Idara ya Ustawi wa Jamii ipo ipo tu ?

Iga

Senior Member
Dec 17, 2007
112
0
Katika idara ambazo hazibahatiki kuwa na watu wanaozifuatilia na kudhibiti utendaji wake hapa nchini ni idara muhimu zaidi kwa watu masikini, wanyonge na dhaifu katika jamii kuliko zote-Idara ya Ustawi wa Jamii ! Si viongozi wala wanasiasa wa upande wowote wanaonesha kuwa eneo hili lina maslahi na umuhimu kwao binafsi na kwa vyama vyao. Hali hii ni lazima ibadilike. Na hasa tukizingatia serikali yetu imekuwa legevu, vivu na bahili katika kusaidia masuala ya ustawi wa jamii karibu katika kila eneo husika.

Jamii wakati wowote huwa na watu wanaopaswa kuangaliwa na wanajamii wengine kutokana na sababu mbalimbali. Sababu hizo ni pamoja na uzee, ulemavu, maradhi, uyatima, umaskini na magonjwa ya akili.

Katika jamii pia wamo watoto ambao kwa hali yao wanaruhusiwa pia kuangaliwa na wazazi wao au walezi wao kwa aina moja au nyingine. Watu ambao kwa muda pia huwa hawana kazi inayowapatia riziki yao ya kila siku hulazimika pia kuangaliwa na wanajamii.

Kwa bahati mbaya ile inayoitwa Idara ya Ustawi wa Jamii nchini hapa inaonekana kuwa ni idara sio tu ya kutangatanga (na kuna jina baya ambalo sithubutu kulitaja inayopewa idara hiyo.) bali ni idara ambayo aidha yenyewe haijui inachokifanya, au waliomo ndani yake hawajui wanachostahili kukifanya au imeundwa kama sehemu ya kuwatupa watu fulani wasio na imani au huruma kwa aina ya makundi ya watu tuliowataja. Badala ya idara hiyo kuwa kimbilio na faraja kwa watu wa aina hiyo, sasa hivi kuna watu wanayoiona kama yenyewe ni mzigo na tatizo.

Idara hii ili kuwa faraja ni lazima isaidie washikadau wake walioorodheshwa hapo juu. Mathalani, wazee leo wangelikuwa wanatunzwa na kuangaliwa mahala fulani ambapo wangeumaliza uzee wao kwa raha mustarehe au angalau bila taabu, dhiki na maudhi wanayokutana nayo sasa.

Nimetembelea koo kadhaa mijini na vijijini na kubaini kuwa tatizo la ni nani anayestahili kuwaangalia wazee sasa limezidi kuwa kubwa na aghalabu nje ya uwezo wa wanafamilia au wanaukoo. Ninaamini jawabu la tatizo hili liko nje ya mtu au familia moja moja. Ni tatizo la kitaifa na linatakiwa lishughulikiwe kitaifa. Lakini sio na idara ambayo haina shabaha au malengo yoyote mbele yake yanayojulikana achilia mbali kudhihirika.

Haitakuwa kitu cha kushangaza kuona jinsi kadri wazee wetu wanavyozidi kuhangaika basi siku moja baadhi yao wakaamua kukomesha maisha yao kutokana na dhiki na mashaka makubwa uzeeni. Kitaifa inaonekana wakubwa kwa kuwa taifa linawaangalia wao hawana habari na wazee wenzao hohehahe ili mradi wao mahitaji yote wanatimiziwa. Kadri jambo hili litakavyokuwa nje ya katiba ya nchi basi tusitegemee kabisa viongozi wastaafu na watumishi wa umma wastaafu kama watahangaika kuhakikisha kuwa wazee wote wa Kitanzania wanaipata nafuu kama ile wao wanayoipata uzeeni.


Ni nani anayestahili kuwaangalia mayatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu, watoto wa mafukara wa kutupwa na watu kama hao. HIli kama inavyoonekana sasa limetoa mwanya kwa wajanja wachache kujifanya wana huruma ya kuangalia watu kama hao lakini kumbe ni miradi ya kujinufaisha wao wenyewe pale wanapowadanganya wafadhili wa ndani na nje na kisha fedha zikaanza kutiririka kwenye akaunti zao. Aghalabu, fedha hizo huishia katika wajanja hao kujenga majumba ya kifahari na kununua motokari za bei mbaya.

Changamoto kwa upande wa walemavu, wagonjwa, wendawazimu na wajane nazo ni kama hapo juu. Mfumo mzima wa kijamii na kiuchumi bado kujengwa kwa ajili ya kuwafaa na kuwasaidia watu kama hawa. Lakini idara yenyewe inavyoendesha mambo yake ni kama vile inahitaji zaidi ya miaka mia moja kutekeleza hata yale mambo ya msingi ambayo nchi nyingine duniani yamekwishayatekeleza.

Ukizungumzia malezi ya watoto na vilevile hifadhi ya watu wasio na kazi kwa muda fulani nayo ni ya kusikitisha na kukatisha tamaa. Ni kama vile hakuna msaada wowote mtu anaopaswa kutegemea pindi akijikuta katika rika au masahibu ya aina fulani. Nchi yetu bado haijawa na mfumo wa mwenye nacho kumwangalia asiye nacho, wala mfumo wa kumsaidia kumrudisha yule anayeharibikiwa na mambo yake akatoka hali bora na kuwa hali duni.

Nitashtuka sana nikiambiwa kwamba idara yetu ya ustawi wa jamii ina mpango wa miaka mitano achilia mbali mpango-mkakati (strategic plan) kuhusiana na maeneo hayo hapo juu ambayo nimeonesha inastahili kuyashughulikia. Hata kama kutakuwa na mpango hiyo nina hakika hakuna wakati hata mmoja ulipowahi kutekelezwa kwa dhati. Yaani, jinsi idara yenyewe inavyokwenda kwenda haioneshi kabisa kama imetazama mbele miaka 10 achilia mbali inayokuja kama vile ambavyo idara kama hii sehemu nyingine duniani inastahili kutazama.

Makala haya yanaandikwa baada ya kuona kwamba pamoja na wizara hiyo kutokuwa na mpango unaofahamika wa kushughulikia matatizo ya kijamii yaliyopo idara hiyo leo inakuwa ndio kikwazo kikubwa kwa juhudi za watu binafsi wanaotaka kufanya kazi ambayo idara hiyo ilistahili kuwa ndiyo inayozifanya.

Kuna mama mmoja wa Kiswiss (Jina limehifadhiwa) alikuwa na kituo cha kulelea watoto yatima na wanaotoka katika familia masikini hapa jijini. Kwa bahati mbaya mama huyo alianza kuugua na akashindwa kufanya kazi hiyo na kurudi kwao Uswizi. Kituo chake kikalazimika kufungwa kwa miaka kadhaa. Baada ya kufariki mama huyo aliacha usia kwa binti yake kwamba pindi akifariki basi changamoto kwake ni kuja kukifufua kituo hicho na kuhakikisha kinafanya kazi tena. Mama huyo akaacha fungu maalum la fedha kwa ajili ya kazi huyo.

Kutoka uswizi pamoja na kuwa na mchumba, haikuwa kazi. Kazi ilianza hapa Dar alipokuja kufungua kituo akidhani kibali kile cha zamani kinamruhusu kuendelea na shule yao. Maofisa ustawi wa jamii walizuka huko walikozuka baada ya kuambiwa na wambeya na badala ya kuchukulia kwa ustaarabu 'ishuu' nzima wakaanza kuwatisha na kuwanyanyasa wageni hao (nisingependa kurudia unyama na majivuni ya maofisa wa idara hiyo) lakini kwa kuwa binti alikuwa akiongozwa na usia wa mama yake ameendelea kuvumilia upuuzi wa maofisa hao.

Wilaya inayoongoza kwa kuwa na maofisa 'uuaji'
ustawi wa jamii katika mkoa Dar es salaam pamoja na kuwa na maofisa wachache wasafi wasiosukumwa na rushwa na maslahi binafsi ni wilaya ya Kinondoni. Katika wilaya hii kuna mama 'muuaji' ustawi wa jamii ambaye kwa kiasi kikubwa amechangia masahibu yanayomkuta huyu binti wa Kiswizi. Ningelipenda kumuuliza, ingelikuwa yeye ndiye hayati mama wa binti huyu huko aliko akhera angelifurahia yale yanayomuta binti yake ? Na, je, kashkash na ugumu anaoufanya kuhusiana na uanzishwaji tena kituo hiki cha kulea watoto haoni kinanuka harufu ya mazingira ya kutaka rushwa au fursa ya yeye kuleta watoto wa ndugu na jamaa zake kituoni hapo na wale ambao wenye kituo wenyewe wanawataka wasipokelewe ?

KWA KIFUPI BINTI HUYO ANAHITAJI KUKIFUNGUA TENA KITUO CHA KULELEA WATOTO YATIMA NA MASIKINI JIJINI. JE, TATIZO HAPA LIKO WAPI. HUYU NI MTU WA KUSAIDIWA NA KUTETEMEKEWA AU WA KUPUUZWA NA KUENDESHWA PUTA WIKI NENDA, WIKI RUDI ?

Idara ya Ustawi wa Jamii ingelikuwa na uwezo basi ingelikuwa na vituo tosha kwa ajili ya kazi hiyo. Binti huyo ana haki ya kuanzisha upya kituo cha mama yake bila kuingiliwa na mtu yoyote. Maofisa hao wanapotaka kuwachaguliwa wenyewe watoto wa kulea wana maana gani. Si ubabe na maguvu tu yanatumika hapa. Wao wenyewe wana watoto waliowaona na wangelipenda kuwatunza. Vipi iwe kinyume cha hivyo. Kila mtoto na bahati yake. Mbona hamuendi kuwanyang'anya wakubwa nafasi za watoto wao za kwenda kwenye shule nzuri au zile za nje lakini mnataka kuwanyima watoto wa masikini bahati iliyowafuata kule wanakoishi?

Hii ni idara ambayo inatia mashaka kama haitumii fedha nyingi kuliko kazi inayoifanya kwa umma wa Watanzania.

Ni idara ambayo waandishi mahiri wa mammbo ya namna hii wameshawahi kuonesha kabisa kwamba kazi zake zote zinaweza kufanywa bure au kwa posho kidogo na vijana wa Kitanzania wanaomaliza shule na wasiokuwa na ajira. Lakini kwa kuwa haya yanaangukia masikioni mwa wale ambao wamezoea kula tu, bila kuwafanyia chochote cha maana Watanzania basi hakuna anayethubutu kulipigia debe ili lifanyike na kuwanusuru maskini na wenye shida na wakati huo huo kuwajenga vyema vijana wa Kitanzania pamoja na kuendeleza udugu na umoja wao.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) likitumika ipasavyo linaweza kuwa na kitengo cha huduma za Kijamii na kazi yake itakuwa ni pamoja na kuwatunza wazee, mayatima, ombaomba, watoto masikini na wale wanaoishi katika mazingira magumu, vichaa, walemavu, wajane na watu wengine wanaohitaji msaada wa aina moja au nyingine. Serikali itahitaji kutenga sehemu ndogo tu ya maduhuli yake pamoja na fedha za wafadhili ili kuhakikisha sio tu huduma zote zinakuwa bora na hali ya juu bali pia vijana hao wa JKT-Kitengo cha Huduma za Jamii wanapata posho ya kuwaridhisha wakati wa kipindi chao cha utumishi wa kati ya miezi mitatu na tisa.

Nina hakika hili likifanyika basi tutegemee mapinduzi makubwa katika idara ya ustawi wa jamii. Sinstoshangaa kuona watu kutoka nchi nyingine za Kiafrika wakimiminika Tanzania kuja kujifunza juu ya uchawi au formula hii ya kutatua matatizo ya kijamii.
 

IHOLOMELA

JF-Expert Member
Nov 2, 2010
1,798
2,000
wana JF kwa kujenga hoja na kuzitetea nawakubali. Lakini hata nyie mkipewa madaraka, mambo sidhani kama yatabadilika. Labda Yesu ashuke toka mbinguni
 

Froida

JF-Expert Member
May 25, 2009
8,759
2,000
mahala popote lazima watu wafuate utaratibu uliowekwa na nchi husika hawa watu wanatoka kwenye nchi zao wakidhani wanaweza kuwa na dhamana ya kulea watoto wa kitanzania bila kufuata misingi ya sheria za vituo vya kulelea watoto yatima n mitaani,hatutaki watoto wetu waishie katika unyanyasaji wa kijinsia ,kisakolojia na kimwili kwa watoto wanaowekwa kwenye vituo hivyo mwandishi ajaribu kufuatilia manispaa ,ndipo wizarani usikurupuke tuu,hawa wenzetu kwao ni miradi zaidi utajiuliza hapa ni uswiss mpaka yeye aondoke afunge kituo manake hakushirikiana na watanzania ambao wangebaki kukiendesha wakati ameenda kuugua,wewe unataka hao watoto walelewe na wageni asilimia mia,duuh bwana idara wasimpe hicho kibali ovyo ovyo tuu wengi ni waharibifu wanageuza watoto wetu ma gineipiggy
 

Bongolander

JF-Expert Member
Jul 10, 2007
5,053
2,000
wana JF kwa kujenga hoja na kuzitetea nawakubali. Lakini hata nyie mkipewa madaraka, mambo sidhani kama yatabadilika. Labda Yesu ashuke toka mbinguni

Tatizo lililopo si kwa kiongozi mmoja tu, ni system nzima imeharibika. Kwa system iliyopo Tanzania hata kama ukileta rais awe Obama na waziri Mkuu awe David Cameron hakuna kitakachobadilika. matokeo yake ni kuwa mambo yatakuwa ovyo zaidi, system ya sasa ni ovyo inaweza kuendeshwa vizuri zaidi na watu wanaoweza kuendana na system kama hiyo.

Mara ya mwisho nilipokwenda kwenye ofisi ya ustawi wa jamii niliona ofisi chafuchafu tu na wafanyakazi wako hoi. Wenyewe wanaonekana hajawajastawi sasa tunatagemea vipi wafanye kazi za kustawisha jamii. By the way jamii yenyewe imesatawi? kimsingi tunaona kuwa jamii haijastawi kwa hiyo kazi ya idara hiyo haina matokeo yoyote mazuri.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom