Ifahamu Wizara ya Katiba na Sheria na majukumu yake

Feb 28, 2021
42
84
IMG_20210313_160235_031.jpg


Ndugu WanaJF,

Tumeona ni vyema kuitambulisha kwenu wizara hii na majukumu yake ili kuifahamu vizuri.

Ni matarajio yetu kuwa Utambulisho huu utasaidia pia wadau kuuliza maswali sahihi yahusuyo wizara.

KUHUSU WIZARA

Wizara ya Katiba na Sheria ndio muhimili mkuu wa Serikali katika masuala yote ya kisheria katika nchi.

Majukumu ya Wizara ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa kuzingatia utawala wa sheria na misingi ya Haki za
Binadamu kwa kusimamia utoaji haki, hifadhi ya Katiba, kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na taasisi zake, kusimamia hifadhi ya haki za binadamu na kuhakikisha sheria na taratibu za nchi zinafuatwa.

Kwa ujumla, Wizara hii inalo jukumu la kuhakikisha kunakuwepo mfumo wa sheria unaotoa fursa sawa kwa
watu wote katika jamii kuweza kuendesha shughuli zao kwa ufanisi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

DIRA NA DHIMA

Wizara ya Katiba na Sheria inaongozwa na Dira ambayo ni Katiba na Sheria wezeshi kwa maendeleo ya Taifa.

Aidha, Dhima ya Wizara ni kuwa na mfumo madhubuti wa kikatiba na Sheria wenye kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa.

Dira na dhima hizi zinalenga kuweka mazingira rafiki ya kisera na ya kisheria ya kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, kudumisha hali ya amani, utulivu na utangamano wa kitaifa ambazo ni nguzo muhimu kwa mustakabali wa ustawi wa jamii na Taifa letu katika kujenga mazingira wezeshi ya upatikanaji haki na huduma bora za kisheria kwa wakati.

Wizara ya Katiba na Sheria inajumuisha Muhimili wa Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Pia RITA, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto.

Katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kuwa nchi inaongozwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi zake inaendelea
kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Hati ya Mgawanyo wa Majukumu kwa Mawaziri, kupitia Tangazo la Serikali Na. 144A la tarehe 22 Aprili, 2016 na sheria nyingine za nchi.

MAJUKUMU 12 YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

1. Kutunga Sera zinazohusu masuala ya kisheria na kusimamia utekelezaji wake

2. Kushughulikia mambo ya kikatiba

3. Kusimamia mfumo wa haki na utoaji haki

4. Uandishi wa sheria

5. Kuendesha mashtaka

6. Kushughulikia uendeshaji wa mashauri ya madai na mikataba mbalimbali inayohusu Serikali na uratibu wa sheria za kimataifa

7. Kushughulikia masuala ya haki za binadamu na msaada wa kisheria

8. Kurekebisha sheria

9. Kushughulikia urejeshwaji wa wahalifu na masuala ya ushirikiano wa kimataifa kwenye makosa ya jinai

10. Kusajili matukio muhimu ya binadamu (vizazi, vifo, ndoa, talaka na uasili), ufilisi na udhamini

11. Kuboresha utendaji na maendeleo ya rasilimali watu iliyo chini ya Wizara

12. Kuratibu shughuli za taasisi, mipango na miradi chini ya Wizara.

Aidha, kulingana na mabadiliko ya muundo wa Wizara ya mwaka 2018, Wizara imeongezewa jukumu la kuratibu masuala ya utajiri na maliasilia za nchi kulingana na matakwa ya Ibara youra 9 na 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Sura ya 2) ili kuhakikisha rasilimali hizo
zinalindwa, zinaendelezwa, zinatumika, na zinasimamiwa kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom