Ili kupata ubunge uwe na 100m/-, udiwani 10m/- -- Utafiti

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Ili kupata ubunge uwe na 100m/-, udiwani 10m/- -- Utafiti

Shadrack Sagati
Daily News; Friday,October 17, 2008 @21:01

KUKITHIRI kwa rushwa ndani ya vyama vya siasa kumesababisha uongozi nchini hasa kuanzia kiti cha udiwani kugombewa na watu wenye uwezo wa kifedha peke yake, kongamano la kisiasa la kitaifa limeelezwa mjini Dar es Salaam.

Msomi kutoka taasisi ya Utafiti wa Demokrasia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Benson Bana alisema jana wakati akiwasilisha mada kuwa utafiti uliofanywa umeonyesha kuwa kwa sasa mtu anayetaka kugombea udiwani ni lazima atumie kati ya Sh milioni tano hadi 10.

Aliongeza kuwa kwa wale wanaotaka kugombea ubunge wanalazimika kuwa na kiasi cha kati ya Sh milioni 60 hadi 100 wakati wagombea urais wanatakiwa na kiasi cha fedha kinachozidi hapo mara kadhaa.

Dk. Bana alisema matumizi makubwa ya fedha yanasababishwa na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kujitokeza kuvifadhili vyama vya siasa kwa fedha nyingi. "Huko Mwanza mfanyabiashara aliwahi kutoa Sh milioni 150 kwa CCM. Niliwahi kushuhudia hali hiyo Zanzibar…sasa huyu chama kinapochukua madaraka analipwa nini?" alihoji Bana katika mada yake.

Mhadhiri huyo alisema hali ikiachiwa iendelee uongozi utashikwa na watu wenye fedha au wale ambao wana ushawishi wa kufadhiliwa na wafanyabiashara ambao nao wanatarajia kulipwa fadhila.

Alipendekeza kuwapo sheria ambayo itawabana wafadhili na mtu mmoja aruhusiwe kukichangia chama kiasi kisichozidi Sh milioni tano na kama ni kampuni iruhusiwe kuchangia chama kiasi kisichozidi Sh milioni 10.

Lakini pia alipendekeza kuwa mamlaka ya mapato (TRA) iruhusiwe kudai kodi kwa michango yote inayokusanywa na vyama kutoka kwa watu binafsi pamoja na kutoka kwa mashirika.

"Kama mfanyakazi wa kawaida analipa kodi iweje chama kinachokusanya fedha ili kuingia madarakani kisilipe kodi?" alihoji.

Profesa Haroub Othman wa Chuo Kikuu aliunga hoja hiyo na kueleza kuwa katika uchaguzi mkuu uliopita Sh bilioni 46 zilitumika kiasi alichoeleza kuwa ni kikubwa katika matumizi ya vyama vya siasa.


Mtoa mada kutoka CCM, Ramadhan Madabida, alisema suala la CCM kuchangiwa na watu wenye uwezo kiuchumi, limekuwa likitazamwa kwa jicho hasi na baadhi ya watu na hata kufikia hatua ya kuona kuwa CCM inakumbatia matajiri.

Alisema ni vema jamii ikubali kuwa nchi hii ina wananchi ambao uwezo wao wa kipato unatofautiana, alisema kuwapo kwa tofauti hizo hakuondoi ukweli wa hoja ya msingi kuwa binadamu wote ni sawa.

Jaji Joseph Warioba alisisitiza kuwa rushwa ndani ya vyama vya siasa ni tatizo la kitaifa hivyo viongozi wa kisiasa waone wana wajibu wa kuchangia kuwapo na sheria itakayosaidia kupunguza tatizo hilo.
 
Back
Top Bottom