IMF yasema walioiba BoT washughulikiwe haraka

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,004
Posted Date::2/28/2008
IMF yataka mafisadi wabanwe
*Yasema walioiba BoT washughulikiwe haraka

* Yaibua machungu ya umeme kwa Watanzania

* Wahoji athari za gharama za umeme nchini

* Wafanyabiashara wadai zinawakandamiza

Tausi Mbowe na John Stephen
Mwananchi

SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF), limesema kuwa limeridhika na hatua zilizochukuliwa na Serikali, jinsi ilivyoshughulikia ufisadi wa Sh133 bilioni katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuitaka serikali kutochukua muda mrefu kuwashughulikia watu wote waliohusika katika kashfa hiyo.

Ukaguzi wa tuhuma za ufisadi katika benki hiyo, zilifanywa na Kampuni ya Ernst& Young katika Akaunti za Malipo ya Nje (EPA) na kubaini upotevu wa kiasi hicho ambacho kililipwa katika makampuni mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano na viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali, akiwemo Waziri wa Mipango na Fedha, Mustafa Mkullo, Gavana wa BoT, Prof Beno Ndullu na Mkaguzi wa Mahesabu ya Serikali, Lodovick Utouh, Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Ambroise Fayolle alisema shirika lake limepokea hatua hizo vizuri na linataka hatua zaidi zichukuliwe.

Fayolle aliitaka serikali kutochukua muda mrefu kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi wa fedha za EPA.

Akizungumzia kilimo, alisema IMF inaliangalia kilimo kama sekta muhimu na kwamba benki hiyo imekuwa ikitoa pesa katika sekta ya uchumi ambayo inajumuisha kilimo.

Afisa mwingine wa IMF, Peter Gakunu alisema, Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zinazokabiliwa na changamoto katika sekta ya kilimo na kwamba shirika hilo limekuwa likiangalia jinsi ya kuwawezesha wakulima kupitia misaada yake kwa sababu asilimia 80 ya wananchi wake ni wakulima.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkullo aliwaeleza wakurugenzi hao juhudi zilizofanywa na serikali katika kushughulikia tuhuma za ufisadi BoT na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu wanaohusika na wizi huo.

Mkurugenzi natumaini una taarifa za tuhuma za wizi uliotokea BoT miaka miwili iliyopita, na kuondolewa kwa gavana wa zamani na kuteuliwa mwingine, kuundwa kwa kikosi kazi na kuteuliwa kwa bodi mpya katika benki hiyo, alisema Mkullo.

Katika hatua nyingine, ujumbe huo wa IMF ulifanya kikao na watendaji wa sekta binafsi na asasi za kiraia ambako waliibua upya machungu ya kupanda kwa gharama za umeme baada ya kuwahoji wadau hao kama kuna athari zozote zinazosababishwa na upatikanaji wa nishati hiyo.

Ujumbe huo ambao unawajumuisha wakurugenzi wa shirika hilo uliuliza swali hilo wakati wa mkutano wao na viongozi wa ngazi za juu wa sekta binafsi na Muungano wa Asasi za Kiraia jijini Dar es Salaam jana.

Kufuatia swali hilo, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa Shirikisho la Wafanyabiashara Tanzania (CTI), Hussein Kamote alisema tatizo kubwa kwa Tanzania ni kwamba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeshindwa kudhibiti kukatika kwa umeme, hivyo kusababisha uzalishaji wa viwanda vyao kuwa wa mashaka na gharama kubwa.

Alifahamisha kuwa, pamoja na kutokuwa na umeme wa uhakika na kupanda kwa gharama za umeme kumesababisha uzalishaji kuzorota katika sekta ya viwanda.

"Umeme wetu umekuwa si wa uhakikika, unakatika bila taarifa wakati shughuli za uzalishaji zikiendelea jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kuizoretesha sekta yetu," alisema na kutoa mfano wa Kiwanda cha Saruji kinavyoathirika kwa kiasi kikubwa.

"Unapokuwa kwenye utaratibu wa kuandaa bidhaa na kuingiza malighafi katika mashine ghafla umeme unakatika, hivyo mali yote inabidi kutolewa kwa kuwa haifai tena kwa ajili ya uzalishaji na kusababisha hasara kubwa kwa kiwanda," alisisitiza.

Sambamba na hilo, Kamote alisema tatizo la kupanda wa kwa gharama za umeme mara kwa mara umekuwa kukiathiri sekta hiyo kwa kiasi kubwa.

Alisema kwa mwaka jana pekee utafiti uliofanywa na sekta hiyo uligundua kuwa kuna ongezeko la hasara kati ya asilimia 20 hadi 25 katika sekta hiyo, iliyosababishwa na kupanda kwa gharama za umeme.

Aliitaka serikali kutafuta ufumbuzi wa kuongezeka kwa gharama za umeme ili kuiwezesha sekta ya viwanda nchini kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Taifa, Ester Mkwizu alisema kwa sasa juhudi zinafanywa kwa kushirikiana na serikali ili kutafuta njia ya kupunguza gharama za umeme na kwamba wana matumaini kuwa nishati hiyo itapatikana kwa bei rahisi.

Alisema kuongezeka kwa gharama za umeme kunaathiri shughuli za usindikaji wa mazao ambayo yangeweza kuuzwa Afrika na sehemu nyingine za nje ya nchi na kuwaongezea wakulima kipato.

Wakurugenzi hao pia walisema mfumo wa sheria huchagia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maedeleo ya sekta hiyo na kutoa mfano wa Mahakama ya Biashara kwamba ada zao ni kubwa, ikiwemo ya kufungua kesi.

Jana jioni ujumbe huo wa IMF ulikutana na Waziri wa Mipango na Fedha, Mustapha Mkullo.
 
Back
Top Bottom