Huu mchezo hauhitaji hasira: Yaliyompata Lowassa, yalimpata Malecela

MZK

JF-Expert Member
Sep 13, 2012
223
303
AKIHUTUBIA Mkutano Mkuu Maalumu wa uchaguzi mjini Dodoma mwaka huu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete, alidai kuwa uteuzi wa jina la mgombea urais wa chama hicho mwaka jana, kuanzia kwenye Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) hadi Mkutano Mkuu ulikuwa mgumu zaidi katika historia yake na nusura ukisambaratishe.

Akikabidhi uenyekiti kwa mwenyekiti mpya na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli, Kikwete alisema kuwa kwa vile CCM imeweza kuhimili kwa usalama kipindi hicho kigumu, maana yake ni kuwa hakitakufa tena.

Kikwete alikuwa akizungumzia matukio ya CC na NEC kufuatia kukatwa kwa jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa, aliyedhaniwa kuwa na ushawishi mkubwa na wafuasi wengi zaidi ndani ya chama na kuibua mtikisiko.

Kwa kuona kwamba ameonewa, Lowassa alihamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukidhi kiu yake ya kuwania urais.

Nataka kutofautiana kidogo na maneno yale ya Kikwete. Kwa maoni yangu, ukiondoa mkutano wa mwaka 1962 uliofanya Waziri Mkuu wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kulazimika kuachia ngazi miezi miwili tu baada ya uhuru akipinga “ukaburu” ndani ya chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kwa kutaka kutoa vyeo na madaraka serikalini kibaguzi kwa waafrika weusi tu (Africanisation) na kufukuza wazungu wote; pengine Mkutano Mkuu mgumu zaidi kwa CCM ulikuwa ule wa Desemba 1992, ambao, mithili ya huu wa hivi karibuni, uliyumbisha chama na serikali kwa jina la Waziri Mkuu, John Samwel Malecela.

Lakini tofauti na wa mwaka huu, Mkutano Mkuu wa mwaka 1992 ulikuwa na wapiga jaramba wengi, visu mkononi. Kulikuwa na Waziri Mkuu, Malecela; Waziri wa Fedha, Profesa Kighoma Malima na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba, wote wakikodolea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama iliyokuwa ikiachwa wazi na Rashid Kawawa, waweze kujisafishia njia kugombea urais mwaka 1995.

Lakini jina la Malecela lilitia hofu wote na mbinu chafu kumwandama. Ilikuwa patashika nguo kuchanika. Kikwete na wengine tuliokuwa kwenye “Intelijensia” ya chama ni mashahidi.

Mikasa kwa Malecela, kama ilivyokuwa kwa Lowasa, halikuwa jambo jipya. Siku moja mwaka 1985 baada ya kung’atuka madarakani, Mwalimu Nyerere alikuwa akijaribu kumsaidia mrithi wake, Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuandaa orodha ya waliostahili kufikiriwa kuteuliwa kushika nafasi ya Waziri Mkuu baada ya Uchaguzi Mkuu na jina la Malecela likajitokeza juu ya mengine, wakiwamo aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mustafa Nyang’anyi, Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu, Joseph Warioba na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba.

Kwa njia zisizo rasmi, kambi ya Malecela ikapata habari juu ya kilichokuwa kikipikwa Ikulu, ikaanza kushangilia na jaramba kwa ushindi wa chee; Ikulu ikanusa “shangwe” hizo. Jina la Malecela likakatwa; na kwa mshtuko wa wengi, akapoteza pia jimbo lake wakati uchaguzi ulipowadia. Nafasi ya Waziri Mkuu ikaenda kwa Joseph Sinde Warioba.

Baadaye, Malecela aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, kabla ya kuteuliwa kuwa balozi nchini Uingereza. Inadaiwa uteuzi huo ulikuwa shukrani ya Rais Mwinyi kwake, kwamba, wakati alipojiuzulu nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani mwaka 1976 kuwajibika kwa mauaji ya “wachawi” mkoani Shinyanga, ni Malecela aliyempendekeza Mwinyi kwa Mwalimu kuwa balozi wa Tanzania nchini Misri.

Kipindi cha pili cha Mwinyi kilimrejesha Malecela kutoka Uingereza kushika nafasi ya Waziri Mkuu. Alitaka Waziri Mkuu mtiifu asiye na minyororo ya kiitikadi, akiwaona viongozi waandamizi wengine ndani ya chama na serikali kuwa ama wenye kulemewa na mzigo wa itikadi kali, wenye majivuno, au wasio na utii na wenye kutaka kujijenga kimadaraka na alishindwa kuwadhibiti.

Kwa kumrejesha Malecela nchini na kumteua Waziri Mkuu, Mwinyi alitegemea utii mkamilifu kutoka kwa Waziri Mkuu asiye na kitako na jimbo la uchaguzi bali Mbunge tu wa kuteuliwa, lakini zaidi mwenye kufahamika vyema kwa viongozi wa Afrika na Mwanadiplomasia nguli.

Kinyume na sera za uchumi za Ujamaa na Kujitegemea kwa nchi enzi hizo, Malecela alikuwa muumini wa sera za Ubepari. Alitaka ubinafsishaji wa uchumi na kwa mtu kujipatia mali kadri ya ukali wa meno yake na alikuwa na uswahiba mkubwa na tabaka la wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi.

Haya yote yalimwingiza kwenye migongano ya kiitikadi na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba mara kwa mara ndani na nje ya Bunge na hivyo kudhibiti nguvu ya Malecela.

Kama ilivyotarajiwa, kampeni zilikuwa nzito na zenye ushawishi kwa mbinu halali na chafu kwa makundi. Kundi lililojiita “Kakakuona”, likihusisha baadhi ya makada wa Umoja wa Vijana wasomi wa TANU/CCM wa zamani, likijumuisha kina Jakaya Mrisho Kikwete, Edward Lowassa, Paschal Mabiti na wengine, lilimpigania Malecela.

Hapakuwa na kundi la kiharakati wala la utetezi wa itikadi ya nchi. Kazi ya kufikiri na kuitikadisha aliachiwa Kingunge Ngombale Mwiru na akajizolea jina “Profesa” wa siasa.

Wenyeviti wa mikoa nao walikuwa na kundi lao lisilo rasimi kuhamasisha kura dhidi ya Kighoma Malima; wakati kundi la Zanzibar lilikuwa na mtu wao kwa misingi ya kidini zaidi. Lakini Mwenyekiti wa CCM, Mwinyi alipendelea Kolimba awe Makamu wake na aliwadokeza wasiri wake. Baadhi ya vigogo ndani ya chama, akiwamo Kawawa, walikuwa hawaivi na Kolimba.

Katika chaguzi kama hizi, si utamaduni kwa Makamu wa Rais kutupwa: haikuwa hivyo kati ya Kawawa na Oscar Kambona (1962), Mwinyi na Salim Ahmed Salim (1985).

Hivyo, Malecela kama Makamu wa Rais akapeta; Kolimba, Kighoma Malima na wapambe wengine wa Mwinyi kama Hassan Diria na Fatuma Saidi Ali wakaendelea kubwagwa kwenye NEC na CC, Mwinyi akalegea; njia ya Malecela kuelekea kwenye urais mwaka 1995 ikawa nyeupe kusubiri uteuzi wa chama.

Kwa Malecela kupeta, chama kilitikisika. Na ili kuepuka mpasuko, kililazimika kuwateua vigogo kama Cleopa Msuya na Paulo Bomani kuingia kwenye CC kuzuia wasikimbilie CHADEMA, huku Pius Msekwa akipewa jukumu la kudhibiti mbio za Malecela; kisha akaongezwa kwenye orodha Augustine Lyatonga Mrema, Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa kupewa cheo kisichokuwepo kikatiba, cha Naibu Waziri Mkuu kupunguza nguvu ya Malecela.

Na ilipofika uteuzi wa mgombea urais mwaka 1995, jina la Malecela, (kama ilivyokuwa kwa jina la Lowassa mwaka 2015) lilikatwa bila maelezo, na jina la Benjamin William Mkapa, bila ya kutarajiwa (kama tu ilivyokuwa kwa JPM mwaka 2015), likapeta na kupitishwa.

Yaliyompata Lowassa ni historia kujirudia kwa duru za siasa nchini zisizotaka hasira ya mkizi. Vijana wa siku hizi wana msemo; “Huu mchezo hauhitaji hasira”

source: RAIA MWEMA
 
1472397908836.jpg

Laana itawatafuna tuu
 
duuh.. kwahyo wenye mashiko kukatwa katika siasa za tanzania ni swala doogo sana.... nahisi viongoz walio juu wanajua vigisu kama hizi kwahyo hawawez kua na hasira kama zilizopo kwetu sababu hatuna uzoefu wa figisu hiz, hii yachangiwa na wao kua wasiiiri sana kwani kujua vitu hiv vyahtaji nawe uwe kati yao.... hongera mkuu
 
Back
Top Bottom