Humphrey Polepole: "Kuiishi misingi, imani na ahadi za CCM ni tunu ya siasa safi na uongozi bora"

AUGUSTINO CHIWINGA

JF-Expert Member
Apr 23, 2017
220
689
Imeandikwa
Na
Debora Charles✍

“Uwe makini sana kwenye ujana wako kwa sababu uzee upo na unakusubiria. Ninyi hapa ni viongozi, mnapaswa muanze kujitazama kama viongozi kuanzia mienendo mpaka matendo yenu. Kukubali kuwa kiongozi ni kukubali kujinyima uhuru wa kufanya mambo ya hovyo pamoja na kuishi maisha ya ujana”. Hayo yalisemwa na aliyekuwa mgeni rasmi Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Halmashauri Kuu CCM Taifa mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi katika Kongamano la Umoja wa Vijana Vyuo na Vyuo Vikuu Kagera lililofanyika mnamo 29/04/2017 alipokuwa akiwaasa vijana wasomi wanaohitimu juu ya kuiishi misingi ya uongozi bora na siasa safi zenye tija kwa Taifa. Akiendelea kutoa ufafanuzi, Ndg. Humphrey Polepole alisema,

Uongozi upo wa aina mbili, kuna uongozi kwenye NAFASI YA MADARAKA (position in authority) na ule usiokuwa wa nafasi ya madaraka. Lazima uwe ni mtu ambaye wakikutazama wanasema wenyewe huyo mimi namkubali ni KIONGOZI. Mwenendo wako usiwe mtu ambaye ukikosekana katika mazingira yako hata wiki hakuna ambaye anakukumbuka, Kiongozi ni yule akikosekana kwa muda mfupi watu wanamuulizia, na hicho ndicho kipimo cha kujua mchango chanya unaoutoa kwa jamii ya watu wale wanaokuzunguka, alisema.

Lakini zaidi ya hayo lazima ufanye vizuri shuleni. Kiongozi mzuri haifai kila mtihani anafeli. Hasa vijana wa CCM lazima mfanye vizuri kwenye masomo yenu ili kutimiza maandiko ya kwenye ahadi za mwanachama wa CCM ile ya 6 “Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote”.

“Kuwa mwangalifu, baadae yako ipo kwenye dhamana ya mikono yako sasa. Nyinyi ni viongozi wa leo na kesho na ni hazina ya Chama Cha Mapinduzi. Chunga sana mwenendo wako. Hata disko nenda lakini cheza kwa timing hupaswi kujiachia kupita kiasi. Usiwe yule tu ambaye unacheza mpaka mziki unatambua kuwa leo upo”.

Akiendelea kutoa ufafanuzi juu ya misingi ya siasa za Chama Cha Mapinduzi, Ndg. Humphrey polepole alisema, Ukisoma katiba, Miongozo na Nyaraka zote za Chama Cha Mapinduzi, utagundua kuwa hakuna Chama Tanzania na Afrika nzima chenye maandiko, maarifa na hata taarifa zenye tija kama Chama Cha Mapinduzi. Chama Cha Mapinduzi hapa Tanzania ndio Chama pekee chenye ITIKADI inayoeleweka, ndio pekee ambacho unachama wake sio ushabiki, mapenzi wala ukereketwa bali unachama wake ni IMANI.

Imani ya Chama Chama Mapinduzi inasema kwenye ibara ya 4, na mambo haya watanzania wanayataka jana, leo na hata kesho, “Binadamu wote ni sawa, kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”. Binadamu wote ni sawa maana yake awe maskini awe tajiri kwenye Chama Cha Mapinduzi wote ni sawa, awe mkulima awe mfanyakazi na awe mwanamke awe mwanaume kwenye Chama Cha Mapinduzi wote ni sawa.

Na ndio maana CCM ikailekeza Serikali, watoto wote wa maskini na wenye uchumi wa kati waende shule bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Ushahidi wa kwanza kuonyesha kulikuwa hakuna usawa wa elimu, ulionekana baada ya kuwa na ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi kwa mara tatu zaidi, yaani shule iliyokuwa inachukua watoto 300 ikapata watoto 900.

Akiendelea kuhutubia hadhara, Ndg. Humphrey Polepole alitoa ufafanuzi juu ya MTAALA WA DARASA LA ITIKADI kwa kusema, Zamani Darasa la Itikadi lilikuwa likifundishwa kwa miezi tisa, mtaala wake ulikuwa umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo zilitolewa kila baada ya miezi mitatu. 1. Historia ya nchi yetu, 2. Historia ya Chama cha Mapinduzi, na 3. Political economy.

HISTORIA YA NCHI YETU, wanafunzi walifundishwa namna ilivyokuwa kabla ya wageni hawajaja (Inaeleweka wageni walikuwa wamegawanyika katika makundi kadhaa walikuwepo wafanyabiashara, watu wa dini, wakoloni waingereza, wareno, waarabu, wajerumani). Wanafunzi walielezwa namna ambavyo hali ya kisiasa ilikuwa kabla ya kupata Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, Msingi wa vuguvugu la kudai Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar, hali ya kisiasa baada ya kupata Uhuru na Mapinduzi, Demokrasia baada ya Uhuru na baada ya Mapinduzi, Muungano (msingi wa kuunganisha mataifa haya mawili yaliyopata Uhuru), mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kisheria, kikatiba na ya kimazingira katika uongozi wa Taifa la Tanzania. Namna Tanzania ilivyohangaika kuwasaidia watanzania miongoni mwao wenyewe na nchi nyingine za kaskazini na kusini mwa bara la Afrika kuhakikisha ya kwamba na wao pia wanakuwa huru.

Historia ilifafanua pia njia tuliyoipita, kiuchumi shughuli za kijamii maendeleo, nyakati ngumu tulizowahi kupitia katika Taifa, mfano miaka ya 70,71,72,73,74 Nchi hii ilikumbwa na baa la njaa. SIASA NI KILIMO haikuja tu kwa sababu tulitaka tuhamasishe watu walime, WITO WA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MAJI haikuja tu kwa sababu viko vyanzo vya maji katika nchi ya Tanzania, yalikuwepo mazingira ambayo yalisukuma Chama Cha Mapinduzi kufanya uamuzi na kuielekeza Serikali.

Miezi mitatu baade mtaala ulifafanua juu ya HISTORIA YA CHAMA CHA MAPINDUZI kujua kimetoka wapi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilianza mwaka 1977 lakini kabla yake ilikuwepo TANU kwa upande wa Tanganyika na ASP kwa upande wa Zanzibar. Historia ilifafanua hali ilivyokuwa kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania, historia ilieleza kwa kina TANU na ASP vilitoka wapi, kwamba kwa upande wa Tanganyika ilianza TANU ambayo nyuma yake ilianza Tanganyika African Association TAA nayo nyuma yake ilikuwepo African Assiosiation AA ambayo kabla yake lilikuwepo VUGUVUGU. Kule Zanzibar kulikuwa na African Assosiation AA na Shiraz Party SP ambao waliuungana wakatengeneza Afro Shiraz Party ASP.
Historia ilitoa ufafanuzi kwa nini TAA ilifudhu na kuwa TANU, Kwamba kwa kipindi chote hiki AA lengo lake lilikuwa ni kupata stahiki sawa kati ya waswahili, wazungu na waasia. TAA wao wakanza kuangalia maslahi ya wafanyakazi, mishahara lakini bado hawakuwa wakijielekeza KUPATA UHURU, ilikuwa ni kama harakati, walitetea haki kama asasi za kiraia. Baadae wakasema hapana tuanzishe Chama cha kudai Uhuru. Ndipo ikatengenezwa TANU. Historia ilieleza kwa nini TANU na ASP waliungana mwaka 1977 na kuunda CCM halafu baada ya kuungana Chama kimekuwa kikiendelea namna gani.

Miezi mitatu ya mwisho, mtaala ulifafanua juu ya POLITICAL ECONOMY. Hapa walifundishwa uhusiano uliokuwepo kati ya uzalishaji, biashara, kodi, maamuzi ya kisiasa, matumizi ya rasilimali za Taifa kwa pamoja. walijifunza kuhusu maana ya ujamaa na ubepari na kwanini sisi ni wajamaa. Lakini walifafanuliwa namna ujamaa wetu unavyotofautiana na ule wa wachina na waasia.

Walifundishwa mambo mbalimbali yaliyotokea kipindi tofauti tofauti, siasa zetu miaka ya 60, 70, 80 na kisha mabadiliko ya muelekeo wa utekelezaji wa siasa yetu ya ujamaa na kujitegemea. Walifafanuliwa namna ambavyo Serikali ilifanya uzalishaji, iliaajiri kila mtu, ilisambaza chakula, ilijenga miundombinu ya barabara, huduma za kijamii hospitali, mahoteli, namna ambavyo Serikali ilikuwa ikimiliki treni, mabasi, Shirika la simu, Shirika la Posta, Shirika la ugawaji na mengine mengi, namna ambavyo Serikali ilijenga zaidi ya viwanda mia nne ili watanzania wakafanye kazi humo na namna maendeleo na ukuaji wa uchumi yanaathiriwa chanya au hasi na maamuzi yetu ya kisiasa.

Ndg. Humphrey Polepole aliendelea kusema, Muongozo wa 1981 Katika fungu la 138 unasema *“Chama kinapanga na kuendesha mafunzo ya Siasa yake kikiwa na malengo makubwa matatu, mafunzo ya siasa ya Chama yanatolewa kwa wananchi kwa jumla kwa lengo la kuineza siasa hiyo ili ieleweke na kukubalika na wakati huo huo kupinga vita upotoshaji na uzushi juu ya siasa ya ujamaa unaoenezwa na maadui wa ujamaa kwa nia ya kukifanya Chama kifarakane na umma”*.

Inaendelea kusema *“ni wakati wote nia iwe kuelimisha umma na kuufanya uwe karibu zaidi na chama ili ushinde katika kutekeleza maelekezo na mwito wake kwa hari na hiari”*.

Kifungu cha140 *“lengo la tatu la mafunzo ya siasa ya chama ni kuhakikisha kuwa wanachama na viongozi wanimarika katika itikadi ya ujaamaa na kujitegemea, kuwapanua wanachama na viongozi upeo wao wa kuyaelewa masuala mbalimbali upeo wa viongozi wetu na wanachama katika masuala mbalimbali”*. Kuwapa methodolojia na manitki ya kutafakari na kufanya uchambuzi wa masuala. Tunataka viongozi wetu na wanachama wapewe methods na logic za kutafakari na kufanya uchambuzi wa masuala (analysis of issues).

Chama Cha Mapinduzi mwaka huu kitaanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha CCM ambacho viongozi wote na wanachama makada watafika pale ili wapikwe juu ya Itikadi na misingi ya kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi. Kila kiongozi kwenye Chama lazima atapita pale na kwa utaratibu mzuri utakaokuwa umewekwa ili akanolewe. Wakamdhatiti kwa hoja, kwa methodolojia, kwa Mantiki na uchambuzi wa masuala mbalimbali na kufahamu misingi ya kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (malengo yake, imani yake, nidhamu yake). lazima akafahamu uhusiano uliopo kati ya Serikali na watu na nafasi ya Chama Cha Mapinduzi. Yatakuwepo mafundisho zaidi kuhusu uzalendo, uadilifu, uaminifu, unyenyekevu maana ya kuchapa kazi, kupiga vita rushwa, kukataa ubadhilifu wa mali za Chama na Serikali, kuwaheshimu wananchi, kuwa mpole lakini mkali kwa mambo ya hovyo.

Tukishaenea chuo hiki pia kitakuwa msaada wa kuendelea na kuimarisha udugu, urafiki na kuwajengea maarifa vyama vingine vitano vya kusini mwa Afrika kwa maana ya FRELIMO, ZANUPF, ANC, SWAPO pamoja na LPLA watakuja hapa kwa sababu hakuna sehemu nyingine nzuri, madhubuti na iliyosimama imara Afrika kama Tanzania, Alisema.

Chuo hiki ujenzi wake utaanza hivi karibuni. Kitaweza kuchukua watu 200 kwa wakati mmoja ndani ya mafunzo ya muda mfupi. Wapo watakaokuja watafundishwa mafunzo ya kufundisha wengine ili ndani ya muda mfupi tuweze kuwafikia sio tu wanachama lakini viongozi na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi. Hii ni katika kuendelea kudumisha misingi na uelewa wa kwa nini Chama Cha Mapinduzi kilianzishwa.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa Bukoba Ndg. Rahel Ndegeleke, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Kagera Ndg. Yahya, makatibu wa CCM wilaya, uongozi mzima wa Jumuiya za Chama Cha Cha Mapinduzi, Vijana, Wanawake Na Wazazi, madiwani na viongozi wengine wa Umoja wa Vijana CCM kutoka Vyuo na Vyuo Vikuu mkoani humo

Ziara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ilidumu kwa siku tatu mkoani humo 27-29/04/2017 ambapo mbali na kongamano alipata fursa ya kufanya kikao na Mkuu wa mkoa Mkoani humo na kusisitiza juu ya utolewaji wa fungu la wanawake na vijana 10% kwenye mfuko wa Halmashauri na pia alipata fursa ya kuzungumza na kusilikiza Changamoto za wanachama na wananchi kupitia viongozi Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake katika ngazi zote za wilaya ya Bukoba Mjini na Vijijini.
 
Chuo cha propaganda kikipatikana kigamboni enzi hizo, sasa sijui wamefyatua vasheni ya moving classes?
 
188713.jpg
 
CCM ni lini mlifanya siasa safi???Ni lini mlitekeleza ahadi zenu???Hayo yote mngeyafanya tanzania tungekuwa mbali sana kimaendeleo
 
Huwa namuelewa sana Polepole yani Polepole mmoja sawa na lisu 20
 
Back
Top Bottom