Jando, unyago kiini cha mimba shuleni Newala

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,317
33,114
Salim Said

KUNA utani uliozoeleka katika jamii kwamba mabinti wa Kimakonde hawajui kusema ‘hapana’ pale wanapoifuatwa fuatwa na wanaume kimapenzi. "Kunkatalia ntu dhaambi!" inadaiwa hujisikia fahari kusema.

Huo unaweza kuwa utani tu, lakini unapotazama takwimu za kitaifa za wanafunzi wa kike kuacha masomo kutokana na mimba kuna kila sababu ya kuamini usemi huo. Kanda ya mikoa ya kusini ndiyo inaongoza kwa utoro wa watoto wa kike na sababu kuu ni ujauzito.

Wilaya ya Newala mkoani Mtwara ni moja ya maeneo ya kanda hiyo, yanayokabiliwa na tatizo hilo kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi au hata taasisi binafsi, mikoa ya Mtwara na Lindi haijapata dawa ya kuzuia tatizo hilo.

Tatizo hilo haliwasumbui watoto au wazazi pekee bali hata Mkuu wa Wilaya ya Newala Dk Rehema Nchimbi ambaye anasema moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu wilayani kwake, ni ujauzito kwa wanafunzi.

Dk Nchimbi anaona kuwa, tatizo hilo linasababishwa kwa kiwango kikubwa na uendelezaji wa mila na desturi za watu wa Newala ambao asilimia 99 ni watu wa kabila la Wamakonde.

“Unajua, kwa mujibu wa mila na desturi za Wamakonde ni lazima msichana na mvulana apitie jando na unyago. Hapa hakuna tajiri wala masikini, wote lazima wapitie katika hatua hiyo ambayo kwa Wamakonde ni hatua muhimu katika makuzi yao,” anasema Dk Nchimbi.

"Kwa Newala hatuna kesi nyingi za unyanyasaji wa watoto au walemavu hata wale wenye ulemavu wa ngozi yaani albino, hii ni kwa sababu sisi hatuna biashara kubwa kama za madini au mashamba makubwa ya chai. Unaweza kuwakuta watoto wanaokota korosho lakini wanakuwa kama wanawasaidia wazazi wao muda usiokuwa wa shule".

Ingawa ratiba za jando na unyago haziingiliani na ratiba za masomo kwa sababu hufanywa wakati wa likizo au kabla ya mtoto kuanza shule ya msingi, zinaathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu kwa sababu inampa msichana kiburi na uelewa wa mambo ambayo hakupaswa kuyaelewa kwa umri wake.

“Kutokana na mila na desturi hizi msichana anakuwa na kiburi na sauti kubwa zaidi kuliko hata mvulana baada ya kuchezwa. Hujiona tayari amekuwa mkubwa, yuko huru, anajua mambo mengi zaidi na hataki tena kufuatiliwa fuatiliwa sana hata na wazazi wake,” anasema Dk Nchimbi.

"Sasa kutokana na hali hii ndiyo maana utakuta kesi za mimba kwa wasichana ambao wengine ni wadogo ni nyingi wilayani hapa.

Halmashauri kwa upande wake hujitahidi na kuwafikisha mahakamani wahusika, lakini tatizo ni kwamba wasichana wenyewe hawako tayari kuwataja waliowapa mimba hata kama utawapeleka polisi au mahakamani".

Ugumu huo unatokana na aibu na uhalisia wa wasichana kuona aibu kuzungumzia mambo yanayowahusu na yanayohusu farahga zao.

Katibu wa Mtandao wa taasisi zisizo za kiserikali Newala (New-Ngonet) na Mratibu wa mradi wa jali watoto, Halima Nambunga anasema: "Tatizo la mimba za utotoni ni kubwa sana hapa Newala."

Anatoa mfano, "Katika mradi wetu huu, tumechukuwa watoto 1200 wanaoishi katika mazingira hatarishi kutoka katika kata saba. Watoto hawa huwa tunawasomesha hadi kidato cha nne au sita, lakini tayari baada ya kuwafanyia vipimo tumegundua mimba 30, halafu wenyewe ni wadogo."

“Kwa mazingira ya Newala mtoto anapopata ujauzito mara nyingi ndio unakuwa mwisho wa nuru na taa yake katika kutafuta elimu, labda wale wanaotoka katika familia zinazojiweza, ambao wanaweza kupelekwa katika shule binafsi au katika vyuo vya ufundi,” anasema Nambunga huku akiwatupia lawama watendaji wa halmashauri na walimu kwa kile alichodai uwajibikaji mdogo.

Baadhi ya wasichana wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya kata ya Dk. Alex wanathibitisha kuwa, tabia ya wazazi kuwacheza mapema wasichana wao ni kichocheo kikubwa cha wasichana wengi kupata ujauzito wakiwa shuleni.

Wanadai mara nyingi mporomoko wa maadili ya wasichana huanza baada ya kumaliza suala la kuchezwa kutokana na mafunzo mbalimbali wanayoyapata huko. Mwanahamisi Shaibu wa shule hiyo anasema, wasichana wengi hubadilika kitabia baada ya kutoka unyago, jambo ambalo huwaweka katika mitego ya kushawishika na hatimaye kupata ujauzito.

"Hivi sasa wasichana wanachezwa kabla kuanza darasa la kwanza, yaani kuanzia miaka minne hadi saba. Tatizo ni kwamba msichana anapochezwa katika umri huu huwa hakumbuki yale mafunzo ya msingi anapofikia ukubwani bali hukumbuka yale ya matusitusi,"anasema.

"Na mara nyingi huyakumbuka kwa sababu tu anataka kujaribu kuyafanyia kazi kwa vitendo na madhara yake ni kupata ujauzito. Mimi mwenyewe nilienda unyago nikiwa na umri wa miaka minne hivi sasa nina miaka 16, sikumbuki yale yote ya maana ambayo nilifundishwa ninayokumbuka ni matusi matupu," anaeleza Mwanahamisi.

Wanafunzi wapatao 38 wa kidato cha tatu katika shule hiyo ya Dk Alex wanathibitisha darasani kwamba, tangu waanze kidato cha kwanza mwaka 2007 tayari wasichana wanane wameshaacha shule kwa kupata ujauzito ndani ya darasa moja tu.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Majengo Newala, Shakira Ahmad anathibitisha kuwa, suala la kuchezwa kwa wasichana linachangia kwa kiasi kikubwa mabinti kupata ujauzito wakiwa hawajamaliza hata kidato cha nne, kwa sababu wanayofundishwa kule ni mambo ya matusitsi.

"Mimi naona kama tunataka kweli kupunguza mimba za utotoni lazima turudie taratibu zetu za zamani, badala ya kumcheza mtoto akiwa na miaka minne tumcheze baada ya miaka 18 au kumaliza kidato cha sita," anashauri Shakira.

Lakini hilo linawezekana? Hili ni swali muhimu la kujiuliza kwa sababu Shakira anasema hivi sasa baadhi ya wasichana huwatenga wenzao baada ya kuwagundua hawajachezwa na baadhi ya wakati hukataa hata kucheza nao.

"Ukisikia 'Mnemba' huyo ni msichana ambaye hajachezwa au 'Nahako' mvulana ambaye hajapelekwa jando na baadhi ya wakati mvulana ambaye hajaenda jando huitwa ‘Firimbi," anasema Shakira.

"Sasa kutokana na hali hii msichana au mvulana hujiona dhaifu, mnyonge, asiye na thamani katika jamii na baadhi ya wakati hata kutoka kwenda kucheza hatoki, bali huishia kujifungia ndani tu na kuwalazimisha wazazi wake wamfanyie jando kama ni mvulana au unyago kama ni msichana".

Afisa Elimu wa Sekondari Newala, Julius Nestroy anasema tatizo la kukithiri kwa mimba za utotoni wilayani hapo kunasababishwa na utamaduni wa kulindana baina ya wanajamii pamoja kukithiri kwa rushwa.

"Ukichunguza sana utakuta kesi nyingi za ujauzito zinaishia kwa watendaji wa kata au vijiji. Hii ni kutokana na kulindana kwa sababu unaweza kupanga mnaenda kumkamata mhusika, wenzako huko wanafanya mipango ya kumtorosha," anasema.

"Lakini lengo langu ni kufufua kesi zote za ujauzito ambazo zimekwama kwa watendaji wa kata au vijiji ili angalau tupunguze kero hii"

http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=15451
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom