Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,463
- 39,929
Mtoto nipe kalamu, nikae chini nitunge,
Niseme jambo muhimu, na hoja zangu nipange,
Siyo kwamba natuhumu, fikara zangu nilonge,
Ni nani alo kuwadi, kuwadi wake fisadi?
Wapo wamejaa tele, majina twayasikia,
Wapo na kimbelembele, kila kona Tanzania,
Tena na kihelehele, ughaibuni watulia,
Amfichaye fisadi, ni kuwadi wa fisadi!
Wapo na mapesa yao, kurubuni waandishi,
Watumia vyombo vyao, kuendeleza uzushi,
Umekwisha muda wao, wako kama matapishi,
Mwenye kutunga uongo, ni kuwadi wa fisadi
Wapo wajitangazao, bila wao hatuendi,
Wanadai nchi yao, wengine tuko sitendi,
Wadunda kivyaovyao, maswali hawayapendi,
Watambao kifisadi, ni kuwadi wa fisadi!
Wapo wanaogawana, hazina za nchi yetu,
Kwa mafungu wapeana, wala hawajali kitu,
Tukihoji wananuna, mitima yajaa kutu,
Amlindaye fisadi, ni kuwadi wa fisadi!
Wapo wanaotazama, mafisadi wakiyeya,
Wamekubali kutama, wahalifu wapepeya,
Mwenye kuchuma achuma, kwao yote ni muuya,
Aliyekata tamaa, ni kuwadi wa fisadi!
Wapo wanaobariki, pale wanaponyamaza,
Kwa kimya wanaafiki, mlango wamevugaza,
Kumbe ndio manafiki, kwa kimya wanatuuza,
Mwenye kukaa kimya, ni kuwadi wa fisadi!
Wapo wale wanaswao, kwa mbinu za mikuyati,
Washikwa kama mbachao, hawana tena sauti,
Wacheza ngoma si yao, wamebanwa katikati,
Rafiki yake fisadi, ni kuwadi wa fisadi!
Wapo wale wakanao, hadharani wanapinga,
Kumbe ndio hao hao, sirini wamejifunga,
Gizani wapewa vyao, mafisadi wanaringa,
Fisadi wa sirisiri, ni kuwadi wa fisadi!
Hoja nimeshaitunga, beti hazienda tena,
Mwenye hoja za kupinga, kizuizi mimi sina,
Toka Iringa na Tanga, na magwiji kila kona,
Fisadi ndiye kuwadi, kuwadi wake fisadi!
Shairi hili nimeliweka kwa heshima na kumbukumbu ya Mwalimu wangu wa Kiswahili Marehemu Mzee Hamisi Akida (wengi mlikuwa mkisikia kwenye RTD kipindi cha "Lugha Yeto" akiwa na kina Prof. Zakaria Mokiwa) aliyefariki katikati ya wiki hii. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amin.
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
Email: mwanakijiji@klhnews.com
+ 1 248 686 2010