Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,885
Maswali ya Lissu kuhusu Jecha yapigwa 'stop' kortini
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imezuia shahidi wa upande wa Jamhuri kuhojiwa na mshtakiwa Tundu Lissu kuhusu Katiba ya Zanzibar na mamlaka ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya huko, Jecha Salum Jecha, kwa kuwa haina mamlaka ya kuzungumzia katiba hiyo.
Kadhalika mahakama hiyo imesema haina mamlaka wala uhalali wa kuzungumzia majukumu ya Jecha na kwamba imekubali ombi la upande wa Jamhuri la kusitisha kumhoji shahidi wake kuhusu suala hilo.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), kumhoji shahidi wa Jamhuri, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi), Salum Hamidu, kuhusu Katiba ya Zanzibar.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Machi 8 na 9. Mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu, Dar es Salaam, Lissu na wenzake walikula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia Lissu na wenzake walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.
Aidha, ilidaiwa kuwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu. Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti.