Iringa: Vijana waeleza wanatishiwa na wazazi wao wakitaka kuomba mikopo

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
414
1,027
Imeelezwa kuwa kutokana na uelewa mdogo na hofu ya baadhi ya wazazi juu ya mikopo mbalimbali inayotolewa na Halmashauri na taasisi nyingine za kifedha imesababisha kurudisha nyuma maendeleo ya baadhi ya vijana katika Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa ambao wamekuwa wakizuiwa na wazazi wao kujitokeza kuomba mikopo.

Haya yamebainika juzi Machi 23, 2022 wakati wa warsha ya siku 10 ya ujasiriamali kwa vijana 100 wanaotoka katika mazingira magumu Kata za Ihanu, Mdabulo na Luhunga Wilay ya Mufindi, walisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia kujiunga vikundi vya vijana ili kuomba mikopo mbalimbali itakayowezesha wao kupiga hatua katika uanzishaji wa miradi ya kiuchumi.

Anles Msindila kutoka Kijiji cha Iyegeya alisema kuna haja ya mafunzo ya elimu juu ya ujasiriamali na faida ya kuchangamkia fursa mbalimbali zinapotangazwa kuendelea kutolewa kwa vijana pamoja na wazazi ili kuondokana na masikitiko ya ugumu wa maisha huku fursa zinapotangazwa za mikopo zikiendelea kuwapita kushoto kutokana na hofu ya baadhi ya wazazi.

"Vijana baadhi hatukuwa na elimu ya kutosha juu ya uibuaji wa fursa na jinsi ya kuzitumia fursa husika na jinsi ya kufikiwa na mikopo mbalimbali lakini kupitia mradi huu wa Youth Agence Mufindi (YAM) tumeweza kubaini fursa mbalimbali ambazo tunaweza kwenda kuziibua na kuzitumia ili kuondokana na changamoto ya hali duni ya maisha," alisema.

Alisema kuwa wao kama vijana wanatamani kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo serikali imekuwa ikitangaza lakini wamekuwa wakiwakatisha tamaa kwa hofu ya mikopo hiyo kutorejeshwa na kuingia kwenye matatizo ya kuchukuliwa hatua ya kushindwa kurejesha mikopo.

Hata hivyo alisema kutokana na mafunzo hayo kwa sasa anaamini kabisa atakwenda kuwa chachu kwa wenzake kwa kuchangamkia mikopo na fursa nyingine ili kubadili mwelekeo wa maisha yake kiuchumi.

Pia aliomba serikali kuendelea kutoa mikopo kwa vijana pamoja na elimu juu ya usahihi ya kuendesha miradi na jinsi ya kurejesha mikopo husika.

Kwa upande wao wajumbe wa kamati za ulinzi kwa watoto na vijana vijijini (VCPC) Anold Kinayevene na Augustino Julius walisema kuwa kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya mwenendo wa kimaisha na kiuchumi kwa vijana ambao wapo kwenye mradi huo tofauti na awali kabla ya mradi kuanza.

Kuwa vijana hao wana fursa kubwa za kufanya katika vijijini vyao zikiwemo za ufugaji wa nguruwe, kuku na mifugo mingine kikiwemo kilimo cha mahindi mabichi (gobo) pamoja na changamoto ya kuzuia wanyama waharibifu kama ngedere.

Hivi karibuni akizungumza na vijana hao Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambule mbali ya kuwapongeza waratibu wa mradi huo bado aliwataka vijana ambao wamebahatika kuingizwa kwenye mradi kwenda kuwa wabunifu wa miradi vijijini kwao na kuwataka vijana kupitia mradi huo kuunda vikundi vya kiuchumi ili kunufaika na mikopo isiyo na riba toka Halmashauri badala ya kukaa Vijiweni bila kazi.

Alisema serikali ya wilaya haitapenda kuona vijana wakizurula mtaani ama kushinda Vijiweni bila kazi na kuwa watakaokamatwa watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili wafungwe gerezani wakafundishwe kufanya kazi huko.
6943b161-51bc-4e09-8000-b99e5fdd93d5.jpg

Augustino Julius Mjumbe wa Kamati ya Utetezi wa Watoto na Vijana Vijijini (VCPC).

Aliongeza kuwa baada ya kupata mafunzo hayo jambo la msingi ni kuyatekeleza kwani utekelezaji wao utapunguza mazingira ya vitendo vya uhalifu na ukatili wa kijinsia katika jamii zao huku akiwataka kuwatumia viongozi wao wakati wanapohitaji msaada.

Meneja wa mradi wa YAM Zilpa Mgeni alisema mradi huo unaendeshwa Kwa ushirikiano na serikali na hivyo wanaishukuru serikali kwa kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu na mradi wao ambao kiujumla una msaada mkubwa sana kwa vijana.

''Mimi na timu yangu tumeona huu mradi unasaidia kwasababu tumegundua kuwa kuna mbadaliko makubwa tangu tumeanza kuwabainikwani hapo mwanzo walikuwa hawajiaamini kwamba wanaweza kufanya biasharalakini baada ya kupata mafunzo ya saikolojia na ujasiriamali wao wenyewe wamekiri kwamba wanaweza kufanya kitu,” alisema Zilpa.

Pia aliiomba serikali kuzidi kutoa ushirikiano hasa kwa kusaidia kupatikana kwa mikopo hiyo ili wanufaika hao wapate mitaji na kuweza kujiendeleza kimaendeleo.
5e6b56a7-cbd1-4918-a200-1dfc597cea4b.jpg

Washiriki wa mafunzo.

Akizungumzia faida ya mafunzo hayo Meneja wa Mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM) Zilipa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana zaidi ya 770 wakiwemo watoto 150 yatima kutoka kata hizo tatu ambazo zote zitaunganishwa na vijiji 16 za mradi huo.

Alisema mradi huo wa YAM ni wa miaka minne tangu mwaka 2021/2024 umefadhiliwa na serikali ya Filands chini ya taasisi yake ya Diaconess kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na taasisi ya Foxes Community and Wild Life Conservation (FCWC).

Mgeni alisema baada ya mafunzo hayo kutolewa kwa walengwa watawezeshwa mitaji ya kuendeshea miradi ambayo watakuwa wamechangua kuifanya kwa kuwaongezea nguvu ya kuiboresha zaidi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Diwani wa Kata ya Luhunga, Festo Mgina aliwataka vijana hao kusikiliza vyema mafunzo hayo huku akiwaahidi kuwa pamoja na kuwahakikishia kupata mikopo baada ya mafunzo yao kutokana na serikali kujipanga vyema katika kuwasaidia wahitaji.


Source: Matukio Daima Blog
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom