Hoyce Temu na Wabaguzi Mamboleo!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,485
40,014
NILIDHANI walioziacha fikra za Mwalimu ni viongozi wa CCM peke yao, kwa hakika nilikuwa nimekosea sana. Jumamosi iliyopita wakati Watanzania wengine walikuwa wanafurahia ushindi wa Taifa Stars dhidi ya The Cranes ya Uganda, kuna kundi la Watanzania waliokuwa wananung’unika kwanini binti mwenye asili ya Kihindi kachaguliwa kuwa Vodacom Miss Tanzania 2007.

Kwa vile Watanzania tuna mazoea ya kusahau mambo muhimu, hasa timu yetu ya taifa inapocheza, nimeonelea nililete jambo lililotokea Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam mapema kabla ya mechi ya marudiano na Msumbiji.

Kama nilivyosema hapo juu kuwa mwanzoni nilipokuwa naliangalia suala la “kuziacha fikra za Mwalimu” nilikuwa naangalia kwa mtazamo wa vyama vya kisiasa zaidi, lakini baada ya kusikia mwitikio wa watu baada ya Richa Adhia kuwashinda warembo wengine 25 na kutwaa taji hilo maarufu zaidi la urembo Tanzania, nimejikuta nikihitimisha kuwa si viongozi wa CCM tu walioziacha fikra za Mwalimu bali pia wananchi wa kawaida na wengine wenye nafasi kubwa katika jamii ambao si tu wameziasi fikra hizo, bali pia bila haya wala kusitasita wanatangaza hadharani hoja zao mbovu na zisizo na nafasi katika Tanzania hii.

Sijui ni makosa ya nani au ni kutokana na sababu ipi kwamba Watanzania tumeanza kuwa wabaguzi wa rangi. Kwa taifa ambalo lilimwaga damu yake kuupinga ubaguzi wa rangi, na kutoa rasilimali zake kuwasaidia wapigania uhuru, inaudhi na inatisha kuona kuwa leo hii bila hata aibu, tunatangaza hadharani kuwa sisi ni wabaguzi! Gazeti moja liliandika kwa kichwa cha habari kikubwa kuwa kitendo cha binti huyo wa Kitanzania kuchaguliwa ni “aibu”.

Nilijikuta nikitetemeka kwa hasira, huku macho yangu yakinitoka kama gololi kwa mshangao kuona kuwa taifa ambalo lilitetea usawa wa watu wetu na ambalo kwenye katiba yake linasema kuwa “kila mtu anastahili haki ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, leo hii, baadhi ya watu wameanza kutenga nani hastahili tunu hizo.

Hawa ni wabaguzi mamboleo, ambao leo najitolea kuwapinga hadharani, kuwa hoja zao ni mbovu, hazina msingi, za kibaguzi, na ambazo zisipopingwa zitaendelea kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama katika jamii yetu. Hawa watu ni wa kupingwa kama kuupiga vita ugonjwa mbaya wa kuambukiza.

Wanasema ati Adhia hakustahili kuwa mwakilishi wa Watanzania kwa vile ana asili ya India. Watu hawa bila haya wameanza kutukuza unasaba wa watu, kwamba watu wanaostahili kushinda mashindano kama haya ni lazima wawe wanatoka Tanzania.

Hata hivyo, watetezi hawa wa ubaguzi mamboleo wanashindwa kutuambia ni nani Mtanzania ambaye ana asili ya ardhi hii. Wangoni wanatoka wapi? Wachagga wanatoka wapi? Wamakonde je? Na Wahaya asili yao wapi? Tutawauliza hawa wabaguzi mamboleo (neo-segregationists) je, kama Richa wazazi wake wangekuwa ni Watanzania ambao asili yao ni Nigeria, nao ni weusi, ingekuwa sawa kwa binti huyo kushinda?

Vipi kama ingekuwa ni mtoto wa Wamarekani weusi waliohamia Tanzania miaka ya 60 na licha ya kuwa ni weusi, lakini familia zao zimekaa miaka mia tatu huko Marekani, angestahili kushinda?

Wanasema si hilo tu la wapi anatoka, wanatuambia kuwa Richa hawakilishi rangi ya Watanzania. Kwa hawa wabaguzi mamboleo, rangi ya Watanzania wote ni nyeusi na kama wewe si mweusi, basi Utanzania wako ni robo au theluthi (kutegemea na weusi wako).

Sasa anapotokea binti ambaye ni Mtanzania (kiuraia), lakini si mweusi, wabaguzi wetu wanataka tumtenge kwa vile si Mtanzania kamili? Watu hawa wanashindwa kwa moyo mweupe kuelezea mbona tuna wabunge wenye asili ya Uhindi, tunawafadhili wa klabu wenye asili ya Uhindi, tuna madaktari wa Kihindi, n.k ambao ni Watanzania kwa kuzaliwa.

Leo hii, tuna mbunge wa kuchaguliwa, singasinga, tuna Waziri wa Fedha mwenye asili ya Asia, tuna mweka hazina wa CCM mwenye asili ya Iran, lakini hawa wote ni sawa kushika nafasi hizo, na kutuwakilisha bungeni isipokuwa Richa hawezi kutuwakilisha kimataifa.

Wengine wanapinga binti huyo ati kwa vile jamii yake ni watu wanaojitenga, na hivyo si Watanzania kamili. Kuna watu wanataka binti huyu asingepewa nafasi hiyo kwa vile tu Wahindi hawaoani na Watanzania weusi au kuruhusu watoto wao kuwa na marafiki weusi. Watu hawa wenye hisia ya uduni wanataka tuamini kuwa, kuona kati ya Wahindi na Watanzania wa makabila mengine, basi kunawafanya Wahindi wakubalike zaidi! Hii ni hisia ya kitumwa!

Ni makabila mangapi ambayo watoto wao huoa ndani ya makabila yao? Je, Wahindi walioko Uingereza, Marekani, n.k wanaoana vipi na watu weupe? Je, inawezekana kuwa kuna sababu nyingine kabisa inayowafanya wasioane na watu wa makabila mengine kuliko hiyo ya kuwa “wanajitenga”? Hivi kweli kama Richa angekuwa na boyfriend aitwae Musa, tena Mndengereko, ingemfanya akubalike kuwa Miss Tanzania? Hoja za namna hii ni za kipumbavu na lazima zionyeshwe kuwa ni za kipumbavu.

Baada ya kusikia maneno haya ya watu mbalimbali nimeamini ya kuwa Mwalimu alikuwa mbele ya muda wake kwa miaka mingi kweli. Mwaka 1955 akizungumza kwenye mojawapo ya vikao vya Umoja wa Mataifa wakati wa mazungumzo yaliyozaa uhuru wa Tanganyika, Mwalimu aliainisha wazi kabisa kuwa, katika nchi mpya itakayozaliwa; “tunawaona Waasia na Wazungu ambao wamechagua (Tanzania) kama nchi yao kuwa ni (Watanzania) wenzetu. Na hatuna haja yoyote ya kuona wafukuzwe au wabaguliwe kwa namna yoyote.”

Mwaka mmoja baadaye, akizungumza tena kwenye Umoja wa Mataifa, Mwalimu alielezea kuwa; “tumedhamiria kuona kuwa Waasia na Wazungu waliochagua kufanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kabisa, kwamba wanapata haki zote za kisiasa kama wengine. Tutapinga ubaguzi wowote kwa misingi ya nasaba, rangi, au imani.”

Na wakati Tanganyika inajiandaa kupata uhuru na mswada wa uraia ulipoletwa (Oktoba 1961) bungeni, Mwalimu alizungumza kwa kirefu kuhusu kile alichokiita; “Kanuni za Uraia” na kuhusu suala la ubaguzi wa rangi, alisema kwa uzito mkubwa; “Mheshimiwa (Spika), hawa wanaojifanya wanajua kama wangekuwa na uwezo fulani, nina uhakika wangesema kuwa binadamu wote wameumbwa sawa isipokuwa weupe, Wahindi, Waarabu na Wachina ambao wanaishi Tanganyika (isomeke Tanzania).

“Hawatakoma hapo Mheshimiwa; wataendelea, kwani kanuni ina kawaida ya kulipiza kisasi. Ukiivunja kanuni, hiyo kanuni itatafufa namna ya kukuvunja wewe. Na endapo watu wanavunja kanuni kubwa, basi hiyo kanuni itapata njia ya kuwavunja watu hao.”

Anachosema Mwalimu ni kuwa, huwezi kubagua ukakoma. Mtu ambaye anaanza kubagua watu huwa hakomi kwani ukiishavunja ile kanuni ya usawa utajikuta unaanza kubagua si kwa rangi tu, bali kwa lugha, kwa mahali, kwa dini, na hata kwa lafudhi! Haya yote yameonekana kwenye suala la binti huyu.

Hawa wabaguzi mamboleo hawawezi kukoma na Richa. Baadaye watasema mbona wanaochaguliwa wanatoka Dar zaidi na hakuna Miss Tanzania kutoka Kigoma, na akipatikana kutoka Kigoma watasema mbona hakuna kutoka Maswa? Na hata wakipatikana ma-Miss Tanzania kutoka kila kona na mahali, wabaguzi hawatakoma, maana wataanza kusema mbona ma-Miss Tanzania wengi ni warefu? Na akichaguliwa mfupi, watasema mbona wengi wanaochaguliwa ni Waislamu? Na hata wakipatikana Waislamu watakuja na idadi n.k Ubaguzi huwa haukomi hadi ukomeshwe.

Watanzania tumeziasi fikra za Mwalimu, fikra ambazo zilitufanya tuwe mashujaa wa usawa na haki ya mtu mweusi. Tulipopigania haki ya kutambuliwa utu wetu na kuthaminiwa utu huo, haikuwa na maana kuwa basi tuwe na haki ya kuwabagua wengine na kuwanyima wengine haki hiyo.

Kilichonishtua zaidi ni kuwa, hadi hivi sasa hakuna kiongozi yeyote mwenye dhamira safi, ambaye amejitokeza kumtetea binti huyu! Tumeanza kukubali kuwa Watanzania wenye asili ya Uhindi hawastahili mambo fulani. Magazeti yetu na vyombo vyetu vya habari vinaporipoti sumu hii, vinawaumiza hasa watoto wetu.

Leo hii watoto wetu wanashangaa. “Mama mbona amechaguliwa Mhindi?” Wazazi wanabakia kujiumauma badala ya kuwaelimisha watoto wetu kuwa Watanzania tunatoka katika lugha nyingi, tunatoka sehemu mbalimbali na tuna rangi mbalimbali. Badala ya kuwaambia watoto hawa kuwa Richa ni binti wa Kitanzania, tunabakia kuitetea sumu hiyo kwa kuondoka ukumbini kwa hasira, kisa, “kwanini hakuchaguliwa Mtanzania mzawa?”

Ndugu zangu, hoja za wabaguzi hawa si mahali wazazi wa Richa wanatoka au si lugha anayozungumza. Wanaodai kuwa Kiswahili kingetumika wanataka tuamini kuwa Watanzania wote weusi wanazungumza Kiswahili sanifu na fasaha! Leo wanamcheka binti mmoja kwenye mashindano hayo kwa vile lafudhi yake “haikuwa nzuri!” Wabaguzi hawakomi. Akija binti ambaye anazungumza Kiswahili kwa lafudhi ya Kimatumbi, au Kikinga mtu huyo inabidi ajitahidi kujibadilisha ili awe na yeye Mtanzania kweli kweli. Nimeliona hili kwenye baadhi ya watu siku hizi ati wakizungumza wanajitahidi kuzungumza Kiswahili kama wazungu wanavyozungumza!

Ninachosema ni kuwa, ukiondoa upendeleo au ufisadi kwenye mashindano hayo, Richa Adhia ana haki ya kuliwakilisha taifa hili, na Watanzania wote tuone fahari kuwa tumefikia mahali kuwa tunaamini katika usawa wa wananchi wetu kiasi cha kusimama upande mmoja na binti huyu.

Kama nchi za Marekani na Afrika Kusini ambazo zilikuwa na sera rasmi za kibaguzi, leo zinawakilishwa katika nafasi mbalimbali na watu ambao wanaonekana si wa asili ya nchi hizo, kwanini sisi tuone aibu na kujiona duni? Mtu mweusi amewahi kuliongoza Jeshi la Marekani, na leo hii Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ni mtu mweusi, kwanini tunaona aibu na kuona vibaya kuwakilishwa na Richa? Mwalimu alionya kuhusu ubaguzi wa aina hii kwenye ile hotuba yake kule Mbeya, na leo hii Watanzania tumeshaanza kusahau! Laana nyingine ni za kujitakia.

Baada ya kusema hayo, ni lazima pia niseme jambo moja, kwani nafasi hii imejitokeza. Kwa ndugu zetu, Watanzania wenzetu na wana na mabinti wa Kitanzania wenye asili ya nje ya Bara la Afrika, wakati umefika wa nyinyi nanyi kushiriki kwenye sekta moja muhimu sana ambayo mnakosekana.

Tunawaona wengi wenu kwenye biashara, siasa, utabibu, uanasheria n.k, lakini mnakosekana kwenye sekta moja. Hamuonekani kwenye majeshi yetu ya ulinzi na usalama. Ninawakumbuka maofisa wachache wa polisi ambao walikuwa na asili ya Asia (sitashangaa leo watakuwa wameshastaafu) na kwenye JWTZ ninamkumbuka kamanda mmoja ambaye alikuwa ana asili ya nje ya bara la Afrika.

Hakuna kitu kinachoonyesha utii wa mtu kwa nchi aliyoko kama kuwa tayari kuifia. Na hakuna mahali ambako panaonyesha utii huo kama kwenye vyombo vyetu vya usalama. Suala la kuoana au lugha linaweza kuwa ni la mila na desturi, lakini unapokuja ulinzi wa taifa letu, ni lazima wote tupate nafasi sawa ya kuitumikia nchi yetu.

Mwanzoni nilikuwa nadhani kuwa Wahindi ni “lelemama” na “goigoi”, kuwa hawawezi suluba za mambo ya kijeshi, lakini baada ya kutembelea India na Pakistan na kuona wanajeshi wao walivyo imara, najiuliza ndugu zetu Wahindi wa Tanzania ni kweli hawawezi kumudu suluba za mafunzo ya kijeshi?

Ninafahamu baadhi ya vijana kadhaa wa Kiarabu ambao wanalitumikia Jeshi la Polisi, wakati umefika kwa familia za Wahindi kuanza kuwatia moyo vijana na watoto wao kuchagua ajira katika majeshi yetu, si tu kuonyesha utii wao, bali pia kushiriki katika ulinzi na usalama wa nchi yao! Hili linatokea Afrika Kusini, linatokea Zimbabwe, linatokea Namibia, na kwa hakika linatokea Uingereza na Marekani.

Ninachoshauri ni kuwa, ndugu zetu wenye asili ya Asia wakae chini na kuamua kwa dhati na kwa makusudi kuwatia moyo na kuwasaidia vijana wao kuyatumikia majeshi yetu ya ulinzi na usalama. Haiwezekani Watanzania weusi ndio wawe walinzi pekee wa taifa hili. Na kwa wale wachache ambao tayari wamejiunga na vyombo hivyo, kwa hakika wanastahili kutambuliwa na kupewa pongezi, kwani wamefanya kile ambacho vijana wengi wa Kitanzania wanakifanya kila mwaka, nacho ni kusimama kula kiapo cha kuilinda nchi hii kutoka maadui wa ndani na wa nje!

Baada ya kusema hayo yote, naomba warembo wengine walioshindwa kama wanaamini Richa ameshinda kwa haki, wajitokeze kumuunga mkono badala ya kumuacha pweke, nashauri uongozi wa Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni ujitokeze na kukemea mawazo hayo ya kibaguzi, na ninatoa ushauri na wito kwa Hoyce Temu ambaye aliwahi kuwa Miss Tanzania, kusimama hadharani na kuliomba radhi taifa kwa mawazo na sumu mbaya kabisa ya kibaguzi aliyoinyunyiza siku ya Jumamosi. Ni yeye ndiye amelitia taifa letu aibu na wenzake wenye mawazo ya kibaguzi kama ya kwake.

Na mwisho, ninatoa wito kwa Watanzania kuwapinga wabaguzi hawa mahali popote wanapojitokeza, kwani sumu yao inatia ganzi fikra, inapumbaza akili, na inasababisha mtindio wa mawazo. Wabaguzi hawa mamboleo hawana nafasi, hawakubaliki, na wasipewe nafasi wala kukubalika, tumeanza kuwapinga, na tutaendelea kuwapinga! Hadi pale watakapotambua kuwa raia wote wa Tanzania ni sawa na wanastahili haki ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wao. Vinginevyo tutaanza kuwabagua wao kwa ubaguzi wao hadi tuwe na taifa la wabaguzi wenye kubaguana ambao kila kukicha wanatafuta wa kumbagua.
 
Kauli yako Mh. Mwanakijiji inaweza kuwa sawa, lakini tujiulize: Hao ambao hatutakiwi kuwabagua wao wanajiweka katika kundi gani? Wanajiona watanzania katika nafasi na shughuli wanazoona zinawanufaisha au wanajiona watanzania katika nafasi na shughuli zote.

Mfano najaribu tafuta ndoa ya mhindi na mwafrica????Wakati mwingine huwa naona mifano mingine haifai kuilinganisha(pengine kwa uelewa wangu mdogo)Historia ya mmarekani mweusi kuwa marekani na Wahindi kuja Tanzania.Nia zao kwa nchi hizi mbili sizani kama ziko sawa.
 
Unajua ndugu Mwanakijiji kitu ubaguzi kitakuwepo hadi Yesu atakaporudi katika jamii zote dunia.Na mtu ambaye anaongoza kwa kubagulia ni mtu mweusi,ubaguzi ni dhambi iliyopo moyoni mwa mtu,kujiona yeye ni bora na wengine hawafai.

Hiki kinachoendelea kuhusu miss Tanzania,kinaweza kueleweka kama ubaguzi,maana sijawahi kusikia malalamiko makubwa kuhusu miss aliyechagulia kama huyu wa sasa.Binafsi mie sita-judge rangi yake,anaweza kuwa hafai au anafaa,ila nina maswali machache kuhusu ndugu zetu wahindi tulionao pale nchini.Inawezekana hawa watu tokea enzi hizo walianza kujibagua katika jamii yetu,ndio maana kuna maeneo yanaitwa uhindini,uzunguni,japo sijawahi kusikia uarabuni maana waarabu wapo close na waswahili.Ni vigumu sana kumkuta mtoto wa kihindi kuwa na urafiki na mswahili,wahindi waliopo Tanzania wamejitenga na jamii,wana jamii yao ya kihindi.Ndio tuna wabunge wahindi,lakini hao wanaweza kuwa wapo pale kwa ajili ya vifedha vyao tu,ila ukweli unabakia pale kuwa hawapo close na jamii.

Nimewahi kwenda Mumbai India,nilikutana na mambo ya ajabu sana huko,nikaanza kujiuliza hawa ndio jamaa tunaonunua mavituz kwenye maduka yao?Mie naona huu utakua wakati muafaka na jamii ya kihindi kuweza kuona kuna umuhimu wa kushirikiana na watanzania katika shughuli zote,sio kwamba kuona kuna mshiko basi waananza kujiita watanzania,hapana watanzania kulalamikia hilo jambo la miss Tanzania si kwamba wana wivu au hawana akili,hapana kuna makosa yalifanyika huko nyuma katika uhusiano wa mswahili na mhindi.Hebu jiulize kwa nini watu wengi hawapendi kufanya kazi kwenye makampuni ya kihindi,au viwanda?Hii inatokana na wao wanaichukulia vipi jamii ya kiafrika,labda wanatudharau,labda wanataka wakuze mila zao,huwezi kujua nia yao,ila hawapo tayari kushirikiana na jamii zingine.Kwa hiyo wahindi waanze kusahihisha makosa yao kabla ya kusahihisha waswahili,wote tupo sawa tofauti ni rangi tu,na kila mtu anapenda rangi yake aliyopewa na Mungu.Namshukuru Mungu Wangu kuniumba Mwaafrika,najivunia asili yangu.
 
Mwkjj hoja nzuri sana mzee japo ina maneno makali yanayokatisha tamaa kuwa na mawazo tofauti na yako. Lakini kama mwenzangu alivyouliza hapo juu, na mimi naomba kuuliza hivyohivyo (nadhani nitakuwa sio mbumbavu) hivi ndugu zetu hawa do they feel tanzanian enough? nachukulia katika mtizamo wa watanzania hao wanavyowaona watanzania wengine wenye asili ya kibantu.Hivi ukiachilia nyumba za msajili wanazopangisha wamejenga wapi au wana asset zipi endelevu ukiachilia mbali zinazohusiana na biashara.

Hivi wanaishi wapi kwenye jamii. Hivi wao wanaoa wapi ( acha kuolewa) wanashiriki wapi social activities)(misiba,majumuhiko ya tamaduni zetu.) Umegusia katika mada kuhusu mtanzania mwenye asili ya kinageria kuwa ms tz, kidogo na hapo naomba kuuliza maana ninavyojua mimi kabla ya ukoloni africa haikuwa na mipaka na majina kama tz, ivorycost nk. haya ni mambo ya wazungu tu tumeletewa. Kwa maana nyingine African cultures na kila kitu ni kilekile.

Huoni mzee kama mfano huo uko mbali? India mfano ni subcontinent, kuna wahindi weusi,weupe n.k. hivi mhindi mwenye asili ya kitanzania yupo? au mwenye asili ya kiafrica sijui.nauliza tu mzee.lakini muhindi mwenye asili ya pakstani anaweza kuwa miss india au bangladesh. Mzee sioji uhalali wa utanzania wa watu wenye asili ya kihindi na haki zao zote walizonazo ila naona mada imekuwa nzuri sana kiasi kwamba ina stimulate intellectual thinking.

Unajua nini najiuliza kwa mtizamo huo kama kweli siku moja MWINGEREZA mwenye Asili ya Kiarabu anaweza kuwa Queen au King of England?. maana UK sasa hivi ina waingereza wa makabila yote ya dunia na inabidi tuwasifie kwa juhudi hizo. wengi kati ya hao wamezaliwa hapohapo uingereza. swali ni je utaifa au uraia wa mtu unaweza kuwa na mipaka kutokana na asili yake katika kufahidi baadhi ya Haki zitokanazo na utaifa huo?
 
Bro, hapa ninapoishi ndiyo kuna jamii ya wahindi wengi sana.. guess what? Siwaoni wakichanganyika na weusi au weupe! Kila ukiwakuta wako kivyao vyao tu. Lakini once in a while naenda kwenye hoteli zao kupata msosi (kuku wa biryani).. na wanakutreat vizuri tu. Lakini kwa muda wote nilioishi hapa, sijaona bado binti wa kihindi akideti watu weupe, au weusi!!

Je inawezekana wazazi wa kihindi wanawalinda watoto wao kutoka katika jamii inayowaita "ponjoro", "wahindi koko", na "magabachori"? Wewe ukiwa na demu wa kihindi ambaye rafiki zako wanamuita "ponjoro" ni kweli itamfanya ajisikie mtanzania zaidi?

Hakuna ubaya mtu kujivunia asili yake, tatizo ni kutukuza asili hiyo huku ukizishusha asili nyingine. Hitler alifanya hivyo hadi pale Jesse Owens alipodhihirisha kuwa watu weupe hawakuwa juu ya wanadamu wengine wote. Sasa kujivunia asili yako sawa, lakini usianze kuona wasio na asili ya weusi ni watu duni! Ukishafikia hapo utakuwa unakaribia kuvuka mstari wa Hitler ambapo walio duni na wasio weupe ilibidi waanze kuondolewa "kiaiana".
 
Baada ya kusema hayo yote, naomba warembo wengine walioshindwa kama wanaamini Richa ameshinda kwa haki, wajitokeze kumuunga mkono badala ya kumuacha pweke, nashauri uongozi wa Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni ujitokeze na kukemea mawazo hayo ya kibaguzi, na ninatoa ushauri na wito kwa Hoyce Temu ambaye aliwahi kuwa Miss Tanzania, kusimama hadharani na kuliomba radhi taifa kwa mawazo na sumu mbaya kabisa ya kibaguzi aliyoinyunyiza siku ya Jumamosi. Ni yeye ndiye amelitia taifa letu aibu na wenzake wenye mawazo ya kibaguzi kama ya kwake.

Alikutana na waandishi wa habari jana/juzi na kujaribu kujieleza wazi kuwa yeye hakuwa na nia mbaya kama umma ulivyomnukuu. 'Mlininukuu vibaya' ndivyo alivyosisitiza.

Alisema yeye hana tatizo na u-hindi wa Richa, tatizo ni warembo kuhukumiwa kwa lugha na kutopewa fursa ya kupita na vazi la ubunifu.

Alitumia muda mwingi kusisitiza kuwa suala la lugha lilitumika vibaya na kuwa kwa Richa anayeweza kuongea kiingereza kwa ufasaha ilikuwa ni nafasi ya 'kumpa shavu' kirahisi.

Binafsi: Sikupenda attitude ya Mrembo huyu. Ni kweli wahindi wabaguzi na wako tayari kuukana utanzania wakati wowote na saa yoyote. Anayewatetea hawajui vema. Ni kweli pia kuwa hata viongozi wenu (mimi simo) wenye asili ya kiasia ni wachache ambao wakifa ndugu zao watakubali wazikwe Tanzania (mifano tunayo). Lakini kitendo cha mrembo huyu kumwaga chozi mbele za kadamnasi kilikuwa na ishara mbaya sana na aliniboa. Kwa hili nasema thumb down
icon13.gif
 
Mwkjj hoja nzuri sana mzee japo ina maneno makali yanayokatisha tamaa kuwa na mawazo tofauti na yako. Lakini kama mwenzangu alivyouliza hapo juu, na mimi naomba kuuliza hivyohivyo (nadhani nitakuwa sio mbumbavu) hivi ndugu zetu hawa do they feel tanzanian enough? nachukulia katika mtizamo wa watanzania hao wanavyowaona watanzania wengine wenye asili ya kibantu.Hivi ukiachilia nyumba za msajili wanazopangisha wamejenga wapi au wana asset zipi endelevu ukiachilia mbali zinazohusiana na biashara. Hivi wanaishi wapi kwenye jamii. Hivi wao wanaoa wapi ( acha kuolewa) wanashiriki wapi social activities)(misiba,majumuhiko ya tamaduni zetu.) Umegusia katika mada kuhusu mtanzania mwenye asili ya kinageria kuwa ms tz, kidogo na hapo naomba kuuliza maana ninavyojua mimi kabla ya ukoloni africa haikuwa na mipaka na majina kama tz, ivorycost nk. haya ni mambo ya wazungu tu tumeletewa. Kwa maana nyingine African cultures na kila kitu ni kilekile. Huoni mzee kama mfano huo uko mbali? India mfano ni subcontinent, kuna wahindi weusi,weupe n.k. hivi mhindi mwenye asili ya kitanzania yupo? au mwenye asili ya kiafrica sijui.nauliza tu mzee.lakini muhindi mwenye asili ya pakstani anaweza kuwa miss india au bangladesh. Mzee sioji uhalali wa utanzania wa watu wenye asili ya kihindi na haki zao zote walizonazo ila naona mada imekuwa nzuri sana kiasi kwamba ina stimulate intellectual thinking. Unajua nini najiuliza kwa mtizamo huo kama kweli siku moja MWINGEREZA mwenye Asili ya Kiarabu anaweza kuwa Queen au King of England?. maana UK sasa hivi ina waingereza wa makabila yote ya dunia na inabidi tuwasifie kwa juhudi hizo. wengi kati ya hao wamezaliwa hapohapo uingereza. swali ni je utaifa au uraia wa mtu unaweza kuwa na mipaka kutokana na asili yake katika kufahidi baadhi ya Haki zitokanazo na utaifa huo?

Hilo swali la mwisho ndilo la msingi katika mjadala huu. Sisi ambao tunaishi kama minority kwenye nchi za watu, je watoto wetu ambao ni weusi wakija kushindana kama Miss US au Miss UK wapewe nafasi hiyo au wakataliwe kwa sababu ni weusi na hawana asili ya nchi hizo? Tutakubalia itangazwe na binti mweupe "Mwajuma Did not deserve to win because she is not white, and her parents are not from US/UK", hivi kweli tungesema "ndiyo"?

Hapa niulize ni wangapi wamewahi kujaribu kutongoza binti wa kihindi wakakataliwa? Halafu hili la kumhumuku Richa kwa makosa yanatokana na jamii yake ni vipi kwa vipi? Yaani kwa vile jamii yake au watu wa asili yake kiujumla wako hivi au vile basi Richa naye hastahili kutokuwa Miss Tanzania? Kwanini tumuadhibu binti ambaye amegombea katika jamii ya Watanzani tangu miss kitongoji, amekaa nao kambini n.k Kama kuna mtu ataniambia kuwa Richa alikuwa na chumba chake, alikuwa anapewa chakula tofauti na wengine, n.k hapo naweza kusema kuwa Richa labda hakustahili, lakini hadi hivi sasa hakuna mtu anayedai kuwa Richa alipendelewa kwa vile ni Mhindi, wengi wanasema kwa vile Richa si Mweusi! Huu ni ubaguzi wa rangi in reverse!
 
Alikutana na waandishi wa habari jana/juzi na kujaribu kujieleza wazi kuwa yeye hakuwa na nia mbaya kama umma ulivyomnukuu. 'Mlininukuu vibaya' ndivyo alivyosisitiza.

Alisema yeye hana tatizo na u-hindi wa Richa, tatizo ni warembo kuhukumiwa kwa lugha na kutopewa fursa ya kupita na vazi la ubunifu.

Alitumia muda mwingi kusisitiza kuwa suala la lugha lilitumika vibaya na kuwa kwa Richa anayeweza kuongea kiingereza kwa ufasaha ilikuwa ni nafasi ya 'kumpa shavu' kirahisi.

Binafsi: Sikupenda attitude ya Mrembo huyu. Ni kweli wahindi wabaguzi na wako tayari kuukana utanzania wakati wowote na saa yoyote. Anayewatetea hawajui vema. Ni kweli pia kuwa hata viongozi wenu (mimi simo) wenye asili ya kiasia ni wachache ambao wakifa ndugu zao watakubali wazikwe Tanzania (mifano tunayo). Lakini kitendo cha mrembo huyu kumwaga chozi mbele za kadamnasi kilikuwa na ishara mbaya sana na aliniboa. Kwa hili nasema thumb down
icon13.gif


Hili suala la lugha hebu tuliweke sawa kidogo. Kama angechaguliwa mtu ambaye kiingereza hakipandi, halafu baadaye wanaenda Sanya, China kwenye Miss World, hivi anafikiri ataulizwa maswali kwa Kifipa? As a matter of fact, lugha rasmi za Tanzania ni Kiingereza na Kiswahili na hili liwe changamoto kwa wale wote wanaotaka kugombea Umiss "wherever" bora wapandishe kiingereza chao na hata lugha nyingine za ziada. Hebu fikiria kama angekuwepo binti kati yao ambaye amepandisha Kiingereza na Kifaransa, halafu akijibu anajibu kwa kiingereza halafu anachombezea na kifaransa kidogo, huoni huyo angescore juu kuliko hata Richa!?

Kama tatizo ni kuwa wengine kiingereza kimekuwa "maimuna" sasa kwanini wamlalamike Richa? Sasa walitaka Richa naye azungumze kiingereza cha kuvunja vunja ili alingane nao?
 
Hili suala la lugha hebu tuliweke sawa kidogo. Kama angechaguliwa mtu ambaye kiingereza hakipandi, halafu baadaye wanaenda Sanya, China kwenye Miss World, hivi anafikiri ataulizwa maswali kwa Kifipa?

Babangu nifafanulie kidogo tu, una hakika wanaogombea Miss World wote wanaongea kiingereza? Really? I totally not agree with you babu. Mchina ajibu swali la kiingereza? Uliangalia mashindano ya mwaka jana?
 
Hilo swali la mwisho ndilo la msingi katika mjadala huu. Sisi ambao tunaishi kama minority kwenye nchi za watu, je watoto wetu ambao ni weusi wakija kushindana kama Miss US au Miss UK wapewe nafasi hiyo au wakataliwe kwa sababu ni weusi na hawana asili ya nchi hizo? Tutakubalia itangazwe na binti mweupe "Mwajuma Did not deserve to win because she is not white, and her parents are not from US/UK", hivi kweli tungesema "ndiyo"?

Hapa niulize ni wangapi wamewahi kujaribu kutongoza binti wa kihindi wakakataliwa? Halafu hili la kumhumuku Richa kwa makosa yanatokana na jamii yake ni vipi kwa vipi? Yaani kwa vile jamii yake au watu wa asili yake kiujumla wako hivi au vile basi Richa naye hastahili kutokuwa Miss Tanzania? Kwanini tumuadhibu binti ambaye amegombea katika jamii ya Watanzani tangu miss kitongoji, amekaa nao kambini n.k Kama kuna mtu ataniambia kuwa Richa alikuwa na chumba chake, alikuwa anapewa chakula tofauti na wengine, n.k hapo naweza kusema kuwa Richa labda hakustahili, lakini hadi hivi sasa hakuna mtu anayedai kuwa Richa alipendelewa kwa vile ni Mhindi, wengi wanasema kwa vile Richa si Mweusi! Huu ni ubaguzi wa rangi in reverse!


Naomba tena kuuliza kaswali kaduchu, hivi hao (mimi simo) wanao lalamika kuhusu Richa wanafanya hivyo kwa sababu ni mhindi mweupe au kwa sababu ya asili yake kuwa mhindi. Hivi angekuwa mhindi mweusi au mhindi mwenye asili ya kizungu lisingekuwa tatizo? nauliza hivyo kwa sababu kila nikisoma hoja za wanaokataa mhindi kuwa ms tz, sijaona mahala ambapo wanazungumzia rangi yake bali asili yake, picha ninayopata mimi ni kwamba hata kama angekuwa mweusi lakini ni mhindi watu bado wangelusha mawe, au wewe ili unalionaje?
 
Naomba tena kuuliza kaswali kaduchu, hivi hao (mimi simo) wanao lalamika kuhusu Richa wanafanya hivyo kwa sababu ni mhindi mweupe au kwa sababu ya asili yake kuwa mhindi. Hivi angekuwa mhindi mweusi au mhindi mwenye asili ya kizungu lisingekuwa tatizo? nauliza hivyo kwa sababu kila nikisoma hoja za wanaokataa mhindi kuwa ms tz, sijaona mahala ambapo wanazungumzia rangi yake bali asili yake, picha ninayopata mimi ni kwamba hata kama angekuwa mweusi lakini ni mhindi watu bado wangelusha mawe, au wewe ili unalionaje?

Bwana mdogo, hebu kwa dakika chache tuzungumzie hii "asili". Wanaposema asili yake wana maana ya mtu ambaye asili yake si Afrika au inamhusu mwenye asili ya India peke yake? Je, kama Richa angekuwa ana asili ya Ulaya wangekubali? Sasa kama tatizo ni "asili yake" ni wangapi watanzania ambao asili yao ni nje ya bara hilo? Hivi umewahi kukutana na Wairaqw wa mikoa ya mbulu ukiwaona unajua kabisa wana damu ya nje ya Bara la Afrika, je wanastahili kugombea Umiss Tanzania? Vipi kama huyo binti angekuwa ni mtoto wa waarabu Watanzania ambao asili yao ni toka Oman, watu wangepinga pia?
 
Mimi hakukataa, alikubali kabisa sema wazazi wake waliharibu. Ningejibebea kifaa cha kidosi :)


mimi niliopoa binti wa Kihaya aliitwa Rose Ngaiza.. wazazi wake walipogundua kuwa mimi ni mtu wa pwani, wakanitolea nje. Tuliibia ibia, lakini haikuweza kwenda mbali.. sasa sijui niwafikiri vipi Wahaya wote...
 
Hapo nipo pamoja nawe bwana Mwanakijiji,ila ninachotaka kumaanisha,ni kuwa wahindi inabidi waitambue jamii ya kitanzania kabla jamii ya kitanzania haijawatambua.Hata mie ninapoishi kuna wahindi wengi sana,wapo kivyao tu,guess what?Mie rafiki yangu mkubwa kabisa hapa ughaibuni ni mhindi,tupo course moja tupo masaa yote pamoja,tena huwa namtania kuwa yeye ni mhindi mwenye tabia ya kipekee.Kwa hiyo wahindi wajumuike na jamii yetu ya kitanzania,wasilete unafiki na kujali maslahi yao,tena tumegundua wengine wanashirikiana na watawala wabovu kuuza nchi yetu. Ni Nadra sana kwa mtu mweusi kubagua,ila yeye ni rahisi sana kubaguliwa.Huu ndio muda muafaka wa wahindi kuitambua jamii kabla ya jamii kuwatambua.
 
Hapo nipo pamoja nawe bwana Mwanakijiji,ila ninachotaka kumaanisha,ni kuwa wahindi inabidi waitambue jamii ya kitanzania kabla jamii ya kitanzania haijawatambua.Hata mie ninapoishi kuna wahindi wengi sana,wapo kivyao tu,guess what?Mie rafiki yangu mkubwa kabisa hapa ughaibuni ni mhindi,tupo course moja tupo masaa yote pamoja,tena huwa namtania kuwa yeye ni mhindi mwenye tabia ya kipekee.Kwa hiyo wahindi wajumuike na jamii yetu ya kitanzania,wasilete unafiki na kujali maslahi yao,tena tumegundua wengine wanashirikiana na watawala wabovu kuuza nchi yetu. Ni Nadra sana kwa mtu mweusi kubagua,ila yeye ni rahisi sana kubaguliwa.Huu ndio muda muafaka wa wahindi kuitambua jamii kabla ya jamii kuwatambua.

Mbona unazungumza kama vile Wahindi siyo Watanzania? HIvi unaweza kusema "Wamang'ati ni lazima watambue jamii ya Watanzania kabla jamii haijawatambua" au unaweza kusema "Wahadzabe wajioneshe kuwa wanaikubali Tanzania, kabla Tanzania haijawakubali"? Kuhusu suala la baadhi yao kushirikiana na watawala wabovu nikuhakikishie kuwa wengi wanaotuletea mikataba mibovu ni weusi tii tii kama sisi, tena wengine ni wasukuma, wahaya, wanyakyusa, wamwera, wamakua n.k ! Ufisadi hauna rangi!
 
NI kweli Nyani, na ndio maana ni lazima tujitambue hivyo ili kuweza kujiepusha na tabia za namna hiyo.
 
NI kweli Nyani, na ndio maana ni lazima tujitambue hivyo ili kuweza kujiepusha na tabia za namna hiyo.

Kwa sababu wengi ambao hawajafurahishwa na huyo dada kushinda usikute wala hawajitambui kuwa wanapoingiza rangi yake ya ngozi au asili yake wanakuwa wanafanya ubaguzi. Ukiwauliza je wewe ni mbaguzi jibu lao nina uhakika litakuwa hapana. Lakini watu hao hao wanawatuhumu kuwa Wahindi ni wabaguzi...kweli kazi ipo!!
 
Mbona unazungumza kama vile Wahindi siyo Watanzania? HIvi unaweza kusema "Wamang'ati ni lazima watambue jamii ya Watanzania kabla jamii haijawatambua" au unaweza kusema "Wahadzabe wajioneshe kuwa wanaikubali Tanzania, kabla Tanzania haijawakubali"? Kuhusu suala la baadhi yao kushirikiana na watawala wabovu nikuhakikishie kuwa wengi wanaotuletea mikataba mibovu ni weusi tii tii kama sisi, tena wengine ni wasukuma, wahaya, wanyakyusa, wamwera, wamakua n.k ! Ufisadi hauna rangi!

Waafrika walivyochukuliwa utumwani,walinyanyaswa,walipigwa,wakatengwa,nk.Lakini ilifika muda wakaanza kujijtetea wenyewe,kutetea haki zao,hadi jamii za kizungu zikaanza kuwakaribisha kidogo kidogo katika jamii.Je udhani Tanzania kuna ubaguzi wa rangi kufikia hizi nchi tunazoishi?Je nikisema wahindi wanajibagua wenyewe kabla hata jamii haijawabagua nitakua nimekosea?Kwa hiyo inabidi wahindi wajitambue kuwa ni watanzania na washirikiane na jamii katika shughuli zote,hata kama ni kufyatua tofali wakati wa ujenzi wa shule.Kwa njia hii tutakua na imani nao,tuachane na haya mambo ya u miss,tuzungumze ule ukweli,hawa wahindi wanaichukuliaje jamii ya kitanzania?
 
Back
Top Bottom