India kutafuta njia mbadala ya kufuatilia mawasiliano ya watumiaji wa WhatsApp

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Moja ya sababu zilizofanya mitandao ya kijamii kuaminiwa zaidi na watumiaji ni kutokana na hakikisho la usalama wa mawasiliano kwa kutumia mfumo wa msimbo fiche wa mwisho hadi mwisho (end-to-end encryption). Huu ni mfumo unaoficha ujumbe uliotumwa kutoka kwa mtumiaji mmoja ili usiweze kusomwa na mtu mwingine ambaye si mpokeaji, mfano serikali au vyombo vya usalama. Lakini baadhi ya serikali zimejaribu kushawishi makampuni ya mawasiliano, bila mafanikio, kuwapa uwezo wa kufuatilia mawasiliano ya watumiaji wa mitandao hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukabiliana na ugaidi.

Sasa serikali ya India inataka njia mbadala ya kufuatilia mawasiliano ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, hasa mtandao wa WhatsApp ambao una watumiaji wengi zaidi nchini humo. India inataka kila ujumbe wa WhatsApp kuwekewa alama ya utambulisho ili iwe rahisi kufuatiliwa na kumfahamu mtumaji wa kwanza, lengo likitajwa kuwa ni kudhibiti uhalifu.

Serikali ya India inasema ipo tayari kushirikiana na WhatsApp kutengeneza njia hiyo mbadala ambayo haitaingilia mawasiliano baina ya mtumiaji mmoja na mwingine, hivyo kuendelea kudumisha sera ya WhatsApp ya kutoingilia mawasiliano ya watumiaji wake.

WhatsApp, inayomilikiwa na kampuni ya Facebook, ina watumiaji hai zaidi ya milioni 400 nchini India pekee, imekataa ombi hilo la serikali ikisema haina teknolojia ya kuweka alama maalum kwenye kila ujumbe, ambapo mabilioni ya jumbe hutumwa kila dakika.

Serikali ya India imesema kuwa inafanya mazungumzo na kampuni hiyo, na imeipa miezi mitatu kujibu rasmi ombi lake la mwezi Februari, ingawa WhatsApp haijatoa msimamo wake kuhusu ombi hilo.

India imekuwa kwenye mgongano na mitandao ya kijamii baada ya kutungwa kwa Sheria ya Teknolojia ya Mawasiliano inayotaka mitandao ya kijamii kutoa taarifa za watumiaji ikiwa serikali itahitaji taarifa hizo. Facebook imeendelea kusisitiza kuwa haitaondoa ulinzi wa taarifa za watumiaji wake.

Lakini Kampuni ya Facebook imeingia doa siku za hivi karibuni baada ya mamilioni ya watumiaji wake kuhamia mitandao ya Telegram na Signal kutokana na sera yake yenye utata ya ulinzi wa taarifa binafsi za watumiaji ambayo kampuni hiyo ilijitetea kuwa haikuwa na madhara kwa watumiaji. Kwa sasa Kampuni ya Facebook ipo katika kipindi cha kujisafisha, ikijitahidi kuwajulisha watumiaji wake kila mara kuhusu mabadiliko yoyote inayoyafanya kwa njia mbalimbali ikiwamo kwa 'status' za WhatsApp.

Chanzo: BGR
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom