Igunga: NEC kuamua hatma ya CCM, Chadema leo

Mungi

JF Gold Member
Sep 23, 2010
16,975
9,566
Na Sharon Sauwa




12th September 2011




Kiravu%2811%29.jpg

Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa na mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Leopard Mahona, dhidi ya wagombea wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mahona alikata rufaa dhidi ya wagombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu na Joseph Kashindye wa Chadema, akidai kuwa bado ni watumishi wa umma.
Dk. Kafumu kabla ya kuteuliwa na NEC kugombea, alikuwa Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, wakati Kashindye alikuwa Mkaguzi wa Elimu wa Wilaya ya Igunga.

Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu, jana alisema kuwa uamuzi huo utatolewa leo.

“Tutawapa uamuzi huo kesho (Jumatatu), alisema Kiravu alipozungumza na NIPASHE jana.


Wiki iliyopita, Ofisa wa Uchaguzi wa Igunga, Mary Bayo, alithibitisha kupokea rufaa hizo na kuziwasilisha NEC.

Alisema katika rufaa hiyo, Mahona anadai wagombea hao bado ni watumishi wa serikali kwa hiyo wana maslahi ya serikali kwa kutumia kifungu cha Katiba namba 67 (G).

Hata hivyo, Bayo, alisema hatua ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Protace Magayane, kutupilia mbali pingamizi hizo ilitokana na kuangalia kifungu cha Katiba namba 72 kinachowaruhusu kuendelea na taratibu hizo hata kama ni watumishi wa umma.

Alifafanua kuwa utumishi wa umma hukoma mgombea akiteuliwa na NEC kuwania nafasi ya uongozi na pia aliangalia waraka mkuu wa umma wa mwaka 2000.

CHADEMA YAMBANA NCHEMBA
Katika hatua nyingine, Chadema kimempa siku saba Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM, Mwigulu Nchemba, kuthibitisha madai yake kwamba chama hicho kilimmwagia tindikali kijana wa chama hicho, Musa Tesha, lasivyo watamfikisha mahakamani.

Mratibu wa Kampeni za Uchaguzi Jimbo la Igunga, Waitara Mwikabe, aliwaambia waandishi kuwa Mwigulu alitoa kauli hiyo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika juzi mjini hapa.

“Kitendo cha kudai kuwa Chadema ndio wamemwagia tindikali kijana Musa Tesha ni kitendo cha uzushi, uongo na utapeli wa kisiasa na hakivumiliki hata kidogo,” alisema Mwikabe.

Alisema chama chake kimekuwa kikifanya kampeni kwa uwazi mkubwa na hakina vikundi vyovyote vya siri.

Alisema vijana wa CCM ndio waliratibu zoezi la kummwagia tindikali kijana huyo, ambaye alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi juzi.

Pia alisema Mwigulu anasahau kwamba chama chake kiliwakata watu mapanga katika chaguzi mdogo za ubunge katika majimbo yaTarime, Kiteto, Busanda na Biharamulo.

Aidha, alidai kuwa CCM imeanza kuwakamata wafuasi wa Chadema vijijini wakiwatisha, watendaji wanawahoji wananchi kwanini wamepandisha benderea za chama hicho.

Alidai pia wanawatisha wamiliki wa mahoteli na viongozi wanaoishi katika mahoteli waliyopanga mjini Igunga, jambo ambalo alisema chama chake kimekwisha kuripoti polisi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Kuhusu tuhuma za kupandisha bei ya pamba, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alimtaka Mwigulu kuonyesha uthibitisho wa barua anayodai kuwa iliandikwa na Chadema kuwa bei ya pamba isipandishwe.

“Mi nasema hivi kama hadi Jumanne hajatoa hiyo barua tutatangaza Mwigulu ni Mbunge mwongo na tutaendelea kutangaza hilo hadi jimboni kwake ili Watanzania wajue ni aina gani ya wabunge wanao, kama ni muongo kwenye jambo dogo kama hilo je, kwenye mambo makubwa?” alihoji.

Alisema Mwigulu anasahau Chadema ndicho kinasema kuwekwa kwa mfuko maalum kwa ajili ya mazao makubwa ili bei katika soko la dunia itakaposhuka mwananchi aendelee kupata bei yake.

Kuhusiana na ugawaji wa chakula, Mwikabe, alisema Chadema haina ugomvi na ugawaji wa chakula unaofanywa na serikali kwa wananchi.

Hata hivyo, alisema kuwa chakula kinachopelekwa Igunga kinapelekwa kwa madhumuni ya kisiasa kwa sababu kimekuwa kigawiwa kupitia wenyeviti wa vijiji wa CCM, mabalozi ambao wamekuwa wakiwauliza kadi za vyama vyao kabla ya kuwagawiwa chakula. Alitaka vyama vyote vya siasa vishirikishwe katika zoezi hilo iwapo vinagawiwa wakati wa kampeni ili viweze kuona kama kinagawiwa kwa haki.

CUF WAJIBU HOTUBA YA MKAPA
Kwa upande wake, CUF kimejibu mapigo ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, dhidi yao kuwa hawajaleta maendeleo nchini kwa kumkumbusha kuwa hawajashika serikali hivyo hawana fedha za kuleta maendeleo. Mkapa juzi wakati akizundua kampeni za CCM alihoji wapinzani wamefanya nini katika maendeleo ya nchi.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema wapinzani wanaweza kupimwa katika suala la kuwapelekea wananchi maendeleo pale watapoongoza serikali na kusimamia kodi za wananchi.

Mtatiro pia aliwataka wananchi wa Igunga watakaopata chakula cha msaada na misaada mingine kupokea, lakini watambue kuwa wana wajibu wa kuwaondoa CCM madarakani.

Mtatiro, aliwaambia waandishi wa habari jana na kuhoji kuwa: “Uchaguzi ndio serikali inakimbia kuja Igunga na madebe ya mahindi, hivi Mkapa na CCM wanawafanya Watanzania hawana akili na hawatambui hali halisi ya nchi?”




CHANZO: NIPASHE
 
Ibara aliyotumia mahona inasomeka hivi:
Ibara ya 67. (2)mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge (f) ikiwa mtu huyo ana masilahi yoyote katika mkataba wa serikali wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalum kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo.

lakini ibara ya 72 ya katiba inawaruhusu watumishi wa serikali kuomba nafasi ya kuchaguliwa kuwa wabunge, ambapo inaeleza hivi: ibara ya 72. (b) kuwa mgombea wa uchaguzi wa ngazi yoyote katika chama cha siasa kinyume na masharti ya ajira, mtu huyo atahesabiwa kuwa utumishi wake umekoma tangu tarehe yake ya kuwa mgombea uchaguzi au ya kugombea uongozi katika chama cha siasa.

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom