Hujuma madini

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
803
Hujuma madini

SIKU tatu tangu gazeti hili liandike habari kuhusu kasoro kadhaa zinazohusu udhaifu unaolipotezea taifa mamilioni ya fedha kupitia madini, taarifa zaidi zinaonyesha kuwa wawekezaji wa kigeni katika sekta hiyo ni mabingwa wa ‘kukarabati’ hesabu kwa malengo ya kukwepa kodi.

Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza Madini iliyoongozwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini, Lawrence Masha, imebaini pia kuwa, kampuni hizo za kimataifa za kuchimba madini zimekuwa zikijumuisha fedha wanazotoa kusaidia shughuli za kijamii kama vyanzo muhimu vinavyowapotezea mapato.

Kwa maana hiyo, hesabu za kampuni hizo zinaonyesha kuwa, mitaji iliyotumika kwa mwaka husika ni mikubwa na haijarejeshwa ili kuiwezesha kampuni kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ripoti hiyo ambayo ni miongoni mwa taarifa zinazochambuliwa na Kamati ya sasa ya Kuchunguza Mikataba ya Madini inayoongozwa na Jaji Mark Bomani, inabainisha pia kuwa, kampuni nyingi zimekuwa zikiidanganya serikali kuhusu hesabu zao kwa kutumia kipengele hicho cha kusaidia jamii, ambacho kipo kisheria.

Chini ya mikataba ya uchimbaji wa madini, kampuni hizo za madini hutakiwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika maeneo wanayoendesha migodi yao.

Matokeo yake, hesabu za matumizi ya mtaji za kampuni hizo zinaonyesha wanatumia fedha nyingi na hivyo kuonyesha kuwa kampuni zinapata hasara na hivyo kutokuwa na sifa ya kulipa kodi.

Mbali ya hilo, ripoti hiyo ya Masha ambayo katika habari ya juzi, katika gazeti hili ilibainisha udhaifu mkubwa uliopo katika Mamlaka ya Kodi na Mapato (TRA), inaeleza pia kwamba, baadhi ya gharama zinazotajwa kama za kusaidia jamii, hazihusiani moja kwa moja na miradi ya jamii.

Miongoni mwa miradi ya namna hiyo ni ule wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye mgodi, unahesabiwa kama msaada kwa jamii wakati kinachofanyika ni kuweka mabomba machache ya kuwapatia maji wananchi katika vijiji linamopita bomba hilo, lakini lengo lake kuu ni kuupatia mgodi maji na si wanavijiji.

Aidha, ripoti hiyo yenye kurasa 33, inayaainisha baadhi ya maeneo ambayo serikali inapoteza mapato kuwa ni pamoja na mahesabu ya kampuni za madini nchini, utoroshaji wa fedha nje ya nchi, manunuzi pamoja na ujanja unaofanywa na baadhi ya kampuni kuiweka migodi yao tofauti chini ya umiliki mmoja.

Kwa kiasi kikubwa, ripoti hiyo inasema kuwa serikali inapotea mapato hayo kutokana na udhaifu wa mikataba pamoja na taasisi zake, ikiwamo Wizara ya Nishati na Madini yenyewe, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na taasisi nyingine zionazohusika na kuratibu sekta hiyo.

Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa mikataba, wawekezaji katika sekta hiyo wapo huru kusafirisha mazao wanayozalisha nje ya nchi.

“Ukiondoa mkataba wa Bulyanhulu, mikataba mingine haina vipengele kuhusu utaratibu wa masoko. Kipengele hiki ni muhimu kwa sababu kinaweka uwazi katika masuala ya bei,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ambayo Tanzania Daima imeisoma.

Ikifafanua, ripoti hiyo inabainisha kuwa, wawekezaji wengi katika sekta hiyo wamekuwa wakiwasiliana na mawakala wanaosafisha madini nje ya nchi na wakishayapeleka madini ghafi, yakishasafishwa huuzwa huko huko bila serikali kuwa na habari ya kiasi cha madini yaliyouzwa.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo ilipendekeza kufanyiwa marekebisho kwa kanuni za uchimbaji madini za mwaka 1999 ili kuweka kipengele kitakachozilazimisha kampuni za madini kutoa kwa serikali mikataba yao ya wanunuzi wa madini.

Kwenye masuala ya kodi, ripoti hiyo inaonyesha kuwa kampuni nyingi zinatumia ujanja katika mahesabu yao, kiasi kwamba kwa miaka mingi zinaonekana kutopata faida na hivyo kutolipa kodi.

Kwa mujibu wa mikataba mingi hapa nchini, kampuni za madini haziwezi kutozwa kodi hadi hesabu zake zionyeshe kuwa zimerejesha mitaji yake kwa asilimia 100.

Baada ya kuonyesha mifano kadhaa ya nchi ambazo hazifuati mtindo huo, kamati hiyo inabainisha kuwa kuacha kampuni irudishe mtaji wake kwa asilimia 100 kunaigharimu nchi na pia kunapingana na taratibu za kodi zilizoainishwa katika kifungu cha 17 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.

Kamati inasema kuwa upendeleo huo wa kurudisha mtaji unatoa mwanya kwa kampuni hizo kupanga hesabu na kuonyesha kuwa hawajarudisha gharama za mitaji, na jambo hilo limeinyima serikali kodi tangu uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini uanze nchini.

Ripoti inasema kuwa ukichanganya na utaratibu wa kampuni kujumuisha migodi yake yote katika hesabu za pamoja, utaratibu huu unazidisha kuonyesha jinsi kampuni hizo zisivyopata faida, kwani uwekezaji mkubwa katika mgodi mmoja unaweza kunyonya faida inayopatikana katika mgodi mwingine na kampuni kuonekana haijapata faida.

Kuhusu utoroshaji wa fedha nje ya nchi, ripoti hiyo inabainisha kuwa mikataba ya madini inayataka makampuni kupata ruhusa ya Benki Kuu (BoT) kufungua akaunti nje ya nchi ili kuwezesha kuweka fedha zinazopatikana nje, hasa mikopo.

Ruhusa hiyo ya BoT inatolewa kwa masharti kuwa ipatiwe taarifa za benki kila mwezi na akaunti hizo zifungwe mara baada ya deni kumalizika kulipwa.

“Imeripotiwa kuwa makampuni mengi hayazingatii masharti haya, hasa kutoa ripoti za benki za kila mwezi. Pia makampuni mengi yanapokea fedha nyingi bila dhamana kutoka kwa kampuni zao mama ya wanahisa wake bila ya kupata ruhusa rasmi kutoka BoT,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kamati hiyo iliishauri Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na BoT, kufanya uchunguzi wa usafirishaji huu wa fedha.

Kuhusu suala la uajiri na mafunzo kwa wazalendo, ripoti hiyo inabainisha kuwa kampuni nyingi haziwasilishi serikalini mipango yake ya uajiri na mafunzo kwa wazalendo, licha ya kutakiwa kufanya hivyo kupitia sheria ya madini ya mwaka 1998.

Pia ripoti hiyo imeonyesha kukinzana kwa sheria ya uhamiaji ya mwaka 1995, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1997 ambayo inasema kuwa uwiano wa wafanyakazi wazalendo na wageni katika miradi ya madini na uchimbaji wa mafuta itapangwa na mwekeaji mwenyewe kulingana na kazi zilizopo.

“Hii inapingana na sera za nchi ambazo zinatoa msisitizo wa kuongeza ajira kwa Watanzania,” inasema ripoti hiyo na kupendekeza ushirikiano wa karibu baina ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Idara ya Uhamiaji, wizara za Nishati na Madini, Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, ili kudhibiti hali hiyo.
 
Back
Top Bottom