kama bomba la maji lililopasuka. Nililia sana na hatimaye nikalia kwa sauti kubwa.
Kilio change hakikuwa cha kumwomba Mungu bali cha maumivu, njaa na uchovu ambao binadamu mwenye afya hafifu ni lazima angezimia. Baada ya kama nusu saa hivi nikasikia mtu akinisemesha na kunigusa kwa mkono kwenye bega langu la mkono wa kushoto kisha akaniinua kichwa.
“Pole sana kijana, umepatwa na nini?” aliniuliza mtu huyo kwa Kiingereza.
“Asante, asante, naomba unisaidie” nilimjibu padre huyo ambaye ndiye aliyeongoza misa muda mfupi uliopita kando yake walikuwapo masista wawili Waafrika ambao nilihisi walitaka kulifunga kanisa ndipo wakanisikia nalia.
“Umetokea wapi na umeumia na nini?” alizidi kunisaili padre huyo kwa Kiingereza.
“Nina hadithi ndefu sana ya kusikitisha lakini kwanza naomba msaada wa kusafisha jeraha langu na chakula cha aina yoyote,” nilijibu huku machozi yakiendelea kunitoka.
“Njoo huku,” aliniambia huku akiondoka. Nilimfuata hadi tukatoka nje ya kanisa na kuelekea kwenye jengo jingine la ghorofa moja ambalo nilihisi linatumika kama ofisi na nyumba ya kuishi mapadre. Alifungua mlango katika chumba kimoja ambacho niligundua ni ofisi tukaingia. “Kaa hapa unieleze yote kabla sijakusaidia,” aliniambia padre huyo tukiwa wawili tu ndani.
Nikaanza kumsimulia yote tangu tulipokamatwa kule Kikagati na askari wa Idi Amin, tulivyoteshwa hadi wenzangu wakapoteza maisha na jinsi nilivyofika hapo kanisani. Hata hivyo sikumweleza kuwa mimi ni askari wa Jeshi la Tanzania bali nilimwambia niliwahi kupitia mafunzo ya askari wa mgambo. Maelezo yangu yalimvutia sana padre huyo na kumuacha kinywa wazi.
“Pole sana, sasa hebu vua hilo shati lako.” Nikavua shati langu na kubaki kidari wazi. “Nitakusafisha kidonda na kukupaka dawa, baadaye nitakupa dawa na chakula lakini siwezi kukuweka hapa itakuwa ni hatari sana kwetu.
“ Idi Amin ni mtu katili sana pamoja na askari wake, kwa hiyo wakigundua upo hapa watatumaliza sote, wewe pamoja na sisi,” alinieleza kwa upole.
“Naomba msaada wako padre, mimi ni mkristo kama wewe nimekimbilia hapa nikijua ni mahali ambapo nitasaidiwa,” alinijibu na kumfanya atikise kichwa chake kuonyesha anaafiki.
“Nitakusaidia” jina lako ni nani? Nelson.
“Ooh Nelson jina zuri sana.” Alijibu huku akifungua kabati na kutoa pamba, dawa na mkasi. Pole pole akanisafisha majeraha na kisha akanitoa risasi moja mwilini.
 
Sehemu ya 7

KWA wiki kadhaa sasa tumekuwa tukiendelea na mfululizo wa simulizi kuhusu kachero wa Tanzania, pamoja na wenzake wawili walivyotekwa na makachero wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin. Tuliona namna kachero wa Tanzania alivyotoroka na kupata msaada katika moja ya makanisa jijini Kampala, Uganda. Leo tunaendelea na sehemu nyingine ya simulizi za kachero huyo, Frowin Kageuka, ambaye ameandika kitabu kuwaenzi wenzake hao wawili. Endelea
…………………….
BAADA ya padre yule kunifunga dawa katika jeraha la risasi akafungua boksi moja lenye nguo akanipa shati, suruali, fulana, jaketi na viatu ambayo ingawa vyote hivyo vilikuwa ni mitumba lakini ‘zilinikaa’ sana. Akafungua boksi jingine akanipa viatu vya michezo na kofia aina ya “cap” ya rangi nyeusi.
Nilizivaa nguo hizo ambazo kwa kweli nilizipenda sana na padre alinithibitishia kwamba ‘zimenichukua’ sana. “Sasa twende ukale,” aliniambia huku akitabasamu. “Asante sana, lakini padre unaitwa nani?” “Oh! Jina langu ni padre Franz au wengine huita Francis.”
“Ah! Vizuri sana, kwa jina hilo bila shaka wewe ni mswiss au sivyo?” “Kweli kabisa, umejuaje? Aliuliza huku akinikazia macho.
“Familia yangu ni wacha Mungu wa kikatoliki na mimi mwenyewe nimesomea shule za kikatoliki kwa hiyo majina ya mapadre wa kizungu siyo mageni kwangu.”
“Ohoo!” alijibu huku tukiingia sehemu ya chakula. Tulikaa hapo kisha padre Franz akamwagiza mhudumu mmoja mwafrika aliyevaa sare nyeupe aniletee chakula kingi na maziwa.
Awali nilifikiri kwamba chakula hicho kitakuwa ugali au wali, kumbe nikaletewa vipande vya mikate iliyotiwa siagi, nyama nyingi ya kukaanga, supu ya mboga na maziwa moto glasi moja ya nusu lita. Kwa kweli mlo huo ulikuwa mzuri sana kuliko ningepewa ugali au wali niliouzoea.
Kabla ya kula aliniambia nisalie chakula hicho, nikajua ananitega ili athibitishe kama kweli mimi ni mkristo au nimemdanganya. Kwa vile nimelelewa katika ukatoliki sala za kikatoliki hazikunipiga chenga, nikasali sala ile ile ya kikatoliki ya kubariki chakula na kumfanya padre huyo afurahi sana. “Wewe kweli ni mkatoliki,” aliniambia huku akitabasamu.
“Kumbe ulifikiri nakudanganya?” nilimuuliza huku nikianza kula. “Sikuamini sana maneno yako, lakini sasa nimeanza kuamini. Hilo tuliache, lakini utarudi vipi nchini kwako kwa sababu nimesikia kuna vita mpakani?” “Vita! Mpakani wapi?” niling’aka kama vile sijasikia.
“Nimesikia majeshi ya Idi Amin yamevuka mpaka na kuiteka Kagera. Hata hivyo siyo mkoa wote wa Kagera, bali mji wa Kakunga, Masanya, Mutukula, Minziro na Murongo ndiyo nimesikia imetekwa. Raia wengi wameuawa na mali zao kuteketezwa,” alinieleza kwa huzuni.
“Umesikia kwenye redio?” niliuliza ghafla. “Redio nimesikia, na watu wamenieleza pia, sasa swali langu ni jinsi wewe utakavyofika huko, kwa sababu siwezi kukuweka hapa ni hatari.”
“Loh! Umenistua sana, lakini naomba kitu kimoja, unipe japo fedha ili ziweze kunifikisha Tanzania kwa kupitia Kenya.” “Fedha? Fedha itabidi usubiri kwa siku tatu au nne hivi kwa sababu hivi sasa hatuna fedha za kutosha hapa.”
“Sasa kwa muda wote huo nitakaa wapi?” niliuliza kwa hofu. “Mimi naweza kukuficha kwenye gereji ya magari, lakini utakuwa hutoki nje na kula mpaka usiku, unaweza?” “Naweza sana” nilijibu kwa furaha baada ya kuhisi mafanikio ya kurudi nyumbani yapo.
Niliishi kwenye chumba kimoja cha hapo gereji ambacho ni stoo kwa wiki nzima bila kugundulika hata na wafanyakazi wa gereji hiyo. Usiku padre Franz alikuwa akinifungulia mlango na kunipeleka kula na kuoga kisha saa mbili usiku nashiriki naye ibada ya rozari (tasbihi) chumbani mwake hadi saa sita usiku ambapo hunifungia tena katika chumba hicho cha gereji. Kwa kweli sikupata taabu sana humo chumbani kwa vile nililala kwenye godoro dogo la inchi tatu na upana wa futi mbili na kujisaidia haja kwenye ndoo.
Kadiri siku zilivyopita ndivyo padre Franz alivyonipenda na hasa kwa jinsi tulivyoshirikiana katika sala ya rozari. Baada ya kama wiki mbili hivi, usiku mmoja padre Franz alinipa habari ya kunishtua sana. Hatukusali siku hiyo kwa vile mazungumzo yetu yalichukua muda mrefu na kwa kweli yalimtia hofu padre huyo.
“Leo hatusali rozari Nelson.” Aliniambia kwa hofu kiasi cha kunifanya na mie niingiwe na wasiwasi. “Kumetokea nini padre?” nilimuuliza kwa shauku. “Maafisa wa usalama wa taifa wa Idi Amin walifika hapa kuuliza habari zako,” alinieleza kisha akanikazia macho. “Maafisa wa SRB?” enhee!”
Mimi niliwaambia kweli ulifika hapa lakini sikukubali kukupokea, kwa hiyo uliondoka zako, wakaridhika na majibu hayo wakaondoka. Lakini nahisi wanaweza kurudi tena hapa kwa hiyo ni lazima kesho asubuhi uondoke. Nitakupa nguo, pesa, dawa na chakula cha makopo kwa cha siku mbili kisha uondoke zako.
Hata hivyo nimesikia kwenye redio kuwa majeshi ya Tanzania yamewatimua askari wa Idi Amin pale Bukoba na sasa wamevuka mpaka wamo ndani ya Uganda. Umenielewa?
“Nimekuelewa sana, kama hali ndiyo hiyo naomba hivyo vitu utakavyonipa nipe pamoja na silaha yoyote ambayo utaona inaweza kunisaidia kujilinda.”
“Hebu subiri kidogo,” aliniambia kisha akatoka. Dakika kama ishiriki hivi alirudi akiwa na begi dogo. “Humu mna jaketi, suruali mbili, shati mbili, kandambili, fulana, makopo sita ya nyama, makopo mawili ya samaki, siagi na mikate na mswaki, silaha niliyokuwekea ya kukusaidia wakati wa shida au matatizo ni biblia, sawa?”
“Sawa padre nashukuru,” nilijibu huku nikitabasamu. “Shika na hizi shilingi laki tatu na dola mia tatu zikusaidie.” Hizi shilingi laki tatu ni sawa na shilingi thelathini elfu kule kwenu Tanzania. Sasa piga magoti nikuombee ili ukalale, kisha kesho asubuhi na mapema uondoke zako. Umenielewa?”
“Nimekuelewa padre lakini naomba labda unitajie mtu au watu unaofikiri wanapinga utawala wa Idi Amin ili kama nikishindwa kuondoka nikimbilie kwao,” nilimwambia huku nikipiga magoti.
Akaniombea dua njema kwa dakika kama tatu hivi kisha akanibariki. “Ukianza kutafuta wapinzani wa Idi Amin utakuwa unajitafutia balaa. Hata hivyo mimi siwajui kwa sababu hata kama wapo hiyo itakuwa siri yao mioyoni mwao. Wengi waliojitokeza kufanya upinzani wa waziwazi wameishia kufia mikononi mwa maofisa wa SRB,” alinieleza huku akinishika kichwa.
“Haya asante padre, kwa heri, nikifika nyumbani Tanzania nitakuandikia barua kwa hiyo naomba anuani yako ya Posta na namba ya simu.” Aliniandikia anuani yake na namba za simu baadaye alinisindikiza chumbani kwangu na kunifungulia.
“Kesho asubuhi kufuli hii ukitoka utaifunga mlangoni,” aliniambia na kuondoka zake.
Kwa kweli usiku huo sikulala, mawazo ya vita yalinijaa, nikaona siwezi kukimbilia kurudi Tanzania kupitia Kenya na mimi ni askari, tena kachero. “Ni lazima nifanye kazi yangu, kazi ya ukachero. Lakini nani atanisaidia na fedha zangu ni kidogo? Itabidi nitafute kazi ili nipate fedha za kuniwezesha kuishi hapa Kampala. Lazima niwapate wapinzani wa Idi Amin ili wanipe habari za Jeshi la Idi Amin na vile vile nitafute mawasiliano ya kuniwezesha kuwasiliana na makao makuu ya Jeshi nyumbani. Loh! Nina kazi kubwa lakini lazima niifanye, kwanza labda ningelazimika kuifanya tangu pale mpakani mkoani Kagera. Nikifa basi, nitakuwa nimekufa nikiwa kazini lakini ole wangu nani atajua kwamba nipo hai? Hapana, lazima nirudi nyumbani nikaonane na familia yangu,” niliwaza mpaka karibu
 
Him ndani nw days waandishi wa riwaya no wengi.. Umejitahidi Ila mpangilio wako haupo vzr, pangilia plz...
Hiki ni kitabu kinachoelezea tukio la kweli. Kimeandikwa na komandoo wa JWTZ aliyetekwa mpakani akiwa wenzake wa wawili waliouawa na yeye akatoroka. Huyu mwanzisha thread amekopi tu kutoka gazeti la raia mwema.
 
Hii stori mimi ningeipenda kama ingekuwa inanadiwa kama stori ya kutunga badala ya kuwa kama ilivyojengewa mazingira ya kuifanya kuonekana kama ni true story.
 
"...Mlango ulifunguliwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aina ya AK 47 kila mmoja wakatuzunguka. Moyo ulinilipuka, mate yakanikauka. "Simama juu". Alituamuru askari mmoja aliyekuwa na cheo cha Sajini. Tulitolewa nje ambako tulikuta askari wengine wanane waliovalia kivita wakiwa na bunduki mikononi. Raia wa kijiji hiko walisimama kwa mbali sana wakishuhudia tunavyokuwa mateka mpakani. Tuliingizwa katika lori moja la kijeshi na safari ya kupelekwa kusikojulikana ikaanza. Baada ya mwendo wa kama kilomita nne hivi, tukaingia katika kambi ndogo ya jeshi inayoitwa Kabiyanda. Tuliteremshwa kwenye gari na kuingizwa katika kijumba cha mabati matupu ambapo ndani kulikuwa na joto kali pamoja na hewa nzito kutokana na kutokuwa na dirisha bali vitundu vidogo vipatavyo sita.
Luteni awakabidhi kwa Koplo awafunze adabu.
"Saa tisa tulitolewa humo kwenye kijumba na kukalishwa chini kwenye uwanja niliohisi ni wa kufanyia kwata. "Nani mkubwa kati yenu?" alituuliza Luteni mmoja mweusi mwenye sura mbaya. Hakuna aliyemjibu hivyo akatuona tumemdharau, akaamua kumwita Koplo mmoja aliyekuwa amesimama kwa mbali. "Funsa adabu hawa" alimwamuru koplo huyo kwa Kiswahili kibaya kisha akaondoka zake kwa hasira. "Ah! Mnataka 'kufunswa' heshima, hebu simameni". Tuliinuka kwa hofu huku tukimwangalia anachotaka kutufanya. "Nyinyi ni askari?", "Hakuna askari kati yetu" nilimjibu kwa hasira. "Eh! Wewe ndiyo mkubwa eenh!" ,"Mkubwa wa nini?" nilimjibu na kumfanya acheke.
"O.K nyinyi mnajua Kiswahili kingi sana, hebu chuchumaeni chini huku mkishika masikio yenu". "Tuoneshe mfano", nilimwambia bila hofu.
"Eh! Nyinyi jeuri sana, hebu laleni chini niwachape fimbo" alituambia huku akitabasamu. Wakati tunalala ghafla alikuja askari asiyekuwa na cheo na kumwambia mwenzake tunatakiwa tupakiwe ndani ya gari na kupelekwa kambi ya Mbarara".
Waswekwa mahabusu na kuhojiwa na maofisa wa jeshi la Uganda.
"Tulifikishwa kambi ya Mbarara giza likiwa limeshaingia, dereva akasimamisha gari nje ya lango la kambi kubwa ya jeshi ambayo baadae niliitambua inaitwa Simba Battalion. Taa kubwa ya usalama ikawashwa na kuzimwa kama ilivyo katika kambi nyingi za jeshi kisha sauti kali ilitaka utambulisho.
"Tumeleta mateka kutoka Kabale" alijibu askari mmoja aliyekaa mbele. Gari iliingia na kuegeshwa nje ya jengo dogo ambalo hata asiyekuwa askari angegundua ni mahabusu.
Tulitelemshwa kwenye gari na kuingizwa mahabusu. Asubuhi ilipofika tulitolewa nje na kupelekwa katika ukumbi mmoja mdogo na kukalishwa chini. Dakika chache baadae waliingia wanajeshi wanne, watatu wakiwa na cheo cha meja huku mmoja alikuwa kanali.
"O.K Watanzania, tunaanza na wewe, inuka ujibu maswali yetu". Alitamka kanali huyo huku akimuonesha kidole koplo Sudi.
Koplo Sudi aangua kilio baada ya kuzidiwa na maswali ya Kanali wa kiganda.
"'Una kitambulisho chochote hapo ulipo?" aliuliza meja mmoja ambaye ni mrefu zaidi ya wenzake. "Sina kitambulisho". "Sawa, vua shati na suruali yako," aliamuru Kanali huyo. Koplo Sudi akavua suruali na shati na kuviweka mbele yake. "Wewe unafanya kazi gani pale Murongo?" aliuliza meja mwingine aliyekuwa akinukuu maelezo yetu. "Nafanya biashara ya kuuza vitabu sokoni", alijibu Koplo Sudi huku akigwaya. "Unajua sisi tunawafahamu nyinyi vizuri sana, nakuonya usiseme tena uwongo" alifoka kanali. "Jina lako nani?" aliuliza Kanali. "Abdallah Salum" alidanganya Koplo Sudi.
"Hatuna jina la Abdallah katika orodha tuliyopewa, nyinyi wote ni wanajeshi lakini wewe unajifanya mfanyabiashara. Hatupo hapa kufanya mchezo," alifoka Kanali.
"Umeelewa, sasa yajibu maswali yetu kwa ukweli. Jina lako nani na unafanya kazi gani pale Murongo?" aliuliza meja huyo.
Swali hilo lilimfanya Koplo Sudi aanze kutoa machozi.
"Unalia kabla hujateswa, sasa ukiteswa si utakufa kabisa" alitamba meja. Maneno haya hayakupunguza kasi ya machozi ya Koplo Sudi, kwahiyo Kanali akamwambia arudi akae chini".
Nukuu ya jasusi wa Tanzania aliyetekwa nyara na wanajeshi wa Uganda mara baada ya kuvuka mpaka na kuingia Uganda akiwa sambamba na askari polisi wawili; Sajini Binda na Koplo Sudi.
Simulizi kama hizi ni nzuri sana na zina jenga uzalendo.
 
Mpaka hapa naona nyota nyota.mwenye uzi ni kama kapigwa butwaa.hata kama kuna mtu mwingine anajua zaidi lakini naona ni vyema ukachuna umuache mwenye uzi wake asonge mbele na wewe uanzishe wa kwako,any way ngoja nirudi zangu ''Geranimo''
 
Mpaka hapa naona nyota nyota.mwenye uzi ni kama kapigwa butwaa.hata kama kuna mtu mwingine anajua zaidi lakini naona ni vyema ukachuna umuache mwenye uzi wake asonge mbele na wewe uanzishe wa kwako,any way ngoja nirudi zangu ''Geranimo''
Inabidi mnunue kitabu maana huko mbele sheria ya haki miliki inanibana.
Imenibana niishie hapo la sivyo kaka ako nitapelekwa keko nikakutane na Scopion
 
Inabidi mnunue kitabu maana huko mbele sheria ya haki miliki inanibana.
Imenibana niishie hapo la sivyo kaka ako nitapelekwa keko nikakutane na Scopion
Pole jamaa! ungekua hapa Mwanza ungekuja nikupe ofa ya samaki wa kuchoma hapa Vila Park ujipoze
 
Back
Top Bottom