Jaji ashauri uchaguzi Z’bar,Bara utenganishwe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Jaji ashauri uchaguzi Z’bar,Bara utenganishwe

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Mtu wa Pwani, Sep 23, 2010.

 1. Mtu wa Pwani

  Mtu wa Pwani JF-Expert Member

  #1
  Sep 23, 2010
  Joined: Dec 26, 2006
  Messages: 4,095
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 135
  hili tunaliangaliaje ?

  Jaji ashauri uchaguzi Z’bar,Bara utenganishwe


  Salim Said na Hawa Mathias
  MAKAMU mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Omar Makungu amesema kuna mgogoro wa kiutendaji baina ya tume yake na ile ya Zanzibar (Zec) ambao alisema unaweza kusababisha uchaguzi wa rais wa visiwa hivyo kuharibika na hivyo kuuweka katikati hatihati uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Muungano.
  “Uchaguzi wa rais wa Zanzibar ukiharibika, basi uchaguzi wa rais wa Muungano hautakuwa salama kutokana na mgogoro wa kiutendaji baina ya Nec na Zec,” alisema Jaji Makungu.
  “Ili kutatua tatizo hili, ni vyema uchaguzi wa Zanzibar ufanyike siku tofauti na wa Muungano.
  ”
  Wananchi wa Zanzibar watapiga kura za kumchagua rais wa visiwa hivyo, rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge wa Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, chombo ambacho ni bunge la visiwa hivyo linaloshughulikia masuala yaliyo nje ya Muungano, na masheha ambao ni sawa na madiwani.
  Lakini wadau wamekuwa wakilalamikia uamuzi wa Nec wa kutumia daftari la wapigakura la Zec, ambayo ina jukumu la kusimamia uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na masheha, kwa ajili ya kuendesha uchaguzi mkuu wa rais na wabunge wa Muungano.
  Akizungumza kwenye semina ya kupiga msasa majaji na mahakimu wafawidhi watakaoshughulikia kesi zitakazotokana na makosa kwenye uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 31, Jaji Makungu alisema changamoto kubwa inayoukabili uchaguzi ni pingamizi la uteuzi wa mgombea urais kukosa haki ya rufaa, matokeo ya urais kutohojiwa mahakamani na daftari la wapigakura la Zec kutumiwa na Nec.
  “Hii ni changamoto kubwa, ingawa hakuna mgogoro wa kikatiba na kisheria, lakini kuna mgogoro mkubwa wa kiutendaji baina ya Zec na Nec,” alisema Jaji Makungu.
  Jaji Makungu aliongeza: “Mgogoro huo utakuwa mkubwa zaidi iwapo itatokea uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani unaosimamiwa na ZEC kuharibika, lazima uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani unaosimamiwa na NEC nao utaharibika.”
  Alisema mazingira hayo yatasababishwa na ukweli kwamba Zec ndio inasimamia uchaguzi rais wa Zanzibar, rais wa Muungano na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na kwamba unafanyika siku moja.
  “Ili kutatua tatizo hili, ni vyema uchaguzi wa Zanzibar ufanyike siku tofauti na wa Muungano, lakini jingine muhimu ni Nec iwe na daftari lake la wapigakura kwa wapigakura wake walio Zanzibar na waachane na utegemezi wa daftari la Zec ambalo haina mamlaka nalo,” alishauri Jaji Makungu.
  Alisema kifungu cha 12(a) cha Sheria ya Uchaguzi kinatamka wazi kwamba Nec itatumia daftari la Zec kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa rais wa Muungano na wabunge wa Bunge la Jamhuri, jambo ambalo linaonyesha kuwepo na utata.
  Alisema utata uliopo ni kwamba Zec inaandaa daftari lake kwa masharti ya kitambulisho cha ukazi wsa Zanzibar (Zan ID), wakati lile la Nec likiandaliwa bila ya masharti ya ukazi.
  “Kwa hiyo huwezi kuwa na wabunge wa Bunge moja wanaochaguliwa na wapigakura walioandikishwa katika madaftari yaliyoandaliwa kwa masharti tofauti,” alisema Jaji Makungu.
  Alisema changamoto hizo zinaathiri kwa kiasi kikubwa uchaguzi wa rais wa Muungano na hata ule wa Zanzibar ambao hufanyika siku moja.
  Alisema suala la mabadiliko ya katiba ya Muungano kumaliza matatizo kwenye uchaguzi mkuu wa Tanzania linaweza kuwa kubwa kuanzia sasa baada ya nchi ya Kenya kufanikisha mabadiliko ya katiba.
  Alisema changamoto nyingine za uchaguzi ni katiba, muundo wa Nec, suala la mgombea binafsi, majaji kuteuliwa kuwa wenyeviti wa tume za uchaguzi na kutokuwapo kwa fursa ya kuhoji matokeo ya urais mahakamani.
  Alisema Nec inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa makini ili kufanikisha uchaguzi ulio huru, haki na uwazi na zinazokidhi vigezo vyote vya kidemokrasia.
  “Kwa upande wa madiwani, malalamiko yanaanzia ngazi ya kata, jimbo hadi Nec. Ubunge malalamiko yanaanzia kwa msimamizi wa uchaguzi wilaya hadi Nec, lakini kwa upande wa urais ni Nec na hakuna fursa ya kukata rufaa mahakamani, hili ni suala la kikatiba,” alisema Jaji Makungu.
  Alisema hadi sasa Nec imepokea rufaa za wagombea ubunge 51 ikilinganishwa na 61 za mwaka 2005 huku za madiwani zikiwa 124 tofauti na 109 za mwaka 2005.
  Naye Jaji Mkuu Agustine Ramadhan alisema hii ni mara ya kwanza kwa majaji na mahakimu wa Tanzania kupigwa msasa kuhusu sheria za uchaguzi na namna ya kushugulikia matatizo ya uchaguzi.
  Alisema haki inatakiwa iangaliwe pande zote za mlalamikaji na mlalamikiwa na sio kwa mlalamikaji pekee, ili uchaguzi uweze kuwa huru na wa haki.


  source: Jaji ashauri uchaguzi Z'bar,Bara utenganishwe « MZALENDO.NET
   
Loading...