Ipi iwe ni kauli ya Wazanzibar, Serikali tatu au……….?

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
[h=1][/h]Written by ole // 24/03/2012 // Habari // 6 Comments


Na B.OLE,
Baada ya miaka zaidi ya nusu karne kupita, tokea Wazanzibar na Zanzibar kupoteza haki yake ya msingi kama Nchi, hatimae Mola wetu amesikia vilio vyetu ,ametukumbuka kwa kututeremshia rehema zake tukufu,na kutuonesha mwanga tena baada ya chombo chetu cha ukombozi kupotea na kupata misukosuko huku dhoruba kubwa zikivamia chombo hichi bila ya huruma baharini na kukitokomeza kwenye mawimbi na kiza kikali .
Hatimae jua limeanza kuchomoza na kuwafanya Manahoza na abiria kupata tena tamaa ya kuweza kuona tena nchi kavu na kufurahia tena uhai wao, wakiwa binadamu huru kama wengine.Hapana budi tukumbuke kwamba hata hivyo kufikia ufukweni na kuwa salama panahitajika kazi nzito na ujasiri mkubwa katika hili. Kazi ambayo iko mbele yetu bado sio rahisi kwani kombe hili lipo uwanjani na lazima apatikane mshindi.
Licha ya dalili zote ambazo tayari zimeshajitokeza lakini bado hatari iko mbele yetu, kutulia kwa upepo wa bahari sio kusema chombo chetu kiko salama,bado kuna wanyama wakali kama vile mapapa na manyangumi wanakifuatilia kwa karibu sana, lengo lao ni kukizamisha chombo hichi, ambacho kutokana dhoruba kuwa kubwa kimefanya ufa ndani yake.
Abiria na Manahodha wana kazi ngumu ya kufanya, kuchomoza kwa mwanga wa jua sio sababu ya kutoka kwa jua,inawezekana vile vile mawingu yakatanda na mvua zenye radi zikanyesha na kuifanya hali kuwa hamkani sio shuari tena. Umahiri wa manahodha na utulivu wa abiria kufuata maelezo ya Nahodha chomboni unahitajika sana na hasa ukiangalia ya kwamba chombo wenyewe kimejeruhiwa vibaya sana.
Kwa mara ya kwanza, dua, vilio na maombolezo ya Wazanzibar yameanza kusikika kuhusu suala zima la Muungano wa Tanzania, baada ya Tanzania kama Tanzania kutaka pawepo Katiba mpya hapo ifikapo 2014.Lakini hatuna budi kujiuliza hasa sisi Wazanzibar kulikoni ? Jee huu ni ukarimu wa wenzetu au ni mapenzi yao kuwa makubwa juu yetu au kuna ajenda ya siri hapa Wazanzibar ?, hili ni lenu. Hapa naona lazima tutizame ncha ya ujiti isijekuwa ina hoho.
Niseme ni jambo zuri sana kama tutaliangalia kwa mtazamo wa kidemokrasia, lakini tukija katika ukweli halisia wa upande wa shilingi, utagundua hawa wenzetu wako mbali sana na hilo,kwani sivyo kama vile wengi wetu miongoni mwa Wazanzibar tunavyofikiria suala hili la Katiba.
Hapa kwa mtazamo wangu katika hili lazima kila Mzanzibar achukue tahadhari, kosa hili likifanyika tena kwa mara nyengine basi kutakuwa hakuna wa kumlaumu tena,kwani hivi sasa wengi wetu tumekuwa na kauli kwamba oh! Karume alituuza, ni sawa lakini leo hii Karume hayupo tena, kama ni hivyo jee tukifanya uzembe tena kwenye katiba hii nani alaumiwe, Karume kenge ?
Kutokna na ukweli ambao tayari umeshaonekana tokea mchakato huu wa katiba kuanza ni dhahiri kwamba wenzetu wa Tanganyika wana ajenda ya siri na hili halitaki mwenge kutuangazia wazanzibar.
Kama hivyo ndivyo basi hapana budi kwa Wazanzibar kukaa na kuibuka na uamuzi wa pamoja bila kuzingatia chama,sera,kabila,mkoa wala kijiji.Lengo ni kuinusuru Zanzibar na raslimali zake halafu kama kuna jengine ndio liwekwe mezani kujadiliwa.Kauli ya siku zote kusema tunaonewa haitoshi kuikomboa Zanzibar, umoja na ukweli ndio suluhisho la tatizo letu.
Sisi kama Wazanzibar tunachohitaji ni Serikali tatu, yaani Serikali ya Tanganyika kwa upande wa Tanzania bara yenye mamlaka kamili ya utawala na mambo yao kama ulivyo sasa na huku Zanzibar iwepo na Serikali yake ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na utawala wake kama vile ilivyokuwa baada ya huru, kabla ya Muungano.
Lakini kama hilo haliwezekani basi sio vibaya kama kila upande ukashughulikia mambo yake na kubakia ujirani na udugu mwema miongoni mwetu.Na hili sio jambo baya wala geni tayari sehemu nyingi imeshatokea duniani.
Kutokana na hali hiyo ni kwamba hatuna budi kuhamasishana na kuelimishana katika hili. Popote pale alipo Mzanzibar hana budi kutoa mchango wake wa hali na mali kufanikisha kazi hii.
Zile Taasisi zisizo za kiserikali ambazo zipo ndani na nje ya nchi hazina budi kulifikiria suala hili na kulifanyia kazi na ikibidi tuandae taratibu maalum ya kuelimishana ili tujue hasa ni upi ndio msimamo wetu na kipi tunadai ili iwe rahisi kwa wenzetu kutuelewa kwani masikio yao wameyatia pamba wanashindwa kusikiliza huzuni na vilio vya Wazanzibar
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom