Azizi Mussa
JF-Expert Member
- May 9, 2012
- 9,172
- 7,428
Siasa za ushindani zinapogeuka kuwa kama ugomvi; mara nyingi mwisho wake unakuwa haupendezi sana. Katika mazingira mengine inaweza kusababisha changamoto kubwa kuliko ambavyo watu wanaweza kudhania kabla.
Inavyoonekana ni kama siasa za ushindani Tanzania zina hako ka muelekeo ka kukaa ki ‘Ugomvi’ na tunaweza kukubaliana kamba “kama muelekeo huo upo” sio mzuri na wakushabikia.Sifikiri kama ikiwa uhusiano uliopo sio mzuri kweli, kuna anayeweza kuamini kwa dhati kabisa kama yeye ananufaika na hilo.
Tunaweza kushauri kuwa, itakuwa ni jambo zuri na muhimu kama Mh. Rais ataona inafaa na kuamua kuitisha maridhiano ya kitaifa.
Kwenye maridhiano hayo kusiwe na vyombo vya habari, viongozi wa vyama vyote waalikwe, wajifungie mahali, kila mwenye lake aseme, anayeona kadhulumiwa mahali afunguke, anayeona amekosewa aseme, anayeona mwenzake kakosea mahali fulani aambiwe; yaani iwe ni kuambiana ukweli.
Baada ya hapo kila mmoja atakuwa katua mizigo aliyo nayo na baada ya hapo yanafanyika maridhiano na kufanya makubaliano kwenye mambo ya msingi juu ya ni nini tunataka, ni nini hatutaki na wapi tunakotaka kwenda kama taifa.
Moja ya mambo ambayo ni vizuri kuwa na muafaka wa kitaifa ni pamoja na ikiwa tunataka demokrasia ama hatutaki, na kama tunataka demokrasia ya namna gani na ni kivipi itekelezwe.
Baada ya maridhiano hayo, itakuwa sasa ni muhimu kila mmoja kutekeleza maridhiano kwa utashi wake mwenyewe. Ikumbukwe ijapokuwa kuwa tuna Katiba na sheria, ila “Utashi wa kisiasa “ ni muhimu sana kwenye kufanikisha karibu kila jambo. Naamini jambo hilo litakuwa la faida kwa wote na hakuna atakayepoteza bali kama nchi tutakuwa tumeshinda wote kwa pamoja.
Ni kweli kwamba wapinzani wa Tanzania wana mapungufu mengi, lakini tukumbuke kuwa nao ni binadamu na ni sehemu ya watanzania hawa hawa ambao tunajijua vizuri sana tulivyo.
Hata hivyo pamoja na mapungufu yao, lakini bado ni watanzania na kuna mahali wanaweza kusaidia. Unaweza hata kukutana na mtu mwenye uwezo mdogo labda kwenye kila kitu, ila angalau akakuambia huko unakoenda nimetoka huko, kuna nyoka kwa hiyo pita pembeni. Kwa hiyo licha ya uwezo wake mdogo, lakini anakuwa amekusaidia pengine kuokoa maisha yako.
Kwa hiyo pamoja na matatizo waliyo nayo, bado wanaweza kusaidia kitu flani , wakati fulani na mahali fulani na mwisho wa siku bado ni wanajamii na Watanzania.
Uzuri pia ni kwamba Mh. Magufuli ni ‘Optimist’, anaangalia ni lipi lenye faida zaidi na ndilo analofanya, na hili tumeliona kwenye kuwasamehe wenye kesi za ufisadi kwa masharti ya kulipa wanachodaiwa kwa kuamini kuwa;kufanya hivyo ni faida kwa wahusika lakini pia faida kwa taifa. Kimsingi kama hilo kaliweza kwa maslahi ya taifa, akiamua hili ni jambo dogo sana kwake kulifanikisha, na kwa kuwa lina faida kuliko hasara; bila shaka ataona umuhimu wake.
Kadhalika, kwa uelwa wake mzuri juu ya dhana hii ya ushirikishwaji, kutoa nafasi ya kila mtu kusema ya moyoni na baadae kufanya maridhiano; mara kadhaa tumeshuhudia akiyafanya haya na makundi mbalimbali ikiwepo wafanya biashara. Kwa hiyo hili nalo linaweza kuwa zuri vilevile.
Kama Mandela aliweza kufanya kikao cha kuelezana ukweli na maridhiano na wana Afrika kusini wakasamehena na kuridhiana licha ya makorokoro yote waliyofanyiana, Tanzania tunayo nafasi nzuri sana katika hili kwa sababu hatuna tatizo kubwa la kutisha kimahusiano.
Wasiwasi ni kwamba, chuki huwa ina tabia ya kuingia kwa haraka kwenye nafsi ya binadamu lakini ni ngumu sana kutoka. Kwa hiyo inapowezekana kuizuia kuingia; ni bora kufanya hivyo hasa kama gharama yake sio kubwa sana, maana ikitokea watu wakianza kuchukiana wenyewe kwa wenyewe watakuwa pia wanatafuta namna ya kuhujumiana wenyewe kwa wenyewe, na watu wakiwa wanahujumiana wenyewe kwa wenyewe, ni rahisi na maadui wa pembeni kutumia mwanya huo huo kuchomekea mokorokoro.
Samahani kwa yoyote atakayekuwa amekwazika kwa kusoma mambo mengi maana wengi hili linawakwaza.