IPTL byebye.. Maazimio ya Bunge yaanza kutekelezwa!

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,888
Kuna kila dalili kampuni ya kufua umeme ya IPTL kutopata leseni ya miezi 55, kama ilivyoomba, kutokana na maombi hayo kuja wakati wananchi wakiwa bado na hasira na kampuni ambayo ilihusika na uchotwaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti maarufu ya Escrow.

IPTL ilikuwa na mkataba wa kuliuzia umeme Shirika la Umeme nchini (TANESCO) katika kipindi cha miaka 21 iliyopita. Katika kipindi hicho cha mkataba na Tanesco, ilianza kufanya biashara na Tanesco miezi 55, kipindi ambacho kilihusisha kufanya uwekezaji.

Wakati IPTL inakuja mezani kuomba leseni kwa Wakala wa Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), tayari kumekuwapo na manung’uniko kutoka kwa wananchi kuhusu namna IPTL ilivyoshiriki kuchota mabilioni kutoka kwenye akaunti ya Escrow.

“Ewura imepokea maombi ya IPTL kuongeza muda wa leseni kwa miezi 55, kuanzia Julai 2017 hadi Julai 2022. Naomba ieleweke kwamba leseni ya kuzalisha umeme hutolewa na Ewura kulingana na pamoja mambo mengine Mkataba wa kuuziana umeme yaani Power Purchase Agreement (PPA) kati ya Tanesco na wazalishaji umeme,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Ewura.

Mkataba wa mauziano ya umeme baina ya IPTL na Tanesco ilisainiwa mwaka 1995 kwa miaka 20 (from Commercial Operation Date (COD). Leseni ambayo imekuwa ikitumiwa na IPTL ni ile iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka 21.

“Maombi yaliyoletwa na IPTL ni kuongeza muda wa leseni uweze kuendana na mkataba wa mauziano ya umeme. Maombi yaliyoko Ewura kwa sasa siyo ya kuidhinisha mkataba wa mauziano ya umeme, bali kuhakikisha uzalishaji wa umeme ambao unafanyika na IPTL unafanyika kisheria kwa kupata leseni kutoka Ewura.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Umeme na Sheria ya Ewura, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Tanesco, ni wadau ambao wameombwa kutoa maoni yao kuhusu maombi haya. Wananchi pia wameombwa maoni yao kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Ewura na kifungu cha 8 cha Sheria ya Umeme,” inasomeka taarifa kutoka Ewura.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), tayari kimejitokeza hadharani kueleza azma yake ya kupinga kampuni ya kufua umeme ya IPTL kupewa leseni na Ewura ili iweze kufanya biashara na Tanesco.

LHRC imetangaza kuweka kusudio la kupinga IPTL kupewa leseni ya kuendelea kuliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku wakihoji usafi na makandokando dhidi ya kampuni hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, amenukuliwa akisema wanamalizia kuandaa pingamizi lao la kisheria ambalo wataliwasilisha Ewura.

Henga amesema IPTL haina sifa tena ya kuendelea kuuza umeme nchini, hasa baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.

“Suala hili tumekuwa tukilifuatilia tangu zamani na tuna ushahidi kwamba IPTL haipaswi kupata tenda hii kwa kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Bunge kuhusu kampuni hii bado hayajatekelezwa.

“Tutapeleka maoni yetu Ewura, tutawaandikia jinsi tunavyoona, lakini kwa hali ya kawaida kwa IPTL, Ewura hawakuhitaji hata kuomba maoni ya wananchi katika kufanya uamuzi kwa kuwa sifa mojawapo ya kupatiwa leseni ni uadilifu wa muhusika,” amesema Henga.

Amesema moja ya mapendekezo yaliyotolewa na iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, hayakutekelezwa, ikiwamo kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), kufanya uchunguzi juu ya umiliki na uwepo wa rushwa katika utendaji kazi wa IPTL na wabia wake.

Maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge

1. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalum wa Malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (‘CAG’) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (‘TAKUKURU’), imeonesha kwamba Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (‘TANESCO’) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing (‘VIP’);

Kwa kuwa, kwa sababu ya kuhusika kwa watu hao na miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Escrow imeliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya shilingi za umma zinazotokana na kutokulipwa kwa kodi mbali mbali za Serikali na kushindwa kwa Tanesco kukokotoa upya kiwango cha malipo ya gharama za uwekezaji (‘capacity charges’) wa IPTL;

Kwa kuwa, mabilioni ya shilingi yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi na maafisa wa Serikali kama vile Mawaziri, Majaji, Wabunge, Wenyeviti wa Kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.

Na kwa kuwa, vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria makosa mbali mbali ya jinai kama vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;

2. Kwa kuwa, vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini, vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;

3. Kwa kuwa, katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco;

Na kwa kuwa, Bunge na/au Kamati zake za Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge;

4. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

Kwa kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’) imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji;

Kwa kuwa, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji;

Na kwa kuwa, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

5. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP katika benki hiyo;

Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba akaunti za PAP katika Stanbic Bank Tanzania Ltd. zimekwishafungwa baada ya fedha zote zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kumalizika na Akaunti ya ya VIP katika Mkombozi Commercial Bank imebakiza kiasi fulani cha fedha;

Na kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba kuna uwezekano fedha zilizotolewa kutoka kwenye akaunti za PAP na VIP zilipelekwa katika benki nyingine;

Na kwa kuwa, vitendo vya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwenye Akaunti ya Escrow ni vitendo vya jinai kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of money laundering concern);

6. Kwa kuwa, vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, hujuma ya uchumi na ufisadi vimeongezeka, kushamiri na kushirikisha viongozi wa kisiasa na maafisa wa Serikali pamoja na wafanyabiashara wakubwa;

Kwa kuwa, kwa mujibu wa sheria iliyounda TAKUKURU inashughulikia vitendo vya aina zote za rushwa zikiwamo rushwa ndogo ndogo (petty corruption) na rushwa kubwa na ufisadi (grand corruption) na matumizi mabaya ya madaraka;

Na kwa kuwa, kwa sababu ya majukumu yake mapana kisheria, Takukuru inaelekea kuelemewa katika vita ya kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa letu kiuchumi, kijamii na kisiasa;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa;

7. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo Tanesco imekuwa ikitumia mabilioni ya shilingi kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;

Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba Tanesco itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.

8. Kwa kuwa, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi za kufua umeme imeisababishia Tanesco hasara ya mabilioni ya shilingi na hivyo kutishia uhai wake wa kifedha;

Kwa kuwa, Bunge lilikwishaazimia kwamba Serikali iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri Serikali;

Na kwa kuwa, Serikali haijatekeleza Azimio hilo la Bunge hadi sasa;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti, Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.

Credit: Jamhuri
 
yale mabilioni yaliyochotwa kwa sandarusi yasipoongelewa na wahusika kufikishwa kizimbani yatakuwa ni maigizo tu...lakini so far so good
 
Back
Top Bottom