Jaribio lolote la kukidhibiti Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ni anguko la haki nchini

radika

JF-Expert Member
Jul 15, 2014
20,427
32,196
[HASHTAG]#Mtatiro[/HASHTAG] J

Kanuni ya msingi inayotumika nchi zote za kidemokrasia duniani, imejenga msingi mkuu kwamba, Vyama vyote vya mawakili ni taasisi huru, zinazojitegemea na zisizofungamana na serikali au mahakama.

Vyama hivyo havijawahi kuwa chini ya Ofisi ya Jaji Mkuu au Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vyama hivi vya mawakili hudhibitiwa na kuongozwa na wanachama wake, huwa havipokei bajeti wala ruzuku kutoka serikalini au mahakamani na haviitegemei serikali kujiendesha.

Mnafahamu kuwa majaji wanapewa kinga ili serikali isiwadhibiti au kuwachezea. Majaji wanafanya kazi ya kulinda haki baina ya pande zinazoisaka na kumpa anayestahili. Ikiwa majaji hawatakuwa na kinga, serikali, watu wenye mamlaka, umaarufu, pesa n.k. wataichezea mahakama, majaji na haki haitamfikia mhusika.

Msingi wa kidunia wa kuvifanya vyama vya mawakili viwe taasisi huru zisizofungamana na serikali wala kuwa chini ya serikali au mahakama ni huo huo unaotokana na uhuru na kinga ya majaji.

Kama ambavyo mahakama si sehemu ya serikali au siyo tawi la serikali kwa sababu za kiuhuru, na ndivyo Chama cha mawakili kisivyoweza kuwa chini ya Jaji Mkuu au Mwanasheria Mkuu wa Serikali au mahakama - achilia mbali serikali.

Uhusiano wa Jaji Mkuu na mawakili ni mmoja tu - mawakili wanaapishwa na Jaji Mkuu ili pamoja na mambo mengine, waweze kutumikia jamii kwenye utafutaji wa haki katika Mahakama ambazo ziko chini ya Jaji Mkuu.

Kwa hiyo, Mawakili na Jaji Mkuu wanakutanishwa na mahakama na uhusiano wao ni wa kimahakama, Jaji Mkuu akiwa Mkuu wa Mahakama - Mawakili wakiwa maafisa wa mahakama (siyo watumishi).

Uhusiano wa Jaji Mkuu na Mawakili umejengwa na unalindwa na Sheria na Kanuni mbalimbali ambazo zinawekwa kwa mujibu wa sheria. Ndiyo maana kwenye uhusiano huo, Jaji Mkuu hana mamlaka ya kuwaamrisha mawakili wafanye jambo lolote isipokuwa Jaji Mkuu na mawakili wanatenda kwa pamoja yale yaliyomo kwenye katiba, sheria, kanuni na tamaduni za kimahakama.

Faida ya kuwa na Chama cha Mawakili kisichofanya kazi kwa kudhibitiwa moja kwa moja na Jaji Mkuu au Serikali ni sababu zile zile ambazo zinazifanya katiba zote duniani kukataa kabisa mahakama kuwa sehemu ya serikali, au Jaji Mkuu kudhibitiwa na Rais, au Bunge kuwa tawi la serikali n.k.

Ili dhana ya utendaji haki itokee na ionekane inatokea, ni lazima kuwepo na Chama huru cha mawakili, maana ni hawa mawakili ndiyo wanaweza kusaidia kuwepo kwa utawala wa sheria katika nchi hasa inapotokea serikali inakiuka misingi ya utawala huo.

Jaribio lolote la kukiweka chama cha mawakili chini ya SERIKALI, KWA AMRI YA RAIS (kwa kumlazimisha Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali) wakidhibiti (actually, kwa maslahi ya serikali) si tu kwamba ni mwanzo wa kuvuruga kabisa taaluma ya sheria hapa nchini, bali pia ni chanzo cha kuua misingi ya utendaji haki na ulinzi wa utawala wa sheria. Jambo hilo likitokea, waathirika wakubwa ni wananchi.

Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye anataka TLS idhibitiwe, AMA mtu huyo hajui kazi ya vyama kama TLS duniani, au anataka kuvuruga misingi yote ya haki kwenye nchi yetu.

Mtu huyo aonywe kwa nguvu zote, akemewe na kutolewa mapepo yote, adhibitiwe, asaidiwe, ausiwe, ashauriwe, akanywe, asimamiwe, aambiwe, apigiwe kelele, azodolewe na atizamwe kwa jicho kali kabisa.

[HASHTAG]#Mtatiro[/HASHTAG] J
#22/04/2018.
 
Back
Top Bottom