ICC yamhukumu kiongozi wa waasi DRC kifungo cha miaka 12 jela

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
16,677
2,000

German Katanga wakati wa hukumu yake hii leo huko The Hague, Uholanzi. (Picha: © ICC-CPI)

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague, Uholanzi leo imemhukumu kifungo cha miaka 12 jela Germain Katanga aliyepatikana na hatia ya makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.Akisoma hukumu hiyo Jaji Bruno Cotte amesema wamezingatia mahitaji ya kisheria, ukweli na haki kwa wahanga wa uhalifu uliotekelezwa na familia zao na kuhakikisha kuwa hukumu hiyo itaepusha wanaotaka kutekeleza vitendo hivyo wasifanye hivyo.


Hata hivyo mahakama imeeleza kuwa muda ambao Katanga alikuwepo rumande kuanzia Septemba 2007 hadi Mei 2014 utapunguzwa katika adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 12. Halikadhalika imesema kulingana na mazingira hakutakuwepo na faini yoyote dhidi ya Katanga.


Mwezi Machi mwaka huu Katanga alipatikana na hatia ya makosa matano ikiwemo moja ya uhalifu dhidi ya binadamu na Manne ya uhalifu wa kivita ikiwemo kushambulia raia na uharibifu wa mali.


Ilithibitishwa pasipo shaka kuwa Katanga alichangia kwa kiasi kikubwa kwa vitendo vilivyotekelezwa na wanamgambo wa Ngiti huko Bogoro jimbo la Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mwezi Februari mwaka 2003.
Kesi dhidi ya Katanga ilianza tarehe 24 Novemba 2007.
Adhabu dhidi ya Germain ni ujumbe kwa masalia ya FRPI: MONUSCO

Martin Kobler (katikati) mkuu wa MONUSCO akiwa na baadhi ya maafisa na askari kutoka jeshi la serikali FARDC na lile la kuingilia kati mashambulizi, (FIB) walipofanya ziara karibu na eneo la Tongo, Mashariki mwa DRC. (Picha: UN /Sylvain Liechti)


Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Martin Kobler amesema adhabu ya kifungo cha miaka 12 dhidi ya kiongozi wa kundi la waasi la FRPI nchini humo Germain Katanga ni ujumbe thabiti kwa masalia wake.
Kobler ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO amesema kundi hilo la FRPI bado linaletekeleza vitendo vyake kwenye wilaya ya Ituri na kutishia usalama wa raia.


Hivyo amesema adhabu dhidi yake iliyotolewa na ICC inatuma ujumbe sahihi kwa wafuasi waliosalia na hivyo wasitishe mara moja vitendo vyao na wasalimishe silaha.


Kobler amesema kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukwepaji sheria ni jambo muhimu katika kuleta utulivu DRC na kwamba MONUSCO inaendelea kusaidia ICC na mfumo wa sheria nchini humo ili kudhibiti ukwepaji sheria dhidi ya uhalifu wa aina hiyo.


Mahakama ya ICC ilimhukumu kifungo cha miaka 12 jela Germain Katanga baada ya kupatikana na hatia ya makosa matano kati ya Kumi.


Chanzo:
unmultimedia
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom