Huu ni wito wa kizazi chetu!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,681
40,623
Jana tumekumbuka tukio la kighaidi la Septemba 11, 2001. Kwa sisi watanzania tukio hilo litupe nguvu ya kudhamiria mambo makubwa zaidi kwa ajili ya nchi yetu, tukiuacha mgogoro wa Marekani na wenye msimamo mkali mikononi mwao wao wenyewe. Tanzania yetu, itajengwa na sisi wenyewe na ni sisi tutakaoibomoa! Pichani, watoto wa Kitanzania wakionesha sura za matumaini. Je tutawarithisha Tanzania gani watoto hawa?
2006-09-11T21_10_27-07_00.jpg


sikiliza: www.mwanakijiji.podomatic.com
 
Tukio la Septemba 11, 2001, ni tukio ambalo halitasahaulika. Ni siku ambayo itabakia katika akili za watu wengi duniani kwa muda mrefu. Mashambulizi dhidi ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara pale New York, na yale dhidi ya Makao Makuu ya Kijeshi ya Pentagon, na jaribio la utekaji nyara wa ndege iliyoanguka kwenye jimbo la Pennsylvania ulikuwa ni mwanzo wa nyakati mpya katika mahusiano na migogoro ya kimataifa. Kwa wengine matukio hayo yalikuwa ni mwanzo wa vita dhidi ya ughaidi wa Kimataifa. Lakini ukweli wa mambo, vita hii haikuanza Septemba 11.

Kwa wale wafuatiliaji wa siasa za Kimataifa watagundua kuwa maghaidi toka mwanzo walipania kushambulia mali na vitu vya Kimarekani. Wanapoamua kushambulia hawajali ni nani yupo hapo, au mali hiyo iko wapi. Februari 26, 1993 wakiongozwa na mafundisho ya Shehe Kipofu Omar Abdul Rahman maghaidi walijaribu kulipua minara ile miwili ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara hawakufanikiwa lakini watu sita walikufa na wengine wengi kujeruhiwa. Mwaka 1996, June 25 maghaidi wa kikundi cha Hezbollah walishambulia jengo la makazi ya watu kwenye mnara wa Khobar, Saudi Arabia ambapo maafisa 19 wa Kimarekani walikufa, na Msaudi mmoja. Maghaidi hawakukoma hapo. August 7, 1998, maghaidi wa kikundi cha Al Qaida wakiongozwa na Msaudi tajiri Osama Bin Laden walifanya mashambulizi pacha dhidi ya balozi za Kimarekani nchini Tanzania na Kenya. Huko Kenya watu 224 walikufa miongoni mwao wamarekani 12, huku watu 4000 wakijeruhiwa. Huko Tanzania, watu 11 walikufa wote wakiwa ni Watanzania na karibu watu 100 kujeruhiwa. Mwaka 2000 huko Yemen kikosi cha Al Qaida walilipua meli ya kijeshi ya Marekani ya USS Cole mabaharia 17 waliuawa. Ughaidi ni tishio kubwa zaidi la kiusalama duniani sasa hivi, kwani madhara yake hayajui mipaka ya kimataifa, dini, au itikadi za kisiasa.

Mgongano kati Marekani na vikundi vyenye msimamo mkali wa Kiislamu, umetuingiza katika mgogoro ambao kwa nje unaoenekana hautuhusu. Lakini hata hivyo ukiangalia kwa karibu utaona kuwa mgogoro huu unatuhusu. Mmojawapo wa Watanzania wenzetu Ahmed Khalfan Ghailani,(Fupi) ni miongoni mwa maghaidi walioshiriki kuandaa mashambulizi yaliyoua Watanzania wenzake mwaka 1998 Sasa hivi yuko mikononi mwa Marekani huko Ghuba ya Guentanamo. Je vita na mgogoro kati ya Wamarekani wakiziongoza nchi za magharibi kwa upande mmoja na vikundi vyenye msimamo mkali wa kiislamu kwa upande mwingine unatuweka sisi katika mazingira gani?

Ni lazima kwanza tukubali kuwa tumeingizwa katika mgogoro huu bila kupenda na hatuna budi kuweka msimamo wetu wazi ili dunia ione na ielewe. Hii si vita au mgogoro kati ya Waislamu na Wanafiki. Ingawa kina Zawahiri na wenzake wanaitangaza hivyo. Na si vita kati ya Watanzania waislamu na wale wasio waislamu licha ya baadhi ya watu kudokezea kuwa ndivyo hivyo. Na tutafanya dhambi kubwa na kizazi kijacho hakitatusamehe kama sisi wa kizazi cha leo hatutasimam kidete na kuhakikisha kuwa umoja wa Taifa letu unadumu

Binafsi, ninachohofia na kuogopa ni kuwa Tanzania yetu imeanza kugawanywa kati ya Waislamu na Wasio Waislamu. Tena sivyo hivyo tu bali wale wenye msimamo mkali na wale wasio na msimamo mkali. Kuna baadhi ya Watanzania wenzetu ambao kwao utii wao wa kwanza ni kwa Umma wa Kiislamu na waislamu wenzao, huku Watanzania wenzao tukishika nafasi ya tatu. Kwa watu hao, kuwadhuru, kuleta mgongano, kwa Tanzania siyo jambo kubwa. Ni watu hao wasioisha kuandamana, wanaokesha kutoa vitisho, na ambao ndoto yao ni kuona kuwa nchi za magharibi, mila na tunu za kimagharibi zinaondoka Tanzania. Usishangae kuwa kuna baadhi ya ndugu zetu kama Ghailani ambao wako tayari kujiunga na Al Qaida ili kuiangamiza Marekani hata kama kwa kufanya hivyo, kutaidhuru nchi yao na Watanzania wenzao. Tusikubali hilo litokee.

Tanzania, tumejifunza kuishi pamoja na kuuguzana pamoja. Tumejifunza kucheka na kuchekeana. Tumealikana wakati wa Kipaimara na wakati wa Maulidi. Tumefurahia X'mass inapokuja na tunangoja kwa hamu sikuu ya Idi. Tumejifunza kuzikana pia na kuanua matanga pamoja. Taifa letu, tumeweka Utanzania wetu mbele na hivyo kushinda sumu ya ujimbo na ukabila. Lakini sasa, tusipoangalia tutajikuta tunajigawa kwa kufuata udini.

Ndugu zangu, wito wetu leo hii, wito wetu wa kizazi kipya cha Watanzania, ni kuhakikisha ya kuwa nchi yetu inaendelea kuwa huru na watu wake wanaendelea kuwa huru. Ni kuhakikisha kuwa katika Tanzania yetu hakuna unyanyasaji au ukandamizaji wa aina yoyote ile. Katika nchi yetu kusiwe na mtu anayelalamika kubaguliwa kwa namna yoyote ile na chombo chochote kile iwe moja kwa moja au taathira zake. Ni wito wetu kuhakikisha kuwa kizazi kijacho cha Watanzania kinafurahia usawa, haki, na matunda ya nchi yao sawa na zaidi kuliko sisi. Ni lazima tujenge nchi ambapo wenye dini zao hawajisikii kuwa duni au bora zaidi, na wale wasio na dini wasijione duni katika nchi yao. Ni lazima tujenge nchi ambapo Waislamu wako huru kutimiza masharti na mambo yale yanayoipasa dini yao bila kuwakwaza watu wenye imani nyingine. Ni lazima tujenge mazingira ambapo tunaweza kuaminiana na kuacha kushukiana kila kukicha. Ili kufanya hivyo nina mapendekezo kadhaa.

a. Kuundwa tume huru ya kuchunguza madai ya ukandimizaji Waislamu tangu Uhuru hadi leo hii. Kati ya mambo mengi ambayo Waislamu watanzania wanadai hili la kukandamizwa na kunyimwa nafasi katika uongozi na nyadhifa mbalimbali ndilo kuu. Minong'ono ya kukandimizwa waislamu ilianza zamani na hakuna kilichofanyika ili kulishughulikia suala hilo. Tume hiyo ipewe uwezo wa kupita nyaraka zote za serikali na vielelezo mbalimbali ili kutafuta ukweli kama ni kweli Waislamu wa Tanzania walidhulumiwa kwa makusudi na serikali ya awamu ya kwanza na nini kifanyike ili kusahihisha hilo.

b. Kila mkoa uunde Kamati ya Usuluhishi ya mkoa ambao lengo lake liwe ni kushughulikia migogoro ya kidini na kikabila katika mikoa hiyo. Kamati hizo ziwe na uwezo wa kutoa maamuzi yanayotambulika kisheria na utatuzi wa jambo ukishindikana huko basi mahakama za kawaida zichukue kesi hizo. Hii itazuia migongano isiyo ya lazima katika jamii.

c. Siku mpya ya mapumziko iongezwe (siku fulani inaweza kuondolewa ) na itangazwe kuwa ni siku ya Shukurani (Thanksgiving Day). Iwe ni siku ambapo Watanzania tunamshukuru Mungu kwa kutupa Taifa zuri lenye amani lenye watu wema na lenye neema. Iwe ni siku ya kukaribishana watu wa dini tofauti, rangi tofauti, n.k iwe ni siku ya kula mlo wa pamoja na watu ambao si wa kundi lako au familia yako.

Ndugu zangu, Taifa la Tanzania litajengwa na Watanzania wenyewe, na litabomolewa na Watanzania hao hao! Kama ni kweli tunataka kujenga Taifa lenye neema kwa kila mtu, ni lazima tuondokane na kila kitu kinachojaribu kututengenisha ili nguvu zetu zielekezwe zaidi katika kujenga nchi kuliko kuibomoa. Huu ni wito wa kizazi chetu, je tutaitika!?

Mimi ni M. M. Mwanakijiji.
 
Mwanakijiji,

Nakuunga mkono 102% kwenye point a. Nadhani si vyema kwa serikali kufumbia macho manung'uniko yao kuwa walikuwa marginalised kwenye elimu. Manung'uniko hayo ndio yanayayotumiwa kupandikiza chuki kati ya waislamu na wakristo. Unajua hata sasa kinachotumika kuchochea ughaidi ni maonevu yanayoondelea mashariki ya kati. Walio UK nadhani wanalielewa hili vyema.

Its high time for the goverment to sort this out mapema kabla halijatufikisha kwenye point of no return. I was really shocked to see the hatred showed to christians during the topic about RO.

I urge the government to put all facts on table and even apologize to moslems if need arise.
 
nahisi,urithi tosha kwa kizazi kijacho ni chuki na visasi dhidi ya wanaolikwamisha taifa hili lisiiendelee na wote wanaolinyonya taifa hili bila aibu wala huruma mbele ya macho ya wazazi wa watoto hao!!
 
Back
Top Bottom