Iweje walimu wanaoshika fimbo kuchapa, leo wao wanachapwa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Iweje walimu wanaoshika fimbo kuchapa, leo wao wanachapwa?

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by jamadari, Apr 28, 2010.

 1. jamadari

  jamadari JF-Expert Member

  #1
  Apr 28, 2010
  Joined: Feb 13, 2010
  Messages: 295
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  [​IMG]
  Editorial Cartoon  Ipo tabia moja isiyopendeza ambayo inaonekana kujirudia katika jamii yetu. Ni matukio matatu sasa ambayo yameripotiwa ambapo walimu wanachapwa viboko, tena mbele ya hadhara kwa mambo ambayo yanazungumzika badala ya kuwadhalilisha.
  Itakumbukwa kipindi cha nyuma, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Vijijini, Albert Mnali alichukua hatua ya kuwachapa viboko walimu wa shule ya msingi kutokana na matokeo ya mitihani ya shule zao kuwa mabaya. Kesi hii bado inanguruma mahakamani.
  Kumbe badala ya kutoa adhabu hiyo, suala hilo lingeweza kufikishwa kwenye kamati ya Nidhamu ya utumishi wa umma na kujadiliwa, kisha hatua zichukuliwe.
  Tukio lingine ni lile la wanajeshi walioamua kuwapiga bakora walimu mkoani Mbeya ambapo taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.
  Mbali na matukio hayo, Huko Meatu mkoani Shinyanga limeripotiwa tukio lingine ambapo walimu wanne pamoja na wananchi kadhaa akiwemo mjamzito, wiki hii wamejikuta katika suluba baada ya sungusungu kuwacharaza viboko hadharani, tena mbele ya wanafunzi kwa kile kilichodaiwa kutohudhuria mkutano wa kijiji cha Sakasaka.
  Inasemekana kwamba adhabu hiyo ilikuwa miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa na wananchi waliohudhuria kikao kilichokuwa kinajadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya kijiji. Pia wanafunzi zaidi ya 700 walihudhuria.
  Sisi tunajiuliza maswali kadhaa kuhusiana na tukio hilo na mengine yaliyotangulia; kwamba je, ulikuwepo ulazima wa kuwachukulia walimu hao hatua hiyo, tena hadharani bila kusikia utetezi wao?
  Na je, adhabu hiyo imeainishwa katika sheria gani? Hivi wananchi wanawezaje kukaa na kuamua kupitisha adhabu fulani ambayo wala haipo kwenye sheria ndogo ndogo katika ngazi hizo za kijiji au halmashauri husika?
  Kusema ukweli matukio yote hayo, yaani lile la Bukoba vijijini, lile la wanajeshi Mbeya na hili la sungusungu ni udhalilishaji mkubwa wa walimu wetu.
  Kama mtu ametenda kosa au amekaidi jambo fulani anastahili kupewa nafasi ya kujitetea badala ya kumhukumu kwa adhabu inayodhalilisha. Zipo kamati za nidhamu katika ngazi zote hadi vijiji ambazo pamoja na mambo mengine ni kusikiliza utetezi wa watuhumiwa wa makosa mbalimbali na ikidhibitika ndipo adhabu ya kinidhamu hutolewa.
  Na adhabu yenyewe, hasa kwa walimu tunaozungumzia hawakustahili kuchapwa kwani yapo makaripio kadhaa na ikishindikana wanafukuzwa. Hili la kuwacharaza viboko ni jipya kabisa.
  Inafurahisha kuona kwamba hata Chama cha Walimu (CWT) kimeguswa sana na matukio haya yanayojirudia na kuonyesha nia ya kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali mahakamani kwa walimu kudhalilishwa na watu ambao wako chini ya serikali.
  Isitoshe, walimu waliohusika katika matukio haya, hakika wameathiriwa kisaikolojia hasa kwa kutambua kwamba wao ndio waliokuwa na mamlaka ya kuchapa wanafunzi kama adhabu kwa makosa mbalimbali, ikiwemo utovu wa nidhamu, lakini badala yake wao ndio wanaochapwa kama watoto wadogo majumbani au mashuleni.
  Ni muhimu matukio ya aina hii yakomeshwe haraka kwani ongezeko lake linatia shaka na itafikia wakati walimu wetu watajiona kama vile hawana watetezi katika dhalili kama hiyo ya kuchapwa bakora ovyo.
  Tunaamini kwamba kwa matukio haya, Chama cha Walimu nchini kitatoa tamko litakalosaidia kuelimisha watu wanaichukua sheria mkononi na kudhalilisha wengine pasipo kufuata taratibu za kinidhabu zilizopo katika kutoa adhabu.  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
   
Loading...