Idadi kubwa ya mahabusu wanaotuhumiwa kwa mauaji katika Gereza la Mpanda

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,500
9,279
Idadi kubwa ya mahabusu wanaotuhumiwa kwa mauaji katika Gereza la Mpanda mkoani Katavi imewashangaza makatibu wakuu watatu wa wizara na wameamua kufanya uchunguzi kubaini kiini.

Makatibu hao ni Profesa Sifuni Mchome (Katiba na Sheria), Dk Laurean Ndumbalo (Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) na Dk John Jingu (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).

Wakiwa ziarani kwenye gereza hilo walishuhudia idadi kubwa ya watuhumiwa wa mauaji wanaofikia 160 na wamepanga kuunda timu itakayofuatilia kwa nini mkoa huo una watuhumiwa wengi wa makosa ya mauaji.

Makatibu wakuu hao walieleza mshangao huo mwishoni mwa wiki walipotembelea gereza hilo ambako walizungumza na wafungwa na mahabusu kujua changamoto na mchakato wa utoaji haki.

“Hebu wenye kesi za wizi nyosheni mikono, wenye kesi za ubakaji nyosheni mikono, wenye kesi za mauaji nyosheni mikono,” alisema Profesa Mchome.

Hata hivyo, wafungwa na mahabusu walionyosha mikono yao kulingana na makosa yao, robo tatu ya mahabusu hao walikuwa ni watuhumiwa wa kesi za mauaji.

Alipowauliza tena kwa nini kuna idadi kubwa ya mahabusu wenye kesi za mauaji, walijibu kwamba wengi wao wamebambikiziwa kesi hizo, au walikamatwa katika zoazoa ya polisi na kubambikiziwa kesi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa gereza hilo, Moses Mbesela, mahabusu wa kiume wenye kesi za mauaji na waliokuwa wanasubiria kikao wako 71 na wenye kesi ambao upelelezi unaendelea wako 80.

Mbesela alisema upande wa wanawake wenye kesi za mauaji na ambao wanasubiri kikao walikuwa sita na wale ambao upelelezi unaendelea wako watatu.

Kauli ya Mbesela ilimfanya Profesa Mchome kusema; “Cha msingi kuna matatizo hapa, tutaunda timu maalumu kuja hapa ili kuchambua kesi mbalimbali, kuna kesi nyingi za mauaji hapa.”

Alisema timu hiyo pia itashughulikia malalamiko katika eneo la utawala bora na ustawi wa jamii na watashughulikia malalamiko ya kesi zilizowasilishwa kwao.

Profesa Mchome alisema mengine watakayoshughulikia ni malalamiko ya kubambikiziwa kesi, uchukuaji wa mali za watuhumiwa na kwamba timu hiyo itakapoundwa itafanya kazi yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Alisema timu hiyo itakuwa na wajumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa upande wake Dk Ndumbalo alisema atafuatilia na katika ngazi za juu baadhi ya malalamiko ya wafungwa na mahabusu, pamoja maombi yaliyowasilishwa na mkuu wa Magereza Mkoa wa Katavi kuhusu upungufu wa maofisa na askari magereza katika mkoa huo.

Kwa upande wake Dk Jingu alisema, si jambo la kawaida kwa magereza moja kuwa na idadi kubwa ya watuhumiwa wa mauaji kwa kiasi hicho, hivyo akaunga mkono wazo la kuunda timu hiyo na kuangalia shida ipo wapi kwa sababu suala hilo linahusu ustawi wa jamii.

Chanzo: Mwananchi
 
Nchi hii ina mambo ya hovyo na kijinga sana, watu wamejaa chuki visasi na roho mbaya tu na ndio maana watu na nchi kwa ujumla aiendelei.
 
yaani mi nilishasema nikikuta Polisi anapigana na Nyoka namsaidia Nyoka.

hakuna kiumbe wa ajabu Dunia hii kama Polisi waja laana hawa
 
Mama Samia Suluhu kwa bahati mbaya bado anadanganywa sana kwenye jeshi la Polisi kuna matatizo yanayosababishwa na serikali yenyewe kutokulisimamia kikamilifu, sheria ya polisi na polisi wasaidizi inampa mamlaka waziri wa mambo ya ndani kulisimamia na kutoa maelekezo na kutengua maamuzi ya ijp kama yatakuwa yanakiuka sheria lakini kila waziri anayepewa wizara hiyo huwa anaogopa polisi!
Mh. Rais anatakiwa asaidiwe kufanya vetting na walio nje ya polisi ili uteuzi na upandishaji vyeo aufanye kwa polisi wenye uadilifu na uzalendo wa nchi yao.

Anachofanyiwa kwenye uteuzi wa sasa ni kupendekezewa majina na walio njiani kustaafu waache wamejenga mtandao wa kuendeleza uhalifu ndani ya jeshi hilo na pia kuwalinda wao wakiwa nje ya jeshi kwa kustaafu au kutenguliwa.
 
Back
Top Bottom