Jamhuri yawasilisha mapingazi manne katika kesi ya kupinga Wagombea kutangazwa washindi kwa kupita bila kupingwa

Influenza

JF-Expert Member
Jul 1, 2018
1,445
3,403
Kesi iliyofunguliwa kupinga wagombea wanaopitishwa bila kupingwa kutangazwa washindi imeshindwa kuendelea baada ya Serikali ya Tanzania kuweka mapingamizi manne.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 20/2019 ilifunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Dar es Salaam na Wakili Gaston Garubindi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Katika kesi hiyo ambayo imetajwa leo Jumanne Septemba 24, 2019 mahakamani hapo ili kuona kama pande zote zimeshakamilisha taratibu ambapo Septemba 16, 2019 Serikali iliwasilisha majibu ya mleta maombi ikiambatanisha taarifa ya mapingamizi kuhusiana na shauri hilo.

Baadhi ya mapingamizi hayo ya upande wa mjibu maombi umeeleza hati ya kiapo iliyoambatanishwa na maombi inakiuka sheria ya mwenendo wa madai (CPC).

Katika pingamizi lingine lililowasilishwa na wajibu maombi wamedai mleta maombi hana uhalali wa kuleta maombi hayo. Pia wamedai kiapo kilichoambatanishwa na maombi hayo kina upungufu wa kisheria.

Mapingamizi hayo yamepangwa kusikilizwa mahakamani hapo Oktoba Mosi, 2019 mbele ya Jaji Benhajj Masoud.

Katika maombi hayo, wakili huyo anaiomba Mahakama ifute kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na kifungu cha 45(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura 292.

Anadai vifungu hivyo ambavyo huruhusu mgombea asiyekuwa na mpinzani kutangazwa mshindi wa nafasi husika bila hata kupigiwa kura ni batili na vinakiuka Katiba ya Tanzania.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Kiongozi Eliezer Feleshi imeahirishwa hadi Oktoba 1, 2019.
 
Back
Top Bottom