Huu ndio utaratibu unaotumika siku ya Uchaguzi

Mwakaboko King

JF-Expert Member
Apr 22, 2015
1,099
207
Wanajamvi habari za majukumu, nikiwa mdau wa Siasa za Tanzania nimeona leo tuzimulike taratibu zinazotumika wakati wa Uchaguzi kwa kuzingatia kuwa mwisho wa Uchaguzi mmoja ni mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine.

Tanzania tutakuwa na Uchaguzi mkuu mwingine 2020, Ukisoma Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kifungu cha 55 na 56 vya pamoja na vifungu vya 56 na 57 vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 utaona kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutangaza siku ya kupiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara na utaratibu mzima wa upigaji Kura.

Tangazo la Uchaguzi

Kwa kuzingatia kifungu cha 47(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, na Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume hutoa Tangazo la Uchaguzi (Notice of Election) siku 8 kabla ya Siku ya Upigaji Kura.

Tangazo hilo, huonesha Siku ya Upigaji Kura, Saa ya Kufungua na Kufungwa kwa zoezi la Upigaji Kura, Anuani ya Kituo au Vituo vya Kupigia Kura, Mfano wa Karatasi za Kura pamoja na Orodha ya Wapiga Kura waliopangiwa kupiga Kura katika kila Kituo.

Aidha, tangazo hilo hubandikwa katika Ofisi za Wasimamizi wa Uchaguzi, Ofisi za Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata na katika kila Kituo cha Kupigia Kura.

Aidha, Tangazo hilo hutolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo chini ya kanuni ya 47 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 pamoja na kanuni ya 40 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani), za mwaka 2015.

Mawakala wa Upigaji Kura

Kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa na kifungu cha 58 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kwa pamoja na kanuni ya 48 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 na kanuni ya 42 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015 kila Chama cha Siasa chenye mgombea wa nafasi yoyote kinaweza kuteua Wakala wa upigaji Kura kwa kila kituo cha kupigia Kura.

Kazi za wakala ni pamoja na:

(i) Kutambua Wapiga Kura;
(ii) Kumwakilisha na kulinda maslahi ya mgombea au wagombea katika kituo, na
(iii) Kushirikiana na Msimamizi wa Kituo na Msimamizi wa Kituo Msaidizi ili kuhakikisha sheria na taratibu zinazohusu upigaji Kura na chaguzi zinafuatwa katika Kituo.

Wakala atapaswa kula kiapo cha kutunza Siri kwenye Fomu na. 6.

Kuridhika au kutoridhika kwa Wakala wakati wa maandalizi ya upigaji Kura katika Kituo

Kwa mujibu wa kifungu cha 61 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, endapo Wakala wa Upigaji Kura, hakuridhika na maandalizi ya Upigaji Kura kwenye kituo, anayo fursa ya kuandika malalamiko yake kwa kujaza Fomu Na. 14 kama ilivyoanishwa katika kanuni ya 51 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 pamoja na kanuni ya 44 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015. Fomu hiyo atamkabidhi Msimamizi wa Kituo na Msimamizi Msaidizi wa Kituo ambaye atapaswa kuonesha namna alivyoshughulikia malalamiko hayo.

Utaratibu wa Upigaji Kura

Upigaji Kura huanza saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. Kwa mujibu wa maelekezo yanayotolewa na Tume ifikapo saa 10:00 jioni Mlinzi wa Kituo atasimama nyuma ya Mpiga Kura wa mwisho kwenye mstari wa Wapiga Kura. Wapiga Kura ambao wanakuwa katika Vituo vya Kupigia Kura kabla ya saa 10:00 jioni huruhusiwa kuendelea Kupiga Kura.

Namna ya kuendesha zoezi la Upigaji Kura.

Ufuatao ni utaratibu unaofuatwa wakati wa Upigaji Kura (i) Msimamizi wa kituo atawaonesha Mawakala wa upigaji Kura na mtu yeyote atakayekuwepo katika kituo hicho kwamba masanduku ya Kura ni tupu, ili waweze kuhakikisha kuwa hayana kitu chochote ndani yake (ii) Kabla Upigaji Kura, Mawakala hupewa Fomu na. 14 kujaza ili kuonesha kuridhika au kutoridhika na matayarisho ya Kituo cha Kupigia Kura.

Wanaoruhusiwa Kuingia kwenye Kituo cha Kupigia Kura

Kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa pamoja na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinawataja wafuatao kuwa wanaoruhusiwa kuingia kwenye kituo cha Kupigia Kura siku ya Uchaguzi - (i) Msimamizi wa Kituo (ii) Msimamizi Msaidizi wa Kituo (iii) Mawakala wa Upigaji Kura (iv)Wapiga Kura kwa ajili ya Kupiga Kura tu (v) Mtu anayemsaidia Mpiga Kura asiyeweza kupiga Kura mwenyewe kwa sababu ya ulemavu au asiyejua kusoma (vi) Mtazamaji wa Uchaguzi aliyeruhusiwa kwa maandishi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (vii) Wagombea (viii) Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ix) Mkurugenzi wa Uchaguzi (x) Askari Polisi au Mlinzi wa Kituo (xi) Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi (xii) Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa.

Sifa za mtu anayeruhusiwa kupiga Kura

(i) Awe amejiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura:
(ii) Awe ana Kadi ya Mpiga Kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi;
(iii) Awe katika kituo alichojiandikisha kupiga kura


Wanaoruhusiwa kupiga Kura nje ya Kituo walichojiandikisha Siku ya Uchaguzi.

Kwa mujibu wa kanuni ya 55 (1) na (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 ikisomwa pamoja na kanuni ya 48 (1) na (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015, wafuatao wanaruhusiwa kupiga kura nje ya kituo walichojiandikisha.

1. Wakala wa Upigaji Kura na Watendaji wa Uchaguzi, Hawa wataruhusiwa kupiga kura kwa kujaza fomu Na. 18
2. Mgombea, Mgombea wa Kiti cha Rais anaruhusiwa Kupiga Kura sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muungano, Mgombea Ubunge anaruhusiwa kupiga Kura katika kituo chochote ndani ya Jimbo la Uchaguzi analogombea na Mgombea Udiwani anaruhusiwa kupiga Kura kituo chochote ndani ya Kata anayogombea, wote hawa watapaswa kujaza Fomu Na. 19.

Utaratibu wa Kupiga Kura kwa Watu wenye ulemavu wa macho


Kwa Watu Wasioona, Tume huweka utaratibu wa Kupiga Kura kwa kutumia kifaa maalum cha Kupigia Kura chenye maandishi ya nukta nundu (tactile ballot folder) na wale ambao hawana uwezo wa kutumia kifaa hicho, huruhusiwa kuja na Wasaidizi.

Tutaendelea na mada hii, Nawatakia siku njema!!!
 
Mkuu sheria zetu siyo mbaya sana tatizo letu ni usimamizi wa watendaji wanapewa maelekezo kutoka kwa wakurugenzi,nina ushuhuda wa baadhi ya wakurugenzi na watendaji kapata (demotion) kwa kuwa wapinzani ktk maeneo yao wameshida.
 
Mkuu sheria zetu siyo mbaya sana tatizo letu ni usimamizi wa watendaji wanapewa maelekezo kutoka kwa wakurugenzi,nina ushuhuda wa baadhi ya wakurugenzi na watendaji kapata (demotion) kwa kuwa wapinzani ktk maeneo yao wameshida.

Mungu wangu sasa hao waliadhibiwa kwa kosa lipi? na ni nani aliwaadhibu?
 
Back
Top Bottom