Jakaya Kikwete atahadharisha wanaokwamisha Serikali

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,302
5,441
msg-1395784623-19432.jpg

Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, ametahadharisha ya watu wanaokwamisha uwepo wa baadhi juhudi za Serikali katika taasisi nyeti za umma zinazohusika na masuala ya biashara na uwekezaji.

Dk. Kikwete amesema ufanyaji kazi kwa mazoea, udokozi, ufinyu wa utafiti, ubora hafifu wa bidhaa ni masuala yanayopaswa kuepukwa ili kufikia malengo ya nchi katika sekta ya uwekezaji na biashara.

Akizungumza Oktoba 6, 2022, Kibaha Mkoani Pwani wakati akifungua maonesho ya tatu ya Wiki ya Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Pwani, alisema taasisi nyingi za Serikali zinafanya kazi nzuri kuwahudumia wananchi, lakini wapo baadhi ya watumishi wanashindwa kuendana na kasi iliyopo.

"Nakumbuka Mzee Mengi enzi za uhai wake nilimtembelea ofisini kwake nikakuta wahasibu ameajiri wahindi, nikamuuliza vipi? Akasema wazawa wananiibia. Tuache udokozi kazini, tuache kufanya kazi kwa mazoea. Tubadilike kama kweli tunataka kufanya vizuri katika eneo hili la uwekezaji," alieleza.

Alisema katika eneo la ubora wa bidhaa zinazozalishwa Nchini, Tanzania ni miongoni mwa nchi 7 wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo zimesaini makubaliano ya biashara huria, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza ubora wa bidhaa ziweze kushindana sokoni.

"Hatua tuliyofikia tupo katika ushindani, lazima tuzalishe bidhaa zetu kuwa bora, nchi yetu imesaini mkataba wa eneo linalojulikana kama "Africa Continental Free Trade Area" hakikisheni bidhaa zinazozalishwa ni bora, vinginevyo itakula kwetu, hatutafanikiwa na mwishowe tutailaumu Serikali," alisema.

Rais huyo mstaafu pia alisema Mkoa wa Pwani umejinasibu kuwepo fursa lukuki za uwekezaji lakini ni muhimu uongozi wa mkoa huo ukaboresha mazingira ya uwekezaji kwa kusimamia maeneo yanayotengwa kwa ajili ya uwekezaji.

"Dar es Salaam imejaa, sasa ni wakati wetu Mkoa wa Pwani, ndio ukweli wa historia anayetaka aje kuwekeza, atakayetaka kuwekeza Dar es Salaam labda ajenge kwenye maghorofa," alisema Dk. Kikwete.

Aliwashauri kusimamia maeneo wanayojenga viwanda kwa sababu vipo viwanda vilivyojengwa wilayani Mkuranga katika maeneo ya barabarani lakini kulingana na mahitaji ya maendeleo, vinaweza kumegwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara.

Kadhalika alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakari Kunenge, kwa kutenga maeneo ya uwekezaji na kongani za viwanda mkoani hapa.

Chanzo: Uhuru
 
Watanzania nunueni haraka hili gazeti ni uthibitisho tosha huko mbeleni kuhusu minong'ono kwamba utawala uliopo madarakani sasa hivi uko chini ya maelekezo yake binafsi kwa matakwa binafsi.
 
Back
Top Bottom