IGP Sirro amuapisha na kumpa majukumu Kamishna wa Polisi Zanzibar

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amemtaka Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Hassan Haji kutatua changamoto zinalolikabili jeshi hilo ikiwemo viashiria vya ugaidi.

Sirro ametoa kauli hiyo leo, Februari 12, 2018 wakati akimuapisha kamishna huyo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuna matukio ya uhalifu yanatokea nchini yakichunguzwa yanaonyesha viashiria vya ujambazi wa kutumia silaha na ugaidi kwa namna yanavyotokea.

“Suala la matukio ya ugaidi ni dunia nzima na yakitokea hayachagui hapa Tanzania au wapi. Sisi pia tuna matukio yenye viashiria vya namna hiyo, hivyo huna budi kuyafanyia kazi pia,” amesema IGP Sirro.

Amesema changamoto nyingine inayolikabili jeshi hilo ni kuchelewa kwa upelelezi wa kesi.

“Kuna kesi zinawahusisha na wenzetu hivyo kuna mambo mengi, ya kuandika barua kwa watu wa dawa za kulevya na taasisi zinazohusika na masuala kama hayo,” amesema.

“Pia ikikamilika inapelekwa kwa mkurugenzi wa mashtaka, hivyo kuna haja ya sisi kukaa na kujipanga namna ya kukabiliana na suala hili.”

Amesema jambo jingine ni rushwa kwa sababu tafiti mbalimbali bado polisi inakabiliwa na changamoto hiyo huku akilitaja jingine kwa kamishna huyo analopaswa kulifanyia kazi ni nidhamu.

“Lazima tuwe na nidhamu ya muda, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma. Nidhamu ya mali za umma, asiye mzalendo na maadili haya achukuliwe hatua na hatua zetu zinajulikana ni ngumu ikiwamo kufukuzwa, ”amesema Sirro.

Kwa upande wake, Kamishna Haji amesema amesikia vipaumbele hivyo na yupo tayari kuvifanyia kazi.

“Nitayafanyia kazi kwa uadilifu mkubwa yale yote niliyoelekezwa na IGP,” amesema Kamishna Haji.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom