IGP Mwema, busara za Uchaguzi Mkuu umemuuzia nani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

IGP Mwema, busara za Uchaguzi Mkuu umemuuzia nani?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ibrah, Jan 8, 2011.

 1. Ibrah

  Ibrah JF-Expert Member

  #1
  Jan 8, 2011
  Joined: Mar 22, 2007
  Messages: 2,721
  Likes Received: 36
  Trophy Points: 145
  VURUGU NA MAUAJI YA ARUSHA
  IGP Mwema, busara za Uchaguzi Mkuu umemuuzia nani?

  Tarehe 5 Januari mwaka huu 2011 Watanzania, hususani wakazi wa Arusha hawataisahau. Haitasahaulika kama haitatokea tena ingawa kwa utendaji kazi wa Askari Polisi wetu kufanya kazi nje ya busara kwa kutumainia risasi na mabomu huenda ikaja kuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida baina ya Wanachama na Wapenzi wa Vyama vya Upinzani pamoja na wenye mapenzi mema na mustakabali wa nchi dhidi ya Polisi. Hii ni kwa sababu Wapinzani wanayo haki ya Kikatiba ya kukusanyika wakati Polisi wetu wanayo haki ya kimabavu ya kukataa na kutumia nguvu pale Wapinzani wanaposhinikiza kuandamana.

  Yaliyotokea tarehe 5 Januari 2011 yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Polisi wetu kupenda kufanya kazi kwa matakwa ya Wanasiasa badala ya matakwa ya kisheria. Baada ya Mbunge wa Arusha kupigwa na Polisi siku ile ambayo Serikali, kupitia Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa kushirikiana na CCM Taifa na Madiwani wake walipoamua kukanyaga haki za wapinzani kushiriki kwenye mchakato wa kumchagua Meya wa Jiji la Arusha. Ni Serikali hiyo hiyo kupitia Mkurgenzi wa Jiji la Arusha Bw Estomih Chang’a walishinikiza Uchaguzi huo batili na kusababisha kupigwa, kujeruhiwa hadi kupoteza fahamu kwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mh. Godbless Lema. Ni vema Serikali ya Mkoa na Taif ikukmbuke kuwa Mbunge ni chaguo la Wananchi na sisi wananchi tuna macho ya kuona na akili ya kupambanua pale ambapo haki imetendeka.

  Vurugu za tarehe 5 Januari ambazo zilisababisha kupotezwa kwa maisha ya Raia watatu ambao ni vigumu sana kuwahusianisha na vurugu zile ambazo kwa kiasi kikubwa zilichangiwa na Jeshi la Polisi kuzoea kukandamiza haki za Wananchi kukusanyika na kutoa maoni yao kwa mujibu wa Katiba. Baada ya tukio la kupigwa kwa Mbunge Lema mwezi Desemba 2010 , CHADEMA walitangaza kufanya maandamano ya kupinga kufanyika kwa Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha na kitendo cha Polisi kumpiga na kumsababishia maumivu Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema. Mkuu wa Polisi wa Mkoa Thobias Andengenye ambaye ndiye aliyetoa amri ya kupigwa kwa Mbunge Lema na amri yake kutekelezwa ipasavyo na OCD wake alipiga marufuku maandamano ya awali ya CHADEMA mjini Arusha na Polisi na CHADEMA wakakubaliana kuwa maandaano na mkutano vifanyike tarehe 5 Januari 2011.

  Busara ya viongozi wa CHADEMA ilionekana hapo baada ya kukubali kuahirisha Mkutano na maandamano ya Desemba 2010 kwa ahadi ya Polisi kuwa maandamano na mkutano vitafanyika Januari 5, 2011; busara hiyo ndiyo ambayo bila shaka Polisi waliichukulia kuwa ni woga na siku chache kabla ya tarehe maandamano IGP Mwema ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kupitia vyombo vya habari akatangaza kufutilia mabali maandamano hayo. Pengine IGP Mwema na RPC Andengenye walishajikusanya na kujiaanda vya kutosha kukabiliana na maandamano hayo na ndiyo maana ilipofika tarehe 5 Januari 2010 siku iliyopangwa maandamano (baada ya CHADEMA) kukataa kuahirisha maandamano hayo haikushangaza Jiji la Arusha kutamalakiwa na Askari wengi na magari mengi kiasi ambacho hatukuona hata wakati ule wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010. Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, IGP Mwema aliongoza Poilsi wake kwa busara ya hali ya juu ambayo hatukupata kuiona katika chaguzi za awali enzi za Mahita. Ni busara za IGP Mwema wakati wa Uchaguzi ndizo zilizoepusha maafa ambayo yangeweza kutokea wakati ule maana ilifanyika mikutano mikubwa kote nchini ambayo mingine iliambatana na maandamano yasiyo na vibali ambayo yaliongozwa na Wanasiana wenyewe ama kwa shinikizo la wapenzi wa vyama vyao au kwa utashi wao wenyewe. Wanasiasa kama Dk. Slaa na Prof. Lipumba waliweza kuwadhibiti wapenzi wao kwa diplomasia ya hali ya juu na hatukusikia vurugu na umwagaji wa damu kama uliotokea Arusha tarehe 5 Januari 2011.

  Yawezekana Polisi wetu ilibidi wawe wapole kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kukabili maandamano na mikutano ya Kampeni wakati ule kwa kuwa mambo hayo yalifanyika kwa utawanyiko na kama wangetumia nguvu, wasingeweza kudhibiti vurugu za wakati ule na hivyo kumlazimisha IGP Mwema kuazima busara za muda ili kutunza amani na kwa wakati ule alifanikiwa. Siku ambayo Wananchi wa Arusha Mjini waliposhinikiza kutangazwa matokeo ya Ubunge nilipita mara kadhaa Ofisi ya Jiji kufuatilia kilichokuwa kinajiri. Idadi ya Wanachi waliojitokeza siku hiyo kushinikiza matokeo kutangazwa ilikuwa kubwa na kusabisha barabara za kuingia na kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Jiji zilifungwa na Wananchi. Pia kulikua na Posi na Magari yao na Washawasha lao, na kwa hakika, munkari wa wananchi wale ulikuwa mkubwa sana kiasi ambacho Polisi waliomba msaada wa Askari wa majeshi mengine ili kujaribu kudhibiti fujo ambazo pengine zingetokea mahali pale. Ajabu ni kuwa pamoja na mashabiki wa CHADEMA hasa vijana kuimba na kucheza mbele ya magari ya Polisi na Polisi kuwa kwenye tahadhari hakuna vurugu zozote zilizotokea! Mkusanyiko ule uliwatisha Wafanyabiashara wa katikati ya Jiji la Arusha ambao siku hiyo walifunga biashara zao ilipofika saa 4 asubuhi! Ninachojiuliza na kukiona ni kuwa Polisi hawakulazimisha watu watawanyike labda kwa kuwa nguvu yao ilikuwa ndogo mno kuweza kuwakabili umati ule maana mambo hayohayo ya kulazimisha kutangazwa matokea yalikuwa yakiendelea majimbo ya jirani na isngewezekana kuhamisha Poisi wa Karatu au Moshi kuja kuwatawanya watu wale. Lakini pia yawezekena kuwa Polisi hawakutumia nguvu siku ile kwa ajili ya busara aliyokuwa nayo Mkuu wa Polisi wa Mkoa wakati ule RPC Basilio Matei ambaye inasemekana baada ya kuona hamasa ya raia imekuwa kubwa na jua linazama alitoa shinikizo kwa Mkurugenzi wa Jiji Estomih Chang’a kutangaza matokeo kama yalivyo! Ukweli ni kuwa Wananchi walishajua matokeo baada ya kukusanya matokeo ya kila kituo na wengi waliamaini kuwa kulikuwa na mchezo unachezwa ili kuvuruga matokeo hayo. Wananchi wa Arusha wanaamini kuwa RPC Matei alihamishwa kwa ajili ya busara yake na kutaka kuona haki inatendeka siku ile ya kutangaza matokeo ya Ubunge ya Arusha Mjini; kwa yaliyotokea tarehe 5 Januari 2011, wananchi wamethibitisha kuwa ni kweli RPC Matei aliondolewa Arusha kwa kuwa hakuwa tayari kushinikizwa na Watawala vinginevyo mabaya zaidi yangetokea siku ile!

  Vurugu za wiki iliyopita Jijini Arusha zimefunua mambo makubwa mawili; kwanza, Jeshi la Polisi lina uwezo mdogo sana wa kupambana na ghasia za Kisiasa; pili, wananchi wa nyakati hizi ni tofauti na miaka iliyopita.

  Ingawa Polisi walikuwa wengi lakini ilidhihirika kuwa bado hawana mbinu za kisasa za kupambana na vurugu. Matumizi ya risasi za moto badala ya zile za mpira yanaonyesha dhahiri kuwa Jeshi letu halina vifaa vya kutosha kukabiliana na vurugu na hivyo kutumia busara kungeweza kabisa kuepusha maafa yaliyotokea.

  Vizingizio vya taarifa za kiintelijensia kuzima na kufinya haki za watu kumepitwa na wakati na yaliyotokea Arusha yameonyesha jinsi gani taarifa za kiinteligensia za Polisi ama zilikwa za kubuni ili kuzima maandamano ya CHADEMA au hazikuwa sahihi. Hii ni kwa sababu Polisi walipowakamata viongozi wa CHADEMA hapakuwepo na uvunjifu wowote wa amani zaidi ya maguvu yao waliyotumia kuwakamata viongozi hao.

  Tangu uchaguzi wa vyama vingi uanze nchini mwaka 1995, hakujawahi kutokea maandamano yoyote haramu ukiondoa yale ya uchochezi ya Mtikila pale Jangwani ambapo Watanzania wenye asili ya Asia walishmbuliwa na waandamanaji baada ya Mkutano wa Mtikila pale Jangwani. Ikumbukwe kuwa wakati ule Wananchi walikuwa na kawaida ya kumbeba ‘Mtetezi’ wao Mtikila kila baada ya mikutano yake kitu ambacho kiliwakera sana Polisi na kuamua kuingilia kati na kuzusha vurugu baina ya waandamanaji na Polisi.

  Hata enzi za Upinzani wa Agustine Mrema, wananchi walikuwa wakimbeba Mrema kiasi kwamba Polisi wakawa wanaingilia kati na kuleta mitafaruku isiyokuwa na sababu hadi Hayati Mwalimu Nyerere alioonekana kukerwa na tabia ya Polisi na Serikali kuingilia mikutano ya Mrema na kusababisha vurugu kila wakati na kuwaambia Polisi kuwa kama watu wameamua kumbeba Mrema wao inawakrea nini? Ndio Polisi na Serikali zikaamua kuwa kimya na hatimaye ule mzegamzega ukaoteza umaarufu wenyewe na wananchi wakachoka kumbeba-beba.

  Baada ya uchaguzi wa 1995, maandamano mengi ya wapinzani imekuwa ikifanyika kwa kuruhusiwa na hata bila kuruhusiwa na Polisi. Vurugu na fujo zimekuwa zikitokea pale tu Polisi wanaoamua kuingilia kati maandamano ywa Wapinzani na kusababisha upotevu na uharibifu wa mali za wananchi kwa sababu za kiitelenjensia zinazopelekea Polisi kutaka kuzima maandamano hayo.

  Nionavyo mimi, dudu hilo la intelejensia huundwa makusudi na Polisi ili kuhalalisha matumizi ya nguvu dhidi ya Wananchi kwa manufaa ya watawala; ikiwa Polisi wataamua kuongoza misafara ya maandamano ya Wapinzani kila wanaotaka, ni wazi kuwa hata mbinu hiyuo ya maandamanao itachuja yenyewe taratibu, lakini Polisi wanaposhindwa kuzifuatilia habari za intelejensia kuwananasa wahalifu kabla ya maandamano na kujiingiza kwenye matumizi ya nguvu matokeao yake ni kuongezeka kwa chuki dhidi ya Jeshi hilo na Watawala kwa ujumla. Waathirika wakuu ni Watawala ambao itabidi watafue mbinu za hali ya juu za uchakachuzi wa matoke ya uchaguzi ifikapo 2015.

  Nimeambatanisha picha za wananchi wa Arusha Mjini waliokuwa mbele a Ofisi za Jiji kushinikiza matokeo ya Ubunge kutangazwa ambapo baadhi ya barabara zilifungwa, polisi walikuwepo na hawakutumia nguvu. Matokeo yalipotangazwa waananchi walitawanyika kwa amani.   

  Attached Files:

 2. The Dreamer

  The Dreamer JF-Expert Member

  #2
  Jan 8, 2011
  Joined: Feb 2, 2009
  Messages: 1,280
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ahsante mkuu. Kuna kaka mmoja hapo ana bango kubwa "CCM na mali zao CDM na wananchi wao" Hii imenikumbusha jinsi makamba alivyolilia mali za ccm badala ya maisha yaliyopotea. kweli makamba na mali zake
   
 3. Ibrah

  Ibrah JF-Expert Member

  #3
  Jan 8, 2011
  Joined: Mar 22, 2007
  Messages: 2,721
  Likes Received: 36
  Trophy Points: 145
  Hilo bango linapendeza sana kuwa Avatar ya Mchukia Fisadi!
   
 4. Mungi

  Mungi JF Gold Member

  #4
  Jan 8, 2011
  Joined: Sep 23, 2010
  Messages: 16,986
  Likes Received: 444
  Trophy Points: 180
  Asante muungwana, hii ndiyo Arusha ya wazalendo wa kweli wa nchi yao.
  Wana wa nchi inatakiwa tuikomboe nchi yetu kutoka kwa mafirauni wa CCM.
   
Loading...