Idara ya Afya Wilayani Bahi kuchunguzwa kutokana na malalamiko mengi ya Wananchi ikiwemo Wahudumu kuripoti kazini wakiwa wamelewa

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,498
9,279
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeagizwa kuchunguza kwa miezi sita, Idara ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kutokana na kuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi, ikiwamo wanafunzi kutozwa fedha kwa ajili ya kujaziwa ripoti ya afya.

Inadaiwa kuwa wanafunzi hao wanalipishwa kati ya Sh.5, 000 hadi 30,000 kwa ajili ya kujaziwa ripoti ya afya pindi wanapotaka kuripoti shuleni.

Malalamiko mengine ni ukosefu wa dawa, kutotumia mashine za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, wagonjwa kutozwa fedha kwa ajili ya gari la wagonjwa na baadhi ya wataalamu wa afya kuripoti kazini wakiwa wamelewa.

Agizo hilo lilitolewa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo katika kikao chake kilichofanyika juzi wilayani hapa.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Donald Mejitii, alisema idara hiyo imesababisha uwapo wa malalamiko mengi.

Alisema kila siku wanahamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa, lakini wakienda kwenye vituo vya afya wanaambiwa dawa hakuna.

“Rais Magufuli amejitahidi sana katika sekta ya afya, fedha za dawa zimeongezeka, lakini kiuhalisia baadhi ya watendaji huku chini wanamwangusha sana. Wanawatesa wananchi kwa kuwakosesha dawa ilhali tunawahamasisha wajiunge na CHF ili wapate huduma. Hapa utaona kabisa adui namba moja wa CHF ni wataalamu wetu,” alisema.

“Kuna usemi kwamba ‘The speed of the team is the speed of the leader’. Huu ndio ukweli, kama walio juu hawaendi na kasi walio chini yao hawawezi kuwapita. Haiingii akilini idara yenye malalamiko hivi lakini hata siku moja haijawahi hata kuleta onyo kwa watumishi au barua ya kuomba kuchukuliwa hatua ili baraza liidhinishe, haiwezekani,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo, alisema kama baraza ni vyema wakaazimia kwa pamoja kuwa TAKUKURU wachunguze na watoe ushauri.

“Tuwaombe wenzetu TAKUKURU washauri kitaalamu wanaudhibiti vipi huo udokozi na mkuu wa utawala asaidie kurekebisha hii idara,” alisema.

Awali, Diwani wa Ibugule, Blandina Magawa, alishauri idara hiyo kuangaliwa vizuri kwa kuwa inaonekana watumishi wanaonekana kuna mahali wanajivunia.

Naye Diwani wa Bahi, Augustino Ndonuu, alisema kuna ukosefu wa mashine za kielektroniki (POS) kwenye vituo vya afya, hivyo kusababisha halmashauri kukosa mapato yake.

“Ukienda kwenye vituo hakuna hizo mashine, baadhi ya watumishi wanapata mwanya wa kufanya wizi. Mgonjwa anaenda na pesa taslimu ya matibabu, lakini ukichunguza utakuta amewekwa upande wa wagonjwa wanaotibiwa kwa CHF. Hapa ujue tayari wizi umefanyika,” alisema.

Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk. Fatma Mganga, alisema kwa mujibu wa sera ya afya mgonjwa hapaswi kutozwa fedha kwa ajili ya gari la wagonjwa.

“Katika dawa tukihamasisha pia wananchi wengi wajiunge na CHF itasaidia sana katika upatikanaji wa dawa maana fedha itakuwapo, lakini katika suala la watumishi sio la DED peke yake kuwaadabisha bali pale unapoona lete taarifa ili nijue na kuchukua hatua,” alisema.
 
Back
Top Bottom