SoC04 Itungwe sheria ya kila nyumba ya ibada kuwa na kituo cha kulea watu wenye mahitaji maalum kama yatima, wazee na walemavu

Tanzania Tuitakayo competition threads

Son of the universe

New Member
May 29, 2024
3
4
Nyumba za ibada kwa maana ya makanisa na misikiti ni sehemu ambazo waumini wa dini kuu mbili yaani wakristo na waislamu hukutana katika siku zao maalumu kwa ajili ya kufanya ibada na mikusanyiko mingine. Kwa kipindi kirefu nyumba hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika jamii kwa kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya na hata baadhi zimekuwa zikitoa pia huduma ya malezi na misaada kwa watu wenye mahitaji maalumu kama yatima na walemavu.

Pamoja na ushiriki wao huo lakini bado kumekuwa na wingi wa watu wenye mahitaji maalumu katika jamii zetu hasa watoto yatima, watoto wa mitaani, wazee na walemavu ambao wanaishi bila misaada ya kiutu na malezi stahiki katika vituo.

Kwa sababu hizo sasa nashauri serikali kupitia bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania, Wizara husika na kamati ya Amani ya Taifa ambayo inajumuisha viongozi wetu wa dini pamoja na mabalaza yote ya kidini kwa dini zote na madhehebu yake kuona umuhimu sasa wa kutunga sheria itakayo itaka kila nyumba ya ibada katika eneo lake kuwa na kituo maalumu cha kutolea huduma ya malezi kwa watoto yatima, wazee na walemavu wanaohitaji msaada huo.

Kulingana na ongezeko kubwa la nyumba za ibada hasa makanisa basi sheria hii itasaidia kuongezeka pia kwa vituo hivyo ambavyo wingi wake utategemea wingi wa nyumba hizo. Hii itasaidia kwenye kila eneo ambalo nyumba hizo za ibada zipo basi na makundi haya yenye mahitaji maalumu kupata msaada ndani ya eneo hilo hilo na hivyo kupunguza ulazima wa watu hawa kwenda mbali kuitafuta huduma hiyo au kubaki tu mitaani bila msaada wowote au kusambaa kama omba omba ambao tafiti zinaonesha wengine wanatumiwa na watu wasio na nia njema kama vyanzo vyao vya mapato.

Sheria hii pia itapunguza changamoto kuu ambayo imekuwa ikijitokeza kupitia vituo binafsi ambavyo baadhi yake vimekuwa havisaidii walengwa na badala yake vimegeuka vitega uchumi vya wamiliki na waanzilishi wake kwa kuwatumia watu hao wa makundi maalumu kukusanya misaada mbalimbali ikiwemo ya kifedha na mali kwa matumizi yao binafsi na sio walengwa.

Utekelezwaji wa sheria hii pia utasaidia upatikanaji wa misaada kwa wakati na kwa uhakika kwa makundi hayo kwa sababu itatokana na sehemu ya sadaka na matoleo yatakayotolewa na waumini kila washirikipo ibada katika nyumba hizo pamoja na taratibu zingine zitakazopendekezwa na nyumba hizo katika kuhudumia vituo hivyo.

Vituo hivyo pia vitawaweka waumini wake karibu zaidi na watu wenye mahitaji maalumu na kulainisha mioyo yao na kuongeza huruma, moyo wa kujitoa kusaidia na upendo kwa watu wenye mahitaji maalumu. Waumini wanaweza kuhamasishwa pia kujenga utaratibu wa kuchangamana nao, kuwatembelea na hata kusherehekea nao siku za kuzaliwa na hata kuasili sehemu ya watoto yatima waliopo kwenye vituo hivyo na kuishi nao kama watoto wao wa kuwazaa katika familia zao.

Utaratibu huu pia utaongeza uelewa na utashi kwa familia zenye watu wenye mahitaji maalumu kuwaweka wazi ili wasaidiwe badala tu ya kuwafungia ndani na kuwaficha pamoja na imani potofu zilizojengeka juu yao. Kwa kufanya hivi kupitia ibada za kwenye nyumba hizo elimu na uelewa utasambaa kwa haraka miongoni mwa waumini na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mitazamo na fikra hasi zilizopo kuhusu watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu wa viungo na ngozi.

Pia pawekwe utaratibu wa kuwachanganya pamoja wazee na watoto yatima katika kituo kimoja na hivyo kuwafanya watoto hao wapate wazazi wa kuishi nao lakini pia wazee hao wapate watoto na wajukuu wa kuishi nao na hivyo kupunguza upweke miongoni mwao kwa sababu wataishi katika mfumo wa familia moja kama ilivyo katika jamii zetu.

Pia nyumba hizi za ibada zinaweza kusaidiwa kupitia wizara ya jinsia na makundi maalumu kusajiri taasisi zisizo za kiraia kusimamia na kumiliki vituo hivyo na kwa kupitia taasisi hizo zinaweza kukusanya misaada mbalimbali duniani pamoja na kuchangisha fedha kwa ajili ya vituo hivyo pamoja na miradi mingine itakayoweza kusaidia wanufaika wa vituo hivyo.

Ni matumaini yangu makubwa sana kuwa jambo hili litafanikiwa zaidi likifanywa na nyumba zetu za ibada ambazo zipo karibu kila mtaa nch nzima na waumini wake wamekuwa na moyo na utayari na hata mafundisho ya dini zetu yamekuwa yakitukumbusha kusaidia watu kama hawa na hivyo sheria au utaratibu huu utarahisisha jukumu hili na kufikisha misaada kwa haraka zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo ni sehemu ndogo tu ya watu wenye uhitaji wanasaidiwa kwenye vituo kwa sababu ya uchache wa vituo na ukosefu wa pesa za kuendeshea vituo hivyo kwa kuwa michango mingi hutegemewa kutoka nje ya nchi hali iliyopelekea hata baadhi ya vituo kufungwa na kuacha kundi kubwa likizagaa mitaani kama omba omba.

Baadhi ya vituo vimegeuka sehemu hatarishi zaidi kwa watoto yatima wanaolelewa huko kwa sababu ya kukosekana kwa fedha kutoka kwa wafadhili na hata baadhi ya wamiliki kubadilisha matumizi ya fedha hizo. Kwa kuwa taasisi nyingi za kidini zimeonesha ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma za kijamii kama elimu na afya na hata ya malezi ya watoto yatima basi naona itakuwa bora zaidi kama jukumu hilo likiwekewa sheria na utaratibu maalumu kama sehemu ya masharti ya kusajiliwa kwa kanisa au msikiti basi lazima liambatanishe na mradi wa kujenga kituo kitakacho hudumia watu wenye mahitaji maalumu hasa yatima na wazee katika mtaa au kata husika.

Ni imani yangu kuwa jambo hili linaweza kutekelezeka ndani ya muda mfupi kama litatungiwa sheria na kuwekewa utaratibu bora kwa sababu maeneo yapo na yanaweza kupatikana, watu wenye mahitaji maalumu wapo wengi mitaani kwetu, waumini wapo na ni watoaji wazuri tu wa sadaka na michango mingine, nyumba za ibada zipo na zinazidi kuongezeka kila kukicha na rasilimali watu ya kusimamia vituo hivi ipo ya kutoka miongoni mwa waumini wa nyumba hizo za ibada.

Kwa maoni haya natarajia kuona ndani ya kipindi kifupi cha miaka 5 Tanzania yenye huruma na msaada kwa watu wenye mahitaji maalumu na hivyo kuwafanya wajione hawana tofauti yoyote na wana thamani sawa na watanzania wengine na hivyo kuwafanya waishi kwa raha na kujivunia utanzania wao.

Serikali kwa nafasi yake imefanikiwa kwa kuanzisha wizara maalumu kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu na inatunga sera nyingi rafiki kwa ajili ya watu hao sasa ni wakati wa sisi kama jamii kuisaidia serikali katika jukumu hilo kwa kupitia utaratibu huu.
 
Pia pawekwe utaratibu wa kuwachanganya pamoja wazee na watoto yatima katika kituo kimoja na hivyo kuwafanya watoto hao wapate wazazi wa kuishi nao lakini pia wazee hao wapate watoto na wajukuu wa kuishi nao na hivyo kupunguza upweke miongoni mwao kwa sababu wataishi katika mfumo wa familia moja kama ilivyo katika jamii zetu.
Hahahaaaah we jamaa, asee una kipaji cha kutatua tatizo comprehensivelly 😆😆

Kwa maoni haya natarajia kuona ndani ya kipindi kifupi cha miaka 5 Tanzania yenye huruma na msaada kwa watu wenye mahitaji maalumu na hivyo kuwafanya wajione hawana tofauti yoyote na wana thamani sawa na watanzania wengine na hivyo kuwafanya waishi kwa raha na kujivunia utanzania wao.
Hakika bro.

Itakuwa kama sehemu yao ya kulipa kwa jamii isiyohusisha kodi wala riba.

Natumaini gharama za uendeshaji hazitakuwa kubwa maana watu wa kujitolea watakuwa wengi na wanaamini katika dini zao.
 
Back
Top Bottom