Hukumu dhidi yangu: Shukrani kwa watanzania – Maxence Melo

Status
Not open for further replies.

Maxence Melo

JF Founder
Feb 10, 2006
4,230
13,415
Wakuu,

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru watanzania kwa ujumla na hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii na kwa namna ya kipekee wanachama wa JamiiForums kwa support ambayo tumekuwa tukiipata toka kwenu tangu mwanzo wa kesi hii hadi mwisho wake.

Hukumu hii ya kesi namba 456 ya mwaka 2016 imetolewa baada ya kuahirishwa mara 5 kwa sababu mbalimbali tangu Novemba 26, 2019. Hatimaye imetolewa na wote naamini mmesikia kuwa imeamriwa nilipe TZS Milioni 3.

Ingawa hakimu Thomas Simba amesema kuwa hakukuwa na ulazima wa kuwapa Data walizotaka Polisi, amesema kosa langu ni kuwa nilikiri kuwa Mkurugenzi wa Kampuni na kuwa mwanzilishi wa JamiiForums; hivyo akahitimisha kuwa nilijua wazi Polisi walikuwa wanafanya uchunguzi na niliwachelewesha kwa kukusudia na sikuwambia kuwa data hizo sina.

Hakimu amemwondolea hatia mshtakiwa namba mbili (Mike Mushi) kwa kusema kuwa Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kwa nyaraka zilizoletwa mahakamani na Jamhuri kuwa yeye si shareholder (mwanahisa) wala si mwanzilishi wa JamiiForums na hajui chochote kuhusiana na shughuli zake.

Nisingependa kuingia kwa undani zaidi juu ya Hukumu ya Shauri hili lakini nipende kuwafahamisha kuwa baada ya hukumu, tayari leo hii mawakili wangu wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala wamewasilisha notisi ya kukata rufaa na imepokelewa (nakala ipo chini). Jopo la Mawakili linawahusisha Benedict Alex Ishabakaki, Peter Kibatala, Jebra Kambole na Jeremiah Mtobesya.



Hapa chini ni notisi ya kukata rufaa:

230D2752-0B29-4528-A80B-B6DC5DAC61B4.jpeg

D8FCA97C-1DB7-4476-9B63-D65E3FA79638.jpeg


Kwa waliotaka kuchangia:

Napenda kuwashukuru watanzania wengi sana waliojitokeza (kunitafuta au kuwatafuta watu wangu wa karibu) kutaka kuchangia ili tulipe faini hiyo; niseme nimefarijika sana kuwa watu walikuwa tayari kufanya hivyo. Niwaombe kuwa msinichangie kulipa faini kwani tayari hili nimefanikiwa kulitekeleza na ndiyo maana nimeachiwa huru. Kwa wanaoona kuwa bado wanataka kunichangia kwa gharama nilizotumia, ninashukuru sana lakini naomba ijulikane kuwa tayari hili limekamilika; ukiamua kufanya hivyo – basi umefanya kwa kupenda na ninashukuru.

Kesi nyingine:

Kuna kesi nyingine yenye maudhui kama haya; kesi namba 458 ya mwaka 2016 ipo mbele ya Hakimu Huruma Shaidi na itaendelea Aprili 23, kutokana na janga la Corona wananchi hawaruhusiwi kusikiliza kesi hizi. Tutawapa update ya kitakachojiri siku hiyo kupitia hapa JF na katika kurasa zetu za mitandao ya kijamii. Soma Kesi namba 458 (Jamhuri v JamiiForums) yaahirishwa tena kwa kukosekana Shahidi. Mara ya mwisho kuwa na Shahidi ni Novemba 12, 2018 - JamiiForums

Kesi namba 457 ya mwaka 2016 iliisha baada ya hakimu Godfrey Mwambapa kuona hatukuwa na hatia hivyo kutuachia huru. Soma Kesi namba 457: Mahakama yasema Maxence Melo na Micke William hawana Kesi ya kujibu! Yawaachia huru - JamiiForums

Sababu za kesi hizi

Tulikuwa tukiandikiwa barua nyingi; hizi chini ni baadhi. Zote zilikuwa zikitaka data ambazo hata mbele ya Hakimu Simba wakati wa utetezi wangu nilimwambia HATUNA. Majibu ya wanasheria yalieleza wazi pia kuwa tulikuwa tayari kutoa ushirikiano wa kutosha endapo tungejua jinai ya wateja wetu; barua tulizojibu hazikupata majibu tena toka Polisi na badala yake nilijikuta nikitiwa mbaroni.

Maamuzi ya Mahakama Kuuyalibainisha kuwa Polisi wangetaka data tukawa hatujawapa, basi wangezingatia kifungu cha 32 (3) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 ambapo wangeenda kuiomba Mahakama itoe amri ya data hizo kutolewa. Bahati mbaya, nilikamatwa na kufunguliwa mashtaka ambayo yanaendelea mpaka leo hii.

Huenda tulichokifanya ni kigeni kwa Polisi na baadhi ya watendaji, lakini ifahamike kuwa barua nyingi zilitoka vitengo mbalimbali vya Polisi na Taasisi nyingine. Kwa mwendo huo, ilitia shaka zaidi hasa anayetaka hizi data za wananchi ni nani na hatma ya hao wananchi itakuwaje. Ifahamike, makampuni haya binafsi yanayodaiwa kulalamika Polisi yalikuja kwetu yakitaka kujua vyanzo vya taarifa fulani… Baada ya kuona hawapati walichotaka, tuliishia kukutwa na kesi 3 nilizotaja hapo juu ambazo hadi leo ndo zimepelekea usumbufu mkubwa na hata kuwa na masharti kuwa nisiruhusiwe kuvuka mipaka ya Dar bila kibali tangu 2016. Nimehudhuria mahakamani kusikiliza kesi hizi mara 146 na kesi mojawapo ikiwa imekaa zaidi ya mwaka bila kuwa na shaidi.

Wito wangu: Kwa umoja wetu, tuendelee kushirikiana kuhakikisha Uhuru wa Kujieleza unalindwa na watoa taarifa zenye nia ya kufichua maovu ndani ya jamii wanalindwa bila kupewa vitisho vya aina yoyote. Mwananchi mwenye taarifa ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa demokrasia ya kweli.

Natambua kazi ngumu na ya kizalendo inayofanywa na Jeshi la Polisi, naheshimu sana mamlaka za dola na kutambua kuwa kuna wakati mambo mengine yanahitaji ushirikiano wetu wananchi katika kuweza kutoa huduma nzuri kwetu kama raia; lakini nadhani bila mfumo unaoeleweka wa kuchakata taarifa za watumiaji wa digital platforms, tutajikuta badala ya kuimarisha jamii inayotoa ushirikiano tunawavunja moyo wananchi hivyo wakafumbia macho maovu wanayoyaona katika jamii.
 
Pole sana tena sana. Kitu kimoja naomba nikuulize, hukumu hii si imeweka precedent kuwa unapashwa kutoa siri za wateja ili polisi wafanye kazi yao? Tunafannyaje sasa. Tunaweza kusaidiaje katika hili? Nimesikia kuwa mtakata rufani, fine, inbetween tunafanyaje?
Hapana, hakimu amesema kuwa hakukuwa na ulazima wa kutoa data hizo ila akahitimisha kuwa niliwazungusha sana Polisi hivyo kuzuia upelelezi wao.
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom