BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,009
Magufuli afichua ufisadi wa bil. 60/- Jeshi la Polisi
WAKATI sakata la mkataba wa Sh. bilioni 37 kati ya polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises wa zabuni ya kufunga vifaa vya kutambua alama za vidole likiwa limeanza kupoa, Rais John Magufuli, amenusa ufisadi mwingine kwenye jeshi hilo wa takriban Sh. bilioni 60.
Rais Magufuli alianika kashfa hiyo mbele ya viongozi wakuu wa polisi nchini waliohudhuria shughuli iliyohusisha Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) ambao aliwapandisha vyeo hivi karibuni walipokuwa wakila kiapo cha uadilifu wa utumishi wa umma.
Alisema ana taarifa kuwa mwishoni mwa mwaka jana, kuna mtu alipewa kazi ya kununua sare za polisi na kupewa fedha zinazotakiwa ndani ya wiki moja, lakini mpaka sasa bado hakuna nguo zilizoletwa.
Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli ameagiza viongozi wa polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanya uchunguzi juu ya suala hilo na wakigundua taarifa hizo zina ukweli, basi watu waliohusika wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Alisema wakati kukiwa na ubadhirifu huo wa mabilioni ya fedha za umma, polisi imeshindwa kukomboa magari yake 77 iliyoyaagiza na sasa yameshikiliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
“Kwa hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, wewe ni mwanasheria na Meja Jenerali, waliohusika wapelekwe mbele ya haki,” alisema na kuongeza:
“Kuna watu wanasema fedha zilizotolewa ni Sh. bilioni 40, wengine Sh. bilioni 60, wengine Sh. bilioni 20, na fedha zote zilitolewa ndani ya wiki moja,” alisema Rais Magufuli.
“Naomba suala hili lifuatiliwe, kama ni kweli, fedha hizi zikombolewe hata zikakomboe magari yenu.”
Kashfa hiyo ya sare za polisi imekuja wakati sakata la ufungaji wa mashine za kutambua alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi lilichunguzwa na Bunge hivi karubuni.
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliunda kamati ndogo kulichunguza suala hilo na Bunge kuagiza serikali kushughulikia kasoro hizo ndani ya miezi mitatu bila ya kuzitaja.
Rais Magufuli aliwahi kuzungumzia anavyokerwa na mikataba mibovu ya polisi na taasisi nyingine wakati alipofungua mkutano wa makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa serikali wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa Mikoa na vikosi, kilichofanyika Aprili 29, mwaka huu mjini Dodoma..
“Oysterbay (jijini Dar es Salaam) pale ni eneo ambalo ni very `prime’ (lenye thamani kubwa), kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua ninyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa,” alikaririwa Rais Magufuli akizungumzia suala hilo.
Katika hatua nyingine jana, Rais Magufuli jana alilitaka jeshi hilo na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya taifa.
Chanzo:Nipashe