Imani za kishirikina zinapogubika chaguzi na uongozi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Imani za kishirikina zinapogubika chaguzi na uongozi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Dr. Chapa Kiuno, Nov 13, 2009.

 1. Dr. Chapa Kiuno

  Dr. Chapa Kiuno JF-Expert Member

  #1
  Nov 13, 2009
  Joined: Sep 11, 2009
  Messages: 445
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0


  [​IMG]
  Joseph Mihangwa​
  [​IMG]

  IMANI za kishirikina kutawala nyakati za chaguzi za kuwania nafasi za kisiasa na uongozi, sasa limekuwa jambo la kawaida lisilotisha wala kuonea aibu miongoni mwa wagombea.
  Waganga wa jadi, wapiga ramli na wanajimu, wamekiri hilo wakisema kuwa kipindi hicho ni cha mavuno kwao ambapo wagombea hupigana vikumbo kujaribu kuangalia hatima ya harakati zao, kwa hofu na mashaka ya kutojiamini.
  Jambo hili si la kinadharia tena. Huko Tanga, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2005, wagombea ubunge kadhaa walikutwa kwa mganga wa jadi wakimnyonyofoa kuku hai manyoya, huku wakitamka maneno fulani fulani ya kukariri [incarcatations] waliyofundishwa na mganga huyo, tukio lililohusishwa na imani za kishirikina.
  Mwaka huo huo, huko Geita, Mkoani Mwanza, wagombea uongozi watarajiwa kadhaa, walikurupushwa na Sungusungu kwa mganga wa jadi wakiwa nusu uchi, wakatimka mbio za mkurupuko na kutokomea vichakani kuficha aibu ya kukutwa katika hali hiyo.
  Na kama tutakavyoona baadaye katika makala haya, tarehe za Uchaguzi Mkuu wa 2005, zilibadilishwa mara mbili kupata siku “mwafaka”, kitendo ambacho kinahusishwa na wengi na imani za kishirikina.
  Hata baada ya uchaguzi kumalizika na wabunge kuchukua nafasi zao, inadaiwa kuwa, mbunge mmoja alinaswa na kamera za ukumbi wa Bunge akiganga usiku bungeni baada ya kikao cha Bunge cha siku hiyo, pengine kwa lengo la kuimarisha nafasi na mambo yake bungeni.
  Haya ni matukio machache tu kati ya mengi kuonyesha kwamba imani za kishirikina zimekuwa sehemu ya utamaduni katika kuwania na kulinda nafasi za uongozi kwa viongozi.
  Moja ya madhara yatokanayo na imani za kishirikina hapa nchini ni lile wimbi la mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi [albino], ambalo Serikali imeapa kulipiga vita kwa nguvu na silaha zote ilizo nazo ghalani.
  Lakini, inapokuwa kwamba viongozi na watunga sheria na sera za nchi hii, wao wenyewe ndio waumini wa ushirikina, Serikali itapata wapi ubavu kupiga vita imani hizo? Pengine ni kwa sababu hii vikongwe na albino wameendelea, na wataendelea kuuawa na Serikali ipo na vyombo vyake vya dola.
  Kwa waumini wa biashara ya ushirikina, hakuna kisichowezekana isipokuwa kwa nguvu ya giza; kwao rushwa pekee haitoshi kuokoa jahazi, bali hiyo ni nyenzo ndogo tu ndani ya injini kuu ya ushirikina.
  Historia imejaa mifano mingi hai ya watawala kujihusisha na imani za kishirikina zenye hatima ya maangamizi kwao na kwa jamii. William Shakespeare, Mwandishi mahiri wa Uingereza, anatuhabarisha katika kitabu chake “Macbeth” juu ya Jemedari mmoja wa Jeshi la Scotland [1500], Macbeth, ambaye wakati anarejea kutoka uwanja wa vita, alikoyasambaratisha majeshi ya waasi, akiwa na mpiganaji mwenzie, Banquo, alisimamishwa na vibibi vizee “vichawi” vitatu [weird sisters], vikamtabiria kuwa angekuwa “Mfalme baada ya hapa na baadaye”.
  Na kuhusu Banquo, vibibi hivyo vilimwambia kuwa, ingawa alikuwa mdogo kwa Macbeth, lakini angekuwa mkuu zaidi kwa sababu watoto wake wangekuwa wafalme ingawa yeye asingekuwa.
  Utabiri huu uliibua tamaa ya Macbeth ya kutawala; na wakati huo huo wakamtia hofu ya kupokonywa utawala na watoto wa Banquo, na hivyo akaamua kumuua Banquo ili kujisafishia njia.
  Kikwazo kilichobaki kwa Macbeth baada ya kumuua Banquo, alikuwa mtawala madarakani, Mfalme Duncan. Kwa hiyo alimwalika kwa chakula cha usiku nyumbani kwake naye Duncan akakubali, na kwa ushawishi wa mkewe [mama Macbeth] Mfalme alikubali kulala kwa Jemedari wake baada ya tafrija.
  Na ili kutimiza ndoto yake, na kwa kujasirishwa na Mama Macbeth, Macbeth alimuua Mfalme wake kwa upanga usingizini na kujivika taji la utawala, ili utabiri wa wachawi wake utimie.
  Lakini, kama ilivyonenwa na wahenga, kwamba, kilichopatikana kwa upanga lazima kilindwe kwa upanga, na kwamba “auaye kwa upanga atakufa kwa upanga”, ndivyo utawala na kifo cha Macbeth kilivyokuja hima.
  Lakini ni tofauti kidogo kwa Julius Caezar [Siza], mtawala wa Rumi ya kale, ambaye Shakespeare, katika kitabu chake kingine kiitwacho “Julius Caezar” anamuonyesha mtawala huyo jasiri kama ntu mwenye kuamini na kutoamini ushirikina, lakini, hasa hasa ujasiri ndio uliotawala maisha yake. Hebu tuone kwa kifupi tu jinsi Shakespeare anavyomwomnyesha Caezar, pale wahasimu wake wa kisiasa [Marcus Britus, Cassius, Casea, Trebonius, Ligarius, Decius Brutus, Cimber na Cinna] walipopania kumuua:
  Caezar [kwa mpiga ramli]: “Una habari gani za kunambia? Sema tena”. Naye mpiga ramli anamuonya Caezar, “Jihadhari na tarehe za katikati ya Machi”; lakini Caezar anampuuza akisema, “Ni mwota ndoto; na tumwache”.
  Lakini mmoja wa wauaji wa Caezar, Brutus, alishafahamu kwamba mtawala huyo alikwishakubali ushirikina, kwani siku waliyopanga kumuuwa alikuwa na wasiwasi kama Caezar atatokea, alisema: “Sijui kama Caezar atatokea [ili tummalize], kwa sababu siku hizi kajawa ushirikina, kaiacha imani yake ya zamani”.
  Na usiku huo Caezar alisumbuliwa na ndoto mbaya, anasema: “Mara tatu [nimeita] mke wangu Calpurnia kalia usingizini yala! Yala! Wanamuua Caezar. Nenda ukawaambie watabiri watambike na waniletee mawazo yao ya matokeo”.
  Na mawazo ya watabiri yalisema: “Caezar asijaribu kutoka nyumbani leo [15 March]; mhanga tuliopasua ulikuwa bila moyo ….. akifanya hivyo atakufa”.
  Ni ujasiru tu Caezar unaovuka mipaka ya ushirikina unaofanya atoke nje, anasema: “Nini chaweza kuepukwa ambacho kimedhamiriwa na miungu wenye enzi? Woga hufa mara nyingi kabla ya vifo vyao; mashujaa hawaonji kifo ila mara moja……… Hatari yajua wazi kwamba Caezar ni hatari kali kuzidi hatari; na Caezar atatoka nje”.
  Licha ya kutahadharishwa kwa mara nyingine na mtabiri wake, mke wake na wapendwa wake wengine, kwamba asitoke nje Machi 15; Caezar alipuuza, akatoka kwenda kukutana na wafitini hao waliomwasi, bila kujua nia yao mbovu; akauawa sawia.
  Kama utabiri wa mtabiri wa Caezar ulikuwa wa kweli, au kama lilikuwa ni jambo la kubahatisha na kubabaisha tu, kama la “mwota ndoto”, na kama Caezar mwenyewe alivyosema mwanzo, ni jambo linalozua maswali mengi kuliko majibu kwa jamii za kale na jamii yetu ya sasa juu ya imani za kishirikina.
  Mtabiri wa Ufaransa, Michelle Nostra Damus, aliyezaliwa mwaka 1503, naye ametokea kuichanganya dunia ya washirikina na ushirikina. Yeye alitabiri kwa usahihi kabisa juu ya Mapinduzi maarufu ya Ufaransa ya 1789 dhidi ya Serikali ya Kimwinyi ya Mfalme Louis wa XVI, miaka 160 kabla ya mapinduzi; na jinsi yalivyotokea, na juu ya Louis na mkewe Marie Anttoinete kukamatwa wakitoroka na kurejeshwa Paris, wakanyongwa.
  Nostra Damus alitabiri pia kwa usahihi kabisa, vita vya Napoleon [1795 – 1815] kufuatia mapinduzi ya 1789; na kuzaliwa kwa Adolf Hitler, dikteta wa Ujerumani; na jinsi alivyozua vita ya pili ya Dunia. Vivyo hivyo, alitabiri kwa usahihi mno kuuawa kwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy, kwa kutaja kwa usahihi siku, na mahali: “Texas, Novemba 22, 1963”, mtu aliyemuuwa akiwa kwenye ghorofa ya pili; na jinsi watakavyomkamata na kumtuhumu mtu asiye na hatia hiyo [Lee Oswald], wakati muuaji halisi ametuama bila hofu.
  Michelle Nostradamus alitabiri kwa usahihi pia juu ya kuibuka, kutawala na kuanguka kwa Shah wa Iran mwaka 1979 na mtu atakayemwondoa madarakani. Aliandika hivi: “Mvua, njaa, vita kabla havijaisha Uajemi; imani kuu [Uislamu] utamuasi mtawala [Shah]; nayo itaanzia Ufaransa; kuleta mwisho wa mtawala; nayo imani kuu [Uislamu] itatawala”.
  Usahihi wa utabiri huu ni kwamba, mapinduzi yaliyomwondoa mtawala wa Iran [Taifa la Kiislamu] Shah Pahlavi, kibaraka mkubwa wa Marekani, mwaka 1979, yalibuniwa, kupangwa na kuongozwa na Ayatollah Khomein akiwa uhamishoni nchini Ufaransa; mapinduzi yanayodhaniwa kuwa ndilo chimbuko la mwamko mpya wa dunia ya Kiislamu dhidi ya sera na utamaduni wa nchi za Magharibi, kutokana na tamko lake kwamba, “Vita hii si ya Iran [Uislamu] na Marekani pekee bali ni kati ya Iran na Wapagani – Makafir wote”, kwa maana ya watu si wote wanaofuata dini ya Kiislamu.
  Nostradamus, wala “Watabiri” wa Macbeth na Julius Caezar, walioingizwa katika orodha ya Mitume au Watakatifu kwa maono yao na kwa mujibu wa imani za dini za mapokeo. Inapokuwa hivyo, wote hawa wanaangukia ndani ya kapu moja la imani za kishirikina, kwa maana kwamba dini zote za asili ni za Kishetani.
  Tunaweza kuwasamehe wenzetu wa enzi za Rumi, Uingereza na Ufaransa ya kale, kwa udhanifu huu, kwa sababu hicho ndicho kilikuwa kiwango cha maendeleo yao; lakini vipi kwa jamii yetu ya leo, ya Sayansi na teknolojia, kwa siasa kutawaliwa na imani za kishirikina?
  Je, Tanzania na Afrika kwa ujumla inaishi miaka ya 1500 ya Rumi na Uingereza? Je, ni ushirikina kweli, kwa muumini wa dini za mapokeo kubeba Biblia kwapani Jumamosi au Jumapili; au Kurani siku ya Ijumaa, wakati huo huo amesheheni hirizi kwapani na kiunoni? Tunamdanganya Mungu yupi asiyejua mawazo ya mwanadamu? [assassinations]
  Hebu tuangalie jinsi ushirikina wa enzi za kina Caezar na Macbeth unavyotawala sasa mustakabali wetu wa kisiasa na Afrika kwa ujumla, kwa gharama ya demokrasia, amani na utulivu; tukianzia na Rais wa kwanza wa Togo, marehemu Sylvanus Olympio.
  Siku chache kabla ya kuuawa kwa Rais huyo, Januari 13, 1963, alionywa na mtabiri wake asisaini hati yoyote ya Kiserikali siku ya 12 Januari; naye kama Macbeth, hakutii onyo hilo. Siku hiyo alitia sahihi hati nane, na jioni akajipumzisha Ikulu, bila kujua kilichomsubiri.
  Usiku huo huo, saa za mapambazuko, Januari 13, 1963; kikundi cha Maafisa wa Jeshi la Togo, kilishambulia Ikulu kwa silaha kali; Olympio aliweza kutoroka na kukimbilia kwenye Ubalozi wa Marekani uliokuwa ukitizamana na Ikulu yake; lakini wakati akigonga lango kuu la Ubalozi huo ili afunguliwe kujisalimisha, Wanajeshi walimwona, na kummiminia risasi, akafia langoni mwa Ubalozi huo.
  Mauaji ya Olympio yalifungua mlango kwa mauaji ya Viongozi wa kisiasa barani Afrika, chini ya dhana ya Mapinduzi ya Kijeshi; na utamaduni uliokuja kujulikana kama “Sundhurst Culture”, kwa maana ya kunyakua madaraka kutoka kwa watawala wa kiraia, pale ilipoonekana kwamba demokrasia haipewi nafasi na watawala hao.
  Naye Rais Leopold Sedar Senghor wa Senegal, mwaka 1972, alionywa na Mtabiri wake mwezi mmoja kabla, kwamba, Desemba 17, 1972, ilikuwa siku mbaya kwa usalama wake, na akashauriwa aondoke Dakar, ili aitumie siku hiyo kwa ziara kwenye mji wa Thies.
  Senghor alikubali; akaondoka na saa chache baadaye, kikosi cha Jeshi lake kilishambulia na kuvamia Ikulu wakimtafuta ili kumkamata na kumuuwa. Na katika kesi hiyo ya kupoteza muda wakimtafuta, vikosi vingine vya usalama vilijiimarisha na kuzima jaribio hilo la mapinduzi kwa nguvu kubwa na kuinusuru Serikali yake.
  Hapa nchini, wakati mmoja, Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kujiamini kwake, kama alivyojiamini Caezar, alisema: “Ni mtu kichaa pekee, ambaye anaweza kufikiria kuipindua Serikali yangu au kujaribu kudhuru uhai wangu”; wengi waliyahusisha majigambo hayo na nguvu za kishirikina kutoa kinga kwake; akaweza kudumu madarakani muda mrefu, kwa kuheshimiwa na kuogopwa, pengine kuliko Kiongozi yoyote barani Afrika.
  Imani hii potofu inathibitishwa pia na Watuhumiwa 19 wa kesi ya Uhaini, kwa kutaka kuipindua Serikali ya Mwalimu, kesi iliyodumu kwa miezi 10 na kumalizika Desemba 28, 1985; pale walipodai Mahakamani kuwa, kama isingekuwa kile “kiona mbali” [uchawi] cha mama mzazi wa Mwalimu, mpango wao wa kuipindua Serikali, kati ya Juni 1982 – Januari 1983, usingebainika; na kwamba mpango huo ulishindwa kwa nguvu ya mzimu wa mama huyo.
  Mashitaka dhidi ya Wanajeshi hao yalikuwa kwamba, wote kwa pamoja, kwa kushirikiana na raia mmoja, Bw. Pius Mtakubwa Lugangira, kwa majina mengine “Father Fom” au “Uncle Tom” [aliyeweza kutoroka nchi bila kukamatwa]; na mtu mwingine, Mohamed Mussa Tamim au “Martin Tamim” [aliyeuawa na vyombo vya Usalama wakati akikaidi kukamatwa], walikula njama kumuuwa Rais [Nyerere], kumwondoa madarakani na kuipindua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
  Walikabiliwa pia na shitaka mbadala la kuficha kosa la uhaini, kwa kushindwa kutoa taarifa kwa mamlaka inayohusika, huku wakielewa juu ya mpango wa kuipindua Serikali.
  Wapo pia wachochezi wachache [kina Brutus], waliopotoka kwa kufikiri kwamba, Serikali ya awamu ya Kwanza ilidumu madarakani na nchi kuwa ya amani na utulivu, umoja na mshikamano, eti kutokana na Mwalimu kuutumia Mwenge wa Uhuru na mbio za Mwenge huo kwa madhumuni ya kishirikina kuwaondolea Watanzania uwezo wa kufikiri, kujiamini na kauli ya kuhoji utawala wake. Hawa, wanapashwa sasa kuficha nyuso zao kwa aibu, hasa wanapofahamu kwamba, Mwalimu alikuwa mcha Mungu, na sasa kuna harakati zinazoendelea za kumtangaza Mtakatifu.
  Nao umaarufu wa mbio za Mwenge wa Uhuru na mantiki yake kwa mustakabali wa Taifa hili, sasa unazidi kuongezeka miaka 10 baada ya kifo cha Mwalimu.
  Ukiondoa matukio kadhaa yakiwamo ya Wagombea wa nafasi za uongozi wa siasa kukutwa kwa Waganga wa jadi katika mikao ya kukanganya, na sasa kauli za ushirikina kuanza kusikika katika kumbi za Bunge; ni kwa kiwango gani Serikali na Watawala kwa ujumla wameingia katika “mkenge” huu? Kwa kubwaga manyanga kwa imani za kishirikina? Hebu tuangalie kwa ufupi tu matukio yafuatayo:
  Wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2005, Watanzania walishuhudia mfano wa Machi 15 ya Julius Caezar, kwa tarehe za uchaguzi kubadilishwa mara mbili kuepuka tarehe ya “hatari” kwa Caezar, hatua inayoweza kuhusishwa na imani za kishirikina kwa Viongozi wa Serikali.
  Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Oktoba 30, lakini ulisogezwa mbele hadi Desemba 18, kufuatia kifo cha Mgombea Mwenza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA], hayati Jumbe Rajab Jumbe.
  Ilielezwa kuwa hatua hiyo ilikuwa ni kukiwezesha Chama hicho kupata muda mzuri kuteua mgombea mwenza mwingine. Lakini Zanzibar kwa upande wao, waliendelea na uchaguzi kama ulivyopangwa, licha ya kwamba mgombea mwenza wa Urais wa CHADEMA ndiye Makamu wa Rais mtarajiwa wa Jamhuri ya Muungano, ambayo Zanzibar ni sehemu yake.
  Wiki hiyo hiyo, wakati Desemba 18 tayari imekwishatangazwa kuwa tarehe ya Uchaguzi Mkuu, kipindi kimoja cha Jumamosi, cha Televisheni ya “Channel Ten”, kilifanya mahojiano na Mnajimu [mtabiri] mashuhuri Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein, kuhusu unajimu wake juu ya uchaguzi Mkuu huo tarajiwa nchini.
  Mnajimu huyo alibainisha kuwa uchaguzi Zanzibar ungekuwa shwari, lakini akaonya, “Ole wake atakayeingia madarakani kwa njia ya wizi wa kura, kwani hatamaliza kipindi cha miezi sita madarakani”. Kura ziliibwa, na washindi kwa njia hiyo bado wamo madarakani bila hofu yoyote; utabiri wa Sheikh Yahya ulikuwa wa kishirikina.
  Kuhusu uchaguzi Tanzania Bara, alitabiri kuwa ungekuwa huru na wa haki; lakini akaonya na kutahadharisha [kama mtabiri wa Caezar] kwamba, Desemba 18 iliyopangwa kwa uchaguzi, ilikuwa tarehe mbaya, na kwamba lolote lingeweza kutokea.
  Bila shaka, kwa utabiri huo, Serikali [Tume ya Uchaguzi – NEC] iliingiwa na kiwewe, kwani haraka haraka siku tatu tu baada ya utabiri huo Tume ilibadili siku ya uchaguzi kuwa Desemba 14.
  Sababu zilizotolewa, kwamba Tume ilifupisha muda huo kwa siku nne ili kupunguza gharama kwa Serikali na kwa Wagombea, hazikuwa za msingi wala mwafaka kwa hoja hiyo; kwani Watanzania walitaka uahirishwe kwa muda mfupi zaidi kabla mori wa uchaguzi haujapoa, na kwa vyama vya Siasa kupenyeza “mchezo mchafu”.
  Isitoshe, Desemba 14, tofauti na Desemba 18, ilikuwa siku ya kazi, na hivyo uchumi wa nchi ungeathirika kutokana na uzalishaji kusimama. Ukweli, Serikali haikuwa inapunguza gharama, bali kinyume chake.
  Na kama ilikuwa na lengo hilo, angalau Desemba 11 ilikuwa tarehe mwafaka zaidi, kwa sababu haikuwa siku ya kazi. Yawezekana kwamba Serikali ilikwishaonywa na Sheikh Yahya mapema, kwamba Desemba 11, kama ilivyokuwa Desemba 18, nayo ilikuwa “balaa” kama Machi 15 ya Caesar; Desemba 17 ya Rais Senghor, au Januari 12 ya Rais Olympio; kwamba lolote lingeweza kutokea?.
  Tunashindwa kujizuia kuamini kwamba, unajimu wa Sheikh Yahya ulipewa nafasi isiyostahili katika uchaguzi huo, kutokana na kwamba awali, alitabiri kuwa, “kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika, mmoja wa Wagombea atafariki”, na kweli Jumbe akafariki.
  Alitabiri pia kwamba, “Rais ajaye atakuwa na uso wa mviringo”, na hapo bila shaka akaifanya NEC isalimu amri kwa utabiri wa Desemba 18 kwenda Desemba 14.
  Kama ni kweli sasa kwamba siasa nchini mwetu zimeanza kutekwa na imani za kishirikina, kama tulivyoeleza hapo mwanzo; basi demokrasia na utawala bora umo matatani na mashakani.
  Kwa sasa, jamii yetu inakabiliwa na majanga matatu makubwa ya kutisha – Ukimwi unaoteketeza watu wetu, na kulipunguzia Taifa nguvu kazi, kama ilivyokuwa zama za enzi za biashara ya utumwa; rushwa na ufisadi vinavyonyonga haki na kupora rasilimali za Taifa. Ushirikina nao sasa unatafuta kujisajili kama janga la nne kutuletea Viongozi wababaishaji, wasiojiamini – Mashetani wanyonya damu; wasiothamini jasho na nguvu ya umma inayowaweka madarakani, bali wenye kuweka imani na matumaini kwa “mafundi” wao huko “Bagamoyo”.
  Kiongozi wa ngazi yoyote ile, aingiaye madarakani kwa imani ya nguvu za giza kama Macbeth, hutawala kwa hofu, hasira, kutojiamini na kutowaamini “wengine, na hivyo kwa mkono wa damu”.
  Na kadri kalamu ya wino wa damu inavyotema maandishi kwenye kurasa ngumu za maovu, uonevu, ukandamizaji na udikteta, siku za Mwandishi huyo [mtawala] huhesabika haraka madarakani.
  Inapokuwa hivyo, jinamizi juu ya jinsi na namna ya kuachia ngazi bila hofu ya kuzomewa au kuwajibishwa [kwa maovu yake], huwa ni agenda nzito na ngumu; matokeo yake ni kwa Viongozi wengi kung’ang’ania madarakani kwa kubadili Katiba; na kufanya hivyo, watahakikisha wanabadili Katiba kuwakinga wasishitakiwe au kwa kuwajibishwa kwa ufisadi na maovu yao ya nyuma. Katiba yetu ni moja ya Katiba hizo mbovu, zinazokingia kifua watawala mafisadi na wahujumu wa Taifa eti [ibara 46 (1): “Wakati Rais atakapokuwa ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba [hii], itakuwa ni marufuku kumshitaki au kuendesha mashtaka ya aina yoyote juu yake Mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai na vivyo hivyo [ibara 46 (2)] kwa mashauri ya madai.
  Tumeyaona haya kwa watawala madikteta kama kina Mabotu Sese Seko [Zaire/DRC], Jean Badel Bokassa [Afrika ya Kati], Marcias Nguema [Guinea ya Ikweta] na Iddi Amin Dada [Uganda] ambao, kwa imani zao za kishirikina, walifikia hatua ya kula nyama ya binadamu ili kudumisha tawala zao, lakini mwisho wa yote, waliyatema madaraka [kama Macbeth] kwa aibu kubwa.
  Na hao Viongozi washirikina wa leo wakoje? Shaaban Robert, katika shairi lake “Nilinde”, anawachambua ifuatavyo:
  “Ni weledi wa kusema, [viongozi] watu wa leo,
  Na elimu na hekima, si haba kwao,
  Bali hawana huruma, katika moyo,
  Na fahari na heshima, ni chache kwao,
  Kisha naweza kumuua, sumu wanayo.​
  Lakini anaendelea kuwaita wajinga; kwa sababu kwa imani za ushirikina, hutaka madaraka kwa kujasirishwa na imani potofu; anasema:
  “Wajinga hutaka nguvu, hata miliki ya enzi,
  Vitu vyenye maumivu, kwao ni maangamizi,
  Nguvu na enzi ni povu, kwa walio maizi,
  Hupendwa na wapumbavu, walegevu wa ujuzi.
  Nguvu si kitu cha sifa, enzi ina wazimu,
  Kwa wasio kifafa, wenye akili timamu,
  Ni mambo yenye maafa, kila namna magumu,
  Matunda yake kashfa, hapana lililo tamu.​
  Tungependa kuona miongoni mwetu Viongozi safi wa Taifa lisilo na uozo wa kiroho; Taifa linalomjua Mungu; Viongozi wanaojali kauli-mbiu ya “mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”, na “mtendee mwenzako kama ambavyo ungependa utendewe wewe”.
  Ni uongozi wa hii pekee utakaoweza kujenga na kudumisha utawala wa Sheria, Utawala Bora na demokrasia ya kweli.  Source: Raia Mwema
   
Loading...