Ikulu Dar: Rais Magufuli amemteua George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mussa Zungu apewa Wizara ya Mazingira

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
627
1,000
Matangazo ya moja kwa moja kutoka Ikulu Jijini Dar es Salaam yatawajia muda mfupi ujao kupitia vyombo vya habari vya Redio, Televisheni na Mitandao ya Kijamii. Aidha, waweza kutazama kupitia Youtube ya IkuluMawasiliano.

B8FD3D87-DB06-47BE-BAB5-3B82EAC27DF4.jpeg


======

UPDATES:

Rais amemteua Mussa Zungu kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira na kumuhamisha George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Zaidi soma....

Rais John Magufuli amemteua mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Simbachawene anachukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Hayo yameelezwa leo jioni Alhamisi Januari 23, 2020 na katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi.

Mabadiliko hayo madogo ya baraza la mawaziri yamefanyika baada ya leo asubuhi katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za askari wa Jeshi la Magereza zilizopo Ukonga, Dar es Salaam, Rais Magufuli kueleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye ambaye naye uteuzi wake umetenguliwa, huku ikielezwa nafasi yake itajazwa baadaye.

Katika uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu kuwa balozi.

Katika hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo, Magufuli alisema Meja Jenerali Kingu aliandika barua ya kujiuzulu na alimkubalia, kueleza kuwa amemheshimu kwa uamuzi wake huo.

“Leo Rais Magufuli amemteua Zungu kuwa Waziri anayeshughulikia muungano na mazingira na kumhamisha Simbachawene kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani kuchukua nafasi ya Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa,” amesema Balozi Kijazi.

Amesema Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa mabalozi watatu watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao, kufikisha umri wa kustaafu.

“Amemteua Meja Jenerali Kingu ambaye alikuwa katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu jana Januari 22, 2020.”

“Amemteua Dk Steven Simbachawene kutoka ofisi ya rais Ikulu na kamishna Jenerali Faustine Kasike ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, nafasi ya Kasike itajazwa baadaye. Vituo vya kazi vya mabalozi hawa watatu vitatangazwa baadaye,” amesema balozi Kijazi.

Balozi Kijazi amesema Rais Magufuli amewaongezea muda mabalozi saba wa Tanzania, akiwemo Asha Rose Migiro ambaye ni balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

zungu.jpg

Azzan Mussa Zungu

Mussa Azzan Zungu (Alizaliwa 25.05.1952) ni mwanasiasa wa chama cha CCM nchini Tanzania na ni mbunge wa jimbo la Ilala tangu mwaka 2005.

Mbunge huyu wa Ilala alipata elimu ya awali na ya msingi katika Shule ya St. Joseph’s (kwa sasa Forodhani) jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1958 na 1965. “Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alichaguliwa kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya Kinondoni mwaka 1966 hadi mwaka 1967 kabla ya kwenda katika Shule ya Sekondari ya Tambaza mwaka 1968 hadi 1969.

Baadaye alikwenda Toronto, Canada kusoma sayansi na ufundi wa vyombo vya anga ukiwamo urubani hadi mwaka 1982. Baada ya masomo alifanya kazi za field aviation huko Toronto, Canada na katika Kikosi cha Anga Tanzania kabla ya kuanza shughuli zake binafsi.

Alianza siasa lini?

Zungu anajitaja kuwa ni muumini mkubwa wa Siasa ya Ujamaa tangu enzi za chama cha siasa cha Tanganyika African National Union – TANU). Alijiunga na TANU mwaka 1969, na muda mfupi baadaye akapewa wadhifa wa Katibu Msaidizi wa Tawi la chama hicho katika Shule ya Sekondari ya Tambaza, jijini Dar es Salaam. Alijielekeza kwenye siasa ili kupata fursa ya kushiriki ipasavyo katika harakati za kutafuta maendeleo endelevu ya Taifa letu, baada ya kukombolewa kutoka katika utawala wa kimabavu wa wakoloni.

Juhudi za Zungu katika tasnia ya siasa zilimwezesha kuchaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Mchikichini, Dar es Salaam, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000. Miaka mitatu baadaye alichaguliwa kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Baada ya kuona wananchi wengi wana imani naye, alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo mwaka 2005, akashinda. Mwaka 2010 aligombea na kufanikiwa kuchaguliwa tena kuwa Mbunge wa Ilala hata 2015


May 10, 2016 Musa Hassan Zungu aliteuliwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tena Mwenyekiti wa Bunge hilo kwa mara ya pili baada ya kuteuliwa mara ya kwanza Jun 18, 2012

simba.jpg

George Simbachawene

Septemba 06. 2017 akiwa Waziri wa TAMISEMI, Mbunge wa Kibakwe George Simbachawene alitajwa kwenye ripoti ya Uchimbaji wa madini ya Tanzanite, na Almasi kupitia Kamati ya Bunge, ripoti ambayo iliwasilishwa kwa Spika Ndugai na yeye kumkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa ili aipeleke kwa Rais Magufuli.

Septemba 06. 2017 baada ya ripoti hiyo kukabidhishwa kwa Rais Magufuli, Simbachawene alitangaza kujiuzulu nafasi Uwaziri wa TAMISEMI ili kupisha tuhuma dhidi yake.

Agosti 28, 2018, Simbachawene alichaguliwa na Wabunge wenzake kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, akichukua nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bi Hawa Ghasia ambaye alitangaza kujizulu.

Julai 21, 2019 rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira akichukua nafasi ya January Makamba. Na leo 23 Januari 2020, Simbachawene anateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya ndani kuchukua nafasi ya Kangi Lugola

Historia na Elimu

George Boniface Taguluvala Simbachawene 2016 aliteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Pombe Magufuli akiwa mbunge wa Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma tangu mwaka 2005.

Simbachawene alizaliwa Julai 5, 1968 na alianza elimu ya msingi mwaka 1978 katika Shule ya Pwaga iliyoko wilayani Mpwapwa. Alisoma shule hiyo hadi mwaka 1982 na mwaka uliofuata alihamia Shule ya Msingi ya Mahomanyika iliyoko mkoani Dodoma ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1982.

Elimu ya Sekondari aliipata kuanzia mwaka 1985 hadi 1988 katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mazengo, pia ya mkoani Dodoma. Mwaka 1989 hadi 1993 alikwenda jijini Arusha na kusoma Chuo cha Ufundi cha Arusha ambako alitunukiwa Cheti cha Ufundi (TFC).

Mwaka 2001 hadi 2005 aljiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambako alitunukiwa shahada ya kwanza ya sheria (LLB). Mwaka 2007 alishiriki mafunzo ya kazi na taratibu za uendeshaji wa Kamati za Kibunge kwenye Bunge la Westminister na kutunukiwa cheti na mwaka 2010 alitunukiwa cheti kingine baada ya kuhitimu mafunzo juu ya bunge hilo.

Baada ya kuhitimu na kubobea katika masuala ya ufundi, ilimchukua miaka miwili kabla ya kuajiriwa na kampuni ya mabasi ya Urafiki, tawi la Dodoma mwaka 1995. Alikuwa kondakta, meneja wa kitengo cha ufundi na ofisa usafiri. Mwaka 1997 hadi 1998 aliajiriwa na Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Future World akiwa mwalimu. Kati ya kipindi hicho hadi mwaka 2000, alifanya kazi kama mkurugenzi mtendaji wa shirika la kiislamu la Muzdalifa linalojishughulisha na masuala ya misaada.

Mwaka 2005 Simbachawene, akiwa na miaka 37, aliachana na ‘ukonda’ akaamua rasmi kuitafuta ofisi kubwa ambayo watu wengi waliokuwa naye hawakudhani kama angeliweza kuifikia. Alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa tiketi ya CCM, akamwangusha aliyekuwa mbunge wa Kibakwe na hivyo kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huo.

Mshindani wake mkubwa alikuwa Benson Kigaila wa Chadema na Gabrile Elias Masinjisa wa NCCR Mageuzi. Matokeo ya mwisho yalimpa Simbachawene ushindi wa asilimia 86.1 (kura 37,359), Benson akifuatia kwa asilimia 12.8 (kura 5,542)

Baada ya ubunge wa miaka mitano, Simbachawene alitupa tena karata yake mwaka 2010, na akaibuka kidedea kwenye kura za maoni za kata 13 kati 16 baada ya kupata kura 8,824 huku mpinzani wake, Aggrey Galawika akiwa na kura 2,537 na hivyo, Simbachawene akapata ridhaa ya kuiwakilisha CCM.

Kwa mara ya pili alikumbana na Kigaila wa Chadema, lakini akamshinda tena kwa kupata kura 22,418 sawa na asilimia 77.12 dhidi ya kura 5,585 sawa na asilimia 19.21% za Kigaila.

Mwaka jana, Simbachawene alitupa ndoano yake jimboni Kibakwe kwa mara ya tatu akashinda kwenye kura za maoni kwa kupata kura 18,159 akiwaacha mbali washindani wake sita ambao ni Gabriel Mwanyingi (kura 6,900), Akrei Mnyang’ali (kura 3,563) na Amani Bendera (kura 410).

Kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, alipambana na Mzinga William wa Chadema na kumshinda kwa kura 37,327 sawa na asilimia 81,55 dhidi ya kura 8,447 za mpinzani huyo.

Baada ya kushinda Ubunge mwaka 2010, Simbachawene aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kuanzia Mei 2012 hadi Januari 2014 alipohamishiwa Wizara ya Nyumba na Makazi akiendelea na unaibu.

Januari 2015 alipandishwa na kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu kutokana na sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

JPM alipotangaza baraza lake mwaka jana, Simbachawene alipangwa Tamisemi akiwa waziri.

Ndani ya CCM alianza kama mwanachama na kiongozi wa matawi, likiwamo la Chuo cha Ufundi Arusha kati ya mwaka 1990 hadi alipomaliza. Pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kati ya mwaka 2002 – 2005.

 

chakii

JF-Expert Member
Sep 15, 2013
18,742
2,000
Wizara nyeti hii ya mambo ya ndani anahitajika mtu wa ku replace kabla mambo hayajaharibika....

Sent from my SM-J700H using Tapatalk
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom