Ili Kumuua Mchawi Wachoma Moto Kituo cha Polisi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WATU 17 wanashikiliwa na polisi mkoani Rukwa kwa tuhuma za kuvamia
kituo cha polisi kwa lengo la kutaka kukiteketeza kwa moto ili kumuua mwanaume waliyemtuhumu kuwa ni mchawi.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa, Isuto Mantage, alisema wanaoshikiliwa na polisi ni wakazi wa kijiji cha Wampembe wilaya ya Nkasi baada ya jaribio lao
kukitekeza kwa moto ili kumuua mzee Daud Kapelo (76) waliyemtuhumu kwa uchawi.

Alisema, chanzo cha tuhuma hizo ni kifo cha Joseph Kapelo (19) aliyeugua kwa muda mfupi na kufa Novemba 22 mwaka huu na kuibua imani za kishirikina wakimhusisha baba wa marehemu, Kapelo (76), na kifo hicho.

Alisema, wakati wananchi hao wakipanga mikakati hiyo, taarifa zilifika kituo kidogo cha polisi cha Wampembe na kufanikisha polisi kumwokoa mtuhumiwa huyo aliyekuwa amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na wananchi wenye hasira.

Kamanda huyo alieleza kwamba wakati wananchi hao wakielekea makaburini, walilipeleka jeneza la marehemu hadi kituo cha polisi na kuliweka wakimtaka Daud atolewe mahabusu ili naye wammalize kisha kumzika pamoja na mwanaye.

“Vurugu za wananchi wale ziliendelea na kuanza kushambulia kituo cha polisi kwa mawe hali iliyowalazimu askari waliokuwepo zamu kupiga risasi hewani lakini wananchi hao hawakuogopa na kuanza kumshambulia askari huyo na kuibua mapigano kati ya askari na wananchi,” alisema.

Alisema, wananchi hao waliwasha moto uliozimwa kwa msaada wa askari na
mgambo waliokuwepo kabla ya wananchi hao kutawanyika.

Kamanda huyo alibainisha kwamba wakati wa mapambano hayo, Imelda Kayanda (46), alipigwa risasi na kufariki huku naye Agnes Kisori (21) akijeruhiwa mguuni ambapo walikimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.

Kadhalika, jeshi hilo limewatia mbaroni Zakaria Francis (28), Ikombe
Yustini (39), Stephano Kambe (18), Benard Kabeja (16), John Kapandila
(22), Said Diwali (36), Vido Tuwakazi (21), Abdalah Vicent (19), Sylveter Kapala (17), Richad Bushota (19), John Mathias (58), Wilbroad Chambi (16) na Kapondo Anatoli (23).

Kamanda huyo alisema, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika na polisi wataendelea kuwatafuta waliokimbia.

Aidha Kamanda Mantage, alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi na kuvamia vituo vya polisi.
 
Back
Top Bottom