Jambazi laua polisi, lajeruhi kachero mkuu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Andengenye(7).jpg

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye



Wakazi wa kijiji cha Nambala na eneo la Shangarai, wilayani Arumeru, mkoani Arusha, jana walikumbana na hali ya ngumu huku wakijikuta hawatoki ndani kwa kuogopa Polisi, waliokuwa wakiendesha msako mkali, baada ya mtuhumiwa wa ujambazi kumua askari polisi.

Mtuhumiwa huyo, Pokea Herry Samson, anatuhumuiwa kumuua askari polisi mwenye namba F. 2218 Konstebo Kijanda Mwandu kwa kumpiga risasi sehemu ya shingoni.

Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi usiku katika eneo la Shangarai, kwenye nyumba ya mkazi mmoja (jina tunalihifadhi) ambaye anadaiwa kugeuza nyumba yake kuwa kichaka cha kuhifadhi majambazi mkoani Arusha.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema kuwa siku ya tukio Polisi walipata

taarifa kuwa nyumba ya mkazi huyo iliyopo katika barabara ya Peace Point, Shangarai, inahifadhi majambazi na ndipo walipojipanga na kwenda katika nyumba hiyo.

“Askari hawa walipofika katika nyumba hiyo, jambazi hilo likawahi kuwaona na kuanza kurusha risasi ovyo hewani na kwa bahati mbaya ikampata Konstebo Kijanda na kufariki dunia hapo hapo na nyingine ilimpata Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha (OC-CID), Faustine Mafwele, kwenye bega la kushoto, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Lutheran Selian kwa matibabu,” alisema Kamanda Andengenye.

RISASI 48 ZAPATIKANA

Andengenye alisema kuwa baada ya tukio hilo, jambazi hilo lilifanikiwa kutoroka na mmiliki wa nyumba na ilipofika asubuhi, Polisi waliingia katika nyumba hiyo na kuendesha msako, walifanikiwa kupata risasi 36 za SMG, risasi 12 za Shortgun, kitako kimoja cha Shortgun, mtutu mmoja, mtambo mmoja wa bunduki ya shortgun na soksi jozi mbili za kuvaa usoni rangi nyeusi.

“Lakini hatukuishia hapo tu, tuliwakamata watoto wawili ambao wana umri wa miaka tisa na 13, wakazi wa Nambala, lengo letu ni kuwahoji kuhusiana na tukio hili na kwa sababu mmoja wa watoto hawa ndiye alimfungulia mlango jambazi na kutoka nje kufanya mashambulizi dhidi ya Polisi,” alisema Andengenye.

Alisema baada ya kuwamata watoto hao, Polisi waliendelea na msako katika kijiji cha Nambala baada ya kubaini kuwepo kwa ushirikiano wa uhalifu kati ya Shangarai na Nambala.
Alifafanua kuwa katika msako huo, walifanikiwa kukamata bunduki aina ya SMG kwenye nyumba ya mkazi mmoja, ambayo ilikuwa

imetupwa chooni.Alisema bunduki hiyo ilikuwa na risasi 12 na wanahofia kuwa bunduki hiyo ilitumiwa na majambazi hayo yaliyoua askari Polisi.Andengenye alisema kuwa hadi sasa wanawashikilia watu watatu kwa ajili ya uchunguzi.
Kuhusu madai ya wakazi wa maeneo ya tukio kuwa jambazi hilo baada ya kumua askari polisi lilimpora bunduki, Kamanda Andengenye alikanusha habari hizo akisema haiwezekani kwa sababu walikuwepo askari wengi.

BINGO YA SH. MILIONI TANO YATANGAZWA

Alisema jeshi lake limetangaza donge nono kwa mtu yoyote atakayefanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na atapatiwa Sh milioni tano.
“Mtu huyu akiachiwa kuendelea kuzagaa mitaani ni hatari kwa watu, hivyo jitihada zaidi zinatakiwa kufanikisha kumtia mbaroni

haraka iwezekanavyo,” aslisema na kuongeza: “Lakini pia jambazi hili lilikuwa na kesi mahakamani ila hatuna uhakika kama alihukumia na kama ndivyo alitokaje gerezani, tunafuatilia kufahamu hili.”
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru, ukisubiri taratibu za mazishi na Polisi wanaendelea na msako mkali kuwasaka waliotoroka katika tukio hilo.

MASHUHUDA WASIMULIA

Wakazi wa eneo la Shangarai ambao walishuhudia, John Pascal, Anna Palangyo na Hamisi Juma, walisema kuwa tukio hilo lilianza saa sita usiku wa kuamkia jana na walishtuka wakiwa usingizini waliposikia milio mikubwa ya risasi.

Walisema kuwa risasi hizo hawajawahi kusikia maishani mwao kwa sababu zilikuwa zinamiminywa nyingi hivyo iliwalazimu kujibana kwenye nyumba zao bila kutoka nje, japo baadhi yao walikuwa wakichungulia madirishani kuona kinachoendelea.

“Lakini tulishuhudia kuona askari wawili wakipigwa risasi mmoja alianguka chini na mwingine akikimbia huku akiwa ameumizwa, baada ya hapo tukaona jambazi anachukua bunduki ya askari aliyeuawa na kuondoka nayo,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Walisema hali ilikuwa tete kwao na wakazi wengine kwani jana walilazimika kujifungia ndani na kuogopa kuwatoa vijana wao nje akuhofia kukamatwa kwa sababu askari walikuwa na hasira na walikuwa wakiendesha msako karibu kila nyumba kwenye eneo hilo.

WANNE MBARONI KIGOMA KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI

Jeshi la polisi mkoani Kigoma linawashikilia watu wanne, Shaban Mrisho 30, Masudi Jafari 32, Joseph Ramadhani 24 na Shija Masulu24 kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 31, mwaka 2011 majira ya 11 huko Ilangulu katika kata ya Mtego wa Noti, Tarafa ya Nguruka.

Kashai alisema polisi wakiwa katika msako endelevu wa uhalifu waliwakamata watu wanne wakiwa na bunduki aina ya Shortgun aina ya Greener na risasi 14, baskeli mbili na fedha taslimu Sh. 89,100 zilizoporwa kwa unyanganyi wa kutumia silaha katika Kijiji cha Mlyabibi.
Alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa walihusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lilitokea katika Kijiji cha Mlyabibi.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao wanatarajia kufikishwa mahakamani upelelezi utakapo kamilika.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom