Inawezekana kweli Kikwete ni chaguo la Mungu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Inawezekana kweli Kikwete ni chaguo la Mungu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MamaParoko, Jul 24, 2008.

 1. MamaParoko

  MamaParoko JF-Expert Member

  #1
  Jul 24, 2008
  Joined: Jan 14, 2008
  Messages: 465
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  JK chaguo la Mungu, ingawa…

  Nkwazi Nkuzi | Tanzania Daima

  HAKUNA ubishi kwa hali ilivyo katika nchi yetu hasa hali mbaya ya Chama Cha Mapinduzi, kuna uwezekano ukawa mwanzo wa mwisho wa zama na enzi zake.

  Kuna kisa maarufu cha mtoto wa mchonga na muuza sanamu wa huko Ukaldayo. Huyu bwana mdogo alichukia masanamu. Yalikuwa yakiabudiwa wakati ule. Ilikuwa ni kufuru kwake na Mungu.

  Katika jitihada za kuwaelimisha watu wa kwao, kijana huyu kwa makusudi alipanga kuyavunjilia mbali masanamu hayo.

  Wanazuoni hudai kijana huyu shupavu alitumwa na Mungu kuwafungua macho ndugu zake na kuangamiza kufuru na machukizo yaliyokuwa yakifanyika kwa kuabudia sanamu hizo.

  Siku moja wakati wazazi na ndugu zake wametoka, kijana huyu aliamua kuyavunjilia mbali masanamu yote isipokuwa kubwa lao. Baada ya kumaliza kazi ya kuyasambaratisha, alichukua shoka alilotumia na kulivisha sanamu kubwa na akaondoka.

  Baba yake alipofika na kukuta zahama iliyoyakuta masanamu yake yaliyokuwa miungu wake, alishangaa na kumuita yule kijana aeleze kulikoni. Yule kijana alipofika alimwambia baba yake aliulize lile sanamu lililokuwa limevaa shoka!

  Baba mtu alishangaa jibu hili na kuhoji sanamu lisilo hai lingewezaje kuyavunja mengine? Kijana alimjibu: Kama sanamu halina uwezo, hivyo ni kwanini walikuwa wakiyaabudu? Huo ulikuwa mwisho wa ibada za masanamu na ukombozi.

  Tukija kwenye mada yetu kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu, tunakuta kuwa kwa staili yake ya kutawala, uwezekano ni mkubwa wa chama tawala CCM kusambaratika na kuondolewa madarakani kama upinzani utajipanga vizuri.

  Laiti kama kutakuwa na upinzani wenye lishe na mikakati hai na inayowezekana, Tanzania kwa mara ya kwanza inaweza kushuhudia kishindo walichosikia Wakenya mwaka 2002 ilipoangushwa KANU.

  Kazi ya kusambaratisha CCM imeishaanza na aliyeianzisha na atakayeifanikisha ni Kikwete, ingawa ni jambo la bahati mbaya sana kwamba ‘kijana wetu' huyo halijui hilo na pengine anaweza akadhani hizi ni hadithi za kufikirika.

  Ingawa waliomsifia Kikwete kuwa alichaguliwa na Mungu walifanya hivyo kwa kubembeleza maslahi na kujikomba, walishindwa kujua upande wa pili kuwa alichaguliwa kubomoa si kujenga. Rejea serikali yake kukumbwa na utitiri wa kashfa na isizishughulikie. Rejea hali za Watanzania kuzidi kudhoofu vibaya sana hata kufika hatua yeye mwenyewe kukiri kwamba mambo ni magumu na watu wanapaswa kuvumilia.

  Rejea mafisadi kuwa na nguvu kwa serikali yake hata kuliko umma.

  Kikwete ama kwa kujua au kutojua amekuwa akitawala kwa mtindo wa bahati nasibu. Amekuwa mgumu wa kujifunza hata kubadilika. Bahati mbaya hakujifunza toka kwa mtangulizi wake Rais mstaafu Benjamin Mkapa wala hali iliyopo sasa na nchi jirani ya Kenya.

  Hii ni heri kwa wapenda mabadiliko na msiba kwa CCM ambayo kwa kiasi fulani licha ya kuzeeka imechusha na kuchoka. Imeishiwa mvuto, ikapoteza sera na kisha kukwama kimikakati. Imegeuka dude kubwa linyonyalo damu za Watanzania.

  Rejea kuhusishwa kwake na ufisadi wa EPA chini ya kampuni yake ya Deep Green Finance. Rejea kushinda uchaguzi kwa kutegemea takrima huku Zanzibar ikitegemea mtutu wa bunduki na ukandamizaji mkubwa. Rejea kuibuka kwa mitandao ya ndani kwa ndani ya chama inayotishia kukisambaratisha. Rejea ukosefu wa sera, falsafa na visheni vya kutawalia. Rejea mtindo mchafu wa kulindana na kufadhiliana bila kujali maslahi ya taifa.

  Wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere tulizoea siasa za vuguvugu za ukombozi wa umma na nchi jirani. Tulikuwa na chama kilichokuwa kimebobea kwenye ukombozi wa kweli. Kwa hakika CCM na kabla yake TANU ya Nyerere si hii tunayoiona leo kwa Kikwete na jeshi la wanasiasa wenzake.

  Baada ya kung'atuka na hatimaye kufariki dunia kwa mwalimu, chama alichokiasisi kilitekwa na wachuuzi wa roho za watu, kiasi cha kubobea kwenye jinai hii ya kuiibia umma. Rejea ubinafshishaji kichaa uliofanywa na awamu mbili zilizofuatia kabla ya hii ambayo hata baada ya Nyerere mwenyewe kulia sana wakati akiwa hai hakuna hata mmoja aliyesikia kilio chake.

  Rejea wakubwa wa serikali na chama kuanza kutumia nafasi zao kuuibia umma na kujitajirisha huku umma ukitopea kwenye lindi la umaskini wa kunuka. Hapa mfano wa karibu ni kadhia ya Mkapa na familia yake; hata kinachoendelea chini ya Kikwete na jinsi familia yake inavyoanza kuiranda ya Mkapa. Rejea NGO ya mke wa rais ambayo ameonywa aifute na akakaa kimya.

  Badala ya CCM kuendelea na siasa za ukombozi, imejiingiza kwenye siasa nyemelezi na angamizi!

  Nani angetegemea wala kuamini kuwa nchi kama Msumbiji na Uganda ambazo licha ya kuzikomboa hazina rasilimali nyingi kama zetu zingetuzidi kiuchumi?

  Huu ni ushahidi tosha wa ukosefu wa mipango na unyemelezi wa CCM kama chama. Ingawa ni aibu, huu ndiyo ukweli. Hebu angalia nchi kama Kenya ambayo ikiunganishwa na Uganda bado haifikii ukubwa wa Tanzania hata kwa rasilimali, inavyotuhenyesha kiasi cha kuiogopa na kuitegemea. Ni aibu ya mwaka.

  Tukirejea kwa Kikwete, yeye kama kijana mvunja masanamu, badala ya kuyabomoa masanamu, ameyapa mashoka yabomoane yenyewe kwa yenyewe yeye akiangalia na kuchekelea!

  Tofauti na kijana mvunja masanamu, yeye hana baba wa kumgombeza wala umma wa kutishia usalama wake, kwa kusababisha masanamu kuvunjika. Kikwete ana faida moja katika hili. Kama kazi yake ikifanikiwa italeta ukombozi bila manung'uniko na mabishano kama ilivyokuwa kwa yule kijana.

  Wanafanana katika moja. Kazi zao zitaleta mwanga na kufungua mboni za kaumu zao.

  Nje ya mada, hakuna jambo limenikera kunisikitisha, kunichefua na kunihuzunisha kama kugundulika kwa wizi unaofanywa na kampuni ya Mama Anna Mkapa dhidi ya walimu maskini.

  Sasa umefika wakati kwa serikali kuacha mchezo na maisha yetu. Imshughulikie Mkapa na familia yake. Maana karibu kila uchafu nyuma yake kuna jina Mkapa ama kushiriki kwake, mkewe, watoto wake au marafiki zake.

  Inakera kiasi cha kuanza kuhoji nia hasa ya Rais Kikwete kwa Watanzania. Aeleze kama yuko kulinda ufisadi au umma uliomchagua kwa kishindo.

  Tuhitimishe. Ingawa Kikwete si chaguo la Mungu kwa maana ya kuwa rais wa nchi. Anaweza kuwa chaguo la Mungu kwa maana ya kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la CCM. Mungu ana njia zake za kutenda. Hakika Kikwete ni chaguo la Mungu ingawa si kwa kujenga bali kukibomoa chama chake.


  nkwazigatsha@yahoo.com
   
 2. Jile79

  Jile79 JF-Expert Member

  #2
  Oct 6, 2009
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 11,359
  Likes Received: 3,124
  Trophy Points: 280
  Jamani naomba msaada tuwarejee wale viongozi wa dini waliopanda majukwaani na kusema Kikwete ni cahguo la Mungu....ninachotaka hapa ni kujua kama kweli kikwete ni chaguo la Mungu? Kwa nini ni chaguo la Mungu? Na waliosema hivi ni nani hasa kwa yeyote anaekumbuka.....
   
 3. Lekanjobe Kubinika

  Lekanjobe Kubinika JF-Expert Member

  #3
  Oct 6, 2009
  Joined: Dec 6, 2006
  Messages: 3,067
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Sasa ulitaka waseme chaguo la shetani? Kiongozi yeyote huwa kiongozi sababu Mungu kaamua iwe hivyo. Ndio maana twaambiwa tuwatii viongozi wetu, maana hao wamewekwa na Mungu. Usipomtii kiongozi wako utawezaje kumtii Mungu usiyemwona? Ndio maana tunawaombea bila kujali dini yako. Hata wewe Mungu anaweza kukuchagua. Kama tunalazimisha pasipo kibali cha Mungu huwa maangamizi.

  Leka
   
 4. PakaJimmy

  PakaJimmy JF-Expert Member

  #4
  Oct 6, 2009
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 16,236
  Likes Received: 308
  Trophy Points: 180
  Kweli wewe ni mgeni humu!

  Mbona kuna mathread mengi sana yanayojibu haya maswali yako yote kwa ujumla humu ndani? Hii ni topic iliyoongelewa mara nyingi sana na wanaJF.
  Embu jaribu kusearch bwa mkubwa!
   
 5. NGULI

  NGULI JF-Expert Member

  #5
  Oct 6, 2009
  Joined: Mar 31, 2008
  Messages: 4,812
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 135
  kipindi cha renascence kiongozi aliyekubalika na watu wengi illiamnika ni chaguo la Mungu, Hata hivyo bado yeye Mh! Rais Kikwete ni chaguo la Mungu na hata wewe ni chaguo la Mungu.
   
 6. B

  ByaseL JF-Expert Member

  #6
  Oct 6, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 2,223
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  Kimsingi kiongozi yeyote ni chaguo la Mungu kwa sababu sio kila mtu anaweza kuchaguliwa na watu awe mbaya au mzuri. Ukisoma Biblia utaona kwamba Mungu aliwachagulia waisraeli Wafalme wazuri na wabaya. Mfalme wa kwanza kuchaguliwa na Mungu kuwatawala waisraeli alikuwa Saulo kupitia kwa mwamuzi Samueli. Saulo akakengeuka na Mwenyezi Mungu akamwacha. Alikufa kifo kibaya. Akateuliwa mfalme Daudi badala ya Saulo akamcha Mungu na hapakutokea mfalme kama Daudi kaika historia ya Israel. Hata Mfalme Suleimani aliyepewa hekima nyingi alimkosea Mungu na akaadhibiwa vilivyo na Mungu. Mifano ni mingi katika biblia.

  Ni katika mantiki hiyo Father Mapunda, Baba Paroko wa Manzese katika ushabiki wake kwa JK alisema katika mahubiri yake wakati wa mchakato wa kutafuta Urais akasema Kikwete ni Chaguo la Mungu. Magazeti yakadakia hilo na kusema Kanisa Katoliki limesema JK ni chaguo la Mungu wakati kusema kweli kanisa halikuwahi kusema hivyo. Matamko rasmi ya Kanisa Katoliki kawaida upitia katika ofisi ya TEC (baraza la maaskofu) na hili la JK halikuwa hivyo ila ni Padre mmoja tu.
   
 7. Jile79

  Jile79 JF-Expert Member

  #7
  Oct 7, 2009
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 11,359
  Likes Received: 3,124
  Trophy Points: 280
  shida yangu bado haijaisha......nataka kujua kwa nini ni chaguo la mungu....na je chaguo la shetani ni lipi?
   
 8. Jile79

  Jile79 JF-Expert Member

  #8
  Oct 7, 2009
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 11,359
  Likes Received: 3,124
  Trophy Points: 280
  inawezekana kweli...lakini je chaguo la mungu maana yake nini.............na ni kwa nini jk ni chaguo la mungu?
   
 9. Jile79

  Jile79 JF-Expert Member

  #9
  Oct 7, 2009
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 11,359
  Likes Received: 3,124
  Trophy Points: 280
  nimekupata vizuri....lakini inamaana hakuna chaguo la shetani? kwanini jk ni chaguo la mungu?
   
 10. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #10
  Oct 7, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,203
  Likes Received: 371
  Trophy Points: 180
  Katika Kitabu cha Warumi tunasoma hivi:

  "Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe. 3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu. 4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya. 5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri." (Rum. 13:1-5).

  Wakati Rum. 13:1 inasema kwamba hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu (General Rule), Rum. 13:4 inasema kwamba mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema (Exception to the General Rule). Kwa maana hiyo Chaguo la Mungu ni yule mwenye mamlaka atendaye mema tu, otherwise ni Chaguo la She****.

  Kuhusu Jakaya Kikwete kama ni Chaguo la Mungu au la kila mtu anatafsiri aonavyo kama alivyofanya Father Mapunda (Rejea Post #5 hapo juu).
   
 11. Andrew Nyerere

  Andrew Nyerere Verified User

  #11
  Oct 7, 2009
  Joined: Nov 10, 2008
  Messages: 3,025
  Likes Received: 1,203
  Trophy Points: 280
  Kiongozi akichaguliwa, baada ya wananchi kupiga kura, basi huyo ni chaguo la Mungu. Sasa wewe sijui unalalamika nini. Kiongozi anapochaguliwa na wananchi huyo ni chaguo la Mungu, hiyo ni Demokrasi, kiongozi amechaguliwa na wananchi, yakitokea matatizo, wananchi hawawezi tena kusema,'' Huyu kiongozi wetu ametoka wapi, sisi hatumfahamu."

  Sasa wewe unauliza chaguo la Mungu vipi? Umesoma katika Biblia, watu watatu wenye hekima wanakuja kutoka Mashariki wanamuuliza Herod, yupo Mfalme amezaliwa hapa, tumekuja kumletea zawadi. Na Mfalme Herod anawauliza,''Mfalme amezaliwa hapa?'' Na wale watu wanamwambia" Ndiyo, tumeiona nyota yake tulipokuwa Mashariki. Huyu Mfalme yupo hapa mahali fulani.'' Halafu Herod anawaambia, wamtafute huyu Mfalme na yeye pia angependa kumfahamu huyu Mfalme ni nani ili na yeye pia amwabudu.

  Umesoma pia katika Biblia, Mwenyezi Mungu anamwambia Nabii Samwel,kwamba amtafute kiongozi mwingine badala ya Saul. Halafu Nabii Samwel anakwenda kumtafuta David. Tuelezee kidogo zaidi kwa faida ya wale ambao hawajaisoma hii hadithi katika Biblia. Nabii Samwel anakwenda kwa baba yake David, na anamwambia awaite watoto wake wote wanaume. Wote wanaitwa na kila mmoja wao anapopita mbele yake, Mwenyezi Mungu anamwambia Nabii Samwel, ''Sijamchagua huyu'', mpaka anapopita yule wa mwisho, pia Mwenyezi anasema, ''Siyo huyu.'' Halafu Nabii Samwel anamuuliza baba yake David, Jesse nadhani anaitwa, anamuuliza,'' Hawa vijana ndio wote, au bado yupo mwingine?'' Halafu Nabii Samwel anaambiwa kwamba yupo mwingine wa mwisho,yupo mbugani,anachunga kondoo. Halafu Nabii Samwel anasema,''Tafadhali,kamwite huyo.Tusikae kula chakula mpaka huyo afike''.

  Kwa hiyo utaona kwamba, imani ya Dini ni kwamba kiongozi anachaguliwa na Mwenyezi Mungu [halafu watu wenye hekima wanjaribu kuamua ni nani anafaa kuwa kiongozi, ni nani chaguo la Mungu]. Hiyo ndiyo Demokrasi. walio wengi wanataka huyu awe kiongozi;hawamtaki yule au yule au yule; yule ni mlevi,yule ni mwizi,yule ni fuska,wanamtaka huyu awe Rais, na huyu anakuwa Rais. Wewe una matatizo gani na njia hiyo ya kumchagua Rais?
   
 12. M

  Magezi JF-Expert Member

  #12
  Oct 7, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  mtoa thread ni mvivu wa kusoma
   
 13. B

  Babuyao JF-Expert Member

  #13
  Oct 7, 2009
  Joined: Jun 6, 2009
  Messages: 1,734
  Likes Received: 29
  Trophy Points: 145
  Chaguo la shetani ni yule anayejichukulia madaraka kwa mapinduzi. Anachukua madaraka kwa kulazimisha bila ridhaa ya watu. Kumbe ukubali usikubali yeye ni kiongozi wako. Huyo ni chaguo la shetani. Lakini anayechaguliwa na watu ni chaguo la Mungu. Walatini wana msemo usemao: vox populi vox Dei (sauti ya watu ni sauti ya Mungu)
   
 14. Mwana va Mutwa

  Mwana va Mutwa JF-Expert Member

  #14
  Oct 8, 2009
  Joined: Jun 9, 2009
  Messages: 429
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 35
  maelezo mengi yanayotolewa hapa na hasa yanayo nukuu vitabu vitakatifu yana maanisha kiongozi akishachaguliwa ndio anakuwa chaguo la Mungu,
  hata hivyo kwa kumbukumbu zangu hawa viongozi wa dini walisema nia chaguo la Mungu kabla hata uchaguzi haujafanyika[kama vile 1995 kakobe alivyomnadi mrema kuwa ni chaguo la Mungu,na akashindwa]
  kwahiyo nadhani majibu yangejikita kutueleza kilichowafanya hawa viongozi wapige kampeni kwa kutueleza kuwa alikuwa chaguo la Mungu?hatukatai akishachaguliwa kweli anakuwa chaguo la Mungu,
   
 15. Mungi

  Mungi JF Gold Member

  #15
  Jul 27, 2011
  Joined: Sep 23, 2010
  Messages: 16,985
  Likes Received: 441
  Trophy Points: 180
  Na Mwigamba | Tanzania Daima

  ALIYEKUWA Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye sasa ni Waziri wa Afrika Mashariki katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Samuel John Sitta, alipata kusema akiwa bungeni kwamba yeye ni mtu wa kufyatuka.

  Sikumbuki Sitta alikuwa akizungumzia nini siku hiyo lakini nilimshuhudia kwa macho na masikio yangu akiwa analalama kitu ambacho hakikumfurahisha na kusema kwamba "Sisi wengine ni watu wa kufyatuka".

  Sitta alisema maneno hayo baada ya muda fulani magazeti kumwandika kwamba anafyatuka sana.

  Kinachonipa shida ni kuona Sitta akisemwa semwa kwamba anawania urais wa 2015 na ingawa yeye mwenyewe hajatamka kama kweli anautaka lakini ni dhahiri amekuwa akisema na kutenda mambo ambayo yanadhihirisha kwamba anautaka urais.

  Swali moja tu na fupi ni ikiwa Watanzania tumefika kweli wakati wa kuongozwa na rais mfyatukaji.

  Hivi karibuni Sitta amefanya nimpe Rais Kikwete sifa ambayo sikuwahi kufikiria kumpa.

  Kwamba kwa kumtimua Sitta kwenye uspika wa Bunge akitumia rungu lake la uenyekiti wa CCM, Kikwete ana akili kuliko marais wengine wote waliopita waliopata kuliongoza taifa hili.

  Ndiyo maana mara kwa mara nimekuwa nikisisitiza kwamba sasa nimekubali Kikwete alikuwa ni chaguo la Mungu. Namwomba msamaha Baba Askofu ambaye mwaka 2005 alitamka wazi kwamba Kikwete ni chaguo la Mungu na mimi nikampinga kwa nguvu kubwa mno.

  Baadaye mwaka jana Baba Askofu alirudia tena kwamba Kikwete bado ni chaguo la Mungu, nikaandika makala kali sana kumlaani baba askofu yule.
  Kumbe sikumwelewa, huenda alimaanisha kwamba Kikwete kachaguliwa na Mungu kuja kuiondoa CCM madarakani na watanzania tupate ukombozi mpya ambao tunauhitaji sana kutoka kwa wakoloni weusi.

  Kikwete aliachwa na Mungu aaminiwe na Watanzania kupita kiasi na kisha aje avurunde kwenye uongozi wake kupita marais wote waliomtangulia.

  Hii matokeo yake ni kuwafanya Watanzania wasimwamini kiongozi yeyote toka katika CCM ambaye atautaka urais.

  Itaonekana wazi kwamba ni yale yale na hakuna jipya na kwamba kama Kikwete alishindwa pamoja na mbwembwe zote zile na mikwara mizito aliyoanza nayo, basi hakuna kiongozi yeyote toka miongoni mwa mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chini ya mfumo ule ule, atakayeweza kutukomboa Watanzania zaidi ya yeye pia kuliangamiza taifa kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi!

  Ni kutokana na ukweli huo kwamba Kikwete alitumwa na Mungu kuja kukiangamiza Chama Cha Mapinduzi na kukiondosha madarakani ndiyo maana Mwenyezi Mungu akamjalia akili ya ziada ambayo marais wenzake walioongoza chama kwenye mfumo wa vyama vingi hawakuwa nayo.

  Nasema hivi kwa sababu kimsingi CCM ilitakiwa kuwa imeng'oka madarakani toka mwaka 1995 wakati ambapo Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipoona kabisa kwamba chama hiki kimeoza na kinanuka rushwa na kuacha misingi yake.

  Mwalimu katika kitabu chake cha "Uongozi wetu na hatima ya Tanzania" alifikia kutamani kuwepo chama kingine mbadala cha upinzani ili kikabidhiwe nchi na kuing'oa CCM.

  Mwalimu aliyatamka maneno hayo akiwa tayari amekwisha kuzungumza na waandishi wa habari na kutamka bayana kwamba chama ambacho alikuwa akikiona kwamba kina sera nzuri na kitakachofaa kuchukua dola badala ya CCM ni CHADEMA.

  Nafasi ikatolewa kwa aliyekuwa rais na Mwenyekiti wa CCM wakati huo mzee Ali Hassan Mwinyi.

  Inasemekana yeye alikuwa na mtu wake aliyetaka amrithi na kuwa rais wa tatu wa Tanzania.

  Inasemekana pia kwamba Nyerere alimdokeza Mwinyi kupitia kwa Kawawa kwamba "Rashid, mwambie Ali kwamba kama jina la John na la Edward yanabaki kwenye orodha ya wanaotaka kuteuliwa na chama kuwa wagombea urais, kadi yangu hii hapa narudi Butiama".

  Ni tishio hili la Mwalimu ambalo inasadikika lilimtikisa mzee Ruksa na kumshawishi mgombea wake ajitoe.

  Kitendo hiki kikawakosesha Watanzania mabadiliko. Watanzania ambao elimu ya uraia bado hadi leo haijafikia kiwango hicho mpaka waweze kuchanganua mambo ya kisiasa na hatimaye kutoa kura yao kulingana na uchambuzi wao.

  Kama Mzee Ruksa angeng'ang'ana na mtu wake pengine Mwalimu angejitoa kwenye chama akajiunga na chama cha upinzani alichokipenda na hatimaye kumpigia debe mgombea urais wa chama cha upinzani na uwezekano wa kushinda ulikuwa mkubwa kama ambavyo alimpigia debe mgombea ubunge wa upinzani kwenye jimbo lake la Musoma Vijijini mwaka huo wa 1995 na akashinda kupitia NCCR.

  Mwaka 2005 ngoma ikahamia kwa Mkapa. Safari hii ni Kikwete na kundi lake ambao walikuwa wamejipanga kwa udi na uvumba kugombea urais. Kwa mara nyingine inasadikika kwamba Mkapa alikuwa na mtu wake aliyejipanga kuhakikisha anamrithi na kuwa rais wa nne wa Tanzania.

  Hata hivyo inasemekana mara hii Kikwete alijipanga vilivyo na kama nilivyodokeza hapo mwanzo Watanzania walifumbwa macho na kudhania kwamba Kikwete ndiye nabii aliyengojewa kuwakomboa.

  Wapo waliofikia kusema eti ni ‘tumaini lililorejea'. Mkapa inasemekana alitaka ‘kukomaa' mithili ya Moi na mrithi wake ili ampitishe hata kwa rungu la mwenyekiti.

  Habari zinasema wafuasi wa JK walijaa Dodoma na kumlima Mkapa ‘mkwara' kwamba asipopitisha jina la Kikwete watamshinikiza JK ahamie upinzani na wao watampigia kura akiwa huko na kushinda urais na asipokubali basi watampigia kura mgombea wa upinzani.
  Hilo likamtisha Mkapa na kukubali yaishe na hatimaye JK akawa rais kwa hasara ya Watanzania.

  Pengine Mkapa angekomaa na mtu wake JK angeogopa kuhamia upinzani mapema vile lakini Watanzania wangeweza kumchagua rais wa upinzani kwa ushawishi wa chini chini wa JK.

  Kwa mara nyingine Watanzania wakakosa mabadiliko kwa woga na kushindwa kutafakari kwa rais aliyekuwapo. Sasa ni zamu ya ‘Chaguo la Mungu'.

  Huyu hafanyi makosa ya kizembe na kitoto namna ile. Ni chaguo la Mungu na hivyo anatekeleza kwa ufasaha bila makosa kile alichotumwa na Mungu.

  Wakati wake huu kuna watu kadhaa wanaotaka urais kupitia chama chake. Lakini wakubwa wanaosemwa sana na wanaoonyesha kwa matendo ni wawili: Samuel Sitta a.k.a Speed & Standard ukipenda waweza kumwita mzee wa viwango pamoja na Mheshimiwa Edward Ngoyay Lowassa a.k.a Hard Decisions, ukipenda waweza kumwita mzee wa maamuzi magumu!

  Lakini napenda niwahakikishie kwamba kwa imani thabiti ya moyo wangu sioni kama kati yao kuna hata mmoja ambaye anatakiwa na JK awe mrithi wake.

  Matendo ya JK yanaonyesha wazi kwamba ana mtu wake mwingine kabisa na ndiyo maana akakubali Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu, jambo ambalo limempa kashfa nzito ambayo si rahisi kuisafisha leo ama miaka michache ijayo kisha apate urais mwaka 2015.

  Lakini hata kitendo cha rais ambaye ni mwenyekiti wa taifa wa chama kilicho madarakani kuwaruhusu vijana wa juzi kwenye siasa kama Nape Nnauye kupita kila mahali na kutangaza kwamba Lowassa ajivue gamba na kuachia ujumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya chama hicho, pia ni dalili kwamba hamtaki Lowassa kumrithi kwenye urais.

  Ni matukio hayo na kitendo cha kuteuliwa kwake kwenye Baraza la Mawaziri la JK ambavyo vimempa matumaini mapya mzee wa viwango na kudhani njia sasa ni nyeupe kwa yeye kwenda Ikulu.

  Kuna viashiria kadhaa lakini niseme tu kwa kifupi kwamba kulikuwa na mvutano kwenye uspika ambapo kundi la Lowassa liliutaka mwanzoni ikisemekana kupitia kwa Lowassa mwenyewe baadaye ikawa ni mwakilishi wake pacha mwenzake kwenye tuhuma dhidi ya ufisadi, Andrew Chenge, ‘mzee wa vijisenti.'

  Baada ya malumbano makali JK akaona hana jinsi isipokuwa kuwang'oa wote kwenye uspika na kuweka mwanamke.
  Lakini baada ya hapo ilitarajiwa sasa JK ata-balance kwa kuwateua wawakilishi wa makundi yote mawili kuingia kwenye baraza lake la mawaziri.

  Hakufanya hivyo. Kinyume chake aliwaacha wazee wa maamuzi magumu wote na kuchukua kadhaa kwa mzee wa viwango.

  Hakuishia hapo bali alikwenda mbali zaidi kwa kuwataka sasa wote wenye mwelekeo wa mzee wa maamuzi magumu kujiondoa kwenye nafasi zote za uongozi kwenye chama vinginevyo chama kitawafukuza.

  Hali ilivyo ni kwamba JK hatarudi nyuma kwa hili. Maana akirudi nyuma akaogopa wimbi la Mzee wa Maamuzi Magumu hataeleweka kwa watanzania.

  Wenzake walijitahidi kuwaepuka wasiotaka wawarithi lakini hawakuwachafua hadharani iwe ni kupitia serikalini ama kwenye chama.
  Yeye katangaza kashfa nzito kwa mzee wa maamuzi magumu na kumtaka ajiondoe kwenye chama. Ole wake JK baadaye aje ageuke na kudai "hakuna kama Lowassa" eti hajaona mfano wake.

  Ole wake baadaye aje atuambie kwamba eti Lowassa ni jembe la zamani linalostahili kupewa urais wa nchi hii!

  Itakuwa tiketi kwa JK kuikabidhi nchi kwa upinzani. Najua hatapenda hilo.

  Kwa upande mwingine wananchi tujiandae kama JK anataka Sitta awe mrithi wake tumkatae kwa nguvu zetu zote.

  Sitta hafai kabisa kuwa rais wa nchi hii. Huyu ni kiongozi wa maslahi. Majuma mawili yaliyopita nilieleza kwa kinagaubaga kilicho nyuma ya vita vya Sitta dhidi ya ufisadi.

  Nawashukuru sana waliowasiliana nami na kuniunga mkono juu ya Sitta. Lakini tumwangalie hivi karibuni tu alipoachiwa uwaziri mkuu kwa siku chache alivyofyatuka mara nyingi.

  Waziri Mkuu Pinda alikuwa safarini nje ya nchi kwa siku kadhaa akamkabidhi Sitta uongozi wa shughuli za serikali bungeni.

  Angalia alivyotumia nafasi hiyo kwa muda mfupi kufyatuka na kutoa ‘mafyongo' ndani na nje ya Bunge.

  Ni kama wasemavyo Waswahili kwamba ‘kichaa akikabidhiwa rungu atamtwanga mpaka aliyemkabidhi'.

  Kwanza alitafuta kila nafasi hata ya kulazimisha ili kumjibu Lowassa kauli yake ya kutaka serikali ifanye maamuzi magumu.

  Waziri mkuu unachukua dakika za bunge kurusha vijembe kwa masilahi yako binafsi?

  Akirusha vijembe hivyo akafyatuka na kusema kwamba wengine wanasema tufanye maamuzi magumu, maamuzi magumu hayana maana kama watu si waadilifu, wanaingia mikataba ya kitoto.

  Hii maana yake ilikuwa ni kumwambia Lowassa kwamba unasema sisi tumeshindwa kufanya maamuzi magumu wakati wewe si mwadilifu, umeingia mikataba mibovu.

  Hii si sahihi kwa kiongozi anayetarajiwa kuongoza nchi. Kikwete alikuwa sahihi kumfanya Sitta kuwa spika wa miaka mitano tu.
  Adam Sapi Mkwawa alikuwa spika tokea uhuru hadi 1994, miaka zaidi ya 30. Pius Msekwa aliyekuwa Naibu Spika wa Mkwawa akawa Spika tokea 1994 hadi 2005 miaka zaidi ya 10. Sitta kakaa miaka mitano tu.

  Uspika uliompa umaarufu akakaa nao miaka mitano tu. Wapo Watanzania waliolalamika sana lakini JK hakuwasikiliza, nami nakubaliana na JK.

  Sitta hakufaa kuendelea kuwa spika maana hafai. Ni mfyatukaji na anapenda sana kutumia rungu alilopewa pale maslahi yake yanapoguswa lakini akihakikishiwa maslahi kama alivyodanganywa kwamba atarejeshewa uspika anawaacha wananchi solemba kama alivyozima mjadala wa Richmond, naamini baada ya kuona dalili za rais kumuunga mkono yeye kurejea kwenye uspika.

  Lakini tatu Sitta alifyatuka pale alipowaita wapinzani wanafiki.

  Wapinzani na Sitta nani mnafiki kama si yeye anayetuhumiwa kwanza kutaka kugombea urais kupitia CCJ ambayo eti alitaka ijiunge na CHADEMA ili ipate nguvu lakini alipohakikishiwa kwamba uspika anarejeshewa, akajisalimisha tena CCM. Huyu ndiye mnafiki.

  Akiwa kule Mbeya kafyatuka tena na kuwadanganya watu kwamba eti wabunge wasafi kama yeye wametumwa na rais kuzunguka nchini kukisafisha chama.

  Kama kweli alitumwa alikuwa na haja gani kusema katumwa na rais. Mikakati yenu ya huko ndani hakuna kiongozi makini ambaye angeweza kuimwaga hadharani maana unamdhalilisha rais na mwenyekiti wako.

  Kwamba chama kimemshinda na yeye binafsi hana tena mvuto kwa wananchi mpaka akutume wewe kukirejeshea chama mvuto.

  Lakini pia Sitta alisema yeye ni mbunge asiye na maswali. Sitta, kiongozi makini hajisifii mwenyewe anasubiri kusifiwa kama ulivyoona kwa Dk. Slaa na kwa kawaida husubiri hata watu ndo wamwambie agombee urais kama Slaa alivyoombwa huku yeye akiwa hataki.

  Si wewe kujipigia debe kwamba ni msafi na kuutafuta urais kwa nguvu. Halafu una maswali mengi mno ya kujibu.

  Kwanza kuna ufisadi uliripotiwa ofisini kwako ukiwa spika mpaka leo hujautolea majibu wakati uliahidi kwamba CAG atakagua na kutoa taarifa.

  Halafu umeishi kwenye nyumba ya kukodi kwa dola za Marekani 8000 muda wote ulipokuwa spika na umeendelea kuishi humo hadi leo ingawa wewe si spika hivi sasa.

  Kiasi hicho cha fedha ni sawa na shilingi milioni 12 za Tanzania kwa mwezi.

  Nimalizie kwa kusema sijawahi kusikia waziri akiiponda serikali anayoitumikia halafu akabaki kuwa waziri.

  Aliyeweka rekodi ni Mrema Lyatonga lakini alilazimika kuachia ngazi mara moja kwa kukosa uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility).

  Sitta kaponda serikali anayoitumikia wazi wazi na hana mpango wa kujiuzulu.

  Huyu ni kiongozi kweli anayetafuta kukwea kuelekea kwenye urais kwa kukata mpaka tawi alilolikanyaga ili apande!

  Kikwete shikilia msimamo wako wa kumkataa Lowassa asigombee urais na Watanzania shikilieni msimamo wa kukataa chaguo la Kikwete la watu kama akina Sitta kwenye urais.

  Hilo litaiepusha nchi na makuwadi wa uchumi wa nchi hii na kupata rais mbadala kutoka upinzani kwa mabadiliko ya kweli.
   
 16. DOUGLAS SALLU

  DOUGLAS SALLU JF-Expert Member

  #16
  Jul 27, 2011
  Joined: Nov 13, 2009
  Messages: 11,593
  Likes Received: 4,703
  Trophy Points: 280
  Kumbe Jakaya Mrisho Kikwete ndiye Mikhail Gorbachev wa CCM, safi sana, nampa tano kwa kazi anayoifanya kwa ari zaidi,nguvu zaidi na kasi zaidi, kwaheri CCM.
   
 17. Jumakidogo

  Jumakidogo R I P

  #17
  Nov 25, 2011
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 1,859
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Viongozi wa dini walipata wapi mamlaka ya kutangaza hadharani kuwa JK ni chaguo la Mungu wakati ule wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Kama ni kweli Mungu alihusika, basi alikosea. Ama kama hakukosea basi huenda watanzania tunayo madhambi makubwa hivyo alimchagua JK kwa ajili ya kutoa adhabu hiyo badala yake. Vinginevyo wale wote walitangaza hadharani kuwa JK ni chaguo la Mungu wajitokeze kufuta kauli zao ama walete maandiko kutoka katika vitabu vyao wanavyoviamini watunyeshe aya hiyo. Au, watuambie huyo ni Mungu yupi?
   
 18. m

  mhondo JF-Expert Member

  #18
  Nov 25, 2011
  Joined: Apr 23, 2011
  Messages: 970
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 45
  Ni kweli kabisa. Nakuunga mkono.
   
 19. Ndallo

  Ndallo JF-Expert Member

  #19
  Nov 25, 2011
  Joined: Oct 1, 2010
  Messages: 7,136
  Likes Received: 1,088
  Trophy Points: 280
  Naona hao viongozi wa dini walikosea kulidhalilisha jina la Mungu na ndio maana hii laana tunaipata!
   
 20. palalisote

  palalisote JF-Expert Member

  #20
  Nov 25, 2011
  Joined: Aug 4, 2010
  Messages: 8,352
  Likes Received: 37
  Trophy Points: 0
  watakuja na kutuambia huyo ni Mungu wa shedrack na abednego
   
Loading...