Israel Kiyame- msanii `aliyefanikisha’ ujio wa Papa Yohana Paulo II nchini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Israel Kiyame- msanii `aliyefanikisha’ ujio wa Papa Yohana Paulo II nchini

Discussion in 'Entertainment' started by MIUNDOMBINU, Apr 18, 2010.

 1. MIUNDOMBINU

  MIUNDOMBINU JF-Expert Member

  #1
  Apr 18, 2010
  Joined: Apr 14, 2010
  Messages: 452
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 35
  Israel Kiyame- msanii `aliyefanikisha’ ujio wa Papa Yohana Paulo II nchini


  NINAPOFIKA Kinyerezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kuingia kwenye ofisi na karakana anayoitumia msanii Israel Kiyame katika kufanya kazi za uchoraji, mbali na
  vifaa kama rangi, brashi na kadhalika, lakini ukutani nakutana na maneno yaliyoandikwa ‘Mgeni Karibu Tanzania’.

  Herufi za maneno hayo hazikuwa ni zile zilizochongwa na kubuniwa kiustadi, bali zimefanyiwa ubunifu wa hali ya juu kwa kuchora watu wa jinsia mbalimbali ambao wako katika shughuli zao za kila siku, jambo ambalo linanipa picha ya ustadi wa Kiyame.

  Kiyame aliyejipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi kutokana na sanaa ya uchoraji, katika mazungumzo yaliyozaa makala haya, anasimulia alikoibua kipaji hicho, kwa kusema: “Mama yangu (Malka) aliniambia kuwa nilipoanza kukaa nilianza kuchora kwenye mchanga kwa kutumia kidole cha shahada, na siku moja nikiwa nachora chini ya mti, alitokea nyoka mwenye urefu wa futi sita.

  Nikacheza naye kwa dakika 45 na baadaye nyoka akaondoka. “Mama mmoja mtu mzima (aliyemtaja kwa jina la Joanitha) alimzuia mama kutonifuata pale nilipokaa kuwa kama angefanya hivyo yule nyoka angenigonga.

  Pia alitoa ushuhuda kuwa yule hakuwa nyota wa kawaida, bali ni malaika aliyekuja kuangalia kipaji changu na akasema kutokana na kitendo kile, basi ningekuwa mtu maarufu na kukutana na marais, wafalme, mawaziri na watu mashuhuri duniani ambao wangesaidia kukuza kipaji changu na pia kuwa tegemeo katika familia. “Na kweli, kile alichotabiri ndicho kinachoendelea kutokea mpaka sasa kwani nina umaarufu ndani na nje ya nchi.”

  Ndivyo anavyoanza kusimulia Kiyame, kitindamimba katika familia ya watoto 10 wa Hadoram Kiyame (sasa marehemu) na Malka Kiyame, alizaliwa 1954 katika kijiji cha Kingolwira, Morogoro.

  Alisema akiwa na umri wa miaka mitano (mwaka 1959) wazazi wake walihamia jijini Dar es Salaam na baadaye kujiunga na Shule ya Msingi Wailes, Temeke alikohitimu elimu hiyo mwaka 1968 na alichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari katika shule ya Kibasila (kabla ya kutaifishwa ilijulikana kama St. Xavier’s) ambako alichukua masomo ya sanaa na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1972 na baadaye kidato cha sita katika Shule ya Mkwawa, Iringa mwaka 1974.

  “Lakini hata kabla zijaanza shule, Ubalozi wa India ulikuwa umejenga zahanati na maktaba jirani na ilipo Hospitali ya Temeke kwa sasa (iliyojulikana kama Mahatma Indira Gandhi Benevolent Hospital and Library), pale walikuwa wanakuja wataalamu wa uchoraji kutoka India ambao walichangia sana katika kunifundisha mbinu mbalimbali za kuchora.

  “Nilipoanza shule pale Wailes, wataalamu wale walikuwa wakija kunitembelea na nilipofika darasa la tano walikuja walimu wawili kutoka Marekani walikuwa na majina ya rangi, mmoja alikuwa anaitwa Mr. Black na mwingine Mr. Grey walikuta nimetengeneza ndege za bandia zenye urefu wa futi mbili kwa kutumia `raba bendi’, zilikuwa na uwezo wa kuruka ingawa si kwa umbali mkubwa.

  Anaongeza kuwa: “ Waliniuliza kama nilikuwa nataka kuwa nani hapo baadaye, nami niliwaambia ‘nataka kuwa rubani wa ndege’, waliniambia hawanikatazi bali wananishauri nikazane kwenye masomo ya uchoraji, na masuala ya urubani ningeweza kusoma baadaye hata kwa masomo ya jioni.”

  Anasema kuwa mwaka 1969 walimu kutoka Marekani kwenda kwao waliweka jina lake katika orodha ya wanafunzi ambao wanapaswa kuendelezwa na taasisi yao Wamarekani (Peace Corps) na hivyo kuweza kupata mwaliko wa kwenda kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa ya wanafunzi duniani yaliyofanyika New York.

  Kiyame anasema katika mashindano hayo yaliyokuwa yameandaliwa na Shirika la Serve the Children Federation aliweza kushika nafasi ya kwanza na picha zilizompatia ushindi ni za Mlima Kilimanjaro na Wamasai.

  “Baadaye nilialikwa kuchora picha 100 ambazo zilihusishwa kwenye maonesho ya kuchangia yaliyoandaliwa na Serve the Children Federation na kutokana na ustadi katika picha zilizungushwa katika majimbo yote 50 ya Marekani, na kuanzia hapo nilizidi kuhamasika na sasa nimeamua kijikita katika kuwafundisha watoto waishio katika mazingira magumu hapa nchini.”

  Anasema mwaka 1974 ikiwa ni baada ya kuhitimu kidato cha sita, alishiriki maonesho yaliyofanyika Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam na alionesha picha 150 za masuala mbalimbali ya utamaduni na kijamii na picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

  “Nilikaribishwa na Taasisi ya Watu wazima kushiriki katika maonesho, nikiwa kwenye maonesho walikuja watu wawili kutoka ofisi za Usalama wa Taifa wakitaka kujua mimi ni nani, unajua wakati huo ilikuwa ni kosa kwa mwananchi mzalendo kujihusisha na balozi moja kwa moja, na kutakiwa msaada wowote ule kupitia serikalini.

  “Kwa vile nilikuwa ndio kwanza nimetoka shule, wale watu alitaka uhakika kama kweli zile picha zimechorwa na mimi na nimewezaje kuchora wakati ni mwanafunzi, niliwajibu kuwa; “nilikuwa nachora kidogo kidogo wakati wa likizo,”.

  Wakakuta picha zote nimezibandika bei na nyingine zikiwa zimeuzwa tena kwa dola, lakini ile ya Mwalimu (Nyerere) ambayo ilikuwa upana na urefu mita moja na nimeiwekea fremu, wakaniuliza ‘mbona picha ya Nyerere imeandikwa Not for Sell (haiuzwi), niliwajibu kuwa siwezi kumuuza muasisi wa taifa hili.” Anacheka.

  Kiyame anacheka kidogo na kuongeza kuwa: “Lingekuwa kosa kubwa sana kama ningekuwa naiuza, hiyo ingetosha kuniweka kizuizini. Wakaniuliza kama Serikali inahitaji utaiuza kwa shilingi ngapi, niliwaambia kuwa nitakachoweza kufanya ni kumpa zawadi na naweza kuwapa wampelekee.

  Walinitaka nifike geti la Ikulu (Magogoni, Dar es Salaam) kesho yake saa 1:30 ili wanikutanishe na Nyerere, walidhani nitaogopa, kwa siku iliyofuata nilikuwa getini saa moja kasoro robo. Anasema kuwa baada ya kukutana na Nyerere, alifurahia kazi hiyo na kumpatia fedha kiasi cha Sh 50,000 ambacho kwa wakati huo kilikuwa kikubwa mno.

  Mbali ya fedha, anasema Nyerere aliagiza Kiyame apatiwe kazi Kiwanda cha Nguo cha Urafiki jambo lililomfanya ashindwe kuendelea na masomo ya chuo kikuu. “Nasikia Nyerere hakuwa na kawaida ya kusalimiana na raia akiwa amesimama, lakini mimi alisimama na kushangaa kwa kazi ile niliyofanya.

  Kupitia picha nilipatiwa kazi bila kufanyiwa usaili na nilifanya kazi chini ya wataalamu wa Kichina na baada ya muda waliondoka na kukiacha kitengo chetu kuendeshwa na Watanzania wenyewe.”

  Baadhi ya watu mashuhuri ambao ameshawahi kuwachora ni pamoja na Papa John wa Pili (mwaka 1990), Michael Jackson, Bill Clinton na mkewe Hillary, George Bush na mkewe Laura, Jenerali Ibrahim Babangida, kikosi cha wachezaji wa Arsenal, pia mchezaji mmoja mmoja, kama Alexander Song, Rigobert Song, George Weah, Abeid Pele, Olusegun Obasanjo na wengine wengi.

  Anasema: “ Wengi wa watu mashuhuri niliowachora nimekuwa nikipewa kazi na balozi zao.” Anasema baada ya kuitumikia nchi kwa takribani miaka 10 katika viwanda vya ndani na nje ya Tanzania alikwenda kusoma Lagos, Nigeria ambako alisomea uchoraji na theolojia kwa lengo la kuweza kutafsiri aya za biblia kwenda kwenye michoro.

  “Lengo la kwenda kusoma Nigeria ilikuwa niweze kutafsiri aya za biblia na kuziweka kwenye michoro na Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki wamekuwa wakinitumia sana kuwachorea picha kama vile za Yesu akiwa msalabani na ambazo zinaonesha kweli yale mateso, akiwa na wanafunzi baharini au mlimani.

  “Wamisionari waliovutiwa na kazi zangu na hata nikiwa shule walikuwa wakinikodia ndege na kwenda kuchora na ubora wa kazi nilizozifanya ndio ulifanya nipewe kazi ya kuchora picha ya Papa John Paul wa Pili katika vitenge, kanga na nzile zilizotumika kupiga mnada kuchangia fedha za kufanikisha ziara yake hapa nchini.Mpaka sasa makanisa yamekuwa yakinitumia,” alisema na kutolea mfano picha zilizopigwa mnada wa hivi karibuni katika kuchangia ujezi wa Chuo Kikuu cha Bukoba ambacho kinatarajia kujengwa chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

  Akizungumzia mikakati ya kurithisha kipaji chake kwa watu wengine, Kiyame anasema: “Naona kuna baadhi ya vijana wana vipaji, lakini wanahangaika ndio maana nimeamua kutumia taasisi ya Poverty Alleviation Through Education ya Kinyerezi kuwaendeleza.

  Mfano halisi ni kijana aliyekuwa akiishi katika mazingira magumu aitwaye Claud John, lakini sasa anajulikana kwa jina la chorachora ameweza kubadilisha maisha yake na kujenga nyumba kupitia sanaa hii ya uchoraji.

  “Marehemu baba (Hadoram) ambaye alikuwa ni mwalimu na theolojia chini ya Kanisa la Anglikana alikuwa na kazi ya kufundisha vipindi vya dini shuleni na baadaye kufundisha masuala ya biblia wanakijiji na pia wafungwa aliwafundisha neno la Mungu na kubadili tabia kazi ambayo inafanana na ninayoifanya ya kuwabadilisha tabia watoto wa mitaani. “Nadhani Mungu alitaka baadaye mimi niwafungue watu waliofungwa kitabia, kimaadili au jamii kwa kuwapatia elimu na mbinu na ndio maana nimeungana na taasisi ya Poverty ili kuwafungua watu kwa kuwapa elimu.”

  Kiyame ambaye amefanikiwa kupata watoto watatu wa kike, Grace, Annie na Zawadi anasema wote wameweza kufuata nyayo zake katika uchoraji ambao wameweza kuonesha uwezo wao kwa kushiriki mashindano mbalimbali ya uchoraji na kufanya vizuri.

  Ugumu wa kazi Kiyame ambaye pia amewahi kufanya kazi kwenye viwanda vya nguo nchini Zambia, anasema kuwa mwaka 1987, alialikwa na Mpapa Art Gallery ya Lusaka, Zambia inayomilikiwa na akinamama wa Kizungu kwa lengo la kufanya maonesho ya wiki mbili yaliyodhaminiwa na Shirika la Marekani la The Hunger Project.

  “Huwezi kuamini siku ya kwanza maonesho yalifunguliwa na Waziri wa Kilimo wa Zambia kama saa moja usiku na kuhudhuriwa na mabalozi na watalii wengine wakitoka Afrika Kusini na siku ya kwanza ya maonesho iliishia saa tatu usiku. Asilimia kubwa ya picha zilikuwa zimenunuliwa na nilikuwa nimebandika stika ya kuwa imeuzwa.

  Lakini asubuhi yake tulikuta ghala imevunjwa hakukuwa na hata kipande cha picha. “Wale akina mama wakanipa pole, na kwa sababu yalikuwa yamedhaminiwa niliandikiwa cheki na kulipwa picha zangu zote tena mara tatu ya kile nilichokuwa nimekiuza, na walinitaka nichore tena zile zilizokuwa zimenunuliwa, lakini nilikuwa nimeamka tajiri,” anacheka.

  Anakumbuka kazi nyingine iliyoibiwa ni ya vitenge vya Papa John Paul wa Pili zaidi ya doti 1,000 vilivyokuwa vinasafirishwa katika mabehewa mawili ya treni mwenda mkoani Tabora. Anakumbuka kwa kiasi kikubwa kazi yake ilifanikisha ziara ya Papa nchini mwaka 1990, akidai mauzo ya kazi zake yalitunisha kwa kiasi kikubwa fungu la bajeti la ziara hiyo anayosema ilifikia Sh milioni 500.

  Anasema: “ Rais (Jakaya Kikwete) ni mtu wa watu na amekuwa akishiriki harambee za kuchangia shughuli za maendeleo kama ujenzi wa barabara, hospitali na vyuo ni kiongozi ambaye nimechora picha zake nyingi na anashindana na zile za Mwalimu Nyerere kwasababu bado naendelea kuzichora.

  Kiyame anaasa kwa kusema: “ Wito wangu kwa jamii ni kama vijana wanapoonekana kuwa na mwelekeo wa kipaji fulani, basi wazazi waone kuwa ni changamoto na kuhitajika kuwaendeleza na kumhamasisha badala ya kumkatisha tamaa. “Kwa upande wangu, nilikutana na vikwazo kama hivyo, kwani ndugu zangu na marafiki walikuwa wanasema ‘hili toto lenu litakuwa jingajinga na litabaki kuchorachora na halitafika popote hata shule ya msingi halitafaulu,” alicheka na kusema kuwa hali hiyo haikumkatisha tamaa na badala yake alimshukuru Mungu kwa kuwapa uvumilivu wazazi wake.

  Kuhusu ubora wa kazi, Kiyame anasema: “ Siku zote naepuka sana kulipua kazi, nikiwa nachora picha ya rais basi huwa inanichukua wiki moja au mbili na hata mwezi, lakini kwa picha nyingine za kawaida naweza kuchora hata 20 kwa siku.”

  Kiyame ambaye mpaka sasa amekuwa na soko kubwa katika kampuni kadhaa za nguo zikiwemo kiwanda cha Karibu Textile, Eldoret cha Kenya, David White cha Malawi anazishukuru serikali za India, Marekani, Denmank, Finland na UNDP kwa kuchangia kazi yake kufanikiwa.

  Huyo ndiye Kiyame, ambaye kupitia ubunifu wake ameweza kunufaika kwa mambo mengi ikiwa pamoja na kujipatia mamilioni ya shilingi ambayo ameyatumia kwa kufanya tafiti mbalimbali, kusaidia watu wenye vipaji na vikundi vya sanaa, ikiwa pamoja na kuwasomesha watoto wake kwa kiwango cha juu.

  “Sikuitumia fedha yangu kwa starehe, bali kusaidia watu na vikundi mbalimbali, kuwasomesha ndugu na watoto, ndiyo maana mpaka leo natembelea Bajaj…,” anasema Kiyame anayeishi katika nyumba ya kupanga huko Tandika, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

  Anafafanua kwamba, amebahatika kujenga mjini Morogoro ambako amepangisha, lakini kwa Dar es Salaam anakusudia kujenga nyumba ya kuishi na kituo cha sanaa, wakati huko Mtwara, anakusudia kujenga chuo cha sanaa kutokana na imani yake kwamba, mkoa huo una utajiri mkubwa wa sanaa na pia utakuwa kitovu cha biashara.

  source:www.habarileo.co.tz
   
Loading...