Inauma, inasikitisha, inakera sana, na inafikirisha sana kuona viatu vinakupwaya lakini unajipa matumaini ya kuendelea na Safari ya Uongozi

SANCTUS ANACLETUS

JF-Expert Member
Mar 5, 2016
3,263
2,000
Ni ukweli uliokuwa wazi kuwa hata kabla ya yeye kushika wadhifa huo wa juu wa Nchi watu wengi hawakuwahi kuutambua uwezo wake. Uwezo ni jambo ambalo huwezi kuuficha mithili ya Sindano kwenye Koti. Mungu wetu angalikuwa wa ajabu sana kwa uwezo wake mkuu alionao kama angaliumba wanadamu halafu uwezo wao ukafikichika halafu kisha akatutaka tuongazane. Tungaliongozana vipi kama uwezo wa kila mmoja wetu ungalikuwa umefichika?

Uwezo wa mwanadamu uko wazi. Uwezo wa kufikiri,kutenda,kuamua, kusaidia. Huo uko wazi wazi. Unasomeka waziwazi. Uwezo wa kuongoza wengine ni tabia na Sifa ambazo toka kuumbwa mwanadau Mungu anauweka hadharani. Ni kama tabia ya Ucheshi, Upole, Ukali, moyo wa kusaidia, Moyo wa huruma na moyo wa Ibada na Sifa zinginezo zilivyo wazi kupitia macho,kutembea kwa mtu, kuongea kwa mtu, kusikiliza kwa mtu, kula kwa mtu,kuvaa kwa mtu na kadhalika.

Kama nilivyotangulia kusema awali, watu wengi ndani na nje ya chama chake hawakuwahi kukunwa na utendaji wake licha ya kwamba alifanikiwa kushika Nyadhifa kadhaa huko nyuma kwa upande wa pili wa Nchi yetu. Na hata alipoingia kiwadhifa upande huu wa Nchi bado watu hawakuwahi kukunwa na utendaji wake kiasi cha kufikiria kuwa tunaweza kufikiria kumpa kazi ya kutuongoza katika nafasi nzito kama hii ya sasa. Wanaomjua vizuri ndani ya Chama wanakueleza kuwa ndio maana hata mwaka 2015 hakuwa miongoni mwa waliotia nia ya kugombea Uongozi wa juu wa Nchi kwa sababu hata yeye aliamini hana uwezo huo. Ni kwa sababu hata yeye mwenyewe alijua toka sakafu ya moyo wake kuwa Viatu vya Nchi yetu kwa mazingira ya sasa na yajayo vinampwaya. Ilikuwaje basi akateuliwa kuwa Msaidizi wa Mvaa viatu Mkuu wakati ule?Swali hilo sio sehemu ya mjadala wa leo bali siku nyingine.

Basi,imeshatokea yaliyotokea na hakukuwa na namna ya kufanya Zaidi ya kuangalia Katiba yetu inasemaje, Ilitarajiwa basi kwa kujitambua kuwa hata wale waliokwisha kufanya naye kazi wanamjua kuwa uwezo wake sio wa kutisha na wa kuvutia, angalivaa uungwana wa kusema ngoja mimi nishike tu mpaka mwisho wa Muhula wa Kikatiba na kisha nisimamie mchakato wa kumpata mtu mwingine mwenye uwezo sawia au zaidi ya yule ambaye nimeziba pengo lake. Kinyume chake na kwa mshangao mkubwa, tumesikia tu anajitangaza kuwa ATAGOMBEA ifikapo Mwaka 2025! Na la kushangaza Zaidi hajasema kuwa ataruhusu na wengine nao wagombee ili kushindanisha Sifa na uwezo wa kiuongozi kama ilivyotokea kwa yule aliyeziba pengo lake.

Kingine cha kushangaza Zaidi, amesema atatumia BAHATI HIYO ALIYOPEWA NA “MUNGU” (yeye anaiita bahati toka kwa Mungu kwa mwenzie kufa na yeye kisha kurithi utawala) kuhakikisha wanawake nao sasa wanatawala Nchi rasmi kwa kuchaguliwa kwa kura ili kuonyesha kuwa nao wanao uwezo wa kuongoza Nchi. Ilitarajiwa kuwa kama anaridhika kuwa kweli wanawake wanao uwezo wa kutuongoza (na kweli wapo wanawake wenye uwezo) angalisema wakati anajitangaza kuwa mchakato wa kugombea uongozi wa Nchi hapo mwaka 2025 katika Chama chake utahusisha wanawake wengine pia na yeye akiwemo.

Kilele cha kushangaza lakini ukiwa ndio ukweli ambao mtaani unajulikana kwa kila Mtanzania aliye hai (bila hata kuhitaji mashine kama CT SCAN kuchunguza uwezo wake) yeye mwenyewe ameutangazia ulimwengu na Taifa kwa ujumla kuwa viatu vya Mtangulizi wake VINAPWAYA SANA! Huu ni ndio ukweli. Ukimuuliza mtu yeyote mtaani hata wale wanaotafuta kuteuliwa au wale wanaomsaidia ili waweze kupata ujira wao kutoka kwenye sakafu ya mioyo yao watakueleza kuwa uwezo wake ni wa kawaida sana kulinganisha na nafasi alionao.

Kwa hiyo, Bandiko hili nimelenga kukiuliza maswali ya msingi sana Chama chake. Ni muhimu chake kijitokeze kujibu maswali haya kwa faida ya taifa letu na kizazi kijacho. Na bandiko hili ninakaribisha pia maswali mengine yaulizwe dhidi ya Chama chake. Na Zaidi, vile vyombo vinavyohusika na masuala ya Uchaguzi, maswali haya yasipojibiwa na Chama husika na wasipoghairisha uamuzi wake huo, watoke watuthibitishie kuwa ikiwa atapitishwa na Chama chake kugombea bila kushindanishwa na wengine na akanyimwa kura (na watanzania wengi ambao mpaka sasa hawaamini uwezo wake na wala hawapendi kuona mtu kama huyo akipata tena miaka mitano) watamtangaza bila woga mtanzania tofauti na yeye toka Vyama vingine atakayekuwa ameaminiwa kwa uwezo wake?

SASA hebu tuuulizane. Hivi, Chama cha Mapinduzi,CCM:
1. Mlipofanya tathimini baada ya uchaguzi wa Mwaka 2010 na kuamua chama kijisafishe kwa kuwaondoa waliokuwa wanakichafua Chama na matokeo yake ikawa ni kuondolewa kwa akina Lowasa na Mafisadi wengine chamani na matokeo ikawa ni Marehemu Magufuli kukibeba Chama, kabla ya uchaguzi wa Mwaka 2025 mtafanya tathimini tena kuona jinsi halisi kabisa ya jinsi uchaguzi wa Mwaka jana mlivyoshinda au mlivyoshindwa?

2. CCM ikiwa mtafanya tathimini ya ukweli kabisa na kugundua kuwa pamoja na kwamba Marehemu Magufuli alikuwa na uwezo mkubwa sana kiuongozi,kimaono na Kifalsafa (viatu vilikuwa vinamtosha) na aliwafanyia watanzania mambo mengi na makubwa vile kwa muda mfupi lakini bado alihenyeshwa sana na wapinzani, je, huyu mgombea wenu anayetarajia kuwa peke yake chamani (au aliyekwisha kujitangaza kuwa mgombea) ataweza kweli kukivusha Chama kwenye Uchaguzi huo wa mwaka 2025?

3. CCM, kwa kuwa mgombea wenu mwenyewe akiwa na sound Mind amekiri kuwa “Viatu” vya Marehemu Raisi Magufuli vinampwaya anataka kugombea hapo mwaka 2025 ili kufanya nini hasa ikiwa anakiri hadharani kuwa spidi aliyokuwa amelionyesha Taifa letu Marehemu raisi Magufuli kuwa ndio spidi ambayo watanzania wanahitaji kuwa nayo kimaendeleo Na yeye haimudu?

4. CCM, mnapoongea juu ya Chama mnakuwa mnamaanisha nini hasa? Je, chama chenu siku hizi chama ni mwenyekiti au wanachama?

5. Hivi, CCM kwenye Chama chenu Mwenyekiti maana yake ni nini? Ni muongoza wanachama au kufikia kutoa maamzi au yeye ni mtoa maamuzi wa mwisho na tena bila Vikao na akishasema jambo hapingiwi kama jambo lenyewe haliko sawa?

6. Je, Mwenyekiti wenu mlienza kusema hatakiwi kupingwa ndani ya Chama mwaka 2025, kwa misingi ya kwamba wanachama wote ndani ya Chama wana haki sawa, mnaweza kuitisha Mkutano maalumu na kumuuliza ni kwa nini ametangaza kugombea uraisi kabla ya muda? Ni kwa nini mumekaa Kimya bila kumuita kwenye kamati ya maadili ili kumuhoji sababu za kujitangaza ilhali chama hakijaanza mchakato wa ndani wa uchaguzi wa mwaka 2025?

7. Je, CCM hivi na wanachama wengine wa chama chenu wakianza kusimama huko majimboni na kujitangaza kugombea Ubunge na udiwani mtakaa kimya kama mlivyokaa kimya kwa huyu Mgombea wenu pekee wa Raisi?

8. Hivi, CCM Mtu anayejitangaza kuwa ni mgombea anayetaka kuonyesha kuwa wanawake wanaweza ila tu kwa muda mrefu wanaume ndo wamewakandamiza, anawezaje wakati huo huo tena kusimama na kusema uwezo wake haulingani kabisa na wa Raisi ambaye alilinyanyau Taifa letu na Chama chenu angalau kuweza kupewa kura na watanzania kwa sababu watu walikuwa wanamuamini yeye na sio Chama?

9. Mhe. Pole Pole, Katibu Mwenezi wa zamani wa CCM, unayeendesha Shule ya Uongozi(na nikiri napenda Falsafa yako juu ya maendeleo ya Nchi yetu kutegemea rasilimali za Nchi kuliko kuamini kuwa tunaweza kuendelea kwa kubeba mabakuli ya misaada) unaweza kujitokeza katika vipindi vyako vijavyo vya shule ya Uongozi kuchambua kasumba na tabia hii ya Mwanachama Mwenzako kujitangaza yeye mwenyewe kuwa anao uwezo badala ya Chama kumuona kuwa anao uwezo?Je, ukiwa utaogopa kufanya hivyo, Uongozi na Falsafa yako ya kusema Ukweli daima, itakuwa bado na maana na unadhani wanachama wenzio watastahili kuendelea na kuyaamini bado hayo mavipindi yako?

10. CCM, itakuwa ni nidhamu au ndio heshima kwa kuogopa kumuita Mwanachama wenu kumuuliza ni kwa nini amekiuka Taratibu, Miiko na kanuni za Chama kwa kujitangaza mapema kama Mgombea Mwanamke ilhali alishawazuia wanachama wengine kuacha mara moja kuhangaika na jambo hilo kabla ya muda wake?

11. Katibu Mkuu wa CCM,Komredi Daniel Chongolo kama mtunza Dira, Falsafa na Maono ya Chama wakati ule marehemu Holace Kolimba aliposema Chama chenu kilikuwa kimepoteza dira aliitwa Dodoma kujieleza, wewe kwa nafasi yako ya mchora Falsafa ya Chama umekusudia kuchukua hatua gani dhidi ya mwanachama wako aliyejitangaza mgombea wa Uraisi mwaka 2025 kabla Chama hakijakaa na kuruhusu wanachama kuanza kujitangaza?Je, Ukishindwa kuchukua hatua kama zile ulizoelekeza dhidi ya wale wanachama ulioelekeza vikao vya maadili viwajadili kwa kile kilichoonekana kukosa maadili utakuwa bado unaonekana kama Katibu wa Chama mwenye dhamana ya kulinda na kutetea Falsafa,Itikadi, sera, miongozo na maono ya Chama kwa Ujumla?

12. Katibu Mkuu wa Chama, Komredi Chongolo, kwa kuwa tumezoea Kila awamu ya Uongozi wa nchi yetu kupitia Chama chenu, kutanguliwa na uchaguzi au mchujo wa wagombea na kisha awamu ya pili ndio mhusika aliyepeperusha Bendera ya Chama chenu kuwa mgombea pekee wa Chama chenu kama ilivyotokea kwa Maraisi Mwinyi, Mkapa, Kikwete, na hatimaye Raisi Magufuli, je, mtaelekeza mgombea wenu mwaka 2025 agombee baada ya kushindanishwa na wenzie chamani kwa sababu bila kufanya hivyo atakuwa ni mgombea ambaye ataweka historia ya kugombea bila kutoka jasho kama wenzie? Je, Mkimruhsu agombee awamu ya pili bila kushindanishwa uwezo na wenzie chamani hamuoni kuwa mtakuwa mmetunga kanuni na muongozo mpya kuwa ikitokea mtu amerithi nafasi ya marehemu katika nafasi ya uraisi, basi anakuwa amepata mteremko kutawala?

13. CCM, Chama cha Mapinduzi ile ahadi yenu ya kuwaletea watanzania wagombea wenye uwezo wanaopatikana kwa kushidanishwa uwezo mnaelekea kuitelekeza na badala yake hamuoni kama mnaelekea kuasisi aina ya Uongozi wa mtelemko au Uongozi Dezo,yaani uongozi wa wanachama wenu labda kufikia kuwa anaomba Dua ili kiongozi aliye juu yake afe ili achukue madaraka kiulaini kwa kuamini awamu inayofuata atagombea peke yake?

14. CCM, mgombea wenu huyu ikiwa atakuwa wa pekee, mumefanya utafiti mtaani ni kweli anachagulika? Ni mgombea ambaye akishindanishwa na vyama vingine makini mnaweza kusema kwa dhati kuwa kweli atatoboa kabla hata Jogoo hajawika?Ni kwa nini hamumuelezi ukweli kuwa hachaguliki?

15. CCM, mgombea wenu ikiwa atagombea ndani ya chama chenu pekee, akitegemea wanawake wenzie kumbeba, anafahamu kuwa ni wanawake hao hao ambao hawampendi na wanamsema vibaya huku mitaani?

16. CCM, ni kwa nini Mgombea wenu hakujitokeza wakati Marehemu Magufuli yupo hai kutangaza hadharani kuwa angegomembea ifikapo mwaka 2025 ili kudhihirisha kuwa wanawake wakiongozwa na yeye wanao uwezo kwa kuliongoza Taifa hili? Alikuwa anaogopa nini? Kwa nini alificha nia hiyo? Je, Kiongozi anayejiamini anastahili kuficha Nia yake njema katika kuwaonyesha watu wake kuwa anataka kuwapeleka hatua Fulani kimaedeleo au Kiongozi anayejiamini anastahili kutaka kuongoza kwa kuvizia au kunyatianyatia na kujifichajificha?

Itoshe basi. Nimehoji sana na hata nikisema niendelee sitamaliza. Nina maswali mengi sana juu ya Chama chenu na mienendo yenu juu ya jinsi wanachama wenu mnavyokusudia wapatikane kuanzia sasa.Hii Nchi ni yetu sote. Mungu hajawahi kuandika Memorandumu of Understanding na Chama cha Mapinduzi kuwa ninyi ndo muvae pekee nira ya Kuwaletea watanzania maendeleo. Na wala Mungu hajawahi kuufanya Uongozi wa viumbe wake sisi kama fashion. Yeye mwenyewe kupitia mwanaye Yesu Kristu, Mungu kweli kutoka kwa Mungu, hakupata kuridhia nafasi yoyote ya Kiuongozi kwa yoyote yule kujitangazia Uongozi wa Kondoo wake bali yeye mwenyewe aliwaweka wale aliowaona wanafaa na ni mfano huo huo aliotuachia sisi Wakristu na wanadamu wote kupitia Kanisa lake Takatifu na ndio maana hakuna Kasisi au Askofu wa Kanisa lake Takatifu anajiteua katika nafasi yoyote bali anaombewa kuwa Kiongozi katika Kanisa. Tabia hii ya kujisimika madarakani na huku wakati huo huo mkikiri kuwa uwezo wenu ni wa kawaida muiache. Tanzania sasa sio uwanja wa watu kuhitaji kuongoza ilhali wanaamini hawana uwezo unaolingana na matarajio ya wapiga kura.

Basi, kwa hapa nitamatishe kwa kuwaomba wasomaji tuendelee kuwahoji wana-CCM wana mpango gani na Taifa hili kwa kuruhusu misingi ya Chama chao kukiukwa waziwazi na baadhi ya wanachama ilhali wengine hawapumui pale wanapoaminika kuikiuka misingi hiyo hiyo?
 

luangalila

JF-Expert Member
Jan 12, 2014
4,313
2,000
Uma malalamiko mengiii kwan umeambiwa ata tawala milele ? Utafika muda wake ataondoka ata waachie wengine
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom