Ikiwa Ikulu: Rais ana imani na Kamati ya Madini, Hoja ya Zitto yazidi kuvuruga Chadema

Kuntakinte

JF-Expert Member
May 26, 2007
701
30
Ikulu: Rais ana imani na Kamati ya Madini

na Irene Mark

OFISI ya Rais (Ikulu) imesema Rais Jakaya Kikwete bado ana imani kubwa kuwa Kamati ya Kuhakiki Sheria za Madini aliyoiteua wiki iliyopita itafanya kazi iliyotumwa kwa ufanisi.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alipofanya mahojiano kwa njia ya simu na gazeti hili.

Rweyemamu aliieleza Tanzania Daima kwamba, maoni yanayotolewa na wananchi mbalimbali dhidi ya wajumbe wa kamati hiyo hayawezi kumfanya Rais Kikwete apoteze imani aliyonayo kwa timu nzima ya wajumbe 12 wanaounda kamati hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema, katika nchi ya kidemokrasia ni jambo lisilowezekana kuwazuia watu kutoa maoni yanayopingana katika jambo lolote lile.

“Watu wanasema. Wana haki ya kutoa maoni. Hata hivyo ukweli unabakia pale kuwa ile ni Kamati ya Rais na anaendelea kuiunga mkono. Huwezi kuzuia watu wasiseme, acha watoe maoni yao, hiyo ndiyo demokrasia,” alisema Rweyemamu.

Alipoulizwa iwapo kwa kusema maneno hayo ana maana kuwa rais ana imani na Zitto, Iddi Simba na Mark Bomani? (ambao wote ni wajumbe), Rweyemamu hakuwa tayari kukiri hilo na badala yake akasema: “Rais ana imani na timu nzima kwani itafanya kazi kama timu na si mtu mmoja mmoja.”

Kauli hiyo ya Rweyemamu inakuja wakati ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukiwa na fukuto linalotokana na kuwapo kwa mawazo yanayopingana kuhusu uamuzi wa Rais Kikwete kumteua Zitto katika kamati hiyo.

Aidha, watu wenye mtazamo huo, wanasema pia kuwa, wajumbe kadhaa wanaounda kamati hiyo wana mahusiano yanayokinzana na maudhui ya kuanzishwa kwake na hivyo kuyafanya matokeo ya kazi watakayoifanya kuwa yasiyowanufaisha wananchi.

Wakati hilo likiendelea, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Mark Bomani, jana alilieleza gazeti hili kwamba, kamati yake ilikuwa ikikusudia kuanza kufanya kazi rasmi wiki ijayo.

Bomani, Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzalendo, alisema tayari kazi ya kusambaza barua kwa wajumbe imeshaanza na wanatarajia kukutana wakati wowote wiki hii kwa ajili ya kupanga ratiba ya kazi na kupeana majukumu.

Alisema, hadi sasa wapo baadhi ya wajumbe kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam wanaoendelea kupokea barua hizo kuhusu kuwepo kwao ndani ya kamati hiyo itakayofanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Kuanzia wiki ijayo tutatoa ratiba na baada ya ratiba hiyo tu…tutaanza kazi, lakini kwa wiki hii wajumbe wanakusanyana.

“Unajua wajumbe wengine wanatoka mbali na hapa (akimaanisha Dar es Salaam), hivyo baada ya kukutana, nadhani wiki hii tutaandaa ratiba itakayoonyesha wapi, lini na watu wa aina gani tutakaohitaji maoni yao,” alisema Bomani.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania kusubiri matokeo ya kamati hiyo iliyoteuliwa na Rais Kikwete, Novemba 13 mwaka huu kwa lengo la kuikomboa sekta ya madini nchini.

Pamoja na Bomani ambaye ni mwenyekiti, wajumbe wengine ndani ya kamati hiyo ambao ni wanasiasa ni Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela na Ezekiel Maige, Mbunge wa Msalala (CCM), John Cheyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP) na Zitto.

Wengine ni Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Kamishna wa Sera Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi, Wizara ya Ardhi, Edward Kihundwa, Mkaguzi wa Hesabu kutoka Kampuni ya kimataifa ya Ukaguzi wa Hesabu, PriceWater Coopers, David Tarimo na mwanasiasa mkongwe, Iddi Simba.

Wajumbe wengine ni Peter Mchunde kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kejo.

Siku chache baada ya rais kuitangaza kamati hiyo aliitaka kupitia mikataba ya madini na nyaraka nyingine zinazohusu migodi mikubwa na kuchambua mfumo wa kodi unaotumika katika sekta hiyo.

Aidha, kamati itapitia mfumo wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali, itachambua na kuainisha haki na wajibu wa mwekezaji na serikali na pia itakutana na ‘Chamber of Minerals’ na wadau wengine na kutoa mapendekezo kwa serikali.

Wakati huo huo, Zitto ambaye hivi karibuni alieleza kukubali uamuzi wa rais kumteua kuwa mjumbe wa kamati hiyo, aliieleza Tanzania Daima jana kuwa, alikuwa tayari kuheshimu uamuzi utakaotolewa na Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu ushiriki wake ndani ya Kamati hiyo ya Madini.

Akizungumza kwa simu kutoka Kigoma aliko hivi sasa, Zitto ambaye amekuwa gumzo kuu tangu ateuliwe kuingia katika kamati hiyo wiki iliyopita, alisema anaamini uamuzi wa kikao hicho cha chama kitakachofanyika mwishoni mwa wiki hii kitafikia uamuzi sahihi.

Zitto (31), ambaye amekuwa mwanachama wa CHADEMA tangu akiwa na umri wa miaka 16, alisema siku zote amekuwa mwanachama mtiifu kwa chama chake.Wakati huo huo: Nyumbani kwetu:

Hoja ya Zitto yazidi kuivuruga Chadema
:: Tundu Lissu amtaka ajiondoe haraka
:: Adai Kamati haina maslahi kwa Taifa
:: Asema Serikali imenuia kuua mjadala
:: Yabainishwa CC haiwezi kumfukuza

na mwandishi wetu

HALI ya hewa ya kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inazidi kutetereka.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho, kuendeleza msimamo mkali unaohusu uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, katika Kamati ya Kupitia Mikataba ya Madini nchini.

Miongoni mwa wajumbe kwenye Kamati hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Kabwe Zitto.

Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, anayetambulika kwa msimamo wake wa kutetea rasilimali za nchi, hasa madini na mazingira, ameweka bayana msimamo, akidai ni msimamo wake binafsi.

Lissu, kwa nguvu zote, amesema anaendelea kupinga kwa nguvu zote, uamuzi wa Rais Kikwete kumteua Zitto, kuwa mmoja wa wajumbe kwenye Kamati hiyo.

Mwanasheria huyo machachari, anasema wananchi hawajajua vema hoja ya wanaopinga Zitto kuwamo kwenye Kamati hiyo.“Msimamo wangu uko hadharani, hii si Kamati ya kufanya kile kilichokusudiwa kufanywa ili kilete manufaa kwa Taifa. Kamati hii ya Rais haina nguvu za kisheria za kuwaita, kuwauliza na hata kutaka maelezo yoyote kutoka kwa watu mbalimbali.

“Nipo tayari kutetea popote pale msimamo wangu. Kamati iliyokuwa inafaa, ni ya Bunge ambayo waliikataa. Kamati Teule ya Bunge inakuwa na nguvu za kisheria za kudai nyaraka, maelezo na kuwaita watu kuwahoji.

“Hii Kamati ya sasa tunayoiona haina nguvu hizo, hii ni kama ‘kitchen party’, haiwezi kulazimisha watu kisheria kutoa nyaraka, lakini Kamati ya Bunge ina uwezo.

“Kamati hii ya Rais, ikiomba nyaraka, na anayeombwa akakataa kutoa, haitakuwa na mahali pa kumshitaki maana haina nguvu za kisheria, lakini Kamati ya Bunge ina nguvu za kisheria mahali popote pale. Kamati ya Rais ina nguvu gani?” amehoji.

Alisema kamati za aina hiyo zilizoundwa kupitia madini, zilikosa meno ya kisheria, na ndiyo maana kuna sehemu watu waliotakiwa watoe nyaraka au maelezo, waligoma, na hawakufanya jambo lolote kwa sababu hapakuwapo nguvu za kisheria.

“Mimi namtaka Zitto ajiondoe kwenye Kamati hii, anatumiwa kama toilet paper, amewekwa tu kama mtego kwa sababu siku ya siku akizungumza, ataambiwa ‘na wewe ulikuwa mjumbe wa tume’. Naweza kusema hii ni Kamati ya kudanganya watu ili waone Serikali imekusudia kweli kurekebisha mambo.

“Serikali inatafuta mbinu tu. Tazama wajumbe waliomo kwenye Kamati ya Madini. Mbona hamuwasemi ni kina nani? Yumo…huyu akiwa Mwanasheria wa Serikali, mwaka 1993 alishiriki kupitisha mkataba wa Loliondo. Kuna tuhuma kwamba alihongwa.

“Ameshiriki sana katika mkataba wa IPTL (Independent Power Tanzania Limited). Kwenye hati za kiapo za arbitration (usuluhishi), viongozi watatu walisema mjumbe huyo aliwaahidi hongo.

“Kwenye kiapo hicho mjumbe…anasema aliahidiwa hongo ya Sh milioni 200, na maofisa wengine wawili walisema aliwaahidi kila mmoja Sh milioni 100. Huyu mtu aliyefanya madudu haya, leo anakuwa kwenye Kamati.

“Ripoti ya Transparent International inamhusisha mjumbe mwingine…kwamba alihusika sana na ujio wa IPTL, hata akatumia jukwaa la Bunge kuhakikisha inakuwapo.

“Mjumbe mwingine…ni Mkurugenzi wa kampuni ambayo Waziri Nizar Karamagi ni mwanahisa. Huyu akienda Buzwagi, atafanya nini? Atamchunguza rafiki yake na kutoa maelezo gani?

“Mjumbe huyu katika mgogoro wa Richmond, alienda bungeni akiwa na mwanasheria (jina tunalo), leo atakuwa na utukufu gani wa kufanya kazi kubwa ya kitaifa? Wajumbe wengi kwenye Kamati ya Madini, hawana sifa, hawafai,” alisema Lissu.

Mwanaharakati huyo alisema suala la Zitto kuondoka kwenye Kamati hiyo, litajadiliwa wiki hii katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Chadema.

“Suala hili haliwezi kutugawa, lakini kama chama, lazima tuwe na msimamo. Chama kinaweza kufikia uamuzi wowote, mimi si msemaji wa chama, lakini kwangu binafsi, siafiki hata kidogo Zitto kuwamo kwenye Kamati hii.

“Sijaona hoja yoyote ya Zitto kubaki, CCM wanasema tuache siasa, lakini wao tangu lini wameacha siasa? Lazima tujue maslahi ya Taifa ni yepi na ni nani anaya-define. Miaka yote CCM wanasema.

“Hii Kamati ni ya kutumia fedha za walipa kodi na imelenga kunyamazisha mjadala wa rasilimali za nchi,” alisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mark Bomani, alikaririwa na gazeti hili juzi akisema kwamba Kamati hiyo haikuundwa kumchunguza mtu, bali itapitia sera, sheria na taratibu kwenye sekta ya madini.

Alisema kwa sababu hiyo, suala la wajumbe kuwa na uhusiano na baadhi ya viongozi, haliwezi kuathiri kwa namna yoyote, maudhui ya kuundwa kwa Kamati.

Aliwahakikishia wananchi kwamba Kamati itafanya kazi zake kwa uadilifu na kutoa majibu yatakayosaidia kufanya sekta ya madini iwe na tija kwa Watanzania na wawekezaji.

Jana, Jaji Bomani alizungumza kwa simu na MTANZANIA kuhusu Kamati yake kuwa au kutokuwa na nguvu za kisheria za kudai maelezo kutoka kwa walengwa mbalimbali.

Mwenyekiti huyo alijibu kwa kusema: “Nisingependa kujiingiza kwenye malumbano na hao wanaosema hivyo, kama wanasema haina nguvu kisheria, hilo watajua njia zao. Sisi tunachongoja ni kuanza kazi rasmi kama tulivyotumwa na Mheshimiwa Rais.”

Alisema mambo yakienda kama yalivyopangwa, wiki ijayo huenda Kamati hiyo ikaanza kazi rasmi. Alisema wamechelewa kwa sababu wajumbe wanatoka maeneo mbalimbali. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyeko masomoni nchini Uingereza, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya kikao cha CC.

Tayari suala la Zitto la ama kuwamo, au kutokuwamo kwenye Kamati ya Madini, limezua mgawanyiko ndani ya chama hicho. Wapo wanaomuunga mkono, lakini wengine wanampinga, akiwamo Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe.

Pia, viongozi kadhaa, akiwamo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, wamekuwa vigeugeu. Wakati awali walipongeza uamuzi wa kuwamo Zitto kwenye Kamati hiyo, baadaye wamebadilika na kumtaka ajitoe.

Wakati huo huo, imeelezwa kwamba Kamati Kuu (CC) ya Chadema haina ubavu wa kuchukua hatua dhidi ya mbunge wake wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto kuhusiana na hatua ya mbunge huyo kusisitiza kuwa atashiriki kikamilifu katika Kamati ya Rais ya Kuangalia Mustakabali wa Madini nchini, habari za kuaminika zinasema.

Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zinasema kuwa jambo ambalo kikao cha CC kilichoitishwa Jumamosi wiki hii kinaweza kufanya, ni kukubaliana na msimamo wa mbunge huyo kuhusu ushiriki wake katika kamati.

Habari hizo zinasema kuwa Chadema katika hali ya sasa haiweza kumlazimisha Kabwe kujitoa katika kamati hiyo, na hata baada ya kukataa kujitoa, hakiweza kumfukuza.

Ofisa mwandamizi wa chama hicho alilieleza gazeti hili jana kuwa kikao hicho kitajaribu kupunguza mgogoro uliosababishwa katika chama hicho na suala la Kabwe, kwa kukubaliana na msimamo huo wa mbunge huyo.

Ofisa huyo anakiri kuwa Chadema kwa sasa, haina ubavu wa kumchukulia hatua mbunge huyo ambaye msimamo wake unaonekana kuungwa mkono na wananchi wengi ambao wanaamini kuwa kamati hiyo itaondoa dosari zilizopo katika sera, sheria na taratibu za sekta ya madini.

Ofisa huyo anakiri kuwa hatua yoyote dhidi ya Kabwe inaweza, kwa urahisi kabisa kukigawa kabisa chama hicho ambacho, kama vilivyo vyama vingine vya upinzani nchini, bado ni kichanga na hakina nguvu za kuhimili mvutano mkubwa kama uliozushwa na suala la Zitto.

“Kwa kadri inavyoonekana kikao cha Jumamosi ni geresha tu ya kuwatuliza wanachama na mashabiki wa chama, lakini hakiweza kumlazimisha Kabwe kujitoa katika kamati hiyo,” anasema ofisa huyo.

Aliongeza: “Katika hili, Kabwe anaonekana kuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko chama. Kabwe ni mmoja wa wabunge wawili ama watatu wanaoleta sura ya kitaifa katika chama hicho, vinginevyo wakiondolewa hao, Chadema itabakia chama cha kikanda tu.”

Ilitangazwa katika magazeti jana kuwa Chadema kimeitisha kikao cha CCM ili kujadili uteuzi wa Kabwe katika kamati hiyo ya madini ya Rais Kikwete.

Kamati hiyo imepewa miezi mitatu kuwa imekamilisha kazi ya kuangalia mustakabali mzima wa sekta ya madini katika uchumi wa Tanzania.

Baada ya awali, viongozi wa juu kuwa wamekubali na kuupokea kwa mikono miwili uteuzi wa Zitto, walibadilika ghafla mwishoni mwa wiki wakiibeza kamati hiyo na kumtaka Kabwe ajitoe. Kabwe mwenyewe, zaidi ya mara nne, amesisitiza kuwa hatajitoa na kwamba anakusudia kushiriki kikamilifu katika kamati hiyo.
 
Dah nilifikiri nivya leo kumbe ni hoja ya miaka kumi nyuma
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom