Ili kupata kodi ya mapato ya trilioni 2 na zaidi, Serikali itumie sensa kikamilifu na itambue raia wanaozaliwa na wanaotimiza umri wa miaka 18.

Richard

JF-Expert Member
Oct 23, 2006
12,891
2,000
Suala la sensa katika nchi yoyote ile ni muhimu sana. Sensa hutoa picha halisi ya idadi ya watu katika nyumba katika nchi nzima.

Sensa pia hutoa taarifa rasmi ambazo zitasaidia serikali kupanga namna ya kutoa huduma mbalimbali nchini kama usafiri, elimu na afya. Hivyo kila nyumba katika nchi nzima ni lazima ijaze taarifa zake katika fomu maalum.

Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo wa kukusanya taarifa za sensa unaboreshwa na kuhakikisha kuwa mfumo huo unapatikana kirahisi mitandaoni ambapo wananchi wote wanapaswa kuutumia kujaza taarifa zao.

Kwa Tanzania tayari zipo taarifa za madereva kupita leseni ya udereva , kitambulisho cha uraia, taarifa za kupata TIN number kwa raia na taarifa za vitambulisho vya wamachinga.

Pia serikali yaweza kupata taarifa zaidi kupitia wamiliki wa simu zote ambazo zimesajiliwa au pia kupitia idara ya uhamiaji na kuzioanisha zote kupata taarifa rasmi.

Sikumbuki ni lini taifa lilifanya zoezi la sensa nchi nzima lakini inatakiwa sensa ifanyike kila baada ya miaka 10.

Hivyo basi, idara yetu ya takwimu iwe huru zaidi na kujimwambafwai kwa kuboresha mifumo yake ya kieletroniki kuhakikisha inakwenda na wakti.

Pia Idara hiyo yatakiwa kuwa na ofisi ndogo katika kila manispaa ambapo ukusanyaji wa taarifa waweza kufanywa kiufanisi zaidi na kufanya zoezi kumalizika katika muda mfupi ulopangwa.

Kuna wananchi hawafahamu maana halisi ya sensa hivyo huitaji ufafanuzi na pia kuambiwa kuwa endapo hawatajaza taarifa zao basi watakabiliwa na faini kubwa. Pia kuwepo muda maalum wa kujaza taarifa hizo pamoja na kusema ni nani khasa ambae apaswa kujaza taarifa hizo.

Hivyo idara ya takwimu yapaswa kutengeneza vipeperushi ambavyo vitakuwa na taaifra zote muhimu za namna ya kujaza fomu iwe ni kwenye kompyuta, simu za mkononi na kwa njia ya simu za kawaida.

Kodi ya maendeleo pia ni muhimu ikawa wazi kwa wananchi kwamba wanatozwa kodi kiasi gani na wanaelezwa kodi yao imetumika vipi katika maeneo yao.

Kwa mfano kodi ipo ya aina mbalimbali, kuna kodi ya maendeleo, kodi ya biashara ndogondogo, kodi ya makampuni katika eneo husika.

Mimi niliwahi kuishi nchi nyingi za Ulaya na katika kipindi hichi niliweza kujifunza kuwa mtoza kodi au huitwa "Taxman" ni mtu rafiki ambae hutaka kukutambua na kisha kufanya mawasiliano na wewe mlipa kodi.

Lakini hapohapo mtoza kodi huyu ana nguvu za kisheria za kuchungulia katika akaunti yako kubaini ni kiasi gani unacho katika akaunti yako na kama ni nyingi basi hachukui bali hurudi tena kwako kukujulisha udukuzi wake na kisha kukupa njia za wewe mlipa kodi kuweza kumalizana nae bila yeye kukushitaki kwa ukwepaji kodi.

Hivyo kodi ya kawaida ya mapato kwa wafanyakazi au waajiriwa, kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya barabara au ile ya bandarini hizi ni kodi za lazima kwa taifa kwani ndizo zinazoleta maendeleo kwa nchi nzima na huingiz moja kwa moja katika mfuko wa hazina.

Nilipokuwa naishi katika moja ya miji nchini Uingereza miaka ya mwishoni mwa 90 niliweza kuona barua ikidondoshwa mlangoni ikidai kupewa jina la mtu yoyote ambae hajasajiliwa kulipa kodi.

Ingawa barua hiyo yamlenga mmiliki au mkazi wa nyumba hivyo lakini siku zote nyuma ya bahasha ya barua hiyo huwa na kichwa cha habari kisemacho "kama wewe si mtu ulieandikiwa barua hii, basi tafadhali jaza sehemu ya hapo chini taarifa zako zote likiwemo jina lako, lini umeingia katika nyumba hiyo na tarehe gani umenunua nyumba hiyo au lini umeanza kupanga nyumba hiyo".

Lengo la ujumbe huo ni kuhakikisha asiesajiliwa kulipa kodi anapaswa kufanya hivyo chini ya sheria ya kodi.

Pia barua hiyo inakuwa imeambatanishwa na barua kwa mlipa au walipa kodi ikionyesha nyumba ipo katika daraja lipi au "band" ipi A, B, C , D hadi H na hiyo ni kwa kodi ya wafanyabisahara khasa wa maduka ambao hulipa kodi ya biashara au "Business Tax".

Barua hii inakuelezea makadirio yako ya kodi kwa mwaka mzima na inakuelezea njia za za kulipa kodi hiyo lakini la muhimu au "crucially" katika barua hiyo kuna ushauri kwa mlipa kodi kama ni yule anaehitaji punguzo kwa sababu kadha wa kadha.

Jambo jingine la muhimu katika barua hiyo ni kukuelezea mlipa kodi jinsi kodi yako inavyotumika katika manispaa unayoishi na kukuchambulia asilimia ngapi yaenda kwenye huduma za jamii, polisi, huduma za zimamoto na uokoaji, na kodi ya manispaa wenyewe.

Kwa mfano kwa mwaka wa fedha manispaa yaweza kuwekla lengo la kukusanya kodi ya pauni milioni 458 ya ujumla lakini kodi ya maendeleo pekee ikiwa kama pauni milioni 99 hivi.

Hivyo ilibakia ukitoa hiyo milioni 99 ni kodi inayotokana na wafanyabiashara, tozo mbalimbali ndani ya manispaa, pamoja na msaada wa kutoka hazina.

Hii ya kutoa fedha kutoka katika mfuko wa hazina si jambo la tija kwani lazifanya manispaa nyingi zidorore kiasi cha kushindwa kubuni njia mbalimbali za kujipatia mapato ndani ya manispaa.

Kodi katika manispaa yatumika kujenga au kuimarisha miundombinu kama barabara. mashule, hospitali na shughuli zingine za jamii katika manispaa kama sehemu za kupumzikia na burudani.

Huduma zinazoweza kutolewa na manispaa.

Huduma hizo ambazo huitaji fedha za kodi ili kuhakikisha zinatekelezwa ni pamoja na usafi wa mitaa na uzoaji taka, hospitali na zahanati, huduma za maktaba, huduma za burudani na bustani na huduma zingine muhimu.

Lengo la kuelezea sehemu ya hapo juu ni kuonyesha umuhimu wa kuhakikisha kwamba kila raia ambae ni mlipa kodi kwa mujibu wa sheria anatambulika na kisha yanajengwa mawasiliano baina ya TRA na mlipa kodi.

Lakini pia umuhimu wa kuhakikisha raia wote wanopaswa kulipa kodi wanatambulika pamoja na makazi yao.

Watoto wanozaliwa waweza kusajiliwa majina yao moja kwa moja wakiaambatanishwa na wazazi wao na taratibu hizi kuhakikisha zinafuatwa nchi nzima.

Hivyo ni muhimu raia wote ambao wanatimiza umri wa miaka 18 ni lazima watambulike na wapewe namba za TIN kuwajulisha kwamba sasa ni watu wazima na wajiandae kuwa walipa kodi.

Wenzetu Ulaya wanayo "Land Registry" ilotengenezwa kwa mkono na idara ya mapato tangu mwaka 1862 ili kusajili ardhi na nyumba zote. Hivyo kila nyumba au kitalu, jengo na ghorofa zote hutakiwa kuandikishwa.

Faida za kuwa na "Land Registry" ni kwamba sehemu hizo na wamiliki wake zitambulika kirahisi, mmiliki hulindwa kisheria dhidi ya hujuma, kuwezesha kupatikana "title deed" na pia kurahisisha ubadilishanaji au uuzaji wa nyumba au majengo hayo.

Tanzania tumekwamia hapa, ambapo hadi leo ndio tumekumbuka kusajili vitalu na majengo yote nchi nzima zoezi litaloanza mwezi Julai. Hatujachelewa lakini hii ndo itakuwa njia sahihi ya kuhakikisha kila taarifa za wamiliki wa ardhi, nyumba na majengo wanajulikana kwa makusudio ya kupata kodi stahiki.

Hatua ya mheshimiwa raisi Mama Samia Hassan ya kumpa chagizo waziri wa fedha Mwigulu Nchemba kwamba akusanye kodi ya kufikia trilioni 2 kwa mwezi kwa kutumia akili ni ya kuungwa mkono.

Watanzania wote, TRA na manispaa zote nchini zinapaswa kupokea changamoto hii ambayo inatoa mwanya kwa kuhakikisha tunabuni njia sahihi za kujipatia mapato na njia ambazo ni rafiki, zisizosumbua wala kuharibi uhusiano baina na serikali na walipa kodi.

Jambo la msingi ni kufanya kampeni nchi nzima kuhimiza ulipa kodi, kwa matangazo na vipeperushi na kuhakikisha maofisa wote waso waaminifu walioko katika manispaa na TRA na ambao bado wanadunda wanaondolewa na nafasi zao zajazwa na vijana wapya ambao mpaka leo wanazururura wakitafuta ajira.

Pia TRA ni lazima ijifanyie tathmini katika mifumo yake inayotumia kukusanya kodi kielektroniki. Njia hii yaitwa "Office Automation" ambapo njia zote za kutumia fomu zinabadilishwa na njia za kielektroniki kuondoa mianya ya wizi na ubadhilifu.

Tovuti dhaifu ya TRA ni moja maeneo yenye shida ambapo haionyeshi kuwa ipo user friendly na haitumii nyenzo za programs za kisasa na zinazokwenda na wakti kiasi cha kuweka nyuma ya tovuti za idara za mapato za Rwanda, Kenya na Uganda.

Hivyo, TRA wanapaswa kutumia makampuni yanotambulika kwa shughuli za ubunifu na utengenzaji tovuti ambazo hata zikitoza fedha za kazi zao haionyeshi kuwepo kwa ufisadi badala ya kutumia vijikampuni vya kawaida sana.

Kwa kuhitimisha hili ningependa kuona nchi yangu ikijiondoa katika minyororo ya kushindwa kubuni njia sahihi za kujikwamua kimaendeleo na kushindwa kutatua matatizo ya kukusanya kodi.

Naamini njia hizi mbili kupitia sensa na maboresho uorodheshaji wa kila nyumba, majengo na ardhi katika nchi nzima, itakuwa njia sahihi za kuwezesha serikali kujipatia mapato kirahisi na bila mabavu au ugomvi na walipa kodi.

Pia uboreshaji wa idara ya mapato yaani TRA katika mifumo yake ya kielektroniki itasaidia kukusanya mapato katika njia zote sahihi na zingine mpya zilizobuniwa ili kuiweka idara hivyo katika picha chanya kwamba haiko kusumbua walipa kodi na yatumia njia za kiuelevu na zilizo rafiki lakini imara.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom