Ika mjadala wa muundo wa muungano wa tanzania katika rasimu ya katiba mpya?

ulanga

New Member
Aug 31, 2013
3
1
IKA MJADALA WA MUUNDO WA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA
RASIMU YA KATIBA MPYA?
Nimesoma na kusikia na baadae kuisoma kwa makini rasimu ya katiba mpya na kuona kuwa kuna hoja ambazo zimejificha, ambazo kama zikiwekwa wazi, zinaweza kutoa ufumbuzi wa hoja ya msingi ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania. Hoja ya kwanza ni matumizi ya maneno “Nchi”, “Taifa” na “Serikali”. Maneno haya matatu yana umuhimu wa pekee katika muundo wa Jamhuri ya Muungano na yametumika sana katika rasimu ya Katiba, kuanzia paragraph ya kwanza ya Utangulizi wa Rasimu ya Katiba. Aidha wachangiaji wengi katika maandishi na hata mazungumzo wametumia maeneno haya. Mimi sina uhakika kuwa tuna uelewa wa pamoja kuhusu tafsiri ya maneno haya, kwani uelewa huo ni msingi wa uamuzi wa muundo wa muungano. Kwa uelewa wangu, “Nchi” ni sehemu ya ardhi katika dunia ambayo hujulikana kwa mipaka ya kijiografia badala ya au urithi, au kugawana au kuinunua au mapambano ya kuikomboa ili Taifa kwa kutumia Serikali iitumie kwa ajili ya kutekeleza lengo la Taifa. “Taifa” ni jamii ya watu wanaoishi au katika nchi moja au zaidi ya moja, wanaounganika kutokana na tukio la kihistoria linalohusu au mapambano ya imani au mifumo ya jamii na kujitambulisha kwa alama au chini ya uongozi moja au dola moja yenye mamlaka kamili juu ya nchi. Taifa huwa na lengo, misingi na utaratibu wa utawala wa nchi unaoitwa Serikali ili kujenga, kulinda na kutetea maslahi ya yake kizalendo ili lengo la Taifa litimie. Katika tafsiri hiyo Taifa hutazamwa kama taasisi yenye lengo, wadau ambao ni wananchi na mazingira yanalolizunguka. Taifa huwa na alama zake kama zinavyoonyeshwa katika Ibara ya 3 Sehemu ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba. “Serikali” ijapokuwa rasimu ya Katiba imetoa matumzi yake, lakini siyo maana yake. Kwa maoni yangu “Serikali” ni au chombo au utaratibu unaotumika na Taifa katika kutawala nchi ili kutekeleza lengo la Taifa. Kuna mifano ya Mataifa ambayo kwa kutumia Serikali yaliweza au yanatawala nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kutekeleza malengo ya Mataifa yao. Umuhimu wa tafsiri ya “Nchi” Taifa” na “Serikali” utaonekana katika maelezo ya hoja zinazofuata. Hoja yangu ya pili inajengwa kutokana na tafsiri nilizotoa hapo juu. Je! Kupatikana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilizoungana ni Nchi mbili au Mataifa Mawili? Hoja yangu ni kwamba yaliyoungana tarehe 26/4/1964 yalikuwa mataifa mawili huru, Taifa la Tanganyika na Taifa la watu wa Zanzibar. Hoja yangu inatokana na sheria Na. 22 ya 1964 inayoitwa “The Union of Tanganyika and Zanzibar Act” kwa upande wa Tanganyika na “The Union Zanzibar of and Tanganyika Law 1964, sheria iliyotangazwa katika tangazo la Serikali Na. 243 la 1964, kwa upande wa Zanzibar. Kifungu cha 4 cha sheria ndicho kilichotamka Muungano wa Mataifa mawili kwa maneno yafuatayo, “The Peoples’ Republic of Zanzibar and the Republic of Tanganyika, shall upon union day and forever after be united into one sovereign republic”. Tafsiri yangu ni “Jamhuri ya watu wa Zanzibar na jamhuri ya Tanganyika, kuanzia siku ya kuungana hadi milele, zitaungana na kuwa Taifa moja la Jamhuri”. Historia inatuambia kuwa Tanganyika lilikuwa Taifa 9/12/1962 ilipokuwa Jamhuri. Kabla ya hapo Tanganyika ilikuwa nchi iliyotawaliwa na Taifa la Uingereza. Hata baada ya Uhuru 9/12/1961, katika Tanganyika alikuwepo “Governor General” aliyemwakilisha Malkia wa Taifa Uingereza. Zanzibar lilikuwa Taifa 12/1/1964, baada ya Mapinduzi matukufu. Kabla ya hapo Zanzibar ilikuwa nchi iliyotawaliwa na Sultani kutoka Oman. Kwa kitendo cha kuungana, Taifa la Tanganyika na Taifa la Zanzibar yalifutika na kutoweka rasmi katika orodha ya Mataifa ya Umoja wa mataifa na kuzaliwa Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taifa jipya likajiwekea utaratibu wa kutawala wenyewe nchi zao zilizokuwa zinatawaliwa na mataifa ya kigeni. Nimesoma kitabu cha moja wa Waasisi wa Muungano, Baba wa Taifa, Mwl. J. K. Nyerere, kiitwacho “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania”. Kuna hoja moja ambayo imejificha nami naona ni vema ikaeleweka, hasa baada ya maelezo ya hoja ya kwanza na ya pili hapo juu. Hoja yenyewe ni uhusiano kati ya Nchi, Taifa na Serikali. Nchi inaweza kubadilika ikawa Taifa. Kama vile nchi ya Tanganyika ilipobadilika na kuwa Taifa terehe 9/12/1962 na vile vile nchi ya Zanzibar ilivyobadilika ikawa Taifa tarehe 12/1/1964. Nchi inapobadilika na kuwa Taifa, eneo lake la kijiografia hubakia vilevile, isipokuwa wananchi wa Taifa lile, hutawala nchi yao wenyewe, kwa kutumia utaratibu wa Serikali waliojiwekea wenyewe, ili kutekeleza lengo la Taifa ambao pia hujiwekea wenyewe. Hapa kwetu, maelezo ya uhusiano kati ya Taifa na Serikali yanaonekana katika hotuba aliyoitoa Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere Bungeni tarehe 30/5/1962, aliposema kuwa Mkuu wa Nchi alikuwa Malkia wa Uingereza akiwakilishwa na Mteule wake “Governor-General” na Mkuu wa Serikali ni Waziri Mkuu. Kwa misingi ya hoja nilizotoa hapo awali, Taifa la Tanganyika na Taifa la watu wa Zanzibar baada ya kuungana 26/4/1964, walikubaliana juu ya utaratibu wa kutawala nchi zao, kama ifuatavyo:- Kuwe na Rais wa Taifa la Jamhuri ya Muungano ambaye pia atakuwa Mkuu wa Serikali ya Muungano itakayotawala nchi ya Tanganyika au Tanzania Bara kwa ajili ya kutekeleza lengo la Taifa. Kuwe na Makamu wa Rais wa Taifa la Jamhuri ya Muungano ambaye pia atakuwa Mkuu wa Serikali ya Mapindui ya Zanzibar itakayotawala Nchi ya Zanzibar kwa ajili ya kutekeleza lengo la Taifa. Hoja hapo ni kwamba katika mfumo wa Muungano Taifa lolote, ukiacha Taifa la Imani ya dini, lazima liwe na nchi ya kutawala. Nimesema hapo awali kuwa Taifa huwa na lengo na kwamba Taifa hujengwa. Hoja hiyo imo katika kubuniwa kwa lengo la Taifa la Tanganyika 1962 ambalo baadae likawa lengo la taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Ujamaa na Kujitegemea. Baada ya melezo mengi na mikakati ya utekelezaji lengo hilo liliwekwa katika Ibara ya 3(i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 na utekelezaji wake katika Ibara 9 ya Katiba hiyo. Kwa utaratibu huu lengo la Katiba huwa pia lengo la Taifa na ndio mustakabali wake. Na ndio maana hata katika Rasimu ya Katiba mpya, lengo la Katiba limewekwa katika Ibara ya kumi na moja – ijapokuwa kuna mapungufu ambayo sitaki kuyazungumza leo. Baada ya hoja hizi, sasa nataka kurudi kidogo katika Rasimu ya Katiba. Katika Ibara ya 1 ya sura ya kwanza, sehemu ya kwanza, sioni tatizo la kupendekeza muundo wa shirikisho, lakini napata tatizo kuuhusisha muundo wa shirikisho na Hati ya makubaliano wa muungano wa 1964. Katika kitabu cha “uongozi wetu na Hatima ya Tanzania”, Baba wa Taifa Mwl. J.K. Nyerere, uliupinga sana muundo wa shirikisho. Aidha, maneno ya “kadri itakavyorekebishwa” yanaonyesha kuwa Hati ya Makubaliano inaruhusu kurekebishwa; wakati sheria inasema wazi wazi, “… shall upon union day and forever after, be united into one sovereign republic”. Tafsiri yangu, “… kuanza siku ya kuungana hadi milele, zitaungana na kuwa Taifa moja la Jamhuri”. Sijaona mahali panaporuhusu au kuvunjwa au kurekebishwa kwa Hati ya Muungano, isipokuwa labda kuvunjika. Jambo ambalo pia haliwezekani. Isipokuwa ni kweli, upande moja wa Muungano – Zanzibar – kwa hoja ya kero za Muungano umeruhusiwa kujiongezea alama za Taifa hadi kufikia mahali, kwa mujibu wa alama za Taifa zilizopo katika Ibara 3(i) ya Rasimu ya Katiba, sasa Zanzibar ni Taifa kamili. Kwa maoni yangu hiyo ndiyo sababu inayowafanya wananchi wa upande wa pili wa Muungano (Tanzania Bara) nao wadai Taifa lao. Ikifikia hapo tutakuwa na Mataifa matatu na siyo Serikali tatu. kwani huwezi kuwa na Serikali tatu wakati Zanzibar tayari imeshakuwa Taifa. Taifa la Jamhuri ya Muugnano litakuwa wapi? Litatawala nchi gani? Kwa Mataifa matatu hoja ya shirikisho inawezekana, lakini njia ya kufikia hapo siyo kwa msingi wa Hati ya makubaliano ya 1964. Hizo ndiyo hoja zilizojificha katika mjadala wa muundo wa muungano wa Tanzania katika Rasimu ya Katiba mpya. Je! Ni mimi tu ninayeona hivyo au kuna wenzangu?
 
Haitoshi tu kuwa na mawazo mazuri bali namna ya kuwawasilisha. Ulanga, una mawazo mazuri ila namna ulivyoyaleta haivutii kusoma.
 
Hoja zako ni nzuri,lakini kwa sasa zanzbr haitaji tena muungano bali inahitaji mamlaka yake kamili,tuachiwe tupumue zanzbr kwanza.
 
Back
Top Bottom