IPI TAMTHILIYA bora........... | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

IPI TAMTHILIYA bora...........

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mizambwa, Jun 18, 2012.

 1. mizambwa

  mizambwa JF-Expert Member

  #1
  Jun 18, 2012
  Joined: Oct 8, 2008
  Messages: 4,409
  Likes Received: 569
  Trophy Points: 280
  Wana jamvi nauliza, nipate kuelimika
  Kutwa kucha ninawaza, na ninazidi teseka,
  Hili jambo lanikwaza, linarudi kila mwaka,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Tarehe kumi na nne, mwezi wa sita hakika,
  Ni siku tena nyingine, kushuhudia vibweka,
  Hili si jambo lingine, bali bajeti husika,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Mwaka jana bungeni, Mkulo alipeleka,
  Aliisoma kwa makini, kwa wote ikasikika,
  Bajeti aloibuni, Tanzania kutumika,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Koba kubwa alibeba, lenye bajeti husika,
  Tukasema baba baba, mkombozi amefika,
  Akaingia kwenye nyumba, Bungeni kukaripuka,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Matarajio ya wengi, kwa kilio kusikika,
  Matatizo ya msingi, kwamba yatatatulika,
  Ahadi zikawa nyingi, ni kweli zilisikika,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Na wabunge kwa pamoja, bajeti kuipa shaka,
  Wapemba pia Unguja, na wote walicharuka,
  Waliipinga kwa hoja, kwamba kutokubalika,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Serikali ikawaza, na mbinu kuipeleka,
  Wa sisiemu wa kwanza, na vikao kuwaweka,
  Uongo kubambikiza, bajeti kuongezeka,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Bajeti ilipopita, kumbe ngumu kutumika,
  Serikali wakajuta, wapi pesa watashika,
  Kila walipojikita, kuna moto unawaka,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Mheshimiwa Mgimwa, hiki kiti kakishika,
  Na bajeti alotumwa, kuileta ina shaka,
  Heri enzi za utumwa, kuliko sasa hakika,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Maisha ya Tanzania, bado yazidi kuruka,
  Kila mwaka Historia, bei bidhaa kushuka,
  Viongozi jivunia, maisha yalotukuka,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?

  Kwa sasa naishia, machozi yananitoka,
  Nina mengi endelea, sasa kwikwi zanishika,
  Bajeti waliyotoa, ni usanii hakika,
  Ipi Tamthiliya bora, mwaka jana au huu?
  ========================================
  MIZAMBWA
  INANIUMA SANA!!!
   
Loading...