Ikangaa, Kiganja na Nyambui Wajitosa kwenye Uchaguzi Mdogo RT

Melubo Letema

JF-Expert Member
Apr 1, 2020
306
281
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) inatarajiwa kufanya uchaguzi Novemba 27 mwaka huu jijini Dodoma, nafasi zinazowaniwa ni Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati Tendaji Kanda ya Pwani, ambazo waliokuwa wakizishikilia, John Bayo na Robert Kalyahe, walijiuzulu kutokana na sababu mbalimbali.

Zoezi la utoaji fomu kwa wagombea lilianza rasmi Novemba 5 na kufikia tamati Novemba 11, na sasa ni urejeshaji fomu ambao utahitimishwa Novemba 20 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa RT, Lwiza John, hadi Novemba 14 saa 9:30 alasiri, wagombea watatu walikuwa wamekwisha rejesha fomu kuwania Umakamu wa Rais.

John, aliwataja wagombea hao kuwa ni Kanali mstaafu Juma Ikangaa, Mohammed Kiganja na Suleiman Nyambui.

Kanali mstaafu Ikangaa mwanariadha maarufu wa mbio ndefu wa zamani, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa RT enzi hizo TAAA, Kiganja ambaye hivi sasa ni Ofisa Michezo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), huku Nyambui ambaye pia ni mwanariadha nguli, aliwahi pia kuwa Katibu Mkuu wa RT.

"Zoezi la urejeshaji fomu linaendelea na tunawasisitiza waliokwisha chukua fomu, warejeshe wakiambatanisha nyaraka husika ikiwemo stakabadhi ya malipo ndani ya muda husika na hakutakuwa na uongezaji muda ifikapo tarehe 20," alisisitiza John.

Wakati majina hayo maarufu yakiwa yamejitosa rasmi, inatarajiwa vigogo zaidi kurudisha fomu na kufanya uchaguzi huo kutarajiwa kuwa na ushindani mkali.

Kusuasua kwa urejeshaji fomu, kunaelezwa na baadhi ya wagombea kuwa ni ugumu wa kuwapata viongozi wa vyama vya mikoa, ambao wanapaswa kuwathibitisha.

Mara baada ya kufungwa zoezi la urejeshaji fomu Novemba 20, Novemba 21 itakuwa ni usaili na kutangaza matokeo huku Novemba 23 hadi 24 ni kupokea mapingamizi na Novemba 24 hadi 27 itakuwa kampeni na uchaguzi wenyewe jijini Dodoma.
 
Back
Top Bottom