Ijue Sheria:- Ndugu hawana nafasi katika umiliki mali za familia

Ushimen

JF-Expert Member
Oct 24, 2012
36,774
83,939
Mali za familia hupatikana kwa jitihada za pamoja za mke na mume kila mmoja akiwa na mchango wake kwa namna moja au nyingine na baadaye watoto kushirikishwa.
Hii yaweza kuwa matokeo ya mali za mmoja wa wanandoa alizozipata kabla ya kufunga ndoa na kuamua kuzimiliki kwa pamoja kama wanandoa aidha kwa kuziongezea thamani au zikiwa kama zilivyopatikana.
Hata hivyo mali zote zilizopatikana kuanzia tarehe ya ndoa ni za wanandoa wote wawili bila kujali mnunuzi alikuwa nani au mchango wa kila mmoja ulikuwa kiasi gani.
Umiliki wa mali limekuwa tatizo kubwa hasa unaposhirikishwa mchango wa ndugu katika upatikanaji wake kiasi cha wakati mwingine mke au mume kusahaulika kabisa.
Inapofika kwenye ununuzi na uendelezaji wa mali unawashirikisha ndugu au wazazi mwenzi wako, unakuwa unapanda mbegu ya ubaguzi huko mbeleni. Matokeo yake huwa ni vilio, vurugu na dhuluma endapo mmojawapo atafariki.
Kisheria ndugu, jamaa na marafiki ni wageni ambao wanaweza kukaribishwa kuchangia mawazo au nguvu kufanikisha upatikanaji wa mali husika. Wazazi na ndugu yeyote au rafiki hawezi kuchukua nafasi ya mume, mke au watoto katika uendeshaji na umiliki wa mali za familia.

Familia ni taasisi inayojitegemea na yenye uongozi wake, kuruhusu iongozwe na mtu ambaye si mhusika mkuu na hana mamlaka kisheria ya kuendesha mambo ya serikali hiyo ni kuhatarisha usalama na uimara wa familia yenyewe.

Kuruhusu wazazi au ndugu waamue namna mtakavyofanya biashara na kumiliki mali zenu kama familia ni kutweza mamlaka, haki na wajibu wa kila mwana familia.
Kanuni za uendeshaji bora wa biashara pamoja na miradi mbalimbali zinataka maamuzi yoyote ya umiliki wa mali au biashara inayofanywa na familia yanapaswa kujadiliwa na kuhitimishwa na familia husika si ndugu wala rafiki.

Pamoja na mchango mzuri wa ndugu katika kushauri, kuwezesha na kusaidia kufanikisha mambo mbalimbali, mustakabali wa uchumi na mali za familia anapaswa kuwa wa wana familia wenyewe.
Ni makosa makubwa kufanya biashara, kuanzisha mradi au kununua mali yoyote kwa shinikizo kutoka kwa wazazi au ndugu na kumficha mume au mke wako na watoto na kuwashirikisha wazazi na ndugu zako tu.
Unapotoa mwanya kwa watu ambao hawana mamlaka ya kumiliki mali za familia kisheria kwa kumficha mke au mume wako unakaribisha mgeni ndani ya familia ambaye baadaye anaweza kuja kuwasumbua msipokuwa makini au kuisumbua familia wakati haupo tena duniani.
Baadhi ya wanandoa wamepofushwa na mapenzi ya nyumba ndogo au vimada na mwisho wa siku wakajikuta wanakabidhi kila kitu huko zikiwamo nyaraka muhimu za umiliki wa mali au kununua mali nyingine na kuwaficha wenza na watoto wao jambo ambalo ni kosa kisheria.

Hiyo ni dalili tosha familia haiko imara. Japokuwa sio wote, lakini asilimia kubwa ya ndugu wanaweza kuwa miongoni mwa watumainio cha ndugu. Hawajishughulishi, hawana malengo wala mipango yoyote zaidi ya kutarajia kurithi mali zako kwa kumnyanyasa mkeo au mumeo na watoto wako.
Wengine ni wepesi kuingilia uamuzi wenu lakini wao hawataki kuingiliwa wala kukushirikisha katika maamuzi ya familia zao.
Mafanikio katika biashara na uchumi imara hayapatikani kwa miujiza bali kujenga familia imara isiyoendeshwa kama gari bovu na kuyumbishwa kama bendera.

Mafanikio katika biashara yanaanza kwa kuithamini familia yako. Huwezi kuwa mpole na mkarimu kwa wengine halafu ukawa mkali, katili na mchoyo kwa familia yako ukategemea kufanikiwa. Haiwezekani.
Ndugu, jamaa na marafiki wanaweza kujifunza jinsi mnavyoshirikiana kufanikisha mambo yenu lakini si kuyaingilia kwa namna yoyote.


BY Wakili Justine Kaleb
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom