Uchaguzi 2020 Ijue na itambue Ilai ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025

Bekiri

Member
Jun 30, 2013
14
75
Kama ilivyo ada na kawaida kwa vyama vya siasa kuandaa Ilani yao ya uchaguzi yenye vipaumbele na sera wanazoenda kutekeleza baada ya kushinda uchaguzi na kuunda serikali, Chama Cha Mapinduzi kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imetoa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-25 liyoeleza vipaumbele na maeneo yote wanayoenda kuyatekeleza kwa miaka mitano ijayo baada ya kushinda uchaguzi na kuunda serikali.

Ilani hii ya uchaguzi ya CCM yenye jumla ya kurasa 303, imegawanywa kwenye jumla ya Sura 10 zilizogusa na kueleza kwa mapana mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa miaka mitano iliyopita ya awamu ya 5 na kueleza zaidi mipango na mikakati inayoenda kuchukuliwa na kutekelezwa kwa miaka mitano ijayo baada ya kushinda uchaguzi Oktoba 28 na kuunda serikali.

Ni Ilani kubwa kuliko Ilani zote za CCM kuwahi kuundwa, ni Ilani iliyogusa maeneo yote ya maisha ya Mtanzania, ni Ilani iliyoongeza mambo mengine mengi sana ambayo hayakuguswa huko nyuma. Siri hii ya Ilani hii kuwa kubwa ni kutokana na CCM kuyatilia mkazo mambo mengine mengi sana ambayo hayakujumuishwa kwenye Ilani zilizopita na kasi kubwa ya utekelezaji wa Rais Magufuli kwa miaka mitano iliyopita, hivyo kwa kasi yake ikaona iongeze mambo yote ili yashughulikiwe kikamilifu. Haijaacha kitu.

Sasa leo tutaichambua Ilani hii Sura kwa Sura kwa kuangalia maudhui na mambo yaliyoelezwa ndani yake na kutajwa kwenye kila Sura ya Ilani hii. Hii itakusaidia kuijua na kuitambua kwa mapana na kwa ujumla Ilani nzima ya CCM, Chama tawala. Tuanze sasa hapo chini kuangalia Sura kwa Sura kwa Sura zote 10 zilizoko ndani ya Ilani hii.

*SURA YA KWANZA: UTANGULIZI.* Sura hii inafungua ukurasa wa Ilani hii kwa kueleza Taifa zima la Tanzania toka kuzaliwa kwake kutokea kwenye uasisi wa vyama viwili vya TANU na ASP iliyokuja kuzaa CCM. Hapa inaieleza CCM kujengwa katika misingi ya ujamaa na kujitegemea inayozingatia utu, usawa na haki na kueleza namna CCM inavyoendelea kuhakikisha Serikali zake zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inalinda na kudumisha misingi hii adhimu iliyolifanya Taifa letu kuendelea na amani, umoja na mshikamo na kuwa mfano note duniani. Sura hii imeanza ukurasa wa kwanza tu mpaka ukurasa wa 8.

Sura hii pia imeeleza CCM itaendelea kuamini katika uzalendo, kuhamasisha watu kufanya kazi kwa bidii kama msingi wa maendeleo, kutumia mtaji wa rasilimali kedekede tulizobarikiwa kujiletea maendeleo, kudumisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na kueleza mapinduzi makubwa ya kimaendeleo yaliyopatikana kwenye sekta ya uchumi kwa serikali zake zote mbili.

*SURA YA PILI: MAPINDUZI YA UCHUMI KWA MAENDELEO YA WATU.* Sura hii ni kama Sura mama ya Ilani hii hasa kwa kutambua nafasi ya uchumi kwa maendeleo na ustawi. Sura hii imeanzia ukurasa wa 9 mpaka wa 123 na imejikita kueleza kwa mapana kazi kubwa iliyofanyika kwa miaka mitano iliyopita na kutoa mikakati mipana ya kuendeleza mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa miaka mitano mingine ijayo.

Sura hii ya Pili imegusa hali ya kiuchumi ilivyoimarika maradufu, sekta ya fedha, ushiriki wa Sekta Binafsi katika uwekezaji, kupambana na umaskini na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi hasa kuwezesha kimitaji na kimikopo makundi ya vijana kiujasiriamali, wafanyabiashara wadogo na mpango wa kukomboa kaya maskini kupitia TASAF. Pia Sura hii imegusa uchumi wa Rasilimali za Maji (Blue Economy), kutumia fursa ya kijiografia za nchi yetu kuchochea maendeleo, kuongeza fursa za ajira kufikia milioni 8, kuimarisha vyama vya ushirika ambavyo ni muhimu kiuchumi na kuimarisha zaidi sekta ya kilimo ambayo ndio uti wa mgongo na inayotegemewa na Watanzania wengi sana kwa kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu wote.

Pia Sura hii kama tulivyoona kuwa kama mama na yenye mchango mkubwa kwa maendeleo imegusa pia kwa mapana sana sekta zingine muhimu kiuchumi na maendeleo kama ufugaji, uvuvi, viwanda hasa kwa adhima yetu ya kujenga uchumi wa viwanda, biashara, barabara, uchukuzi, mawasiliano, nishati ya umeme, mafuta na gesi asilia, madini, utalii, maliasili, malikali kale na kumbukumbu za Taifa na usimamizi bora wa ardhi.

*SURA YA TATU: HUDUMA ZA JAMII. Sura hii imeeleza adhima ya serikali ya CCM kuhakikisha kila mwananchi wa Tanzania anakuwa na fursa ya kupata huduma bora za jamii na za kutosha bila kikwazo chochote kwa zingine kuzitoa bure kabisa. Sura hii imepiga kisawasawa mafanikio yaliyootwa miaka kwa miaka na kueleza mikakati na mipango madhubuti ya kuboresha zaidi huduma za jamii kuwa bora, zinazopatikana kwa urahisi na za viwango vya kimataifa.

Hapa imeelezwa kwa hoja na takwimu za mafanikio ya utoaji elimu bure na namna serikali itakavyoendeleza mpango huo, kuboresha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, elimu ya juu, pameguswa eneo la afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, watumishi wa kada ya afya, matibabu ya kibingwa, mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko kama Corona, mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, ustawi wa jamii, ustawi wa wazee, huduma za watoto na familia na watu wenye ulemavu.

Sura hii ya huduma za jamii pia imegusa eneo la maji hasa kwa kutambua maji ni msingi wa uhai wa binadamu na injini ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambapo jumla ya miradi ya maji 1,423 imeendelea kutekelezwa mijini na vijijini hali iliyoongeza upatikanaji wa maji mijini kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020 na vijijini kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 70.1 mwaka huu 2020 na mikakati mingine mikubwa inayokuja kwa miaka mitano ijayo.

Sura hii imeonyesha kazi kubwa iliyofanyika katika kuboresha huduma za jamii kama kutoa elimu bure, kujenga vituo vya kutolea huduma za afya zaidi ya elfu 1 na mambo mengine mengi yanayoenda kufanyika kwa miaka mitano ijayo ili Watanzania waendelee kupata huduma bora za afya na stahiki. Sura hii imeanzia ukurasa wa 124 mpaka ukurasa wa 150.

SURA YA NNE: SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU. Kwa kutambua umuhimu wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika maendeleo na utatuzi wa changamoto mbalimbali katika nchi, Sura hii imegusa namna CCM itakavyoendelea kuboresha eneo hili ili likasaidie zaidi katika kuwezesha matumizi ya rasilimali zetu kwa ufanisi zaidi. Ni sura iliyoanzia ukurasa wa 151 mpaka 154. Mwisho sehemu ya kwanza!

Tutaendelea tena kwenye sehemu ya pili ya kuijua Ilani hii ya CCM kupitia kuichambua maudhui yake. Kwenye sehemu ya pili tutaangalia Sura zingine zilizobaki ambazo ni Ulinzi na Usalama, Utawala bora, Utawala wa Sheria na madaraka ya wananchi, mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa, maeneo mengine na Chama Cha Mapinduzi. Usikose.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom